-
Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi UliopoJe, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
Kani Mbili za Nyuklia
Muundo wa ulimwengu wahusisha mengi zaidi ya vipimo sahihi kabisa vya nguvu za uvutano na kani za sumaku-umeme. Kani nyinginezo mbili zinahusika na uhai wetu.
Kani hizo mbili zinatenda katika kiini cha atomu, nazo huonyesha kwamba ziliwekwa hapo na mtu mwenye kufikiri. Fikiria kani ya nyuklia yenye nguvu, ambayo hushikanisha protoni na nutroni pamoja katika kiini cha atomu. Kwa sababu ya mshikano huo, elementi kadhaa zaweza kufanyizwa—zile nyepesi (kama vile heli na oksijeni) na zile nzito (kama vile dhahabu na risasi). Inaonekana kwamba kama nguvu hiyo yenye kushikanisha ingekuwa dhaifu kwa asilimia 2 tu, ni hidrojeni pekee ambayo ingekuwako. Kwa upande mwingine, kama hii kani ingeongeza nguvu kidogo tu, ni zile elementi nzito pekee ambazo zingekuwako, lakini hidrojeni haingepatikana. Je, uhai wetu ungeathiriwa? Naam, kama ulimwengu ungekosa hidrojeni, jua letu halingepata kitu ambacho linahitaji ili kuwaka na kuendeleza uhai. Na, bila shaka, hatungekuwa na maji wala chakula, kwa kuwa hidrojeni ni sehemu muhimu ya maji na chakula.
Kani ya nne katika mazungumzo haya, inayoitwa kani dhaifu ya nyuklia, hupunguza atomu za vitu vyenye mnururisho. Pia inahusika na utendaji katika jua letu. ‘Je, kani hiyo imepimwa kwa usahihi kabisa?’ huenda ukauliza. Mtaalamu wa hesabu aliye pia mtaalamu wa fizikia Freeman Dyson aeleza: “Ile [kani] dhaifu ni dhaifu mara mamilioni kuliko nguvu za nyuklia. Ni dhaifu kiasi tu cha kuwezesha hidrojeni iliyo katika jua ichomeke polepole kwa kiwango kilekile. Kama hii [kani] dhaifu ingekuwa na nguvu zaidi au kuwa dhaifu zaidi ya ilivyo, aina yoyote ya uhai inayotegemea nyota zilizo kama jua zingepata matatizo.” Ndiyo, kiwango kifaacho kabisa cha kuchomeka hudumisha dunia yetu ikiwa na joto—lakini bila kuteketea—na kuendeleza uhai wetu.
Isitoshe, wanasayansi huamini kwamba ile kani dhaifu huchangia ile milipuko mikubwa sana ya nyota, ambayo kulingana na wanasayansi ni utaratibu wa kutokeza na kusambaza elementi nyingi. “Kama kani hizo za nyuklia zingalikuwa tofauti kidogo na jinsi zilivyo hasa, nyota hazingaliweza kutengeneza elementi ambazo zimekufanyiza wewe na mimi,” aeleza mtaalamu wa fizikia John Polkinghorne.
-
-
Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi UliopoJe, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 20]
“Matukio Yenye Kupatana”
“Ukifanya ile kani dhaifu kuwa yenye nguvu kidogo tu, heli haiwezi kufanyizwa; ukiifanya iwe dhaifu kidogo tu, karibu hidrojeni yote itageuzwa kuwa heli.”
“Uwezekano wa kuwako kwa ulimwengu ambamo mna heli kwa kiasi fulani na pia kuwako kwa milipuko mikubwa ya nyota ni mdogo sana. Maisha yetu yategemea matukio yenye kupatana, na hasa tukio lenye kutokeza zaidi la viwango vya nishati vya nyuklia vilivyotabiriwa na [mtaalamu wa anga Fred] Hoyle. Tofauti na vizazi vyote vilivyopita, sisi twajua jinsi tulivyopata kuwa hai. Lakini, kama ilivyo na vizazi vyote vilivyopita, bado hatujui ni kwa nini tuko hai.”—New Scientist.
-