Je! Wewe Ni Ndege Mpweke, Mwenye Huzuni?
YEYE hangeshinda katika mashindano ya urembo wa ndege—ama kwa rangi zake ama kwa umbo lake lenye kung’aa. Nimewaona walio wa kahawia katika Florida, U.S.A., wakijifyatusha chini kwa uhodari kama ule wa ndege Stukasi ya Ujerumani iliyokuwa ikijifyatusha chini kwa kutupa makombora katika Vita ya Ulimwengu ya Pili.a Katika Chile walikuwa weupe, wakiwa weusi katika mabawa na mwilini. (Ona picha.) Walikuwa wamepumzika wakiwa wenye huzuni juu ya miamba ya Pasifiki kule Valparaiso—labda wakimalizia kusaga chakula tumboni.
Huenda akawa na uzito wa kufikia kilo 14, urefu wa meta 1.5, na marefu ya meta 3 kwenye mabawa.[1a] Ni mmoja wa ndege walio wakubwa zaidi. Akiwa nchi-kavu ni ndege wa miendo mizito isiyovutia na sura ya kuchekesha; anaporuka ni wa kupendeza macho, naye huonekana akiruka kama kwamba kuruka ni mswaki kwake. Alapo chakula, aweza kuchota zaidi ya lita 10 za maji pamoja na samaki![2] Huyo ni nani? Ni mwari (pelikani).
Mwari hupatikana katika maziwa na mito na kandokando ya pwani katika sehemu nyingi za ulimwengu. Mdomo wake mrefu na tumbo lake kubwa lililo kama mfuko vimeumbika vizuri kabisa kwa kusudi la uvuvi wake wa namna maalumu. Yeye hujitumbukiza ndani ya maji, akijaza maji na samaki katika tumbo lake lililo kama mfuko. Halafu huyaondoa upesi maji hayo, kisha samaki aliyenaswa mwishoni ndiye huyoo, kateremka kooni kwa kugugumizwa.[3]
Mwari hutajwa mara kadhaa katika Biblia. Kwa sababu ya ndege huyo kupenda sana mahali pa upweke, pa ukiwa, yeye hutumiwa katika Biblia kama kifananishi cha ukiwa wa kabisa.[4] (Isaya 34:11; Sefania 2:13, 14) Ensaiklopedia ya Biblia Insight on the Scriptures hutaarifu hivi: “Mwari awapo ameshiba kwelikweli, mara nyingi yeye hurukia mbali mahali pa upweke, ambapo yeye hukaa kihuzuni, akiwa amepachika kichwa chake juu ya mabega yake . . . Ndege huyo hutwaa mkao huo kwa muda wa saa nyingi kwa safari moja, hivyo akilingana na kule kutokutenda ambako mtunga-zaburi hurejezea atoapo kielezi cha wingi wa mpenyo wa kihoro chake kwa kuandika hivi: ‘Niko kama mwari nyuni wa jangwani.’ (Zaburi 102:6)” Kwa hiyo wewe ukipata kuwa mpweke na mwenye huzuni wakati mmoja, kumbuka kwamba ungeweza pia kufanana na mwari!—Imechangwa.
[Maelezo ya Chini]
a Ile ndege Junkers Ju 87 iliyokuwa ikijifyatusha chini kwa kutupa makombora, yenye bawa lililokunjwa kombokombo kwa umbo la herufi “W.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Mwari katika Chile.
Picha ya ndani: Mwari- kahawia wa Florida