Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Maagizo Yalitoka Wapi?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • Unaingia kupitia mlango ulio kwenye ngozi ya nje ya kiini, au utando, na kutazama huku na huku. Ndani mna kromosomu 46. Zimepangwa kwa pea zinazofanana lakini zinatofautiana kwa urefu, pea iliyo karibu nawe ina urefu wa ghorofa 12 hivi (1). Kila kromosomu imebonyea katikati, na hivyo inafanana kidogo kama soseji iliyokunjwa lakini nene kama shina la mti mkubwa. Unaona mikanda tofauti-tofauti kutoka upande mmoja hadi mwingine wa kromosomu hiyo ya mfano. Unapokaribia, unatambua kwamba kila mkanda uliolala unagawanywa na mistari iliyo wima. Kati ya mistari hiyo kuna mistari mifupi iliyolala (2). Je, ni rundo la vitabu? Hapana; ni kingo za vitanzi vilivyopangwa na kufungwa pamoja katika safu. Unavuta kitanzi kimoja, nacho kinatoka kwa urahisi. Unastaajabu kuona kwamba kitanzi kimefanyizwa kwa koili ndogo (3), ambazo pia zimepangwa kwa utaratibu mzuri. Ndani ya koili hizo kuna kitu muhimu—kitu kinachofanana na kamba ndefu sana. Ni nini hicho?

      UMBO LA MOLEKULI YENYE KUSTAAJABISHA

      Acheni tuifananishe sehemu hii ya kromosomu ya mfano na kamba. Ina unene wa sentimita 2.6 hivi. Imefungwa kwa mkazo sana kuzunguka vibiringo (4), ambavyo husaidia kutengeneza koili ndani ya koili. Koili hizo zimeunganishwa kwa kitu kama nguzo ambayo huzishikilia. Maelezo kwenye ubao yanaonyesha kwamba kamba hiyo imepangwa vizuri. Ikiwa ungeivuta kamba hiyo kutoka kwenye kila kromosomu hizo za mfano na kuinyoosha yote kutoka mwisho mmoja hadi mwingine, urefu wake unaweza kufika karibu nusu ya dunia!a

      Kitabu kimoja cha sayansi kinauita mfumo huo wa kupanga “mafanikio makubwa ya uhandisi.”18 Je, maoni ya kwamba hakuna mhandisi aliyehusika katika mafanikio hayo yanakusadikisha? Ikiwa jumba hilo la maonyesho lingekuwa na bohari kubwa yenye mamilioni ya bidhaa za kuuza ambazo zimepangwa vizuri sana hivi kwamba ungeweza kupata chochote unachohitaji kwa urahisi, ungesema kwamba hakuna mtu aliyepanga bohari hiyo? Bila shaka hapana! Hata hivyo, utaratibu huo ni wa hali ya chini ukilinganishwa na ule tunaozungumzia.

      Kwenye ubao wa maelezo katika jumba la makumbusho, unaalikwa kuchukua kiasi fulani cha kamba hiyo na kuitazama kwa ukaribu (5). Unapoipitisha kwenye vidole vyako, unatambua kwamba hiyo si kamba ya kawaida. Imefanyizwa kwa nyuzi mbili zilizosokotwa pamoja. Nyuzi hizo zimeunganishwa kwa fito ndogo-ndogo zinazoachana kwa nafasi ileile. Kamba hiyo inafanana ngazi iliyosokotwa mpaka ikafanana na ngazi ya mzunguko (6). Kisha unatambua: Mkononi mwako una molekuli ya DNA ya mfano—mojawapo ya maajabu makubwa ya uhai!

      Molekuli moja ya DNA iliyopangwa kwa utaratibu pamoja na vibiringo na nguzo zake, hufanyiza kromosomu moja. Vipago vya ngazi huitwa pea za msingi (7). Hivyo hufanya kazi gani? Vyote hivyo ni vya nini? Unapata maelezo rahisi kwenye ubao wa maelezo.

      MFUMO WA PEKEE WA KUHIFADHI HABARI

      Kulingana na ubao wa maelezo, ili kuelewa DNA, lazima mtu aelewe kwanza vile vipago, yaani, fito zinazounganisha sehemu mbili za ngazi. Wazia ngazi ikiwa imekatwa mara mbili. Kila kipande kina vipago vinavyotokeza. Vipago hivyo ni vya aina nne tu. Wanasayansi huviita A, T, G, na C. Wanasayansi walishangaa kugundua kwamba mpangilio wa herufi hizo hutuma habari kwa njia fulani iliyofupishwa.

      Huenda unajua kwamba mawasiliano ya Morse yalianzishwa katika karne ya 19 ili watu waweze kuwasiliana kwa njia ya telegrafu. Mfumo huo ulitumia “herufi” mbili tu—nukta na kistari. Hata hivyo, “herufi” hizo zingeweza kutumiwa kuwakilisha maneno au sentensi nyingi. Mfumo wa DNA una herufi nne. Mpangilio wa herufi hizo—A, T, G, na C—hufanyiza “maneno” yanayoitwa codons. Codons zimepangwa katika “maghorofa” yanayoitwa chembe za urithi. Kwa wastani, kila chembe ya urithi ina herufi 27,000. Chembe hizo pamoja na mitanuko iliyo kati yake huungana na kufanyiza vitu kama sura za kitabu—kromosomu mojamoja. Kromosomu 23 zinahitajika ili kutengeneza “kitabu” kizima—habari zote kuhusu chembe za urithi za kiumbe kilicho hai.b

  • Maagizo Yalitoka Wapi?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • a Kitabu Molecular Biology of the Cell hutumia kipimo tofauti. Kinasema kwamba kujaribu kupanga nyuzi hizo ndefu ndani ya kiini cha chembe ni kama kujaribu kupanga uzi mwembamba sana wenye urefu wa kilomita 40 ndani ya mpira wa tenisi—lakini kwa utaratibu mzuri hivi kwamba kila sehemu ya uzi huo inaweza kufikiwa kwa urahisi.

      b Kila chembe ina nakala mbili kamili za chembe za urithi, jumla ya kromosomu 46.

  • Maagizo Yalitoka Wapi?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
    • [Mchoro katika ukurasa wa 14, 15]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      “Mafanikio ya uhandisi”

      Jinsi DNA Inavyopangwa

      Kupanga DNA ndani ya kiini ni mafanikio makubwa ya kihandisi—kama vile kupanga uzi wenye urefu wa kilomita 40 ndani ya mpira wa tenisi

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki