Matumizi ya Kisasa ya Mfano
MFANO wa Yesu juu ya “karamu kubwa” unatuambia namna wale walioalikwa walivyoanza kutoa udhuru (sababu) wa namna mbalimbali, wasihudhurie. Katika siku zetu ulimzuia mkulima Mnorway aliyealikwa ajifunze Biblia, asiweze kujifunza. Baada ya kutolewa nafasi hii mara nyingi, mkulima huyo alitoa udhuru, akisema kwamba alikuwa amenunua ng’ombe dume wachanga wanane ambao wangehitaji kuangaliwa daima. Walakini alionyeshwa maneno ya mfano wa Yesu katika Luka 14:18, 19: “Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. . . . Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.”
Basi, mkulima huyo Mnorway alishangaa kuona udhuru wake katika Biblia Miezi miwili baadaye, alirudi, akisema: “Nimeuza wale ng’ombe; sasa naweza kujifunza Biblia.” Upesi akafanya mabadiliko yaliyohitajiwa maishani mwake ili yapatane na kanuni za Kikristo. Na, ili apate wakati zaidi wa kumtumikia Mungu, hata aliamua kuuza tingatinga lake pamoja na vifaa vingine vya ukulima, akachukua kazi ya namna nyingine.