-
Kemikali Chungu Nzima Zilizotengenezwa na WatuAmkeni!—1998 | Desemba 22
-
-
Kemikali Chungu Nzima Zilizotengenezwa na Watu
KARNE hii ingeweza kuitwa kwa kufaa karne ya kizazi cha kemia. Kemikali zilizotengenezwa na watu zimebadili maisha yetu. Nyumba zetu, ofisi zetu na viwanda vimejaa vipulizaji, vikolezo bandia, vipodozi, rangi za nguo, wino, rangi, dawa za kuua wadudu, dawa, plastiki, vituliza-joto, vitambaa sanisia—idadi ya kemikali zinazotumiwa ni kubwa sana.
Ili kutimiza mahitaji ya ulimwengu ya bidhaa hizi, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), gharama za kutengeneza kemikali tufeni pote zinakaribia kufikia dola trilioni 1.5. Shirika la WHO linaripoti kwamba kemikali zipatazo 100,000 tayari zinauzwa na kwamba nyingine mpya 1,000 hadi 2,000 zinaongezwa kila mwaka.
Hata hivyo, kemikali hizi chungu nzima hutokeza maswali kuhusu namna zinavyoathiri mazingira na vilevile afya yetu. Kwa wazi tuko katika hali ambayo haijapata kuonekana tena. “Sisi sote ni sehemu ya kizazi kinachofanyiwa uchunguzi, na matokeo kamili hayatajulikana kwa miongo kadhaa ijayo,” akasema daktari mmoja.
Je, Kemikali Zaidi Huzidisha Hatari?
Mara nyingi zaidi watu wanaoathiriwa na vichafuzi vya kemikali, lasema shirika la WHO, ni “maskini, watu wasiojua kusoma na kuandika, wenye ujuzi kidogo au wasiokuwa na ujuzi wowote au maarifa ya msingi juu ya hatari zinazoletwa na kemikali wanazoshughulika nazo kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kila siku.” Jambo hili ni kweli hasa kuhusu dawa za kuua wadudu. Lakini sote tunaathiriwa na kemikali.
Asilimia 20 hivi ya visima vya maji vya California, chasema kitabu A Green History of the World, vina viwango vya uchafu wa kemikali, kutia ndani dawa za kuua wadudu, vinavyozidi mipaka rasmi ya usalama. “Katika Florida,” kitabu hicho chaongezea, “visima 1,000 vimefungwa kwa sababu ya uchafuzi; katika Hungaria miji na vijiji 773 vina maji yasiyofaa kutumiwa, nchini Uingereza asilimia kumi ya maji yaliyo chini ya ardhi yamechafuliwa kupita mipaka ya usalama ya Shirika la Afya Ulimwenguni na katika sehemu fulani za Uingereza na Marekani watoto wachanga hawawezi kupewa maji ya mfereji kwa sababu yana nitrati nyingi.”
Kemikali-sumu nyingine yenye faida lakini iliyo hatari ni zebaki. Hiyo huingia kwenye mazingira kupitia vyanzo kama vile bomba la moshi wa viwanda na mabilioni ya taa zenye kuakisi mwanga. Vivyo hivyo, risasi yaweza kupatikana katika bidhaa nyingi, kutoka kwa fueli hadi rangi. Lakini kama vile zebaki, risasi yaweza kuwa sumu, hasa kwa watoto. Ripoti moja kutoka Cairo, nchini Misri, yasema kwamba mtoto wa kawaida akiishi mahali palipo na uchafuzi wa risasi, “kiwango chake cha kufikiri chaweza kupunguzwa kwa pointi nne.”
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, kila mwaka tani zipatazo 100 za zebaki, tani 3,800 za risasi, tani 3,600 za fosfati, na tani 60,000 za dawa za kusafisha huingia katika Bahari ya Mediterania likiwa tokeo la utendaji wa kibinadamu. Kwa kueleweka, bahari hiyo ina matatizo. Lakini si bahari hiyo pekee. Kwa kweli, Umoja wa Mataifa ulitangaza mwaka wa 1998 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Bahari. Ulimwenguni pote, bahari zote ziko taabani, hasa kwa sababu ya uchafuzi.
Ingawa tekinolojia ya kemikali imetutokezea bidhaa nyingi zenye faida, tunatumia na kutupa nyingi zazo kwa kudhuru sana mazingira. Je, tumejifanya kuwa “mateka wa maendeleo,” kama alivyosema mwandishi mmoja wa habari katika gazeti la habari hivi majuzi?
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Kemikali na Utendanaji wa Kemikali
Neno “kemikali” hurejezea vitu vyote vinavyofanyiza ulimwengu unaotuzunguka, kutia ndani zaidi ya elementi za msingi mia moja, kama vile chuma, risasi, zebaki, kaboni, oksijeni, nitrojeni. Misombo ya kemikali, au miunganisho ya elementi mbalimbali, hutia ndani vitu kama vile maji, asidi, chumvi, na vileo. Nyingi ya misombo hii hutokea kiasili.
“Utendanaji wa kemikali” umefasiliwa kuwa “hatua ambayo kitu kimoja kinabadilishwa kwa njia ya kemia kuwa kitu kingine.” Moto ni utendanaji wa kemikali; hugeuza kitu kiwezacho kuchomeka—karatasi, petroli, hidrojeni, na kadhalika—kuwa kitu au vitu tofauti kabisa. Utendanaji mwingi wa kemikali hutukia bila kukoma, kutuzunguka na ndani yetu.
-
-
Kemikali—Je, Ni Rafiki na Adui?Amkeni!—1998 | Desemba 22
-
-
Kemikali—Je, Ni Rafiki na Adui?
TUNAFANYA maamuzi mengi maishani kwa kulinganisha faida na hasara. Kwa kielelezo, watu wengi hununua gari kwa sababu ya manufaa yake. Lakini wanapaswa kulinganisha mafaa hayo na gharama za gari—bima, kusajiliwa, kupunguka kwa thamani—na kudumisha gari katika hali inayofaa listahili kuwa barabarani. Pia wanapaswa kufikiria hatari ya kujeruhiwa au kifo kwa sababu ya aksidenti. Hali inafanana na hiyo kwa njia fulani kuhusu kemikali-sanisia—faida zake zapaswa kulinganishwa na hasara zake. Chukua mfano wa kemikali inayoitwa MTBE (methyl tertiary buty lether), ikiwa nyongeza ya fueli inayozidisha kuchomeka kwa mafuta na kupunguza moshi wa gari.
Kwa sehemu, kwa sababu ya MTBE, hewa katika majiji mengi ya Marekani ni safi zaidi ya ilivyokuwa kwa miaka kadhaa. Lakini hewa safi “imeleta athari,” laripoti New Scientist. Hii ni kwa sababu MTBE ni kemikali inayoweza kusababisha kansa, na imevuja kutoka kwenye makumi ya maelfu ya matangi yaliyo chini ya ardhi ya kuhifadhi petroli, mara nyingi ikichafua maji ya ardhini. Tokeo ni kwamba, sasa mji mmoja unahitaji kuleta asilimia 82 ya maji yake kutoka nje, kwa gharama ya dola milioni 3.5 kwa mwaka! Gazeti New Scientist lasema kwamba msiba huu “ungeweza kuwa mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya uchafuzi wa maji ya ardhini nchini Marekani kwa miaka mingi.”
Kemikali fulani zimepigwa marufuku na kuondolewa kwenye masoko kabisa kwa sababu ya madhara ambazo zinasababisha kwenye mazingira na kwa afya. Lakini huenda ukajiuliza, ‘kwa nini hili linatokea? Je, kemikali zote hazichunguzwi kikamili kujua ikiwa zina sumu kabla hazijaanza kuuzwa?’
Matatizo ya Kuchunguza Sumu
Kwa kweli, kuchunguza kemikali ikiwa zina sumu ni mchanganyiko wa sayansi na kukisia. “Wakadiriaji wa sumu hawajui kubainisha waziwazi kati ya kemikali ‘salama’ na ‘zisizo salama’ kushughulika nazo,” asema Joseph. V. Rodricks katika kitabu chake Calculated Risks. Hiyo ni kweli hata kuhusu dawa, ambazo nyingi hutengenezwa kisanisia. “Hata uchunguzi uliofanywa kwa makini sana,” yasema The World Book Encyclopedia, “sikuzote hauwezi kufunua uwezekano wa kwamba dawa hiyo ingeweza kutokeza athari zisizotazamiwa.”
Maabara yana dosari fulani za kiasili. Kwa kielelezo, maabara hayawezi kuigiza kikamili utendaji wa kemikali ikiwa nje ambako kuna vitu vya namna mbalimbali na vilivyo tata. Nje ya maabara kuna mamia, hata maelfu ya kemikali-sanisia zilizo tofauti, nyingi ambazo zaweza kuingiliana na nyingine na vilevile na vitu vilivyo hai. Baadhi ya kemikali hizi hazina madhara zikiwa peke yake, lakini zinapoungana, zikiwa ndani au nje ya miili yetu, zinaweza kutokeza sumu mpya. Kemikali nyingine huwa sumu, hata husababisha kansa, baada tu ya kuyeyushwa na mwili.
Wakadiriaji wa hatari wanaweza kuamuaje usalama wa kemikali ingawa kuna magumu ya namna hiyo? Kiwango ambacho kinatumiwa kimekuwa kuwapa wanyama wa maabara kemikali iliyopimwa na kisha kutumia matokeo hayo kwa binadamu. Je, njia hii hutegemeka sikuzote?
Je, Uchunguzi wa Wanyama Wategemeka?
Mbali na kuzusha maswali ya kiadili kuhusu kutenda wanyama kikatili, kuchunguza sumu kwa kutumia wanyama huzusha maswali mengine. Mathalani, mara nyingi wanyama mbalimbali huathiriwa na kemikali kwa njia tofauti. Kiasi kidogo cha dioksini yenye sumu kali kitaua nungubandia, lakini kiasi hicho kitahitaji kuongezwa mara 5,000 ili kuua buku! Hata wanyama wenye uhusiano wa karibu kama panya na buku huathiriwa na kemikali nyingi kwa njia tofauti.
Kwa hiyo ikiwa jinsi aina moja ya mnyama anavyoathiriwa haiwezi kuonyesha kwa uhakika jinsi aina nyingine itakavyoathirika, watafiti wanaweza kuwa na uhakika gani kwamba kemikali fulani itakuwa salama kwa binadamu? Ukweli ni kwamba, hawawezi kuwa na uhakika.
Hapana shaka wanakemia wana kazi ngumu. Wanahitaji kuwafurahisha wateja wao, kuwafurahisha wale wanaohangaikia hali njema ya wanyama, na kubaki wakiwa na dhamiri safi kwamba bidhaa wanazotokeza ni salama. Kwa sababu hizi, maabara fulani sasa yanachunguza kemikali kwa kutumia chembe zilizotolewa kwa binadamu. Hata hivyo, itakuwa wakati fulani ujao kabla hatujajua kama uhakikisho wa usalama waweza kupatikana.
Uchunguzi wa Maabara Ukosapo Kufaulu
Dawa ya kuua wadudu iitwayo DDT, ambayo bado inapatikana kwenye mazingira, ni mfano mmoja wa kemikali iliyotangazwa kimakosa kuwa salama ilipotolewa mara ya kwanza. Baadaye wanasayansi walitambua kwamba DDT hubaki kwa muda mrefu ndani ya viumbehai, jambo linalofanana na sumu nyingine zilizo hatari. Matokeo hatari ya hili ni gani? Naam, mfuatano wa mlishano, ambao umefanyizwa kwa mamilioni ya viumbe duni, kisha samaki, na hatimaye ndege, dubu, fisimaji, na kuendelea, huwa faneli hai, ikitokeza sumu nyingi kwa walaji wa mwisho. Katika kisa kimoja, kibisi, aina ya ndege wa majini, walishindwa kuangua hata kifaranga mmoja kwa zaidi ya miaka kumi!
Faneli hizi zilizo hai hutenda kazi kwa njia nzuri sana hivi kwamba kemikali fulani, ingawa hazigunduliwi kwa urahisi ndani ya maji, huwa zenye nguvu kwa kiwango kikubwa kwa walaji wa mwisho. Kielelezo kizuri ni nyangumi waitwao Beluga wa Mto St. Lawrence, Amerika Kaskazini. Wana sumu kali sana hivi kwamba wanachukuliwa kuwa takataka yenye sumu hatari wanapokufa!
Kemikali fulani zilizo katika wanyama wengi zimepatikana zikijifanya kuwa homoni. Na ni hivi majuzi tu kwamba wanasayansi wameanza kugundua athari zisizo wazi ambazo kemikali hizi zaweza kusababisha.
Kemikali Zinazoigiza Homoni
Homoni ni wajumbe wa kemikali wenye maana mwilini. Hizo husafiri kupitia mishipa ya damu hadi kwenye sehemu nyingine za mwili, ambapo ama zinachochea ama kukandamiza utendaji fulani, kama vile ukuzi wa mwili au vipindi vya kuzaa. Kwa kupendeza, habari mpya za hivi majuzi za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zilisema kwamba “uthibitisho mwingi wa kisayansi unaozidi kuongezeka” waonyesha kwamba kemikali-sanisia fulani, zinapotumiwa, huvuruga homoni ama kwa kuziiga kwa njia inayoleta madhara ama kwa kuzizuia.
Kemikali hizo zatia ndani PCB,a dioksini, furan, na dawa fulani za kuua wadudu, kutia ndani mabaki ya DDT. Kemikali hizi zinazoitwa vivuruga homoni, zina uwezo wa kuvuruga utaratibu wa kawaida wa mwili wa mfumo wa kutokeza homoni.
Homoni moja ambayo kemikali hizi huigiza ni homoni ya kike iitwayo estrojeni. Uchunguzi uliochapishwa katika jarida la kitiba Pediatrics wadokeza kwamba ongezeko la kubalehe mapema miongoni mwa wasichana wengi lingeweza kuhusianishwa na mafuta ya nywele yaliyo na estrojeni na vilevile kemikali zilizo kwenye mazingira zinazoigiza estrojeni.
Mwanamume akiathiriwa na kemikali fulani katika wakati fulani wenye maana sana wa ukuzi wake, aweza kupatwa na madhara makali. “Majaribio yameonyesha kwamba,” yasema ripoti katika gazeti Discover, “PCB zinapotumiwa wakati fulani hususa wakati wa ukuzi zaweza kubadili kasa na mamba wa kiume kuwa wa kike au ‘wawe kati ya jinsia zote.’”
Kwa kuongezea, sumu za kemikali hudhoofisha mifumo ya kinga, zikiwafanya wanyama wapatwe na maambukizo ya virusi kwa urahisi. Kwa kweli, maambukizo ya virusi yanazidi kuenea haraka zaidi kuliko wakati wowote, hasa miongoni mwa wanyama walio katika kiwango cha juu cha mlishano wa chakula, kama vile dolfini na ndege wa baharini.
Miongoni mwa wanadamu, watoto ndio huathiriwa zaidi na kemikali zinazoigiza homoni. Watoto waliozaliwa na wanawake waliomeza mafuta ya makapi ya mchele yaliyokuwa na PCB katika Japani miaka kadhaa iliyopita, “walipatwa na ukuzi wa polepole wa kimwili na wa kiakili, matatizo ya tabia kutia ndani kutotenda sana na kutenda kupita kiasi, uume ulio mdogo kupita kiasi, na kiwango cha akili kilichopungua pointi tano chini ya wastani,” laripoti gazeti Discover. Uchunguzi uliofanyiwa watoto walioishi katika maeneo yaliyo na PCB ya kiwango cha juu katika Uholanzi na Amerika Kaskazini ulifunua madhara makali yaliyo na matokeo sawa na haya kwa ukuzi wao wa kimwili na wa kiakili.
Pia linalohusianishwa na kemikali hizi, laripoti shirika la WHO, yawezekana ni ongezeko katika kansa “zinazohisiwa na homoni” miongoni mwa wanaume na wanawake, kama vile kansa ya matiti, kansa ya pumbu, na kansa ya kibofu. Kwa kuongezea, katika nchi nyingi, bila shaka upungufu unaoendelea katika wastani wa idadi ya shahawa katika wanaume, vilevile ubora wa shahawa, waweza kuhusianishwa na ongezeko la matumizi ya kemikali. Katika mabara fulani, wastani wa idadi ya shahawa umepungua kwa asilimia 50 katika miaka 50!
Katika makala iliyotangulia, daktari mmoja alinukuliwa akisema kwamba sisi ni “kizazi cha kufanyiwa uchunguzi.” Yaonekana yuko sahihi. Kweli, kemikali nyingi ambazo tumevumbua zimetufaidi, lakini nyingine hazijafanya hivyo. Kwa hiyo, tutakuwa wenye hekima tukiepuka kushughulika isivyo lazima na kemikali zinazoweza kutudhuru. Kwa kushangaza, nyingi za kemikali hizi zaweza kupatikana nyumbani mwetu. Makala yetu itakayofuata itazungumzia jambo tunaloweza kufanya ili kujilinda kutokana na kemikali zinazoweza kuwa hatari.
[Maelezo ya Chini]
a Kemikali zinazoitwa PCB (polychlorinated biphenyls), ambazo zimetumika ulimwenguni pote tangu miaka ya 1930, ni elementi za misombo zaidi ya 200 yenye mafuta-mafuta inayotumiwa katika mafuta ya kulainisha, plastiki, mipira ya nyaya za umeme, dawa za kuua wadudu, sabuni za kuoshea, na bidhaa nyinginezo. Ingawa sasa utengenezaji wa PCB umepigwa marufuku katika nchi nyingi, kati ya tani milioni moja na milioni mbili zimetengenezwa. Madhara ya sumu yametokana na PCB zilizotupwa ambazo sasa ziko kwenye mazingira.
-
-
Nyumba Yako Ni Yenye Sumu Kadiri Gani?Amkeni!—1998 | Desemba 22
-
-
Nyumba Yako Ni Yenye Sumu Kadiri Gani?
UCHUNGUZI wa hivi majuzi uliofanyiwa watu zaidi ya 3,000 nchini Marekani na Kanada, kulingana na gazeti Scientific American, ulionyesha kwamba “raia wengi walielekea sana kushughulika na vichafuzi vinavyoweza kuwa sumu . . . ndani ya sehemu ambazo mara nyingi walizifikiria kuwa zisizo na uchafuzi, kama vile nyumbani, ofisini na ndani ya magari.” Vichafuzi vikuu vya hewa katika nyumba vilikuwa mvukizo uliotokana na bidhaa za kawaida kama vile kemikali za kusafisha, vizuia-nondo, vifaa vya kujenga, fueli, viondoa harufu, na kemikali za kuua viini vya maradhi, vilevile kemikali zinazotokana na mavazi yaliyotoka kwa dobi na vifaa vipya vya kutengeneza samani vya sanisia.
“Mafua ya angani,” ugonjwa uliowapata wanaanga mpaka chanzo chake kilipotambulishwa, ulitokana na mivukizo kama hiyo, au “mvuke wa gesi.” Unagundua mvuke wa gesi unapoketi ndani ya gari jipya au unapotembea kandokando ya rafu zenye kemikali za kusafishia ndani ya duka kubwa, hata ingawa ziko ndani ya mikebe iliyofunikwa. Kwa hiyo nyumba inapofungwa kabisa ili kuzuia baridi ya majira ya kipupwe, mvuke wa gesi za namna mbalimbali huongezea uchafuzi ndani ya nyumba ambao ni mwingi kupita uchafuzi ulio nje.
Watoto, hasa wanaotambaa, ndio wanaoweza kudhuriwa zaidi na uchafuzi wa ndani ya nyumba, lasema gazeti la Kanada Medical Post. Wao wako karibu zaidi na sakafu kuliko watu wazima; wanapumua haraka zaidi kuliko watu wazima; wanatumia asilimia 90 ya muda wao wakiwa ndani ya nyumba; na kwa sababu viungo vyao havijakomaa, miili yao hudhuriwa kwa urahisi zaidi na sumu. Wanameza asilimia 40 hivi ya risasi, ilhali watu wazima humeza karibu asilimia 10.
Kudumisha Mtazamo Uliosawazika
Kwa sababu kizazi cha sasa cha binadamu kimeshughulika na kemikali kwa kiwango kisicho na kifani, bado kuna mengi ya kujifunza kuhusu athari, kwa hiyo wanasayansi wanatahadhari. Kushughulika na kemikali hakumaanishi ni lazima upate kansa au ni lazima ufe. Kwa kweli, watu wengi wanakabiliana na tatizo hili vizuri, jambo linaloongeza sifa kwa Muumba wa mwili wa binadamu wenye kustaajabisha. (Zaburi 139:14) Hata hivyo, lazima tutahadhari kwa kiasi fulani, hasa ikiwa tunashughulika kwa ukawaida na kemikali zinazoweza kuwa na sumu.
Kitabu Chemical Alert! chasema kwamba “kemikali fulani ni sumu katika njia ya kwamba zinahitilafiana na usawaziko wa utaratibu wa [mwili] na hivyo zikitokeza dalili zisizo wazi ambazo zaweza kumfanya mtu asihisi vizuri.” Kupunguza kushughulika na kemikali zinazoweza kuwa sumu hakuhitaji mabadiliko makubwa katika mtindo-maisha wetu lakini mabadiliko ya kiasi katika utaratibu wetu wa kila siku. Tafadhali ona baadhi ya madokezo yaliyo katika sanduku kwenye ukurasa wa 8. Baadhi yake yaweza kukusaidia.
Kwa kuongezea kuwa wenye tahadhari tunaposhughulika na kemikali, tunajisaidia tunapoepuka kuwa na wasiwasi isivyofaa, hasa kuhusu mambo ambayo hatuwezi kudhibiti. “Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili,” yasema Biblia kwenye Mithali 14:30.
Hata hivyo, watu wengi husumbuka na kuwa wagonjwa, nyakati nyingine hata dawa zinakosa kuwasaidia kwa sababu ya sumu za kemikali.a Kama mamilioni ya watu wanaotaabishwa na visababu vingi katika siku zetu, wale waliopatwa na magonjwa yanayohusiana na kemikali wana sababu nzuri ya kutazamia wakati ujao kwa hamu, kwa kuwa karibuni dunia haitakuwa na sumu zinazodhuru wakazi wake. Hata mawazo yenye sumu, pamoja na wale wanaoyaweka, yatapitilia mbali, kama makala ya mwisho katika mfululizo huu itakavyoonyesha.
[Maelezo ya Chini]
a Katika miaka ya hivi majuzi idadi kubwa ya watu wamekuwa wakisumbuliwa na hali inayoitwa unyetivu wa kupita kiasi wa kemikali nyingi. Hali hii itazungumziwa katika toleo lijalo la Amkeni!
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Kwa Makao Yenye Afya Zaidi na Salama Zaidi
Kupunguza kushughulika na sumu zinazoweza kuwa hatari mara nyingi hutaka tu mabadiliko ya kiasi katika mtindo-maisha wako. Hapa pana madokezo fulani yanayoweza kukusaidia. (Kwa habari zaidi na hususa zaidi, twapendekeza uchunguze katika maktaba ya kwenu.)
1. Jaribu kuhifadhi kemikali nyingi zinazotoa mvuke mahali ambapo hazitachafua hewa nyumbani mwako. Kemikali hizi zinatia ndani formaldehyde na vitu vinavyoyeyuka na kuwa mvuke, kama vile rangi, vanishi, vitu vinavyonata, dawa za kuua wadudu, na kemikali za kusafisha. Vitu vilivyo kwenye petroli huvukiza sumu. Kikundi hiki chatia ndani benzini, ambayo ikiwa kwa wingi kwa muda mrefu husababisha kansa, kasoro za kuzaliwa, na madhara mengine ya uzazi.
2. Kila chumba kiwe na hewa safi, kutia ndani bafu. Wakati wa kuoga nyongeza fulani kama vile klorini zaweza kuwa ndani ya maji. Hili laweza kuongoza kwenye ongezeko la polepole la klorini na hata klorofomu.
3. Pangusa nyayo zako kabla ya kuingia ndani. Kitendo hiki sahili, lasema Scientific American, chaweza kupunguza kiwango cha risasi kwenye mkeka mara sita. Pia kinapunguza dawa za kuua wadudu, ambazo nyingine zake huisha nguvu kwa urahisi mahali penye mwanga wa jua lakini zingeweza kudumu kwa miaka mingi ndani ya mikeka. Chaguo lingine, ambalo ni kawaida katika sehemu fulani za ulimwengu, ni kutoa viatu. Kivuta-vumbi kizuri, hasa kile chenye brashi inayozunguka, chaweza pia kupunguza uchafuzi kwenye mikeka.
4. Ikiwa unatunza chumba kwa kutumia dawa ya kuua wadudu, weka vitu vya kuchezea vya watoto mbali na chumba hicho kwa angalau majuma mawili, hata ingawa kibandiko cha bidhaa hiyo chasema kwamba chumba hicho ni salama muda wa saa kadhaa baada ya kutumia dawa hiyo. Hivi majuzi wanasayansi wamepata kwamba plastiki na mipira ya aina fulani inayopatikana kwenye vitu vya watoto kuchezea hufyonza kihalisi mabaki ya dawa za kuua wadudu kama sponji. Watoto watafyonza sumu kupitia ngozi na mdomo.
5. Punguza matumizi yako ya dawa za kuua wadudu. Katika kitabu chake Since Silent Spring, Frank Graham, Jr., aandika kwamba dawa za kuua wadudu “zina mahali pake panapozifaa nyumbani na shambani, lakini kampeni za kuziuza zimesadikisha mkazi wa viungani kwamba apaswa kuwa na kemikali za kutosha ili kufukuza tauni ya nzige wa Afrika.”
6. Ondoa vipande vidogo-vidogo vya rangi yenye risasi kutoka kwenye kuta zote, na uzipake rangi tena kwa kutumia rangi isiyo na risasi. Usiwaruhusu watoto wacheze na takataka zilizo na rangi yenye risasi. Ikiwa risasi inashukiwa katika mfereji, mfereji wa maji baridi wapaswa kufunguliwa kwa muda mfupi mpaka kuwe na tofauti ya halijoto katika maji, na maji kutoka kwenye mfereji wa maji moto hayapaswi kunywewa.—Environmental Poisons in Our Food.
-
-
Ni Nani Atakayesafisha Dunia Yetu?Amkeni!—1998 | Desemba 22
-
-
Ni Nani Atakayesafisha Dunia Yetu?
“NINATABIRI kwamba kufikia mwaka wa 2025 neno ‘uchafuzi’ litatoweka kwa kiasi kikubwa kwenye msamiati wa taifa letu kwa kadiri ambavyo viwanda vyetu vinahusika.” Huo ulikuwa utabiri wa hivi majuzi uliofanywa na msimamizi wa shirika la kemikali. Je, unaamini kwamba jambo hilo litatukia? Ikiwa ndivyo, jambo hilo litatimizwa namna gani?
Mara nyingi kutamani faida ndiko huchochea mauzo ya bidhaa zisizokuwa salama. Kwa kielelezo, sheria zinazohusu siri za biashara huruhusu makampuni ya kutengeneza dawa za kuua wadudu zihifadhi fomyula fulani zenye kuleta faida zikiwa siri kwa kuweka kibandiko “tepetevu” kwenye viambato vyao, neno ambalo hufasiriwa kwa urahisi kuwa “-siodhuru.” Lakini, “angalau viambato 394 tepetevu vimetumiwa kuwa dawa kali za kuua wadudu,” laripoti gazeti Chemical Week. Kati ya viambato hivi, 209 ni vichafuzi hatari, 21 vimeainishwa kirasmi kuwa vyaweza kusababisha kansa, na 127 husababisha hatari za kiafya zinazohusiana na kazi!
Kweli, mara nyingi sheria za kuhakikisha usalama za serikali zimekuwa zenye faida. Lakini mahangaiko makubwa ya serikali kadhaa, asema mwandishi mmoja, ni “ukuzi wa kiuchumi na faida inayoletwa na viwanda.” Hivyo, wanakabiliwa daima na mambo mawili wasiyoweza kuyapata wakati mmoja—hatari dhidi ya faida. Kwa asili, matokeo ni ‘uchafuzi uliodhibitiwa.’
Kwa hiyo tutapata wapi majibu? Mmoja wa Mashahidi wa Yehova alimzushia swali hili mwenye nyumba mwenye urafiki. Akionyesha itibari kwa viongozi wa kibinadamu na wanasayansi, mtu huyo alijibu: “Siku moja watarekebisha mambo.”
“Lakini ni nani hao?” akauliza Shahidi huyo. “Je, wao si watu kama wewe na mimi? Huenda wakawa na elimu zaidi, lakini wana mapungukiwa yao, udhaifu wao. Wanakosea.” Ongezea matatizo makubwa sana yanayowakabili vilevile pupa na ufisadi katika jamii ya kibinadamu.
Je, wewe pia waamini kwamba wao watarekebisha mambo? Historia ndefu ya binadamu ya kutoweza kufanya hivyo haitoi sababu ya kuwa na imani katika wanadamu. Gazeti Outdoor Life lilisema: “Wanasayansi na vyombo vyao ni stadi zaidi katika kuchunguza matatizo ya uchafuzi kuliko kuyatatua.” Kuna mataraja gani kwamba wanadamu wanaweza kutatua tatizo hili kubwa?
Je, Wanadamu Wanaweza Kulitatua Peke Yao?
Kudhibiti uchafuzi wa kemikali si tatizo tu la wenye mamlaka wa mahali penu. Hii ni kwa sababu kemikali zinazotumiwa katika nchi moja huathiri watu katika nchi jirani, hata watu ulimwenguni pote! Na wanadamu wameshindwa kushirikiana kutatua matatizo ya namna hiyo ya ulimwengu. Biblia inaonyesha ni kwa nini inaposema: “Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa has[a]ra yake.” (Mhubiri 8:9) Kwa nini wanadamu wanakosa kufaulu kujitawala? Tena, Biblia yaeleza: “Njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Jambo hilo linamaanisha nini?
Linamaanisha kwamba wanadamu kamwe hawakuumbwa wajitawale wenyewe bila mwelekezo wa Mungu. Ni kweli, wanadamu wamefanya mambo yasiyo na kifani—wamejenga makao ya kustaajabisha, wakatengeneza vyombo stadi, hata wakasafiri kwenye mwezi—lakini wanashindwa kujitawala wenyewe bila mwongozo wa kimungu. Hivyo ndivyo Biblia inavyofundisha, na historia inathibitisha usahihi wa Biblia.
Dunia Iliyosafishwa —Kupitia Njia Gani?
Sikuzote Muumba wetu Yehova Mungu, anahangaika kuhusu wanadamu na dunia hii, aliyoitayarisha kwa ajili ya mwanadamu. Baada ya kuwaumba wanadamu, aliagiza kwamba watunze dunia na uhai ulio juu yake. (Mwanzo 1:27, 28; 2:15) Baadaye, wenzi wa kwanza wawili walipoasi maagizo yake, aliagiza taifa la kale la Israeli kuhusu kutunza nchi, kutia ndani takwa la kuiacha ipumzike kwa mwaka mzima baada ya kila miaka saba. Hii iliruhusu nchi istarehe. (Kutoka 23:11; Mambo ya Walawi 25:4-6) Lakini watu wakawa na pupa na wakakosa kumtii Mungu. Wao pamoja na nchi wakateseka.
Bila shaka, uchafuzi wa kemikali kama tulio nao sasa, haungeweza kupatikana huko nyuma. Lakini, nchi ikaharibiwa kwa sababu Waisraeli walikosa kuiacha ipumzike kulingana na kusudi la Mungu, na watu wasiokuwa na hatia wakateseka. Hivyo Mungu aliruhusu Wababiloni washinde Israeli na kuchukua taifa hilo kwenye utekwa huko Babiloni kwa miaka 70. Adhabu hii iliruhusu nchi hiyo ipumzike ili kwamba ipate nguvu tena.—Mambo ya Walawi 26:27, 28, 34, 35, 43; 2 Mambo ya Nyakati 36:20, 21.
Historia hii hutufundisha kwamba Mungu huwatoza hesabu wanadamu kwa yale wanayofanyia dunia. (Waroma 15:4) Kwa kweli, Mungu anaahidi kwamba ‘atawaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.’ (Ufunuo 11:18) La maana, Biblia hufafanua aina ya watu wanaochangia ‘uangamizi’ huu. Tabia zao kuu, kama zinavyoorodheshwa katika Biblia kwenye 2 Timotheo 3:1-5, zinatia ndani kujishughulisha sana na pesa na ubinafsi kufikia kiwango cha kutojali sana Mungu, na zaidi sana, uumbaji wake, kutia ndani wanadamu wenzao.
Kwa hiyo, mafungu haya mawili ya Biblia—2 Timotheo 3:1-5 na Ufunuo 11:18—yaelekeza kwenye mikataa miwili thabiti. Mkataa wa kwanza, akili chafu huongoza kwenye dunia iliyochafuliwa. Mkataa wa pili, Mungu ataingilia kuokoa sayari hii na wanadamu wanaomcha Mungu wakati uchafuzi huo wa aina mbili utakapofikia kilele chake. Mungu ataingiliaje mambo?
Kupitia nabii wake Danieli, Mungu alitabiri hivi: “Katika siku za wafalme hao [kwa wazi akirejezea serikali za kisasa] Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao . . . utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” (Danieli 2:44) Ufalme huo ni serikali halisi ya ulimwengu. Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake waiombee serikali hiyo aliposema: “Basi, nyinyi lazima msali kwa njia hii: ‘Baba yetu uliye katika mbingu, . . . acha ufalme wako uje. Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia.”—Mathayo 6:9, 10.
Chini ya usimamizi wenye upendo wa Ufalme wa Mungu, wakazi wa dunia watafurahia pendeleo kubwa la kuifanya dunia yote kuwa paradiso. Hewa itakuwa safi na yenye kupendeza, vijito vitakuwa na maji safi, na ardhi itatokeza mimea isiyochafuliwa. (Zaburi 72:16; Isaya 35:1-10; Luka 23:43) Baada ya hapo, Biblia inaahidi: “Mambo ya kwanza [magonjwa ya kisasa, kuteseka, uchafuzi, na ole nyingine nyingi] hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.”—Isaya 65:17.
-