-
‘Msafiri Jasiri wa Kueneza Injili’Mnara wa Mlinzi—2004 | Agosti 15
-
-
‘Msafiri Jasiri wa Kueneza Injili’
INASEMEKANA kwamba kufikia umri wa miaka 18, George Borrow alikuwa amejua lugha 12. Miaka miwili baadaye angeweza “kutafsiri vizuri na kwa urahisi” lugha 20.
Mnamo 1833, mtu huyo aliyekuwa na kipawa cha pekee alialikwa ili ahojiwe na Chama cha Biblia cha Uingereza na Nchi za Kigeni, huko London, Uingereza. Kwa kuwa alitaka kutumia nafasi hiyo nzuri na hakuwa na pesa za kugharimia safari hiyo, Borrow aliyekuwa na umri wa miaka 30 alitembea kilometa 180 kutoka nyumbani kwake huko Norwich, kwa muda wa saa 28 tu.
Chama hicho cha Biblia kilimpa kazi ngumu. Kilimpa miezi sita tu kujifunza lugha ya Manchu iliyotumiwa sehemu fulani nchini China. Aliomba kitabu cha sarufi, lakini wakampa nakala ya Injili ya Mathayo katika Kimanchu na kamusi ya Kimanchu na Kifaransa. Hata hivyo, baada ya majuma 19 aliandikia chama hicho barua na kusema, “Nimekijua Kimanchu vizuri” kwa “msaada wa Mungu.” Hilo lilikuwa jambo la pekee hasa kwa sababu wakati huohuo yasemekana Borrow alikuwa akisahihisha Injili ya Luka katika lugha ya Nahuatl, mojawapo ya lugha za wenyeji wa Mexico.
Biblia Katika Kimanchu
Serikali ya China ilianza kutumia Kimanchu katika miaka ya 1600, wakati lugha hiyo ilipoanza kuandikwa kwa kutumia hati iliyokuwa na alfabeti za lugha ya Uighur ya Mongolia. Ingawa mwishowe lugha hiyo iliacha kutumiwa sana, washiriki wa Chama cha Biblia cha Uingereza na Nchi za Kigeni walikuwa na hamu ya kuchapa na kugawanya Biblia katika Kimanchu. Kufikia mwaka wa 1822, walikuwa wamegharimia uchapishaji wa nakala 550 za Injili ya Mathayo, iliyotafsiriwa na Stepan Lipoftsoff wa Tano. Alikuwa mshiriki wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Urusi, aliyekuwa ameishi China kwa miaka 20. Injili hiyo ya Mathayo ilichapishwa huko St. Petersburg, lakini baada ya nakala chache tu kugawanywa, mafuriko yakaharibu zile zilizosalia.
Baada ya muda mfupi, Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yalitafsiriwa. Mnamo 1834, Biblia ilianza kuvutia zaidi baada ya kupatikana kwa hati ya zamani yenye Maandiko mengi ya Kiebrania. Ni nani angeweza kusimamia kusahihishwa kwa Biblia ya Kimanchu iliyokuwapo na kumaliza kuitafsiri? Washiriki wa Chama cha Biblia cha Uingereza na Nchi za Kigeni walimtuma George Borrow akawafanyie kazi hiyo.
Aenda Urusi
Alipofika St. Petersburg, Borrow alianza kujifunza Kimanchu kwa undani zaidi ili aweze kusahihisha na kuhariri maandishi ya Biblia kwa usahihi zaidi. Hata hivyo, hiyo ilikuwa kazi ngumu sana, naye aliifanya kwa saa 13 kwa siku, akisaidia kupanga herufi za kuchapa tafsiri ya Agano Jipya, ambayo baadaye ilitajwa kuwa “chapa nzuri ya nchi za mashariki.” Nakala elfu moja zilichapwa mwaka wa 1835. Lakini mpango wa Borrow wa kupeleka nakala hizo huko China na kuzigawanya ulizuiwa. Serikali ya Urusi ilimkataza Borrow kwenda kwenye mpaka wa China iwapo angebeba “hata Biblia moja ya Kimanchu,” kwa kuhofia kwamba kugawanywa kwa Biblia hizo kungeonekana kuwa kazi ya umishonari ambayo ingehatarisha uhusiano mzuri kati ya Urusi na China.
Nakala chache ziligawanywa miaka kumi hivi baadaye, nazo tafsiri za Injili ya Mathayo na Marko, zilizokuwa na safu za Kimanchu na Kichina, zikatolewa mwaka wa 1859. Hata hivyo, kufikia wakati huo, watu wengi ambao wangeweza kusoma Kimanchu walipendelea kusoma Kichina, na matarajio ya kuwa na Biblia nzima katika Kimanchu yakaanza kudidimia. Lugha ya Manchu ilikuwa inatoweka, na muda si muda Kichina kingechukua mahali pake. Badiliko hilo lilikamilika kufikia mwaka wa 1912, wakati China ilipokuwa jamhuri.
-
-
‘Msafiri Jasiri wa Kueneza Injili’Mnara wa Mlinzi—2004 | Agosti 15
-
-
[Picha katika ukurasa wa 28]
Maneno ya utangulizi ya Injili ya Yohana katika Kimanchu, iliyochapishwa 1835, ambayo yanaanzia juu kwenda chini, nayo husomwa kutoka kushoto kwenda kulia
[Hisani]
From the book The Bible of Every Land, 1860
-