Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Rumania
    2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Nafasi ilitokea wakati Teodor na Mashahidi wengine 50 Warumania hivi walipokuwa wakipelekwa kwenye kambi ya Wanazi huko Bor, Serbia. Walipokuwa safarini kuelekea Bor, walikaa kwa muda mfupi huko Jászberény, Hungaria, ambako ndugu Wahungaria zaidi ya mia moja walijiunga nao. Walipokuwa huko walinzi waliwatuma ndugu kadhaa waende mtoni wakajaze pipa la maji. Walinzi hawakwenda nao kwa sababu waliwaamini. Teodor alijiunga nao na akabatizwa mtoni. Kutoka Jászberény wafungwa walipelekwa hadi Bor kwa gari-moshi na mashua.

      Katika kambi ya Bor kulikuwa na Wayahudi 6,000; Wasabato 14; na Mashahidi 152. Ndugu Miron anasema hivi: “Hali zilikuwa mbaya, lakini Yehova alitusaidia. Mlinzi fulani aliyetupenda alitumwa Hungaria mara kwa mara, naye alituletea vitabu. Baadhi ya Mashahidi ambao aliwajua na kuwaamini walitunza familia yake alipokuwa safarini, kwa hiyo akawa kama ndugu yao. Mtu huyo aliyekuwa luteni alituonya kulipokuwa na hatari. Kambini kulikuwa na wazee 15 wa kutaniko, kama wanavyoitwa leo, nao walipanga mikutano mitatu kila juma. Watu 80 waliihudhuria mikutano zamu zao za kazi zilipowaruhusu. Pia tuliadhimisha Ukumbusho.”

  • Rumania
    2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Mnamo Septemba 1, 1944, vikosi vya Ujerumani vilipoanza kurudi nyuma, mimi, nilikuwa kati ya ndugu 152 na wafungwa wengine walioondolewa kwenye kambi ya mateso ya Bor, huko Serbia, ili wapelekwe Ujerumani. Hatukula kwa siku kadhaa. Tulipopata chakula kidogo, kama vile viazi-sukari vilivyoachwa kando ya barabara karibu na mashamba, tulikila pamoja. Iwapo mmoja alikuwa dhaifu sana asiweze kutembea, wale waliokuwa na nguvu walimbeba kwenye mkokoteni.

      Hatimaye, tulifika kwenye kituo cha gari-moshi, tukapumzika kwa saa nne hivi, kisha ili tupate nafasi ya kusafiria tuliondoa mizigo kutoka kwenye mabehewa mawili ya gari-moshi ambayo hayakuwa na paa. Kulikuwa na nafasi ya kusimama tu, nasi hatukuwa na nguo nzito za kujikinga na baridi, bali kila mmoja alikuwa na blanketi alilolitumia kujifunika mvua ilipoanza kunyesha. Tulisafiri katika hali hiyo usiku kucha. Tulipofika kwenye kijiji fulani saa 4:00 asubuhi siku iliyofuata, ndege mbili zilipiga kichwa cha gari-moshi letu kwa mabomu nasi tukalazimika kusimama. Ijapokuwa mabehewa yetu yalikuwa nyuma tu ya kichwa hicho, hakuna aliyeuawa. Kichwa kingine cha gari-moshi kiliunganishwa na behewa letu nasi tukaendelea na safari.

      Baada ya kusafiri kilometa 100 hivi, tulisimama kwa saa mbili katika kituo fulani. Tukiwa hapo, tuliwaona wanaume na wanawake fulani waliobeba viazi kwa vikapu. Tulidhani wao ni wachuuzi wa viazi. Lakini tulikosea. Walikuwa ndugu na dada zetu wa kiroho waliokuwa wamesikia kutuhusu na kujua kwamba tulikuwa na njaa. Walimpa kila mmoja wetu viazi vitatu vikubwa vilivyochemshwa, kipande cha mkate, na chumvi kidogo. Hiyo ‘mana kutoka mbinguni’ ilitutegemeza kwa siku nyingine mbili hadi tulipofika Szombathely, Hungaria, mwanzoni mwa mwezi wa Desemba.

      Tulikaa Szombathely wakati wa baridi kali, na tulikula hasa mahindi yaliyokuwa yamefunikwa kwa theluji. Katika mwezi wa Machi na Aprili mwaka wa 1945, mji huo maridadi ulipigwa kwa mabomu, na maiti zilizokatwakatwa zikatapakaa barabarani. Watu wengi waliangukiwa na vifusi, na mara kwa mara tuliwasikia wakililia msaada. Tulitumia vijiko na vifaa vingine kuokoa baadhi yao.

      Majengo yaliyokuwa karibu na makao yetu yalipigwa kwa mabomu, lakini jengo letu halikupigwa. Kila mara king’ora kilipolia kutahadharisha kwamba mabomu yangeangushwa, watu wote waliogopa sana na kukimbilia usalama. Mwanzoni, sisi pia tulikuwa tukikimbia, lakini baada ya muda hatukuona tena uhitaji wa kufanya hivyo kwa kuwa hakukuwa na mahali salama pa kujificha. Hivyo, tulikaa tu na kujitahidi kutulia. Muda si muda, walinzi wakawa wakibaki nasi. Walisema kwamba Mungu wetu angeweza kuwaokoa wao pia! Mnamo Aprili 1, usiku wetu wa mwisho katika mji wa Szombathely, mabomu mengi sana yaliangushwa katika mji huo kuliko wakati mwingine wowote. Licha ya hilo, tulikaa katika jengo letu huku tukimsifu Yehova kwa nyimbo na kumshukuru kwa sababu ya kuwa na amani ya moyoni.—Flp. 4:6, 7.

      Siku iliyofuata tuliamriwa tuanze safari ya kwenda Ujerumani. Tulikuwa na magari mawili yanayokokotwa na farasi, hivyo, tulisafiri kwa magari hayo na pia kwa miguu kwa kilometa 100 hivi hadi tulipofika kwenye msitu fulani uliokuwa kilometa 13 kutoka mahali ambapo majeshi ya Urusi yalikuwa. Tulikaa katika shamba la tajiri fulani usiku kucha, na siku iliyofuata walinzi wetu wakatuachilia. Tulimshukuru Yehova kwa sababu alikuwa ametutunza kimwili na kiroho, kisha tukitokwa na machozi tukaagana na wenzetu na kwenda makwetu. Baadhi yetu tulitembea kwa miguu na wengine wakasafiri kwa gari-moshi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki