1 Yohana
3 Ona ni namna gani ya upendo ambao Baba ametupa sisi, ili tuitwe watoto wa Mungu; na sisi ni wa namna hiyo hasa. Hiyo ndiyo sababu ulimwengu hauna ujuzi juu yetu, kwa sababu haujaja kumjua. 2 Wapendwa, sasa sisi ni watoto wa Mungu, lakini hadi hapa haijafanywa dhahiri kile tutakachokuwa. Twajua kwamba wakati wowote afanywapo dhahiri tutakuwa kama yeye, kwa sababu tutamwona kama vile alivyo. 3 Na kila mtu ambaye ana tumaini hili likiwa limewekwa juu yake hujitakasa mwenyewe kama vile huyo alivyo mwenye kutakata.
4 Kila mtu ambaye huzoea dhambi anazoea pia uasi-sheria, na kwa hiyo dhambi ni uasi-sheria. 5 Nyinyi mwajua pia kwamba huyo alifanywa dhahiri aondolee mbali dhambi zetu, na hakuna dhambi katika yeye. 6 Kila mtu anayedumu katika muungano na yeye hazoei dhambi; hakuna mtu azoeaye dhambi ambaye ama amemwona ama amekuja kumjua. 7 Watoto wadogo, msiache yeyote awaongoze vibaya; yeye ambaye huendeleza uadilifu ni mwadilifu, kama vile huyo alivyo mwadilifu. 8 Yeye ambaye huendeleza dhambi hutokana na Ibilisi, kwa sababu Ibilisi amekuwa akifanya dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alifanywa dhahiri, yaani, ili avunje-vunje kazi za Ibilisi.
9 Kila mtu ambaye amezaliwa kutokana na Mungu haendelezi dhambi, kwa sababu mbegu Yake ya uzazi hukaa katika mtu kama huyo, na hawezi kuzoea dhambi, kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. 10 Watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi ni dhahiri kwa jambo hili: Kila mtu ambaye haendelezi uadilifu hatokani na Mungu, wala yeye ambaye hapendi ndugu yake. 11 Kwa maana huu ndio ujumbe ambao mmesikia tangu mwanzo, kwamba twapaswa tupendane; 12 si kama Kaini, ambaye alitokana na yule mwovu akamchinja ndugu yake. Na ni kwa ajili ya nini yeye alimchinja? Kwa sababu kazi zake mwenyewe zilikuwa mbovu, lakini zile za ndugu yake zilikuwa za uadilifu.
13 Msistaajabu, akina ndugu, kwamba ulimwengu huwachukia nyinyi. 14 Sisi twajua tumepita kuvuka kutoka kifo hadi uhai, kwa sababu twapenda akina ndugu. Yeye ambaye hapendi hukaa katika kifo. 15 Kila mtu ambaye huchukia ndugu yake ni muua-binadamu-kikatili, nanyi mwajua kwamba hakuna muua-binadamu-kikatili aliye na uhai udumuo milele ukikaa katika yeye. 16 Kwa hili tumekuja kujua upendo, kwa sababu huyo alitoa nafsi yake kwa ajili yetu; na sisi tuko chini ya wajibu kutoa nafsi zetu kwa ajili ya ndugu zetu. 17 Lakini yeyote yule aliye na njia ya ulimwengu huu ya kutegemeza maisha na amwona ndugu yake akiwa na uhitaji na bado amfungia mlango wa huruma zake nyororo, ni katika njia gani kumpenda Mungu hukaa katika yeye? 18 Watoto wadogo, acheni tupende, si katika neno wala kwa ulimi, bali katika kitendo na kweli.
19 Kwa hili tutajua kwamba twatokana na kweli, na tutahakikishia mioyo yetu mbele yake 20 kwa habari ya chochote kile ambacho mioyo yetu huenda ikatulaumu katika hicho, kwa sababu Mungu ni mkubwa zaidi kuliko mioyo yetu na ajua mambo yote. 21 Wapendwa, ikiwa mioyo yetu haitulaumu, tuna uhuru wa usemi kuelekea Mungu; 22 na chochote kile tuombacho twapokea kutoka kwake, kwa sababu tunashika amri zake na kufanya mambo yanayopendeza machoni pake. 23 Kwa kweli, hii ndiyo amri yake, kwamba tuwe na imani katika jina la Mwana wake Yesu Kristo na tuwe tukipendana, kama vile yeye alivyotupa sisi amri. 24 Zaidi ya hayo, yeye ambaye hushika amri zake hukaa katika muungano na yeye, na yeye katika muungano na mtu kama huyo; na kwa hili twapata ujuzi kwamba anakaa katika muungano na sisi, kwa sababu ya roho ambayo yeye alitupa sisi.