-
Jamhuri Ya Kongo (Brazzaville)2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
-
-
Ndugu jasiri wa Brazzaville, kutia ndani Louis-Noël Motoula, Jean-Marie Lubaki, na Symphorien Bakeba, walijitolea kuwatafuta ndugu waliopotea na kuwasaidia wale waliobaki Brazzaville. Ndugu hao waliendesha mashua zao ndogo katika mikondo yenye nguvu ya Mto Kongo ili wawatafute akina ndugu katika visiwa vidogo na kwenye kingo za mto huo. Walilazimika kuingia katika eneo lenye vita huko Brazzaville ambako watu walikuwa wakiuawa kikatili. Walihatarisha uhai wao kwa ajili ya ndugu zao.
Symphorien, aliyekuwa stadi katika kuvuka mto huo, aliuvuka mara nyingi sana wakati wa vita. Nyakati nyingine alivuka ili kuwasaidia wale waliobaki Brazzaville. Kwa mfano, pindi moja, alivuka akiwa na magunia kumi ya mchele aliyokuwa akiwapelekea ndugu walioishi katika eneo lenye usalama wa kadiri huko Brazzaville. Bila shaka ilikuwa vigumu kuvuka mto huo, lakini ilikuwa vigumu hata zaidi kufikisha magunia hayo bila kunyang’anywa na waporaji. Katika safari hiyo, kulikuwa na abiria mmoja ambaye alionekana kuwa mtu mwenye cheo. Mtu huyo alimuuliza Symphorien alikokuwa akipeleka mchele. Symphorien alimweleza kwamba alikuwa akiwapelekea ndugu zake Wakristo mchele huo, kisha akatumia nafasi hiyo kumweleza kuhusu tumaini lake linalotegemea Biblia. Mashua ilipofika ukingoni, mtu huyo alijitambulisha kuwa afisa wa cheo cha juu. Aliwaita askari kadhaa na kuwaagiza walinde mchele huo hadi Symphorien apate gari la kuusafirisha kwa akina ndugu.
Kwa kawaida, Symphorien alivuka mto ili kuwasaidia ndugu wakimbie Brazzaville. Kuna safari moja ambayo hatasahau kamwe. Anasema: “Mikondo ya Mto Kongo ni yenye nguvu sana, lakini watu wengi wenye mashua wanajua kuvuka bila kupelekwa kwenye maporomoko hatari. Tulipoondoka Brazzaville, mashua yetu ilikuwa na ndugu saba na watu wengine watano. Petroli iliisha tulipokuwa katikati ya mto. Tulifaulu kuiendesha mashua hadi kwenye kisiwa kidogo ambako tulitia nanga. Tulifurahi wakati mashua nyingine ndogo ilipopitia hapo, na nahodha akaahidi kutununulia petroli huko Kinshasa. Tulingojea tukiwa na wasiwasi kwa muda wa saa moja na nusu, mpaka alipoleta petroli.”
-
-
Jamhuri Ya Kongo (Brazzaville)2004 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
-
-
[Picha katika ukurasa wa 158]
Louis-Noël Motoula, Jean-Marie Lubaki, na Symphorien Bakeba
-