Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?
    Amkeni!—1997 | Juni 22
    • Fungu la Kolesteroli

      Kolesteroli ni kitu cheupe kilicho kama nta ambacho ni muhimu kwa uhai. Hicho hupatikana katika chembe za wanadamu na wanyama wote. Ini letu hutokeza kolesteroli, nayo pia hupatikana kwa viwango tofauti-tofauti katika vyakula tulavyo. Damu hupeleka kolesteroli hadi kwenye chembe ikiwa katika molekuli ziitwazo lipoprotini, ambazo huwa na kolesteroli, mafuta, na protini. Aina mbili za lipoprotini ambazo hubeba kiasi kikubwa cha kolesteroli iliyo katika damu ni lipoprotini zisizo na protini nyingi (LDL) na lipoprotini zilizo na protini nyingi (HDL).

      Aina za LDL zina kolesteroli nyingi. Zinapozunguka katika mkondo wa damu, hizo huingia katika chembe kupitia vipokezi vya LDL kwenye kuta za chembe na humeng’enyushwa ili zitumiwe na chembe. Chembe nyingi mwilini zina vipokezi kama hivyo, nazo huchukua baadhi ya LDL. Lakini ini limebuniwa kwa njia ya kwamba asilimia 70 ya kuondoshwa kwa LDL kutoka kwenye mkondo wa damu na vipokezi vya LDL hutukia hapo.

      Kwa upande ule mwingine, HDL ni molekuli zinazohitaji sana kolesteroli. Zinapopita katika mkondo wa damu, hizo hufyonza kolesteroli ya ziada na kuisafirisha hadi kwenye ini. Ini humeng’enyusha kolesteroli hiyo na kuiondosha kutoka mwilini. Hivyo mwili umebuniwa kwa njia ya ajabu utumie kolesteroli unayohitaji na kuondosha iliyobaki.

      Tatizo hutokea wakati kuna LDL nyingi mno katika damu. Hizo huongeza uwezekano wa ujengekaji wa utando kwenye kuta za ateri. Ujengekaji wa utando utokeapo, ateri huwa nyembamba na kiwango cha damu ibebayo oksijeni iwezayo kupita katika ateri hizo hupungua. Hali hii huitwa atherosclerosis. Utaratibu huo huendelea polepole na bila kuonyesha dalili zozote, ukichukuwa miongo ili kudhihirisha dalili ziwezazo kutambuliwa. Dalili moja ni maumivu ya kifuani, kama yale yaliyompata Joe.

      Ateri ya moyo izibikapo kabisa, mara nyingi kwa mgando wa damu, sehemu ya moyo inayopokea damu kutoka kwa ateri hiyo hufa. Tokeo ni kufa kwa ghafula kwa tishu ya tabaka ya katikati ya ukuta wa moyo—hali ijulikanayo vema kuwa mshiko wa moyo. Hata kuzibika nusu kwa ateri ya moyo kwaweza kuongoza kwenye kifo cha tishu ya moyo, hali ambayo huenda isitokeze dalili kama vile kutohisi vizuri kimwili. Kuzibika kwa ateri katika sehemu nyinginezo za mwili kwaweza kusababisha mishtuko ya akili, uozo wa miguu kutokana na ukosefu wa damu, na hata kukosa kwa figo kufanya kazi.

      Si ajabu kwamba LDL huitwa kolesteroli mbaya, na HDL kolesteroli nzuri. Ikiwa upimaji unaonyesha kwamba kuna kiwango cha juu cha LDL katika damu, au kiwango cha chini cha HDL, hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo ni kuu.a Mara nyingi upimaji sahili wa damu utaonyesha hatari iliyopo muda mrefu kabla ya mtu kupatwa na dalili za wazi kama vile, maumivu kifuani. Basi, ni jambo la maana kudhibiti kiwango chako cha kolesteroli iliyo katika damu. Ebu sasa tuone jinsi ulaji wako uwezavyo kuathiri kiwango hicho.

  • Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?
    Amkeni!—1997 | Juni 22
    • a Kolesteroli hupimwa katika miligramu kwa desilita. Kiwango kifaacho cha kolesteroli ya jumla—jumla ya LDL, HDL, na kolesteroli katika lipoprotini nyinginezo na katika damu—ni chini ya miligramu 200 kwa desilita. Kiwango cha HDL cha miligramu 45 kwa desilita au juu huonwa kuwa kizuri.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki