-
Yabisi-kavu Ni Ugonjwa UnaolemazaAmkeni!—2001 | Desemba 8
-
-
Yabisi-kavu Ni Ugonjwa Unaolemaza
“IWAPO HUJAWAHI KUUGUA UGONJWA HUO HUTAWEZA KUWAZIA ULE UCHUNGU UNAOSABABISHWA NAO. NILIFIKIRI NI KIFO PEKEE AMBACHO KINGEWEZA KUMALIZA MAUMIVU YANGU.” —SETSUKO, JAPANI.
“UGONJWA HUO UMEHARIBU UJANA WANGU KWA SABABU NIMEKUWA NAO TANGU NILIPOKUWA NA UMRI WA MIAKA 16.”DARREN, UINGEREZA.
“NIMEPOTEZA MIAKA MIWILI YA MAISHA YANGU KWA KUWA NILIKUWA MGONJWA KITANDANI KWA MUDA HUO.”— KATIA, ITALIA.
“VIUNGO VYANGU VYOTE VILIPOANZA KUUMA, NILIHISI MAUMIVU MATUPU.”—JOYCE, AFRIKA KUSINI.
HAYO ni maelezo yenye kuhuzunisha ya wagonjwa wanaougua yabisi-kavu (arthritis). Kila mwaka mamilioni ya wagonjwa huenda kwa madaktari ili wapate kitulizo cha maumivu, kukakamaa, na ulemavu unaosababishwa na ugonjwa huo.
Zaidi ya watu milioni 42 wanaugua ugonjwa wa yabisi-kavu nchini Marekani pekee, na mtu 1 kati ya watu 6 hulemazwa na ugonjwa huo. Ugonjwa wa yabisi-kavu ni kisababishi kikuu cha ulemavu katika nchi hiyo. Shirika la Taifa la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa linasema kwamba ugonjwa huo huathiri uchumi kama vile ‘kushuka kwa uchumi kunavyofanya,’ kwa kuwa Wamarekani hupoteza zaidi ya dola bilioni 64 kila mwaka kwa matibabu na kwa sababu ya upungufu wa uzalishaji. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, uchunguzi mbalimbali uliofanywa katika nchi zinazoendelea kama vile Brazili, Chile, China, India, Indonesia, Malaysia, Mexico, Pakistan, Thailand, na Ufilipino ulionyesha kwamba ugonjwa wa yabisi-kavu na magonjwa mengine aina ya baridi-yabisi huathiri nchi hizo karibu “sawa na vile yanavyoathiri nchi zilizoendelea.”
Si wazee pekee wanaoshikwa na yabisi-kavu. Ni kweli kwamba wazee ndio wanaoathiriwa zaidi na ugonjwa huo. Hata hivyo, watu wengi wanaougua ugonjwa wa baridi-yabisi (rheumatoid arthritis), ambao ni aina moja ya yabisi-kavu, ni watu wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 50. Nchini Marekani, karibu watu 3 kati ya 5 wanaougua yabisi-kavu wana umri unaopungua miaka 65. Hali kadhalika, huko Uingereza, wagonjwa milioni 1.2 kati ya milioni 8 wana umri unaopungua miaka 45. Zaidi ya watoto 14,500 wanaugua ugonjwa huo.
Idadi ya wagonjwa wanaougua yabisi-kavu inaongezeka kila mwaka. Watu milioni moja watapata ugonjwa huo nchini Kanada katika miaka kumi ijayo. Ingawa ugonjwa wa yabisi-kavu ni wa kawaida zaidi huko Ulaya kuliko katika bara la Asia na Afrika, unaendelea kuenea katika mabara hayo pia. Kwa hiyo, kipindi cha mwaka wa 2000 hadi 2010 kimetangazwa na Shirika la Afya Ulimwenguni kuwa Mwongo wa Mifupa na Viungo. Katika kipindi hicho madaktari na wataalamu wanaotunza afya ulimwenguni pote watashirikiana kuboresha maisha ya watu wanaougua magonjwa yanayoathiri mifupa na misuli, kama vile yabisi-kavu.
Tunajua nini kuhusu ugonjwa huo unaosababisha maumivu makali? Ni nani hasa wanaoweza kuupata? Wale wanaolemazwa na ugonjwa huo wanaweza kukabiliana na ulemavu wao jinsi gani? Je, tunaweza kutarajia tiba? Maswali hayo yatajibiwa katika sehemu zinazofuata.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Picha ya eksirei: Used by kind permission of the Arthritis Research Campaign, United Kingdom (www.arc.org.uk)
-
-
Yabisi-kavu Ni Ugonjwa wa Aina Gani?Amkeni!—2001 | Desemba 8
-
-
Yabisi-kavu Ni Ugonjwa wa Aina Gani?
“NINAPOENDA KULALA USIKU, MIMI HULIA MACHOZI NINAPOTAZAMA MIGUU NA MIKONO YANGU ILIYOHARIBIKA UMBO.”—MIDORI, JAPANI.
UGONJWA wa yabisi-kavu umeathiri wanadamu kwa karne nyingi. Maiti za kale zilizohifadhiwa huko Misri zinathibitisha jambo hilo. Yaelekea, mvumbuzi Christopher Columbus alikuwa na ugonjwa huo. Na mamilioni wanateseka leo. Ugonjwa huo wenye kulemaza ni ugonjwa wa aina gani?
Jina la Kiingereza la ugonjwa huo, “arthritis,” linatokana na maneno ya Kigiriki yanayomaanisha “viungo vilivyovimba,” nalo larejezea magonjwa na hali mbalimbali za yabisi zaidi ya 100.a Mbali na kuathiri viungo, magonjwa hayo yanaweza kuathiri pia misuli, mifupa, na kano (mishipa inayounganisha misuli na mifupa) mbalimbali zinazotegemeza viungo. Aina fulani za yabisi-kavu zinaweza kuathiri ngozi yako, maungo ya ndani ya mwili, na hata macho yako. Tutachunguza hasa magonjwa mawili ya aina ya yabisi-kavu, yaliyo ya kawaida sana—ugonjwa wa osteoarthritis na baridi-yabisi.
Muundo wa Viungo
Kiungo ni mahali ambapo mifupa miwili imeunganishwa. Mfuko unaonyumbuka hufunika viungo fulani vinavyolainishwa na umajimaji mzito. Mfuko huo huvilinda viungo hivyo na kuvitegemeza. (Tazama picha kwenye ukurasa wa 4.) Mfuko huo una utando wa ndani unaotokeza umajimaji huo wenye kulainisha. Ncha ya mifupa iliyomo ndani ya mfuko huo zimefunikwa kwa mfupa mwororo unaoitwa gegedu. Gegedu hiyo inazuia mifupa yako isisuguane. Nayo hulinda viungo vyako kwa kupunguza shinikizo na kwa kufanya mifupa yote ihimili shinikizo kwa usawa.
Kwa mfano, unapotembea, kukimbia, au kuruka, shinikizo kwenye viuno na magoti yako linaweza kuwa mara nne hadi mara nane ya shinikizo la uzito wako! Ijapokuwa misuli na kano za sehemu hiyo zinaweza kupunguza shinikizo hilo, gegedu husaidia mifupa yako kuhimili uzito huo inaposhinikizwa.
Baridi-Yabisi
Mtu anaposhikwa na ugonjwa wa baridi-yabisi, mfumo wa kinga wa mwili huanza kushambulia viungo vyake kwelikweli. Kwa sababu isiyojulikana, chembe nyingi za damu—kutia ndani chembe za T, ambazo ni chembe muhimu katika mfumo wa kinga wa mwili—huingia ghafula katika vitundu vya kiungo. Jambo hilo husababisha utendaji mwingi wa kemikali ambao hufanya kiungo kifure. Huenda chembe zinazotokeza umajimaji zianze kuongezeka kwa wingi sana, na kusababisha uvimbe unaoitwa pannus. Kisha uvimbe huo hutokeza vimeng’enya vinavyoharibu gegedu. Sasa kwa sababu mifupa inaweza kugusana, inakuwa vigumu kusogeza kiungo na hiyo husababisha maumivu makali sana. Misuli na kano pia hupoteza nguvu. Hiyo inafanya kiungo kianze kulegea na kuteguka kwa kadiri fulani, na mara nyingi kuharibika umbo. Kwa kawaida ugonjwa wa baridi-yabisi huathiri viwiko, magoti, na miguu kwa wakati mmoja. Asilimia 50 hivi ya wagonjwa wanaougua baridi-yabisi hupata pia uvimbe au vinundu chini ya ngozi. Wengine wana upungufu wa damu, na wanaumwa na koo na macho makavu. Uchovu na dalili za mafua, kama vile homa na maumivu ya misuli, ni dalili nyingine za baridi-yabisi.
Si wagonjwa wote wanaougua baridi-yabisi walio na dalili zilezile, na hata muda ambao wagonjwa huugua hutofautiana vilevile. Huenda mtu mmoja akaanza kuumwa na kukakamaa polepole kwa muda wa majuma kadhaa au hata miaka. Lakini mtu mwingine anaweza kuwa mgonjwa ghafula. Baadhi ya watu huugua baridi-yabisi kwa muda wa miezi michache tu kisha wanapona kabisa. Wengine wanaweza kujisikia vibaya sana wakati fulani na kujisikia nafuu wakati mwingine. Na wengine wanaugua kwa miaka mingi, wakiendelea kulemazwa.
Ni nani hasa wanaoweza kupata ugonjwa wa baridi-yabisi? Dakt. Michael Schiff anasema kwamba “hasa wanawake wa makamo wanapata ugonjwa huo.” Hata hivyo, Schiff anasema pia kuwa “mtu yeyote wa umri wowote ule, watoto, na vilevile wanaume, wanaweza kupata ugonjwa huo.” Wale walio na watu wa ukoo wenye baridi-yabisi, wanakabili hatari ya kuupata kuliko watu wengine. Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba kuvuta sigara, kunenepa kupita kiasi, na kutiwa damu mishipani huzidisha hatari ya kushikwa na ugonjwa huo.
Yabisi-Kavu Aina ya Osteoarthritis
Jarida la Western Journal of Medicine lasema kwamba “ugonjwa wa osteoarthritis hufanana na hali ya hewa kwa njia nyingi—upo kila mahali, mara nyingi hautiliwi maanani, na nyakati nyingine una athari mbaya sana.” Ugonjwa wa osteoarthritis (OA) hutofautiana na baridi-yabisi kwa kuwa hauenei hadi sehemu nyingine za mwili bali huathiri kiungo kimoja tu au viungo vichache. Gegedu inapoharibika hatua kwa hatua, mifupa huanza kusuguana. Wakati huohuo mifupa mipya inayotokeza huanza kukua karibu na kiungo. Uvimbe unaweza kutokea, na mfupa ulio chini ya gegedu huwa mzito na kuharibika umbo. Dalili nyingine za ugonjwa huo ni, vinundu kwenye viungo vya vidole, sauti ya kusugua katika viungo vilivyoathiriwa, mishtuko ya ghafula ya misuli, na vilevile maumivu, kukakamaa, na kushindwa kusogeza viungo.
Zamani, ilidhaniwa kwamba ugonjwa huo ulitokea tu kwa sababu ya uzee. Hata hivyo, wataalamu wametupilia mbali dhana hiyo ya kale. Jarida la The American Journal of Medicine lasema hivi: “Hakuna uthibitisho wowote kwamba kiungo cha kawaida kinachofanya kazi ya kawaida tu kitaharibika katika kipindi cha maisha.” Basi, kisababishi cha ugonjwa huo wa osteoarthritis ni nini? Gazeti la Uingereza la The Lancet linasema kwamba jitihada za kuelewa kisababishi cha ugonjwa huo “zimetokeza ubishi mwingi.” Baadhi ya wachunguzi wanafikiri kwamba huenda mfupa ulikuwa umejeruhiwa mbeleni bila kugunduliwa. Halafu, huenda madhara hayo yakasababisha ule ukuzi wa mfupa unaotokeza na vilevile kuharibika kwa gegedu. Wengine wanadhani kwamba ugonjwa huo huanzia katika gegedu yenyewe. Wanafikiri kwamba gegedu hiyo inapoharibika na kuchakaa, shinikizo kwenye mfupa unaokinzwa na gegedu hiyo huzidi. Mabadiliko katika viungo hutokea mwili unapojaribu kutengeneza gegedu iliyoharibika.
Ni nani hasa anayeweza kupata ugonjwa huo? Ijapokuwa si uzee unaosababisha ugonjwa huo, uharibifu wa gegedu huwaathiri hasa wazee. Wengine wanaoweza kupata ugonjwa huo ni watu ambao wana kasoro fulani katika viungo vyao, au wale wenye misuli dhaifu ya miguu na mapaja, miguu isiyo na urefu sawa, au kasoro katika uti wa mgongo. Kiungo kilichojeruhiwa katika aksidenti, au kutumia kiungo fulani kupita kiasi kazini kunaweza pia kusababisha ugonjwa huo. Baada ya uharibifu wa gegedu kuanza, kunenepa kupita kiasi kunaweza kuuzidisha.
Dakt. Tim Spector anasema hivi: “Osteoarthritis ni ugonjwa tata ambao mara nyingi husababishwa na hali ya mazingira tunamoishi lakini hurithiwa vilevile.” Hasa wanawake wa makamo na wanawake wazee walio na watu wa ukoo wenye ugonjwa huo wanakabili hatari ya kuupata. Ni watu walio na mifupa migumu hasa wanaopata ugonjwa wa osteoarthritis, tofauti na ugonjwa wa osteoporosis unaodhoofisha mifupa. Watafiti fulani wanasema pia kwamba madhara yanayosababishwa na molekuli ya oksijeni yenye idadi ya elektroni isiyogawanyika kwa mbili, na upungufu wa vitamini C na D, unaweza kusababisha ugonjwa huo.
Matibabu
Matibabu ya yabisi-kavu kwa kawaida huhusisha kutumia dawa, mazoezi ya mwili, na kubadili namna ya kuishi. Huenda tabibu wa maungo akaanzisha matibabu ya mazoezi ya mwili. Mazoezi hayo yanaweza kuhusisha mazoezi ya kukaza misuli, mazoezi yanayoboresha mfumo wa kupumua na mzunguko wa damu, kama vile kutembea au kukimbia, na mazoezi ya misuli ya kuinua vitu vizito. Mazoezi hayo yamesaidia sana kupunguza dalili nyingi kama vile uvimbe na maumivu ya viungo, unyong’onyevu, uchovu, na kushuka moyo. Mazoezi hayo hunufaisha hata wale walio wazee sana. Mazoezi yanaweza pia kuzuia kudhoofika kwa mifupa. Watu fulani wanadai kwamba maumivu yanaweza kupunguzwa kwa matibabu mbalimbali ya maungo kwa kutumia joto na baridi na kwa tiba ya vitobo.b
Kupunguza unene kunaweza kusaidia sana kutuliza maumivu ya viungo yanayosababishwa na yabisi-kavu. Inasemekana kwamba chakula kinachoweza kupunguza unene na vilevile maumivu ni chakula chenye kalisi nyingi kama vile mboga, matunda, na samaki wanaoishi katika bahari zenye maji baridi sana wenye asidi-mafuta nyingi inayoitwa omega-3. Chakula kilichotayarishwa katika viwanda na chakula chenye mafuta yenye asidi nyingi kiepukwe. Vyakula hivyo maalumu vinasaidia vipi? Inasemekana kwamba vyakula hivyo huzuia uvimbe. Wengine wanasema kwamba wamesaidiwa kwa kutokula nyama, vyakula vinavyotengenezwa kwa maziwa, ngano, na jamii ya mboga za mtunguja, nyanya, viazi, pilipili, na biringani.
Baadhi ya wagonjwa wanapendekezewa upasuaji unaohusisha kuingiza chombo fulani ndani ya kiungo chenyewe, na kuondoa utando unaotokeza vimeng’enya vinavyoharibu gegedu. Hata hivyo, mara nyingi uvimbe hurudi baada ya upasuaji huo. Upasuaji wenye matokeo ya mara moja unahusisha kuondoa kiungo kizima (mara nyingi nyonga au goti) na kuweka kiungo kingine cha bandia. Mara nyingi maumivu huisha kabisa baada ya upasuaji huo, na viungo vya bandia hudumu kwa miaka 10 hadi 15.
Hivi majuzi madaktari wamejaribu matibabu ya kuingiza asidi fulani ndani ya kiungo. Magoti hasa hutibiwa kwa njia hiyo. Kulingana na uchunguzi mbalimbali huko Ulaya, matibabu ya kuingiza umajimaji mbalimbali unaotibu gegedu yamekuwa na manufaa kwa kadiri fulani pia.
Ijapokuwa ugonjwa wa yabisi-kavu hauna dawa, kuna dawa nyingi za kutuliza maumivu na uvimbe, na yaelekea baadhi ya hizo zinaweza kuzuia kwa kadiri fulani ugonjwa usizidi. Dawa zifuatazo ni dawa ambazo hutumiwa kutuliza dalili za yabisi-kavu: Dawa za kutuliza maumivu, dawa mbalimbali za cortisone, dawa zisizo na steroidi za kutibu uvimbe (NSAID), dawa za kupunguza dalili za ugonjwa zisizo za kutuliza maumivu (DMARD), dawa zinazozuia utendaji wa mfumo wa kinga za aina mbalimbali, na dawa nyinginezo. Hata hivyo, dawa hizo zote zinaweza kuwa na athari mbaya sana. Si jambo rahisi kwa daktari na mgonjwa kuchagua dawa inayofaa.
Baadhi ya wale ambao wameugua ugonjwa wa yabisi-kavu wamewezaje kuvumilia ugonjwa huo mkali?
[Maelezo ya Chini]
a Kati ya hayo kuna ugonjwa wa osteoarthritis, baridi-yabisi, systemic lupus erythematosus (ugonjwa wa mfumo wa kinga wa mwili), ugonjwa wa baridi-yabisi wa watoto, jongo, bursitis (uvimbe wa bega au wa kiwiko cha mkono), homa ya baridi-yabisi, maradhi ya Lyme, maumivu na kudhoofika kwa kiganja cha mkono, fibromyalgia (uyabisi wa misuli na kano za mwili), ugonjwa wa Reiter, na ugonjwa wa baridi-yabisi wa uti wa mgongo.
b Gazeti la Amkeni! halipendekezi matibabu, dawa, wala upasuaji wowote. Kila mgonjwa ana daraka la kuchunguza na kuelewa manufaa na athari za matibabu yanayopatikana.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
KUNENEPA KUPITA KIASI, KUVUTA SIGARA, NA KUTIWA DAMU MISHIPANI KUNAWEZA KUZIDISHA UWEZEKANO WA KUPATA UGONJWA WA BARIDI-YABISI
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
MATIBABU YA BADALA
Dawa fulani ambazo hazipendekezwi na madaktari mara nyingi zinadhaniwa kuwa na athari chache kuliko zile za kawaida. Kati ya dawa hizo kuna protini aina ya type II collagen, ambayo baadhi ya watafiti wanasema inapunguza uvimbe na maumivu ya viungo yanayosababishwa na baridi-yabisi. Dawa hiyo inafanya kazi jinsi gani? Inazuia protini zinazosababisha uvimbe zinazoitwa interleukin-1 na tumor necrosis factor α zisiongezeke. Imeripotiwa kwamba baadhi ya virutubishi katika chakula pia vinaweza kuzuia protini hizo. Baadhi ya virutubishi hivyo ni: vitamini E, vitamini C, niacinamide, mafuta ya samaki yenye asidi nyingi aina ya eicosapentaenoic, na asidi ya gammalinolenic, mafuta ya mbegu za mmea wa borage, na mafuta ya ua la evening primrose. Huko China miti-shamba aina ya Tripterygium wilfordii Hook F, imetumiwa kwa miaka mingi. Inasemekana kwamba imesaidia baadhi ya wagonjwa wenye baridi-yabisi kupata nafuu.
[Mchoro katika ukurasa wa 4, 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KIUNGO KISICHOATHIRIWA NA UGONJWA
“BURSA”
MSULI
GEGEDU
UKANO
MFUKO WA KIUNGO
UTANDO UNAOTOKEZA UMAJIMAJI
MFUPA
UMAJIMAJI WA KULAINISHA
KIUNGO KILICHOATHIRIWA NA BARIDI-YABISI
UWAZI UNAOPUNGUA
UHARIBIFU WA MFUPA NA GEGEDU
UTANDO ULIOVIMBA UNAOTOKEZA UMAJIMAJI
KIUNGO KILICHOATHIRIWA NA UGONJWA WA “OSTEOARTHRITIS”
VIPANDE VYA GEGEDU ILIYOHARIBIKA
GEGEDU INAYOHARIBIKA
MFUPA UNAOKUA ISIVYO KAWAIDA
[Hisani]
Source: Arthritis Foundation
[Picha katika ukurasa wa 7]
Watu wenye umri wowote ule wanaweza kuathiriwa na ugonjwa wa yabisi-kavu
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mazoezi ya mwili na chakula kinachofaa kinaweza kupunguza maumivu
-
-
Tumaini kwa Wale Wanaougua Yabisi-KavuAmkeni!—2001 | Desemba 8
-
-
Tumaini kwa Wale Wanaougua Yabisi-Kavu
“UGONJWA wa yabisi-kavu hauui mara nyingi kama vile maradhi ya moyo na kansa yanavyofanya, hata hivyo, unaathiri sana hali ya maisha,” Dakt. Fatima Mili anasema. Ugonjwa huo unaweza kuathiri kila jambo maishani. Wagonjwa wa yabisi-kavu wanakabili matatizo gani hasa? Je, inawezekana kuvumilia?
Huko Italia, mtu mmoja anayeitwa Katia,a mwenye umri wa miaka 28, anasema hivi: “Maisha yangu yote yalibadilika nilipokuwa na umri wa miaka 20 nilipojua kwamba nilikuwa na ugonjwa wa yabisi-kavu. Ilinibidi kuacha kazi na utumishi wa wakati wote kwa sababu ya maumivu.” Kila mtu anayeugua yabisi-kavu huwa na maumivu. Huko Uingereza, mtu mmoja mwenye umri wa miaka 63 anayeitwa Alan anasema hivi: “Sikuzote, sehemu fulani ya mwili wangu inauma, ijapokuwa huenda maumivu yasiwe makali sana.” Uchovu ni tatizo jingine. Sarah, mwenye umri wa miaka 21, anasema: ‘Ni vigumu zaidi kuvumilia ule uchovu kuliko kuvumilia maumivu na uvimbe.’
Uchungu wa Moyoni
Huko Japani, Setsuko, mwenye umri wa miaka 61, anasema kwamba kupambana kila siku na maumivu ya kudumu “kunachosha mtu kiakili na kihisia.” Hata kushika kalamu au simu ni vigumu! Kazumi, mwenye umri wa miaka 47, analalamika: “Nimeshindwa kufanya hata mambo ya kawaida ambayo mtoto anaweza kufanya.” Janice, mwenye umri wa miaka 60, ambaye hawezi kusimama wala kutembea kwa muda mrefu, anasema hivi: “Ninavunjika moyo kwa sababu siwezi kufanya yale ambayo nilikuwa nimezoea kufanya.”
Hali kama hizo zinaweza kufanya mtu akate tamaa na ajione kuwa asiyefaa. Gaku, mwenye umri wa miaka 27, ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova anasema hivi: “Ninahisi kwamba sifai kitu, kwa sababu siwezi kushiriki kikamili katika kazi ya kuhubiri habari njema wala kutimiza madaraka yangu kutanikoni. Francesca, ambaye amepambana na yabisi-kavu tangu alipokuwa na umri wa miaka miwili, anasema kwamba ‘anaendelea kushuka moyo zaidi na zaidi.’ Mtu anayeshuka moyo hivyo, anaweza kuathiriwa kiroho. Joyce, ambaye ni Shahidi huko Afrika Kusini, anakiri kwamba aliacha kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Anasema: “Sikutaka kumwona mtu yeyote.”
Huenda mgonjwa akawa na wasiwasi mwingi kuhusu wakati wake ujao—wasiwasi kwamba atakuwa mlemavu asiyejiweza, wasiwasi kwamba ataachwa bila mtu wa kumtunza, wasiwasi kwamba ataanguka na kuvunjika mifupa, wasiwasi kwamba hataweza kuruzuku familia yake. Yoko, aliye na umri wa miaka 52, anasema: “Nilipoona jinsi mwili wangu ulivyoharibika umbo, nilikuwa na wasiwasi kwamba hali hiyo ingezidi.”
Huenda watu wa familia wakahuzunika pia wanapowaona wapendwa wao wakiteseka kila siku. Wenzi wa ndoa hata wanaweza kupata matatizo makubwa ya ndoa. Mwanamke mmoja huko Uingereza anayeitwa Denise anasema hivi: “Baada ya miaka 15 ya ndoa yetu, mume wangu alisema, ‘Siwezi tena kuvumilia ugonjwa wako wa yabisi-kavu!’ Aliniacha na binti yetu mwenye umri wa miaka 5.”
Kwa hiyo, wagonjwa wanaougua yabisi-kavu na hali kadhalika familia zao wanakabili hali ngumu. Hata hivyo, wengi wanapambana na hali hiyo kwa mafanikio! Tusikie maoni ya wengine.
Ishi kwa Kupatana na Hali Yako
Kupumzika vya kutosha ni muhimu iwapo unaugua yabisi-kavu; kunaweza kupunguza uchovu. Hata hivyo, hupaswi kukaa kitako tu. Timothy anasema hivi: ‘Lazima ufanye mambo mbalimbali, la sivyo ugonjwa huo utakushinda, nawe utakaa tu huku ukihisi maumivu.’ Tabibu wa Ugonjwa wa Baridi-Yabisi, William Ginsburg wa Kituo cha Afya cha Mayo, anasema hivi: “Mgonjwa hapaswi kufanya mengi mno, wala kidogo mno. Nyakati nyingine, inatubidi kuwakumbusha wagonjwa wapunguze shughuli na kuishi kwa kupatana na hali yao.”
Huenda jambo hilo likamaanisha kubadili maoni yako juu ya hali yako. Daphne anayeishi huko Afrika Kusini, anasema hivi: “Imenibidi kusawazisha maoni yangu na kutambua kwamba sijapoteza uwezo wangu wa kufanya mambo mbalimbali; ninahitaji tu kuyafanya polepole. Badala ya kuhangaika au kuvunjika moyo, ninafanya kidogo-kidogo tu.”
Pia inafaa kuelewa vifaa mbalimbali vinavyopatikana. Huenda ukaweza kuzungumzia jinsi vinavyoweza kukusaidia pamoja na daktari wako au tabibu fulani wa maungo. Keiko anasema: “Sisi tumeweka kifaa cha kunipandisha kwenye ngazi. Vifundo vya milango viliumiza mikono yangu kwa hiyo tumevirekebisha. Sasa ninaweza kufungua milango yote kwa kuisukuma kwa kichwa changu. Tuliweka kifaa cha kurahisisha kufungua mfereji wa maji ili niweze kufanya angalau kazi fulani za nyumbani.” Mgonjwa mwingine wa yabisi-kavu anayeitwa Gail anasema hivi: “Funguo za gari langu na nyumba yangu zimeunganishwa na mpini mrefu ili kurahisisha kufungua milango hiyo. Chanuo changu na burashi vina mipini mirefu pia na vinaweza kupindwa ili niweze kuchanua nywele zangu pande zote.”
Familia Wanaweza Kutia Moyo Sana
Carla anayeishi huko Brazili, anasema hivi: “Mume wangu amenisaidia na kunitia moyo sana. Nilitiwa moyo alipoambatana nami kumwona daktari. Tulijifunza pamoja jinsi ugonjwa huo unavyoathiri mwili wangu, dalili zake, na matibabu ambayo ningehitaji. Ilinisaidia kujua kwamba alielewa magumu yangu.” Ndiyo, waume na wake wanaotambua udhaifu wa wenzi wao na walio tayari kujifunza juu ya hali yao wanaweza kusaidia sana na kutia moyo.
Kwa mfano, Bette, alifanya kazi ya usafi, mume wake aliposhindwa kufanya kazi yake ya ujenzi kwa sababu ya yabisi-kavu. Mume wa Kazumi alimtunza na alifanya kazi ya nyumbani ambayo Kazumi hakuweza kufanya. Isitoshe, aliwazoeza watoto wao kufanya kazi mbalimbali. Kazumi anasema hivi: “Mume wangu amenitia moyo sana. Bila msaada wake ningekuwa katika hali mbaya sana.”
Mwanamke mmoja anayeitwa Carol, huko Australia, anaonya hivi: “Usifanye mengi mno. Nisipoweza kufanya yote ambayo wengine wa familia wanafanya ninahisi kana kwamba nimeshindwa.” Watu wa familia wanaowaelewa wagonjwa na kuwajali wanaweza kuwasaidia sana na kuwatia moyo.
Msaada wa Kiroho
Katia anasema: “Mtu anapougua ugonjwa huu, anaamini kabisa kwamba hakuna mtu yeyote anayeelewa hali yake. Kwa hiyo, ni muhimu sana kumwendea Yehova Mungu, kwa kuwa yeye anaelewa kabisa hali yetu ya afya na hisia zetu za moyoni. (Zaburi 31:7) Kwa sababu nina uhusiano mzuri pamoja na Yehova, nimepata amani ya akili kiasi cha kwamba sihangaishwi tena na ugonjwa wangu.” Kwa kufaa Biblia yamwita Yehova, “Mungu wa faraja yote, ambaye hutufariji katika dhiki yetu yote.”—2 Wakorintho 1:3, 4.
Kwa hiyo, sala inaweza kuwa chanzo kikubwa cha faraja kwa wale wenye maumivu ya kudumu. Kazumi anaeleza: “Ninaposhindwa kupata usingizi kwa sababu ya maumivu, ninamtolea Yehova sala za moyoni huku nikilia machozi na kumwomba nguvu ya kuvumilia maumivu hayo, na hekima ya kukabili matatizo yangu yote. Yehova amejibu sala zangu.” Mungu amemsaidia Francesca pia. Anasema hivi: “Nimeona utimizo wa maneno ya Wafilipi 4:13: ‘Kwa mambo yote ninayo nguvu kwa njia ya yeye anipaye nguvu.’”
Mara nyingi, Yehova Mungu hutoa msaada kwa kutumia kutaniko la Kikristo. Kwa mfano, Gail anasema kwamba ndugu na dada zake wa kiroho katika kutaniko la Mashahidi wa Yehova walimsaidia. Gail anasema: “Upendo walionionyesha ulinisaidia nisishuke moyo.” Hali kadhalika, Keiko alipoulizwa: “Je, unaweza kutaja jambo lolote ambalo limekufurahisha maishani mwako?,” alijibu: “Ndiyo, upendo na huruma za washiriki wote wa kutaniko!”
Katika makutaniko ya Mashahidi wa Yehova, waangalizi hasa wana daraka la kusaidia na kutia moyo. Setsuko anasema hivi: “Siwezi kueleza jinsi mgonjwa anavyonufaishwa wazee wanapomsikiliza na kumfariji.” Hata hivyo, Daniel anayeugua yabisi-kavu anatukumbusha kwamba, “ndugu na dada zetu wa kiroho wanaweza kutusaidia tu iwapo tutawaruhusu.” Kwa hiyo, ni muhimu kwa wagonjwa kushirikiana na Wakristo wenzao kwa kuhudhuria mikutano kwa kadiri wanavyoweza. (Waebrania 10:24, 25) Wanapohudhuria mikutano wanatiwa moyo kiroho ili waweze kuvumilia.
Maumivu Yatakwisha
Wagonjwa wanaougua yabisi-kavu wanashukuru wataalamu wa kitiba kwa ajili ya maendeleo ya kitiba ambayo yamefanywa hadi leo. Lakini, hata matibabu bora si tiba kamili. Kwa hiyo, wagonjwa wanafarijika hasa wanapokubali ahadi za Mungu za ulimwengu mpya.b (Isaya 33:24; Ufunuo 21:3, 4) Katika ulimwengu huo “kilema ataruka-ruka kama kulungu.” (Isaya 35:6) Ugonjwa wa yabisi-kavu na magonjwa mengine yote yatakuwa yametoweka milele! Kwa hiyo, Peter, anayeugua yabisi-kavu ya uti wa mgongo, anasema: ‘Nina tumaini la kuishi maisha mazuri wakati ujao.’ Hali kadhalika, mwanamke Mkristo anayeitwa Giuliana anasema hivi: ‘Kila siku inayopita inapunguza muda wa kuvumilia kabla ya mwisho!’ Ndiyo, wakati ambapo ugonjwa wa yabisi-kavu na mateso mengine yote yatakapokuwa yamekwisha u karibu!
[Maelezo ya Chini]
a Baadhi ya majina yamebadilishwa.
b Ukitaka mmoja wa Mashahidi wa Yehova akutembelee ili akueleze ahadi za Biblia, wasiliana na Mashahidi wa Yehova wa eneo lako au uandikie wachapishaji wa gazeti hili.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kuna vifaa vingi vinavyoweza kuwasaidia wagonjwa kufanya kazi mbalimbali
[Picha katika ukurasa wa 12]
Wagonjwa wanatiwa moyo kwenye mikutano ya Kikristo
-