Matendo
2 Basi siku ya msherehekeo wa Pentekoste ilipokuwa ikiendelea walikuwa wote pamoja mahali palepale, 2 na kwa ghafula kukatokea kutoka mbinguni kelele sawa na ile ya pepezi yenye nguvu inayovuma kwa kasi, nayo ikajaza nyumba yote ambayo katika hiyo walikuwa wameketi. 3 Na ndimi kama kwamba za moto zikawa zenye kuonekana kwao, nazo zikagawanywa huku na huku, na mmoja ukaketi juu ya kila mmoja wao, 4 nao wote wakawa wenye kujazwa roho takatifu wakaanza kusema katika lugha tofauti, kama vile roho ilivyokuwa ikiwaruhusu kufanya tamko.
5 Ikawa kwamba, kulikuwa na Wayahudi wakikaa katika Yerusalemu, wanaume wenye kumhofu Mungu, kutoka kila taifa la yale yaliyo chini ya mbingu. 6 Kwa hiyo, mvumo huo ulipotokea, umati ukaja pamoja nao ukashikwa na bumbuazi, kwa sababu kila mmoja aliwasikia wakisema katika lugha yake mwenyewe. 7 Kwa kweli, walishangaa na kuanza kustaajabu na kusema: “Oneni hapa, wote hawa wanaosema ni Wagalilaya, sivyo? 8 Na bado ni jinsi gani sisi, kila mmoja wetu, tunasikia lugha yake mwenyewe ambayo katika hiyo tulizaliwa? 9 Waparthi na Wamedi na Waelami, na wakaaji wa Mesopotamia, na Yudea na Kapadokia, Ponto na wilaya ya Asia, 10 na Frigia na Pamfilia, Misri, na sehemu za Libya, ambayo ni kuelekea Kirene, na wakaaji wa muda wa kutoka Roma, Wayahudi na pia wageuzwa-imani, 11 Wakrete na Waarabu, twawasikia wakisema katika lugha zetu juu ya mambo yenye fahari ya Mungu.” 12 Ndiyo, wote wakashangaa na kuwa katika fadhaa, wakiambiana: “Jambo hili lamaanisha nini?” 13 Hata hivyo, watu tofauti waliwadhihaki na kuanza kusema: “Wamejaa divai tamu.”
14 Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja na kuinua sauti yake na kufanya tamko hili kwao: “Wanaume wa Yudea nanyi nyote wakaaji wa Yerusalemu, acheni hili lijulikane kwenu nanyi tegeni sikio kwenye semi zangu. 15 Kwa kweli, watu hawa hawakulewa, kama nyinyi mdhanivyo, kwa maana ndiyo saa ya tatu ya mchana. 16 Kinyume chake, hili ndilo lililosemwa kupitia nabii Yoeli, 17 ‘“Na katika siku za mwisho,” Mungu asema, “Nitamwaga baadhi ya roho yangu juu ya kila namna ya mwili, na wana wenu na mabinti zenu watatoa unabii na wanaume wenu vijana wataona maono na wanaume wenu wazee wataota ndoto; 18 na hata juu ya watumwa wangu wanaume na juu ya watumwa wangu wanawake hakika mimi nitamwaga baadhi ya roho yangu katika siku hizo, nao watatoa unabii. 19 Nami hakika nitatoa mambo ya ajabu mbinguni juu na ishara juu ya dunia chini, damu na moto na ukungu wa moshi; 20 jua litageuzwa kuwa giza na mwezi kuwa damu kabla ya siku kubwa na yenye adhama ya Yehova kuwasili. 21 Na kila mtu aitiaye jina la Yehova ataokolewa.”’
22 “Wanaume wa Israeli, sikieni maneno haya: Yesu Mnazareti, mwanamume aliyeonyeshwa hadharani na Mungu kwenu kupitia kazi zenye nguvu na mambo ya ajabu na ishara ambazo Mungu alifanya kupitia yeye katikati yenu, kama vile nyinyi wenyewe mjuavyo, 23 mwanamume huyu, kama aliyetolewa kwa shauri lililoamuliwa na kwa ujuzi wa kimbele wa Mungu, mlimfunga kwenye mti kwa mkono wa watu waasi-sheria na kumwondolea mbali. 24 Lakini Mungu alimfufua kwa kuyafungua maumivu makali ya ghafula ya kifo, kwa sababu haikuwezekana yeye kuendelea kushikwa sana nacho. 25 Kwa maana Daudi asema kwa habari yake, ‘Nilikuwa na Yehova mbele ya macho yangu daima; kwa sababu yeye yuko kwenye mkono wangu wa kuume ili nisipate kutikiswa kamwe. 26 Kwa ajili ya hilo moyo wangu ulipata kuwa mchangamfu na ulimi wangu ukashangilia sana. Zaidi ya hayo, hata mwili wangu utakaa katika tumaini; 27 kwa sababu hutaacha nafsi yangu katika Hadesi, wala hutaruhusu mwaminifu-mshikamanifu wako aone uharibifu. 28 Umefanya njia za uhai zijulikane kwangu, utanijaza uchangamfu mwingi kwa uso wako.’
29 “Wanaume, akina ndugu, yaruhusika kusema nanyi kwa uhuru wa usemi kuhusu Daudi kichwa cha familia, kwamba alikufa na pia akazikwa na kaburi lake limo miongoni mwetu hadi siku hii. 30 Kwa hiyo, kwa sababu alikuwa nabii na alijua kwamba Mungu alikuwa amemwapia kwa kiapo kwamba angemketisha mmoja kutoka katika matunda ya viuno vyake juu ya kiti chake cha ufalme, 31 aliona kimbele na kusema kuhusu ufufuo wa Kristo, kwamba hakuachiliwa mbali katika Hadesi wala mwili wake haukuona uharibifu. 32 Yesu huyu Mungu alimfufua, uhakika ambao sisi sote ni mashahidi. 33 Kwa hiyo kwa sababu alikwezwa kwenye mkono wa kuume wa Mungu na kupokea roho takatifu iliyoahidiwa kutoka kwa Baba, amemwaga hiki ambacho nyinyi mwakiona na kukisikia. 34 Hakika Daudi hakupaa hadi mbinguni, bali yeye mwenyewe asema, ‘Yehova alimwambia Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kuume, 35 mpaka niweke maadui wako kuwa kibago kwa ajili ya miguu yako.”’ 36 Kwa hiyo acha nyumba yote ya Israeli ijue kwa hakika kwamba Mungu alimfanya Bwana na pia Kristo, Yesu huyu ambaye nyinyi mlimtundika mtini.”
37 Basi waliposikia hili walichomwa hadi kwenye moyo, nao wakamwambia Petro na wale mitume wengine: “Wanaume, akina ndugu, tufanye nini?” 38 Petro akawaambia hao: “Tubuni, na acheni kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo kwa msamaha wa dhambi zenu, nanyi mtapokea zawadi ya bure ya roho takatifu. 39 Kwa maana ahadi ni kwenu na kwa watoto wenu na kwa wote wale walio mbali, wengi kadiri ambayo Yehova Mungu wetu huenda akawaita kwake.” 40 Na kwa maneno mengine mengi akatoa ushahidi kamili na kufuliza kuwahimiza kwa bidii, akisema: “Pateni kuokolewa kutokana na kizazi hiki kilicho kombo.” 41 Kwa hiyo wale waliokubali neno lake kwa ukunjufu wa moyo wakabatizwa, na katika siku hiyo nafsi karibu elfu tatu zikaongezwa. 42 Nao wakaendelea kujitoa wenyewe kwa fundisho la mitume na kushirikiana, katika kula milo na katika sala.
43 Kwa kweli, hofu ikaanza kuwa juu ya kila nafsi, na mambo mengi ya ajabu na ishara nyingi zikaanza kutukia kupitia mitume. 44 Wote wale waliopata kuwa waamini walikuwa pamoja katika kuwa na mambo yote shirika, 45 nao wakaanza kuuza miliki na mali zao na kugawia wote hayo mapato, kama vile yeyote angekuwa na uhitaji. 46 Na siku baada ya siku walikuwa wakihudhuria daima kwenye hekalu kwa umoja, nao walikula milo yao katika nyumba za faragha na kushiriki chakula kwa shangilio kuu na weupe wa moyo, 47 wakimsifu Mungu na kupata upendeleo kwa watu wote. Wakati uleule Yehova akaendelea kuongeza kwao kila siku wale wenye kuokolewa.