Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Belize
    2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • “BI. PRATT, TAFADHALI TUOMBEE”

      Kwa siku tatu mfululizo mnamo Oktoba 2000, wakaaji wa mji wa San Pedro kwenye Kisiwa cha Ambergris walikumbwa na Kimbunga Keith. Kimbunga hicho kiliandamana na mvua nyingi, na upepo ulivuma kwa mwendo wa kilomita 205 kwa saa. Eneo la Ladyville lililo umbali wa kilomita 16 kutoka Belize City, lilifurika kwa maji ya mvua yenye kina cha sentimita 80. Ndugu 42 walikimbilia Jumba la Kusanyiko huko Ladyville. Karibu nyumba zote kwenye Kisiwa cha Caulker ziliharibiwa. Wahubiri 57 kwenye kisiwa cha Ambergris na Caulker walipoteza karibu mali zao zote, na baadhi yao wakapoteza kila kitu. Kwa majuma kadhaa, visiwa vyote viwili havikuwa na umeme, maji, wala huduma za simu. Waziri mkuu alitangaza wilaya ya Belize, Orange Walk, na Corozal, na pia kisiwa cha Ambergris na Caulker kuwa maeneo ya msiba. Amri ya kutotembea usiku ilitekelezwa katika eneo lote lililoathiriwa ili kuzuia uporaji.

      Cecilia Pratt, aliyekuwa painia wa pekee huko kisiwani Caulker, alisikia maonyo kuhusu kimbunga hicho, hivyo akapanga kwenye mfuko vitu ambavyo angehitaji iwapo angelazimika kukimbia wakati ambapo kimbunga kingekumba eneo hilo. Siku hiyo, alikuwa amekusanya ripoti za utumishi wa shambani kutoka kwa dada 12, na alikuwa amepanga kuondoka alasiri kwa mashua ili kuzipeleka kwenye ofisi ya tawi barani. Cecilia alifunga ripoti hizo vizuri kwa plastiki na kuziweka kwenye ule mfuko wake. Kama ilivyotarajiwa, usiku Cecilia na baadhi ya dada hao walilazimika kukimbilia shule moja iliyojengwa kwa matofali ya sementi, nao dada wale wengine wakakimbilia kituo fulani cha umma.

      Cecilia anasema, “Upepo uling’oa mabati ya darasa tulimokuwa. Ilibidi sote tuchukue vitu vyetu na kukimbilia darasa lingine. Tulihisi kana kwamba jengo zima lilikuwa likitikiswa na upepo, hata ingawa lilikuwa limejengwa kwa matofali. Tulipotazama nje, ilikuwa kana kwamba tumezungukwa na bahari—eneo lote lilikuwa limejaa maji. Sisi akina dada tulikaa pamoja, na kusali kwa bidii. Watu 40 wa dini tofauti-tofauti ambao walikuwa katika darasa hilo waliogopa sana. Baadhi yao walisema, ‘Hii ni kazi ya Mungu.’ Mhubiri mmoja Mkatoliki alinikaribia na kuniambia, ‘Bi. Pratt, tafadhali tuombee.’ Nami nikamjibu, ‘Siwezi kuwaombea. Mimi ni mwanamke, na sina kofia.’ Naye akasema, ‘Basi, unaweza kutumia kofia yangu.’ Sikuwa na hakika kama ningeweza kumwombea kila mtu, lakini nilitaka watu hao wajue kwamba si Yehova aliyeleta kimbunga hicho. Kwa hiyo, nilisali pamoja na wale dada kwa sauti kubwa ili kila mmoja asikie. Baada tu ya kumaliza sala, na kila mmoja kusema ‘Amina,’ upepo ulitulia! Wakati huo kiini cha kimbunga kilikuwa kikipita juu yetu. Yule mhubiri Mkatoliki alisema: ‘Hiyo ni sala nzuri. Mungu wako ndiye wa kweli.’ Baada ya hapo, hawakutaka sisi Mashahidi watano tuondoke hapo, na kwa siku tatu zilizofuata, walitupa chakula na kahawa.

      “Hata hivyo, nilikuwa na wasiwasi kuwahusu wale wahubiri wengine. Asubuhi iliyofuata, niliondoka kwenda kuwatafuta upepo ulipotulia. Kulikuwa na miti iliyoanguka na uharibifu kila mahali. Baadhi ya nyumba zilikuwa zimebebwa na upepo umbali wa mita 10 hadi 15 kutoka mahali zilipokuwa awali. Nilienda kwanza kwenye kituo cha umma ambapo niliwapata dada wawili na watoto wao. Nyumba ya dada mmoja ilikuwa imeharibiwa kabisa lakini alikuwa hai.”

      Baada ya kimbunga hicho, ilikuwa vigumu kwa ofisi ya tawi kukusanya ripoti za utumishi wa shambani za makutaniko yaliyokuwa yameathiriwa. Lakini ripoti kutoka Kisiwa cha Caulker ndizo zilizokuwa za kwanza kufika. Cecilia alikuwa ameziweka vizuri kwenye ule mfuko wake, na aliwapa akina ndugu waliokuja kuwajulia hali kutoka ofisini.

      Katika majuma yaliyofuata, ndugu kwenye visiwa vilivyoathiriwa walipata msaada, nao wafanyakazi wa kujitolea wakawasaidia kusafisha na kukarabati nyumba zao na pia Jumba la Ufalme kwenye Kisiwa cha Ambergris.

      Merle Richert, mmoja kati ya wafanyakazi hao wa kujitolea kisiwani Caulker, anasema: “Kwanza tuliandaa mahali pa kulala na kupanga jinsi ambavyo msaada ungegawanywa. Siku iliyofuata, tulianza kukarabati nyumba za wahubiri. Jumapili, sote tulienda kuhubiri asubuhi. Kisha tukatayarisha mahali pa kufanyia mikutano kwenye ua wa nyumba ya dada fulani. Tulitengeneza viti vya mbao kwa ajili ya wasikilizaji na pia jukwaa kwa kutumia kisiki cha zamani cha mnazi. Tulibadili saa za mikutano ili tusivunje ile amri ya kutotembea nje kuanzia saa 2:00 usiku. Watu 43 walisikiliza hotuba ya watu wote na Funzo la Mnara wa Mlinzi.”

  • Belize
    2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • 2000 Kimbunga Keith chakumba Belize.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki