Yohana
3 Basi kulikuwako mtu mmoja wa Mafarisayo, Nikodemo lilikuwa jina lake, mtawala wa Wayahudi. 2 Huyo alimjia wakati wa usiku na kumwambia: “Rabi, twajua kwamba wewe ukiwa mwalimu umekuja kutoka kwa Mungu; kwa maana hakuna awezaye kufanya ishara hizi ambazo wewe wafanya isipokuwa iwe Mungu yuko pamoja naye.” 3 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Kwa kweli kabisa mimi nakuambia, Isipokuwa yeyote azaliwe tena, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.” 4 Nikodemo akamwambia: “Mtu awezaje kuzaliwa wakati yeye ni mzee? Hawezi kuingia katika tumbo la uzazi la mama yake mara ya pili na kuzaliwa, je, aweza?” 5 Yesu akajibu: “Kwa kweli kabisa mimi nakuambia, Isipokuwa yeyote azaliwe kutokana na maji na roho, hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu. 6 Kile ambacho kimezaliwa kutokana na mwili ni mwili, na kile ambacho kimezaliwa kutokana na roho ni roho. 7 Usistaajabu kwa sababu nimekuambia wewe, Nyinyi watu lazima mzaliwe tena. 8 Upepo huvuma ambako wataka, nawe wasikia mvumo wao, lakini hujui ambako huo watoka wala uendako. Ndivyo alivyo kila mtu ambaye amezaliwa kutokana na roho.”
9 Kwa kujibu Nikodemo akamwambia: “Mambo haya yawezaje kutukia?” 10 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Je, wewe ni mwalimu wa Israeli na bado hujui mambo haya? 11 Kwa kweli kabisa nakuambia, Yale tujuayo twasema na yale ambayo tumeona twatoa ushahidi juu yayo, lakini nyinyi watu hampokei ushahidi ambao twatoa. 12 Ikiwa mimi nimewaambia mambo ya kidunia na bado nyinyi hamwamini, mtaaminije nikiwaambia mambo ya kimbingu? 13 Zaidi ya hayo, hakuna mtu ambaye amepaa kuingia mbinguni ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, Mwana wa binadamu. 14 Na kama vile Musa alivyoinua nyoka mkubwa nyikani, ndivyo Mwana wa binadamu lazima ainuliwe juu, 15 ili kila mtu anayemwamini apate kuwa na uhai udumuo milele.
16 “Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu sana hivi kwamba akatoa Mwana mzaliwa-pekee wake, ili kila mtu anayedhihirisha imani katika yeye asipate kuangamizwa bali awe na uhai udumuo milele. 17 Kwa maana Mungu alimtuma Mwana wake kuingia katika ulimwengu, si ili ahukumu ulimwengu, bali ili ulimwengu uokolewe kupitia yeye. 18 Yeye ambaye hudhihirisha imani katika yeye si wa kuhukumiwa. Yeye ambaye hadhihirishi imani amehukumiwa tayari, kwa sababu hajadhihirisha imani katika jina la Mwana mzaliwa-pekee wa Mungu. 19 Basi huu ndio msingi wa hukumu, kwamba nuru imekuja ulimwenguni lakini watu wamependa giza kuliko nuru, kwa maana kazi zao zilikuwa mbovu. 20 Kwa maana yeye ambaye huzoea kufanya mambo maovu huchukia nuru na haji kwenye nuru, ili kazi zake zisipate kukaripiwa. 21 Lakini yeye ambaye hufanya lililo la kweli huja kwenye nuru, ili kazi zake zipate kudhihirishwa kuwa zilikwisha kufanywa kwa kupatana na Mungu.”
22 Baada ya mambo haya Yesu na wanafunzi wake walienda kuingia katika nchi ya Yudea, na huko akatumia wakati fulani pamoja nao na alikuwa akibatiza. 23 Lakini Yohana pia alikuwa akibatiza katika Ainoni karibu na Salimu, kwa sababu kulikuwa na kiasi kikubwa cha maji huko, na watu wakawa wakifuliza kuja na kubatizwa; 24 kwa maana Yohana alikuwa hajatupwa bado ndani ya gereza.
25 Kwa hiyo bishano likatokea kwa upande wa wanafunzi wa Yohana pamoja na Myahudi mmoja kuhusu utakaso. 26 Kwa hiyo wakaja kwa Yohana na kumwambia: “Rabi, mtu aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya Yordani, ambaye wewe umetoa ushahidi juu yake, ona, huyu anabatiza na wote wanaenda kwake.” 27 Kwa kujibu Yohana akasema: “Mtu hawezi kupokea hata kitu kimoja isipokuwa awe amepewa hicho kutoka mbinguni. 28 Nyinyi wenyewe mwanitolea ushahidi kwamba nilisema, Mimi siye Kristo, bali, nimetumwa kumtangulia huyo. 29 Yeye aliye na bibi-arusi ndiye bwana-arusi. Hata hivyo, rafiki ya bwana-arusi, asimamapo na kumsikia, ana shangwe nyingi sana kwa sababu ya sauti ya bwana-arusi. Kwa hiyo shangwe yangu hii imefanywa kuwa yenye kujaa. 30 Lazima huyo aendelee kuongezeka, lakini mimi lazima niendelee kupungua.”
31 Yeye ajaye kutoka juu yuko juu ya wengine wote. Yeye atokaye duniani ni wa kutoka duniani na husema juu ya mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yuko juu ya wengine wote. 32 Kile ambacho ameona na kusikia, yeye hutoa ushahidi juu yacho, lakini hakuna mtu anayekubali ushahidi wake. 33 Yeye ambaye amekubali ushahidi wake ameweka muhuri wake kwenye huo kwamba Mungu ni wa kweli. 34 Kwa maana yeye ambaye Mungu alimtuma husema semi za Mungu, kwa maana yeye hatoi roho kwa kipimo. 35 Baba humpenda Mwana na ametia vitu vyote mkononi mwake. 36 Yeye ambaye hudhihirisha imani katika Mwana ana uhai udumuo milele; yeye ambaye hukosa kutii Mwana hataona uhai, bali hasira ya kisasi ya Mungu hukaa juu yake.