Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Abrahamu—Kielelezo cha Imani
    Mnara wa Mlinzi—2001 | Agosti 15
    • Abrahamu—Kielelezo cha Imani

      “[Abrahamu alikuwa] baba ya wote wale walio na imani.”—WAROMA 4:11.

      1, 2. (a) Wakristo wa kweli leo wanamkumbuka Abrahamu kwa sababu ya mambo gani? (b) Kwa nini Abrahamu anaitwa “baba ya wote wale walio na imani”?

      ALIKUWA babu wa taifa lenye nguvu, nabii, mfanyabiashara, na kiongozi. Hata hivyo, leo yeye anakumbukwa sana miongoni mwa Wakristo kwa sababu ya sifa iliyofanya Yehova Mungu amwone kuwa rafiki—imani yake thabiti. (Isaya 41:8; Yakobo 2:23) Jina lake ni Abrahamu, nayo Biblia humwita “baba ya wote wale walio na imani.”—Waroma 4:11.

      2 Je, wanaume walioishi kabla ya Abrahamu kama vile Abeli, Enoki, na Noa, hawakuonyesha imani? Ndiyo, lakini agano la kubariki mataifa yote ya dunia lilifanywa pamoja na Abrahamu. (Mwanzo 22:18) Hivyo akawa baba kwa njia ya mfano kwa wote ambao hudhihirisha imani katika Mbegu aliyeahidiwa. (Wagalatia 3:8, 9) Kwa kadiri fulani, Abrahamu anaweza kuonwa kuwa baba yetu, kwa kuwa imani yake ni kielelezo cha kuigwa. Maisha yake yote yanaweza kuonwa kuwa udhihirisho wa imani, kwa kuwa yalikuwa na majaribu mengi sana. Naam, muda mrefu kabla ya Abrahamu kukabili lile linaloweza kuitwa jaribu kubwa zaidi la imani yake—amri ya kumtoa dhabihu mwana wake Isaka—Abrahamu alidhihirisha imani yake katika majaribu mengi madogo-madogo. (Mwanzo 22:1,2) Acheni sasa tuchunguze baadhi ya majaribu haya ya imani yaliyotokea mapema na kuona tunaweza kujifunza nini kutokana nayo.

      Amri ya Kuondoka Uru

      3. Biblia inatuambia nini kuhusu malezi ya Abramu?

      3 Biblia inamtaja Abramu (ambaye baadaye aliitwa Abrahamu) kwa mara ya kwanza kwenye andiko la Mwanzo 11:26, ambalo lasema: “Tera akaishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani.” Abramu alikuwa mzawa wa Shemu aliyemcha Mungu. (Mwanzo 11:10-24) Kulingana na Mwanzo 11:31, Abramu aliishi na familia yake katika mji wenye ufanisi wa “Uru wa Wakaldayo,” ambao wakati mmoja ulikuwa mashariki ya Mto Eufrati.a Hivyo, hakukua akiwa mhamaji mwenye kuishi mahemani bali alikuwa mkazi wa mji wenye anasa nyingi. Bidhaa kutoka nchi za nje zingeweza kununuliwa kwenye masoko ya Uru. Mitaa ya Uru ilikuwa na nyumba kubwa zilizopakwa chokaa ambazo zilikuwa na maji ya mfereji.

      4. (a) Ni magumu gani ambayo waabudu wa Mungu wa kweli walipata huko Uru? (b) Abramu alikuja kudhihirishaje imani katika Yehova?

      4 Mbali na manufaa za kimwili, maisha katika mji wa Uru yalifanya hali iwe ngumu sana kwa mtu yeyote aliyetaka kumtumikia Mungu wa kweli. Mji huo ulikolea ibada ya sanamu na ushirikina. Naam, jengo lililokuwa kubwa zaidi mjini humo ni hekalu refu lililomtukuza mungu-mwezi aitwaye Nanna. Yaelekea Abramu alishinikizwa sana, hata na watu fulani wa jamaa yake ashiriki ibada hiyo iliyopotoka. Kulingana na mapokeo fulani ya Wayahudi, Tera babake Abramu alikuwa mtengeneza sanamu. (Yoshua 24:2, 14, 15) Kwa vyovyote vile, Abramu hakushiriki ibada isiyo ya kweli na iliyopotoka. Babu yake Shemu aliyekuwa mzee alikuwa bado hai na yaelekea alimwambia Abramu kuhusu Mungu wa kweli. Kwa sababu hiyo, Abramu alidhihirisha imani katika Yehova badala ya Nanna!—Wagalatia 3:6.

      Imani Yajaribiwa

      5. Mungu alimpa Abramu amri na ahadi gani alipokuwa Uru?

      5 Imani ya Abramu ingejaribiwa. Mungu alimtokea na kumwamuru hivi: “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”—Mwanzo 12:1-3; Matendo 7:2, 3.

      6. Kwa nini Abramu alihitaji kuwa na imani ya kweli ili kuondoka Uru?

      6 Abramu alikuwa mzee na hakuwa na mtoto. Angewezaje kufanywa “kuwa taifa kubwa”? Nayo nchi aliyoamriwa aende ilikuwa wapi? Mungu hakumwambia. Kwa hiyo Abramu alihitaji kuwa na imani ya kweli ili kuondoka mji wa Uru wenye ufanisi na anasa. Kitabu kiitwacho Family, Love and the Bible chasema hivi kuhusu nyakati za kale: “Adhabu kali zaidi ambayo ingeweza kutolewa kwa mshiriki wa familia mwenye hatia ya kufanya uhalifu mbaya ni kumfukuza, kumnyima haki ya kuwa ‘mshiriki’ wa familia. . . . Hivyo kwa njia ya pekee Abrahamu alionyesha utii kamili na tumaini alipoitikia amri ya Mungu na kuacha nchi yake na watu wake.”

      7. Huenda Wakristo leo wakakabiliwaje na majaribu kama yale yaliyomkabili Abramu?

      7 Huenda Wakristo leo wakakabiliwa na majaribu kama hayo. Kama Abramu, huenda tukahisi tunashinikizwa kutanguliza mambo ya kimwili badala ya mambo yanayohusiana na ibada ya kweli. (1 Yohana 2:16) Huenda tukapingwa na watu wa familia wasioamini, kutia ndani watu wa ukoo waliotengwa, ambao huenda wakajaribu kutushawishi tushirikiane nao isivyofaa. (Mathayo 10:34-36; 1 Wakorintho 5:11-13; 15:33) Hivyo, Abramu alituwekea kielelezo kizuri. Aliweka uhusiano wake na Yehova mbele ya kitu kingine chochote—hata uhusiano wa kifamilia. Hakujua hasa ni lini, ni wapi, na ni jinsi gani ahadi za Mungu zingetimizwa. Hata hivyo, alikuwa tayari kutegemeza maisha yake juu ya imani aliyokuwa nayo katika ahadi hizo. Ni kitia moyo kizuri kama nini kwamba tutangulize Ufalme katika maisha yetu leo!—Mathayo 6:33.

      8. Imani ya Abramu ilikuwa na matokeo gani kwa washiriki wa karibu wa familia yake, nao Wakristo wanaweza kujifunza nini kutokana na jambo hilo?

      8 Vipi washiriki wa karibu wa familia ya Abramu? Yaelekea imani na usadikisho wa Abramu ulikuwa na matokeo yenye kutokeza kwa familia yake, kwa kuwa Sarai mke wake na mpwa wake Loti, aliyekuwa yatima, walichochewa kutii amri ya Mungu ya kuondoka Uru. Nahori, nduguye Abramu, na baadhi ya wazao wake waliondoka Uru baadaye, wakawa wakazi wa Harani ambako walimwabudu Yehova. (Mwanzo 24:1-4, 10, 31; 27:43; 29:4, 5) Hata Tera babake Abramu alikubali kuondoka pamoja na mwanawe! Hivyo, Biblia inasema kwamba Tera, akiwa kichwa cha familia, ndiye aliyechukua hatua ya kuhamisha familia yake kwenda Kanaani. (Mwanzo 11:31) Sisi pia tunaweza kufurahia mafanikio ya kadiri fulani tukiwatolea jamaa zetu ushahidi kwa busara.

      9. Ilimpasa Abramu afanye matayarisho gani kwa ajili ya safari yake, na kwa nini huenda matayarisho hayo yalitia ndani kujidhabihu?

      9 Kabla ya kuanza safari yake, Abramu alikuwa na shughuli nyingi. Ilimpasa kuuza mali na bidhaa na kununua mahema, ngamia, chakula, na vifaa alivyohitaji. Huenda Abramu alipata hasara kwa sababu ya matayarisho hayo ya harakaharaka, lakini alifurahia kumtii Yehova. Ilikuwa siku muhimu kama nini wakati alipomaliza matayarisho hayo na msafara wake ukasimama nje ya kuta za Uru, ukiwa tayari kusafiri! Msafara huo ulisafiri kuelekea kaskazini-magharibi, kandokando ya sehemu iliyojipinda ya Mto Eufrati. Baada ya kusafiri umbali upatao kilometa 1,000 kwa majuma kadhaa, msafara huo ulifika kwenye mji uliokuwa kaskazini mwa Mesopotamia uitwao Harani, kituo kikuu cha misafara.

      10, 11. (a) Yaelekea ni kwa nini Abramu alikaa Harani kwa muda fulani? (b) Wakristo wanaowatunza wazazi wao wazee wanapewa kitia moyo gani?

      10 Yaelekea Abramu alikaa Harani kwa sababu ya babake Tera, aliyekuwa mzee. (Mambo ya Walawi 19:32) Vivyo hivyo Wakristo wengi leo wana pendeleo la kutunza wazazi wao wazee au wagonjwa, wengi hata wakifanya marekebisho fulani ili kufanya hivyo. Inapokuwa lazima kuwatunza wazazi, watu hao wanaweza kuwa na hakika kwamba kujidhabihu kwao kwa upendo ‘kunakubalika machoni pa Mungu.’—1 Timotheo 5:4.

      11 Muda ulipita na “siku za Tera zilikuwa miaka mia mbili na mitano; Tera akafa katika Harani.” Bila shaka Abramu alihuzunishwa sana na kifo hicho, lakini kipindi cha kuomboleza kilipomalizika, aliondoka mara moja. “Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu [“Loti,” NW] mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani.”—Mwanzo 11:32; 12:4, 5.

      12. Abramu alifanya nini alipokuwa huko Harani?

      12 Inapendeza kuona kwamba Abramu ‘alijipatia vitu’ alipokuwa Harani. Japo alikuwa ameacha vitu vya kimwili alipoondoka Uru, Abramu aliondoka Harani akiwa tajiri. Bila shaka jambo hilo lilitokana na baraka za Mungu. (Mhubiri 5:19) Ingawa Mungu haahidi watu wake wote utajiri leo, yeye hutimiza ahadi yake ya kutosheleza mahitaji ya wale ambao ‘wameacha nyumba, ndugu, au dada’ kwa ajili ya Ufalme. (Marko 10:29, 30) Abramu pia ‘alijipatia watu,’ yaani watumishi wengi. Maandishi yaitwayo The Jerusalem Targum na Chaldee Paraphrase yanasema kwamba Abramu ‘alibadili watu imani.’ (Mwanzo 18:19) Je, imani yako inakuchochea kuzungumza na majirani, wafanyakazi wenzako, au wanashule wenzako? Badala ya kukaa tu huko Harani na kusahau amri ya Mungu, Abramu alitumia wakati wake huko kwa matokeo. Lakini wakati wa kukaa huko sasa ulikuwa umeisha. “Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru.”—Mwanzo 12:4.

      Ng’ambo ya Eufrati

      13. Abramu alivuka Mto Eufrati lini, na kuvuka huko kulimaanisha nini?

      13 Ilimbidi Abramu asafiri tena. Aliondoka Harani na kusafiri umbali upatao kilometa 90 kuelekea magharibi. Huenda ikawa kwamba Abramu alikaa kwa muda katika eneo fulani kwenye Eufrati, ng’ambo ya kituo cha kale cha biashara cha Karkemishi. Kituo hicho kilikuwa muhimu kwa misafara iliyovuka kwenda ng’ambo ya pili.b Msafara wa Abramu ulivuka mto huo lini? Biblia inaonyesha kwamba ulivuka miaka 430 kabla ya kule Kutoka kwa Wayahudi nchini Misri mwezi wa Nisani 14, 1513 K.W.K. Andiko la Kutoka 12:41 lasema: “Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi ya Misri.” (Italiki ni zetu.) Basi inaelekea kwamba lile agano la Kiabrahamu lilianza kufanya kazi Nisani 14, 1943 K.W.K., wakati ambapo kwa utii Abramu alivuka Eufrati.

      14. (a) Abramu angeweza kuona nini kwa macho yake ya imani? (b) Ni katika maana gani watu wa Mungu leo wamebarikiwa zaidi kuliko Abramu?

      14 Abramu alikuwa ameacha mji wenye ufanisi. Lakini sasa angeweza kuona kimbele “jiji lililo na misingi halisi,” serikali ya uadilifu itakayotawala wanadamu. (Waebrania 11:10) Naam, japo Abramu alikuwa na ujuzi kidogo sana, alikuwa ameanza kupata ufahamu wa juujuu tu kuhusu kusudi la Mungu la kukomboa wanadamu wenye kufa. Leo, tumebarikiwa kuwa na ujuzi mwingi zaidi wa makusudi ya Mungu kuliko Abramu. (Mithali 4:18) Sasa “jiji,” au utawala wa Ufalme, ambao Abramu alitumaini unatawala, na ulisimamishwa tangu mwaka wa 1914. Kwa hiyo, je, hatupaswi kuchochewa kutenda mambo yanayoonyesha imani na tumaini katika Yehova?

      Kukaa Katika Bara Lililoahidiwa Kwaanza

      15, 16. (a) Kwa nini Abramu alihitaji kuwa na ujasiri ili kumjengea Yehova madhabahu? (b) Wakristo leo wanawezaje kuwa na ujasiri kama Abramu?

      15 Andiko la Mwanzo 12:5, 6 latuambia: “[Mwishowe] wakaingia katika nchi ya Kanaani. Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa shekemu; mpaka mwaloni wa More.” Shekemu ulikuwa umbali wa kilometa 50 kaskazini ya Yerusalemu kwenye bonde lenye rutuba ambalo limeelezwa kuwa “paradiso ya bara takatifu.” Hata hivyo, “Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.” Kwa kuwa maadili ya Wakaanani yalikuwa yamepotoka, ilimbidi Abramu ajitahidi kulinda familia yake na uvutano wao wenye kupotosha.—Kutoka 34:11-16.

      16 Kwa mara nyingine, “BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao [“mbegu,” NW] wako nitawapa nchi hii.” Ni jambo lenye kusisimua kama nini! Bila shaka, Abramu alihitaji kuwa na imani ili kufurahia jambo ambalo lingenufaisha tu uzao wake wakati ujao. Hata hivyo, Abramu aliitikia kwa ‘kumjengea madhabahu BWANA aliyemtokea.’ (Mwanzo 12:7) Msomi mmoja wa Biblia adokeza: “Kujengwa [kwa] madhabahu nchini humo kulikuwa hasa njia ya kuimiliki nchi hiyo kirasmi kwa kutegemea haki ambayo Abramu alipata kutokana na imani yake.” Pia ujenzi wa madhabahu hiyo ulikuwa tendo la ujasiri. Yaelekea kwamba madhabahu hiyo ilikuwa kama ile ambayo imeelezwa katika agano la Sheria, ambayo ilijengwa kwa mawe ya asili (yasiyochongwa). (Kutoka 20:24, 25) Ingekuwa tofauti kabisa na madhabahu zilizotumiwa na Wakanaani. Kwa hiyo Abramu alichukua msimamo wa kijasiri akiwa mwabudu wa Mungu wa kweli, Yehova, jambo ambalo lingeweza kufanya achukiwe na hata kuhatarisha maisha yake. Namna gani sisi leo? Je, baadhi yetu—hasa wachanga—tunasita kuwajulisha majirani au wanashule wenzetu kwamba tunamwabudu Yehova? Acheni kielelezo cha ujasiri cha Abramu kituchochee sote kujivunia kuwa watumishi wa Yehova!

      17. Abramu alijithibitishaje kuwa mhubiri wa jina la Mungu, na jambo hilo linawakumbusha nini Wakristo leo?

      17 Sikuzote Abramu aliiona ibada ya Yehova kuwa muhimu kokote alikokwenda. “Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliita jina la BWANA.” (Mwanzo 12:8) Maneno ya Kiebrania ‘kuliitia jina’ pia yanamaanisha “kulitangaza (kulihubiri) jina hilo.” Yaelekea Abramu alilitangaza jina la Yehova kwa ujasiri miongoni mwa majirani wake Wakaanani. (Mwanzo 14:22-24) Jambo hilo linatukumbusha jukumu letu la kushiriki kadiri tuwezavyo “kulifanyia jina lake tangazo la hadharani” leo.—Waebrania 13:15; Waroma 10:10.

      18. Abramu alikuwa na uhusiano wa aina gani na wakazi wa Kanaani?

      18 Abramu hakukaa sana katika maeneo hayo. “Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu”—eneo kavu upande wa kusini wa milima ya Yuda. (Mwanzo 12:9, Biblia Habari Njema) Kwa kuendelea kuhamahama na kujithibitisha kuwa mwabudu wa Yehova katika kila eneo jipya, Abramu na jamaa yake ‘walitangaza hadharani kwamba wao walikuwa watu wasiojulikana na wakaaji wa muda katika nchi.’ (Waebrania 11:13) Sikuzote waliepuka kuwa na ukaribu sana na majirani wao wapagani. Vivyo hivyo leo, Wakristo hawapaswi kuwa “sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:16) Japo sisi huwaonyesha fadhili na heshima majirani wetu na wafanyakazi wenzetu, tunakuwa waangalifu tusijiingize katika mwenendo unaoonyesha roho ya ulimwengu uliojitenga na Mungu.—Waefeso 2:2, 3.

      19. (a) Kwa nini maisha ya kuhamahama yalikuwa magumu kwa Abramu na Sarai? (b) Ni magumu gani zaidi yaliyokuwa karibu kumpata Abramu?

      19 Na tusisahau kwamba haikuwa rahisi kwa Abramu na Sarai kuzoea maisha magumu ya kuhamahama. Walipata chakula kutokana na mifugo yao badala ya kukinunua kwenye mojawapo ya masoko ya Uru yaliyojaa bidhaa; waliishi mahemani badala ya kuishi katika nyumba iliyojengwa vizuri. (Waebrania 11:9) Abramu alikuwa na shughuli nyingi katika maisha yake; alikuwa na kazi nyingi ya kusimamia mifugo yake na watumishi wake. Yaelekea Sarai alifanya kazi ambazo kidesturi zilifanywa na wanawake wa utamaduni huo: kukanda unga, kuoka mikate, kusokota sufu, na kushona nguo. (Mwanzo 18:6, 7; 2 Wafalme 23:7; Mithali 31:19; Ezekieli 13:18) Hata hivyo, majaribu zaidi yalikuwa karibu. Muda si muda Abramu na jamaa yake wangekabili hali ambayo ingehatarisha maisha yao! Je, imani ya Abramu ingekuwa yenye nguvu za kukabili hali hiyo ngumu?

  • Mwe na Imani Kama ya Abrahamu!
    Mnara wa Mlinzi—2001 | Agosti 15
    • Mwe na Imani Kama ya Abrahamu!

      “Wale washikamanao sana na imani ndio wale walio wana wa Abrahamu.” —WAGALATIA 3:7.

      1. Abramu alikabilianaje na jaribu jingine nchini Kanaani?

      ABRAMU alikuwa ameacha maisha ya anasa huko Uru kwa kutii amri ya Yehova. Matatizo aliyopata katika miaka iliyofuata yalikuwa mwanzo tu wa jaribu la imani alilokabili huko Misri. Simulizi la Biblia lasema: “Kulikuwa njaa katika nchi ile.” Ingekuwa rahisi kama nini kwa Abramu kulalamika kwa sababu ya hali yake! Badala yake alichukua hatua zifaazo kuruzuku familia yake. “Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.” Jamaa ya Abramu ingetambuliwa kwa urahisi nchini Misri kwa kuwa ilikuwa kubwa. Je, Yehova angetimiza ahadi zake na kumlinda Abramu asipatwe na madhara?—Mwanzo 12:10; Kutoka 16:2, 3.

      2, 3. (a) Kwa nini Abramu hakutaka ijulikane Sarai alikuwa nani? (b) Abramu alimtendeaje mkewe kwa kuzingatia hali ilivyokuwa?

      2 Twasoma hivi kwenye Mwanzo 12:11-13: “Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu [“dada,” NW] yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.” Ingawa Sarai alikuwa na umri uliozidi miaka 65, bado alikuwa mrembo sana. Jambo hilo lilihatarisha maisha ya Abramu.a (Mwanzo 12:4, 5; 17:17) Jambo lililokuwa muhimu zaidi ni kwamba mambo yaliyohusiana na makusudi ya Yehova yalihusika, kwa kuwa alikuwa amesema kwamba kupitia mbegu ya Abramu mataifa yote ya dunia yangejibariki. (Mwanzo 12:2, 3, 7) Kwa kuwa Abramu hakuwa na mtoto, ilikuwa muhimu sana aendelee kuishi.

      3 Abramu alizungumza na mkewe kuhusu kutumia mbinu waliyokuwa wamekubaliana hapo awali, yaani, aseme yeye ni dada yake. Ona kwamba ingawa Abramu alikuwa na mamlaka akiwa mzee wa ukoo, hakutumia cheo chake vibaya, bali alitafuta msaada wa mke wake na vilevile kuungwa mkono naye. (Mwanzo 12:11-13; 20:13) Katika jambo hilo, Abramu aliweka kielelezo kizuri kwa waume kutumia ukichwa kwa upendo, naye Sarai aliwawekea wanawake wa leo kielelezo kwa kuwa mtiifu.—Waefeso 5:23-28; Wakolosai 4:6.

      4. Watumishi waaminifu wa Mungu leo wanapaswa kutendaje wakati maisha ya ndugu zao yanapokuwa hatarini?

      4 Sarai angeweza kusema kwamba alikuwa dada ya Abramu kwa sababu alikuwa kwa kweli dadake wa kambo. (Mwanzo 20:12) Isitoshe, haikuwa lazima atoe habari kwa watu ambao hawakustahili kuambiwa habari hizo. (Mathayo 7:6) Watumishi waaminifu wa Mungu wa siku hizi hutii amri ya Biblia ya kuwa wanyofu. (Waebrania 13:18) Kwa mfano, hawawezi kamwe kuapa kusema kweli kisha waseme uwongo mahakamani. Hata hivyo, wakati maisha ya ndugu zetu yanapokuwa hatarini kiroho na kimwili, kama wakati wa mnyanyaso au msukosuko wa kiraia, wao hutii ushauri wa Yesu wa kuwa “wenye hadhari kama nyoka na bado kuwa wasio na hatia kama njiwa.”—Mathayo 10:16; ona Mnara wa Mlinzi, Novemba 1, 1996, ukurasa wa 18, fungu la 19.

      5. Kwa nini Sarai alikuwa tayari kukubali ombi la Abramu?

      5 Sarai aliitikiaje ombi la Abramu? Mtume Petro anafafanua wanawake kama yeye kuwa ‘walitumaini katika Mungu.’ Kwa hiyo Sarai alifahamu masuala ya kiroho yaliyohusika. Licha ya hayo, Sarai alimpenda na kumheshimu mume wake. Hivyo aliamua ‘kujitiisha mwenyewe kwa mume wake’ na kuficha kwamba alikuwa ameolewa. (1 Petro 3:5) Bila shaka, kufanya hivyo kulihatarisha maisha ya Sarai. “Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao.”—Mwanzo 12:14, 15.

      Ukombozi wa Yehova

      6, 7. Abramu na Sarai walijikuta katika hali gani zenye kuhuzunisha, naye Yehova alimwokoaje Sarai?

      6 Jambo hilo liliwahuzunisha kama nini Abramu na Sarai! Ilionekana kwamba Sarai alikuwa karibu kunajisiwa. Isitoshe, kwa kutojua kwamba Sarai alikuwa ameolewa, Farao alimpa Abramu zawadi nyingi sana, hivi kwamba “alikuwa na kondoo na ng’ombe , na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia.”b (Mwanzo 12:16) Ni lazima Abramu awe alichukizwa kama nini na zawadi hizo! Ingawa hali zilionekana kuwa mbaya, Yehova hakuwa amemwacha Abramu.

      7 “Lakini BWANA akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu.” (Mwanzo 12:17) Kwa njia fulani ambayo haikufichuliwa, Farao alijulishwa kilichosababisha “mapigo” hayo. Alichukua hatua mara moja: “Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N’nini hili ulilonitenda? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.”—Mwanzo 12:18-20; Zaburi 105:14, 15.

      8. Leo Yehova anaahidi Wakristo ulinzi wa aina gani?

      8 Leo, Yehova hatuahidi ulinzi kutokana na madhara ya kifo, uhalifu, njaa, au misiba ya asili. Tumepewa ahadi kwamba sikuzote Yehova atatulinda na mambo yanayoweza kuhatarisha hali yetu ya kiroho. (Zaburi 91:1-4) Yeye hufanya hivyo hasa kwa kututolea maonyo wakati ufaao kupitia Neno lake na “mtumwa mwaminifu na mwenye busara.” (Mathayo 24:45) Vipi tisho la kifo kutokana na mnyanyaso? Ingawa watu mmoja-mmoja wanaweza kuachwa wafe, Mungu hataruhusu kamwe watu wake wote wauawe. (Zaburi 116:15) Na ikiwa waaminifu fulani watakufa, tunaweza kuwa na hakika kwamba watafufuliwa.—Yohana 5:28, 29.

      Kujidhabihu ili Kudumisha Amani

      9. Ni nini kinachoonyesha kwamba Abramu aliishi maisha ya kuhamahama huko Kanaani?

      9 Kwa kuwa njaa iliyokuwa Kanaani ilikuwa imeisha, “Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu [eneo kavu lililo kusini ya milima ya Yuda]. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu.” (Mwanzo 13:1, 2, BHN) Hivyo wakazi wa Negebu wangemwona kuwa mtu mwenye uwezo sana, mkuu mwenye nguvu. (Mwanzo 23:6) Abramu hakutamani kukaa huko na kujihusisha na siasa za Wakanaani. Badala yake, ‘aliendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai.’ Kama kawaida, Abramu aliiona ibada ya Yehova kuwa muhimu kokote alikokwenda.—Mwanzo 13:3, 4, BHN.

      10. Ni tatizo gani lililotokea baina ya wachungaji wa Abramu na Loti, na ni kwa nini ilifaa tatizo hilo lisuluhishwe haraka?

      10 ‘Na Loti aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu na, wachunga wanyama wa Loti; na siku zile Wakaanani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi.’ (Mwanzo 13:5-7) Nchi hiyo haikuwa na maji wala malisho ya kutosha mifugo ya Abramu na ya Loti. Hivyo kukawa na ugomvi na chuki baina ya wachungaji hao. Haikufaa waabudu wa Mungu wa kweli kugombana. Iwapo ugomvi huo ungeendelea, uhusiano wao ungevunjika kabisa. Hivyo Abramu angesuluhishaje ugomvi huo? Alikuwa amechukua Loti baada ya kifo cha baba ya Loti, na labda kumlea kama mtoto wake mwenyewe. Kwa kuwa Abramu ndiye aliyekuwa na umri mkubwa zaidi kati yao wawili, je hakustahili kuchukua kilichokuwa bora zaidi?

      11, 12. Abramu alimtolea Loti pendekezo gani la ukarimu, na ni kwa nini uchaguzi wa Loti haukuwa wa hekima?

      11 Lakini ‘Abramu akamwambia Loti, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.’ Karibu na Betheli kuna ile ambayo imetajwa kuwa “sehemu nzuri sana ya kutazama eneo la Palestina.” Labda ni kutoka hapo ‘Loti aliinua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.’—Mwanzo 13:8-10.

      12 Ingawa Biblia husema kwamba Loti alikuwa “mwadilifu,” kwa sababu fulani yeye hakumnyenyekea Abramu kwa staha kuhusiana na jambo hilo, wala haionekani kana kwamba alitafuta ushauri wa Abramu aliyekuwa na umri mkubwa zaidi. (2 Petro 2:7) ‘Loti akajichagulia Bonde lote la Yordani; Loti akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akaa katika nchi ya Kanaani, na Loti akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.’ (Mwanzo 13:11, 12) Mji wa Sodoma ulikuwa na ufanisi na manufaa nyingi za kimwili. (Ezekieli 16:49, 50) Uchaguzi wa Loti ulikuwa mbaya kwa upande wa kiroho japo huenda ukaonekana kuwa wa hekima kwa kuzingatia vitu vya kimwili. Kwa nini? Kwa sababu “watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA,” lasema andiko la Mwanzo 13:13. Uamuzi wa Loti wa kuhamia eneo hilo ungehuzunisha sana familia yake hatimaye.

      13. Kielelezo cha Abramu chaweza kuwasaidiaje Wakristo ambao huenda wakawa na ugomvi wa kifedha?

      13 Lakini Abramu alionyesha imani katika ahadi ya Yehova kwamba hatimaye mbegu yake ingemiliki nchi hiyo yote; hakugombania sehemu ndogo tu ya nchi hiyo. Kwa ukarimu, yeye alitenda kupatana na kanuni ambayo baadaye ilitajwa kwenye 1 Wakorintho 10:24: “Acheni kila mmoja afulize kutafuta sana, si faida yake mwenyewe, bali ya mtu yule mwingine.” Hili ni kikumbusho kizuri kwa wale ambao huenda wakawa na ugomvi wa kifedha na waamini wenzao. Badala ya kufuata ushauri ulio kwenye Mathayo 18:15-17, wengine wamepeleka ndugu zao mahakamani. (1 Wakorintho 6:1, 7) Kielelezo cha Abramu chaonyesha kwamba ni afadhali kupata hasara kifedha badala ya kufanya jina la Yehova lishutumiwe au kuharibu amani ya kutaniko la Kikristo.—Yakobo 3:18.

      14. Abramu angethawabishwaje kwa sababu ya ukarimu wake?

      14 Abramu angethawabishwa kwa sababu ya ukarimu wake. Mungu alisema: “Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako utahesabika.” Ni lazima Abramu ambaye hakuwa na mtoto awe alitiwa moyo kama nini na kufunuliwa kwa jambo hilo! Halafu, Mungu akaamuru: “Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo.” (Mwanzo 13:16, 17) La, Abramu hangeruhusiwa kukaa katika mazingira yenye starehe ya mji. Ilimpasa kujitenga na Wakanaani. Ni lazima Wakristo leo pia wajitenge na ulimwengu. Hawajioni kuwa bora kuliko wengine, lakini hawashirikiani kwa ukaribu na yeyote ambaye anaweza kuwashawishi washiriki katika mwenendo ulio kinyume cha Maandiko.—1 Petro 4:3, 4.

      15. (a) Kuhamahama kwa Abramu kulikuwa na maana gani? (b) Abramu aliweka kielelezo gani kwa familia za Kikristo leo?

      15 Katika nyakati za Biblia, mtu alikuwa na haki ya kukagua ardhi kabla ya kuimiliki. Hivyo, huenda ikawa kuhamahama kulimkumbusha Abramu daima kwamba siku moja nchi hiyo ingemilikiwa na uzao wake. Kwa utii, “Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea BWANA madhabahu huko.” (Mwanzo 13:18) Kwa mara nyingine, Abramu alidhihirisha kwamba aliiona ibada kuwa jambo muhimu sana. Je, familia yako huona funzo la familia, sala, na kuhudhuria mikutano kuwa mambo muhimu sana?

      Adui Ashambulia

      16. (a) Kwa nini maneno ya utangulizi ya Mwanzo 14:1 yanaonyesha kwamba jambo baya li karibu kutokea? (b) Kwa nini wafalme wanne wa mashariki walifanya uvamizi?

      16 “Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamuc na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita.” Katika Kiebrania cha awali, maneno hayo ya utangulizi (“Ikawa siku za . . .”) yanaonyesha kwamba jambo baya li karibu kutokea na yanaashiria “kipindi cha majaribu kinacholeta baraka.” (Mwanzo 14:1, 2, NW, kielezi-chini) Jaribu hilo lilianza wakati wafalme hawa wanne wa mashariki pamoja na majeshi yao walipofanya uvamizi wao wenye uharibifu huko Kanaani. Walikuwa na lengo gani? Walitaka kukomesha uasi wa miji mitano ya Sodoma, Gomora, Adma, Seboimu, na Bela. Waliishinda miji hiyo, “wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi.” Loti na familia yake waliishi hapo karibu.—Mwanzo 14:3-7.

      17. Kwa nini kutekwa kwa Loti kulijaribu imani ya Abramu?

      17 Wafalme wa Kanaani walizuia wavamizi hao kwa ujasiri, lakini wakashindwa vibaya sana. “Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao. Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao.” Muda si muda, habari za matukio hayo yenye kuhuzunisha zikamfikia Abramu: “Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu. [Hivyo Abramu akapata] habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka.” (Mwanzo 14:8-14, BHN) Ni jaribu la imani lililoje! Je, Abramu angekuwa na chuki kuelekea mpwa wake kwa kuwa alichukua sehemu ya nchi iliyokuwa bora zaidi? Kumbuka pia kwamba wavamizi hawa walitoka Shina, nchi yake ya asili. Kupigana nao kungefanya isiwezekane kwake kurudi nyumbani. Isitoshe, je, Abramu angeweza kufanya chochote dhidi ya jeshi ambalo majeshi yote ya Kanaani hayakuweza kuyashinda?

      18, 19. (a) Abramu aliwezaje kumwokoa Loti? (b) Ni nani aliyepata sifa kwa ushindi huo?

      18 Kwa mara nyingine, Abramu alimtumaini Yehova kabisa. ‘Akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Demeski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Loti nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.’ (Mwanzo 14:14-16) Kwa kuonyesha imani yenye nguvu katika Yehova, Abramu alipata ushindi kwa jeshi lake lililokuwa dogo sana, akamwokoa Loti na familia yake. Wakati huo ndipo Abramu alipokutana na Melkizedeki, mfalme-kuhani wa Salemu. “Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.”—Mwanzo 14:18-20.

      19 Naam, Yehova ndiye aliyekuwa mshindi. Kwa mara nyingine tena, Abramu aliokolewa na Yehova kwa sababu ya imani yake. Watu wa Mungu leo hawashiriki katika vita halisi, lakini wao hukabili majaribu na magumu mengi. Makala yetu ifuatayo itaonyesha jinsi kielelezo cha Abramu kiwezavyo kutusaidia kukabiliana na magumu hayo kwa mafanikio.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki