Waefeso
Kwa Waefeso
1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kupitia mapenzi ya Mungu, kwa watakatifu walioko Efeso na waaminifu katika muungano na Kristo Yesu:
2 Na mwe na fadhili isiyostahiliwa na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3 Mbarikiwa awe Mungu na Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwa sababu ametubariki kwa kila baraka ya kiroho katika mahali pa kimbingu katika muungano na Kristo, 4 kama vile alivyotuchagua katika muungano naye kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu, ili tuwe watakatifu na bila waa mbele yake katika upendo. 5 Kwa maana alituagiza kimbele kwenye tendo la kufanywa kuwa wana wake mwenyewe kupitia Yesu Kristo, kulingana na upendezi mwema wa mapenzi yake, 6 kwa sifa ya fadhili yake isiyostahiliwa yenye utukufu aliyotukabidhi kwa fadhili kwa njia ya mpendwa wake. 7 Kwa njia yake tuna kuachiliwa kwa njia ya fidia kupitia damu ya huyo, ndiyo, msamaha wa makosa yetu, kulingana na utajiri wa fadhili yake isiyostahiliwa.
8 Hii aliisababisha izidi kutuelekea sisi katika hekima yote na akili nzuri, 9 kwa kuwa alitujulisha siri takatifu ya mapenzi yake. Ni kulingana na upendezi wake mwema alioukusudia katika yeye mwenyewe 10 kwa ajili ya uhudumiaji kwenye kikomo kamili cha nyakati zilizowekwa rasmi, yaani, kukusanya tena pamoja vitu vyote katika Kristo, vitu vilivyomo katika mbingu na vitu vilivyo duniani. Ndiyo, katika yeye, 11 katika muungano na yeye ambaye sisi tulihesabiwa pia kuwa warithi, kwa kuwa tuliagizwa kimbele kulingana na kusudi la yeye atendaye mambo yote kulingana na njia ambayo mapenzi yake hushauri, 12 ili tutumikie kwa ajili ya sifa ya utukufu wake, sisi ambao tumekuwa wa kwanza kutumaini katika Kristo. 13 Lakini nyinyi pia mlitumaini katika yeye baada ya kusikia neno la kweli, habari njema juu ya wokovu wenu. Kwa njia yake pia, baada ya nyinyi kuamini, mlitiwa muhuri kwa roho takatifu iliyoahidiwa, 14 ambayo ni arbuni ya kimbele ya urithi wetu, kwa kusudi la kuiachilia kupitia fidia miliki [ya Mungu] mwenyewe, kwa sifa yake yenye utukufu.
15 Hiyo ndiyo sababu mimi pia, kwa kuwa nimesikia juu ya imani mliyo nayo katika Bwana Yesu na kuelekea watakatifu wote, 16 siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu. Naendelea kuwataja nyinyi katika sala zangu, 17 ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, apate kuwapa nyinyi roho ya hekima na ya ufunuo katika ujuzi wake sahihi; 18 macho ya moyo wenu yakiwa yametiwa nuru, ili nyinyi mpate kujua ni nini tumaini ambalo kwa hilo yeye aliwaita nyinyi, ni nini utajiri wenye utukufu ambao yeye aweka kuwa urithi kwa ajili ya watakatifu, 19 na ni nini ulio ukubwa uzidio wa nguvu yake kuelekea sisi tulio waamini. Ni kulingana na utendaji wa uwezaji wa nguvu zake, 20 ambao kwa huo ametenda katika kisa cha Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu na kumketisha kwenye mkono wake wa kuume katika mahali pa kimbingu, 21 juu zaidi sana kuliko kila serikali na mamlaka na nguvu na ubwana na kila jina liitwalo, si katika mfumo huu wa mambo tu, bali pia katika ule ujao. 22 Alitiisha pia vitu vyote chini ya miguu yake, na kumfanya kuwa kichwa juu ya vitu vyote kwa kutaniko, 23 ambalo ni mwili wake, ujao wake ajazaye kabisa vitu vyote katika vyote.