Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 5/22 kur. 14-16
  • Mbaniani—Mti Mmoja Wawa Msitu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mbaniani—Mti Mmoja Wawa Msitu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Dini na Mbaniani
  • Acheni Tupande Mbaniani
  • Kila Mtu Ataketi Chini ya Mtini Wake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • “Mti wa Uhai” Wenye Kushangaza wa Afrika
    Amkeni!—1995
  • Huzuni kwa Msitu Huo wa Mvua
    Amkeni!—1997
  • Calcutta—Jiji Lenye Pilikapilika na Utofautiano
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 5/22 kur. 14-16

Mbaniani—Mti Mmoja Wawa Msitu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA

KWA kawaida msitu hufanyizwa kwa miti mingi. Lakini kuna msitu mmoja ambao unafanyizwa kutokana na mti mmoja tu. Mbaniani ni mti usio wa kawaida sana, ambao waweza kuenea hadi kufunika eneo la zaidi ya hektari mbili! Huo huanza kukuaje? Huo huendeleaje kujieneza hadi kuweza kikweli kuitwa msitu?

Mbaniani ni wa oda ya mimea iitwayo Urticales na wa familia Moraceae, au familia maliberi, ambayo hutia ndani spishi 800 za mimea ya mtini. Mbaniani, au mtini wa Bengali, huanza maisha yao marefu kutokana na mbegu iliyo ndani ya kinyesi cha tumbili, ndege, au popo ambao wamekula matunda ya mbaniani.

Mbegu humea katika matawi ya mti-kimelewa, nayo mizizi husitawi katika majani yaliyooza yaliyokusanyika katika mianya. Hali nyevu husaidia mizizi ya mti mpya kukua kwa haraka; hiyo huwa minene kuzunguka shina la mti-kimelewa na kukua kuelekea chini kuingia ardhini. Kadiri inavyopata nguvu na ukubwa, ndivyo inavyozidi kuusonga mti-kimelewa, hilo likifanya mimea ya aina hii iitwe mitini inyongayo.

Sasa mbaniani uko tayari kupanuka. Mizizi haienei tu kutoka mwanzo wa shina kuu bali pia matawi hurefuka kwa ulalo, mizizi-hewa huanguka chini kutoka kwayo kuelekea ardhini na kujitia nanga mchangani. Kufanyizwa kwa msitu kumeanza.

Mbaniani, ambao hupatikana katika Afrika ya kitropiki na India, ukiwa na majani yao makubwa na yaliyo bapa, hutumika ukiwa kivuli kwa binadamu na wanyama. Mti mmoja katika India umeenea sana hivi kwamba yasemekana kuwa waweza kufunika zaidi ya watu 20,000! Tunda lao si zuri kuliwa na binadamu, nayo mbao ya mbaniani ni laini na yenye kupapa maji; hata hivyo, kitu cheupe chenye kunata kiitwacho ulimbo, ambacho hutoka kwenye mbao, hutumiwa kukamata ndege.

Mbaniani huishi muda gani? Mti mmoja katika jimbo la Andhra Pradesh wakadiriwa kuwa na umri wa miaka 600; miti mingine yenye kutokeza, inayolindwa ina zaidi ya umri wa miaka 250. Na ukuzi na ueneaji wa mbaniani huendelea bila kukoma.

Usemwao kuwa mbaniani mkubwa kuliko yote ijulikanayo uko Sri Lanka. Una mashina makubwa 350 na zaidi ya mashina madogo 3,000 yanayojishikamanisha kwa mti mmoja mkuu. Katika India mti wenye mizizi-tegemezi zaidi ya 1,100 na mwavuli wa zaidi ya hektari mbili ulipimwa majuzi na kupatikana kuwa ndio mkubwa kuliko yote katika nchi hiyo. Huo hulindwa daima na wanaume wanne wenye silaha ili kuuhifadhi kutokana na uharibifu. Mibaniani mingine ijulikanayo sana katika India hutia ndani mmoja ulioko karibu na Bangalore ufunikao hektari 1.2 na ni mahali papendwapo sana pa mandari kwa wakazi wa jijini. Kisha kuna mti mkubwa ajabu ulioko katika hifadhi ya wanyama wa pori ya Ranthambhore. Ukitajwa katika uandishi wa maliki wa Mogul miaka 500 iliyopita, mti huu huandaa kivuli kwa ndege, popo, nyoka, vichakulo, na wanyama wadogo-wadogo pamoja na wadudu wengi, zaidi ya kuwa mahali pa kuchezea na kuwindia kwa simbamarara na wanyama wawindaji wengine katika hiyo hifadhi.

Labda mbaniani ujulikanao vema zaidi katika India, ni mti wenye umri wa miaka 240 katika Bustani za Kibotania za Kitaifa katika Calcutta. Ukiwa na kimo kizidicho meta 24.5, huo hufunika eneo la hektari 1.2 na una mizizi-hewa zaidi ya 1,800 na sehemu ya juu iliyoenea yenye mduara wa meta 420. Msitu halisi!

Dini na Mbaniani

Tangu nyakati za kale watu wamekuwa wakiabudu miti. Ndivyo ilivyo na mbaniani pia; huo huonwa kuwa mtakatifu katika India hata leo. Miti mitakatifu yapasa kuwakilisha miungu hususa—kwa habari ya mbaniani, mungu Vishnu. Huonwa kuwa ni ibada kwa mungu wa miti wakati mti huo unapopandwa, kutiwa maji na kutunzwa.

Katika jamii za kale za Wapolinesia pia, mbaniani ulionwa kuwa mtakatifu. Sherehe za kidini zilifanywa katika mahali mstatili palipo wazi, au tohua, ambapo kupazunguka nyumba zilikuwa zimejengwa. Kwa kawaida kwenye mwisho mmoja wa mahali hapo palipo wazi kulikuwa na hekalu lenye mbaniani mtakatifu, ambao kwenye matawi yao mifupa iliyofungwa ya washiriki mashuhuri wa kabila waliokufa iliangikwa.

Mti huu mkubwa awali ulipewa jina na Wazungu. Katika Ghuba ya Uajemi na katika India, wasafiri wa mapema Wazungu waliona kwamba mwavuli ulioenea wa mti huo uliandaa kivuli ambacho chini yacho wafanya biashara walitandika vitu vyao ili kuvilinda kutokana na joto lenye kuchoma la jua. Katika mfumo wa jamii wa Hindu, wafanya biashara walikuwa kutoka tabaka kubwa liitwalo Vaisya, na jamii ndogo, mabaniani, walikuwa wauzaji wenye kutokeza wa nafaka na vyakula vinginevyo. Kuona kwamba baniani alikuwa akiuza bidhaa zake chini ya mti huo wenye kivuli kulifanya wageni wauite mti huo mbaniani.

Katika siku hizo mabaniani kwa kawaida walivaa vesti iliyotengenezwa kwa pamba yenye mifuko iliyofichwa ili kuweka fedha zao. Ikisaidia kuzuia joto na ikiwa rahisi kufua, hiyo vesti ilikuwa ya kawaida sana kwa wafanya biashara mabaniani hivi kwamba nguo hiyo iliitwa baniani, na baadaye jina hilo lilitumiwa kwa vesti yoyote ya mwanamume au shati la ndani. Bado jina hili latumiwa kwa shati la ndani la mwanamume katika India, na zoea la mabaniani la kuvaa aina hii ya nguo wanapofanya kazi bado lipo.

Acheni Tupande Mbaniani

Je, ungependa kupanda juu ya sehemu ya kati ya mbaniani? Ungeweza ikiwa ungepata kuzuru Hyderabad kusini mwa India. Karibu na Uwanja wa Ndege wa Begumpet, na karibu na katikati mwa jiji, kuna Machan, mkahawa wa juu ya mti uliojengwa katika matawi imara ya mbaniani na mpipali jirani, ambao pia ni mtini. Panda ngazi nene ya kamba kupita vijukwaa vilivyowekwa baada ya hatua fulani. Jengo ambalo umo limetengenezwa kwa mwanzi, makuti, na kamba. Paa la mwanzi lenye umbo la piramidi hukulinda kutokana na jua na mvua huku ukiingia kwenye chumba cha kula kilicho juu zaidi ya kati ya vile viwili ambavyo vimewekwa kwenye viwango tofauti. Sasa uko meta tisa kutoka ardhini. Fanicha nzuri zilizotengenezwa kwa mianzi myembamba na vibandiko vya kikabila vya kutani huongeza kwenye hisi ya kuwa katika msitu.

Unapokaa, unapewa kadi ya orodha ya vyakula iitwayo Mowgli, jina linalofahamika sana kwa wasomaji wa hadithi za Rudyard Kipling zilizo katika The Jungle Book. Hilo pia huongeza mazingira ya msituni. Sasa tulia kwa ono la kipekee la kula mlo katikati mwa mbaniani. Furahia vyakula vitamu vya India, kama vile biriani iliyokolezwa kwa viungo vingi ambayo imefanya Hyderabad ijulikane sana, kebabu, na vyakula vingine tofauti-tofauti.

Mlo wako umeisha, shuka kwa uangalifu kwenye ngazi ya kamba, ona maporomoko madogo ya maji na kijibwawa chenye yungiyungi, na utoke katika mkahawa huu wa kipekee wa juu ya mti uliojengwa katika mwavuli ulioenea wa mbaniani—mti ambao waweza kuenea na kuenea na kuenea hadi mti mmoja wawa msitu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mbaniani mmoja umekua na kuwa msitu

Juu: Picha iliyochukuliwa karibu ya mbaniani ulioko kwenye Bustani za Kibotania za Kitaifa, Calcutta

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mbaniani katika Bustani za Kibotania za Kitaifa, Calcutta

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mkahawa “Machan” katika mbaniani, Hyderabad

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki