Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Aokolewa Asiliwe na Simba!
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
    • 4 Lingekuwa jambo lenye kushangaza iwapo Dario angemweka Danieli, mhamishwa Myahudi, awe liwali. Lakini hebu wazia zile rabsharabsha wakati ambapo Dario alitangaza uamuzi wake wa kumfanya Danieli awe mmoja wa mawaziri watatu ambao wangesimamia maliwali! Si hilo tu bali pia kwamba Danieli “alipata sifa,” akijithibitisha kuwashinda mawaziri wenzake. Kwa kweli, alikuwa na “roho bora.” Hata Dario aliazimu kumweka juu ya ufalme wote.—Danieli 6:2, 3.

      5. Lazima wale mawaziri na maliwali wengine walihisije Danieli alipopewa cheo, na kwa nini?

      5 Wale mawaziri wengine na maliwali lazima wawe walijawa hasira. Kwani, hawangevumilia kumwona Danieli—asiye Mmedi wala Mwajemi wala mshiriki wa familia ya mfalme—akiwa na mamlaka juu yao! Dario angewezaje kumkweza mgeni na kumpa umaarufu huo, akiwaruka watu wa nchi yake mwenyewe, hata watu wa familia yake mwenyewe? Lazima jambo hilo lilionekana kuwa lisilo la haki. Isitoshe, yaonekana kwamba maliwali waliuona uaminifu-maadili wa Danieli kuwa kizuizi kisichotakikana dhidi ya mazoea yao yasiyo ya haki na ya ufisadi. Hata hivyo, mawaziri na maliwali hao hawakuthubutu kumfikia Dario juu ya jambo hilo. Kwani, Dario alimstahi sana Danieli.

      6. Mawaziri na maliwali walijaribuje kumshushia Danieli heshima, na kwa nini jitihada zao hazikufua dafu?

      6 Kwa hiyo, wanasiasa hao wenye wivu wakapanga njama miongoni mwao. Walijaribu “kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme.” Je, namna alivyotimiza madaraka yake ingeweza kuwa na kosa lolote? Je, alikuwa mtu asiyefuatia haki? Mawaziri na maliwali hao hawakuweza kupata uzembe wowote au ufisadi wowote katika njia ambayo Danieli alitimiza wajibu wake. “Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo,” wakajadiliana, “tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.” Na hivyo ndivyo watu hao wenye hila walivyopanga njama. Walidhani ingemkomesha Danieli daima dawamu.—Danieli 6:4, 5.

      NJAMA YA UUAJI YAANZA KUTEKELEZWA

      7. Mawaziri na maliwali walimpendekezea mfalme nini, nao walifanyaje hivyo?

      7 Dario alifikiwa na msafara wa mawaziri na maliwali ‘waliokusanyika pamoja mbele ya mfalme.’ Usemi wa Kiaramu unaotumiwa hapa una wazo la rabsharabsha zenye kelele. Yaonekana kwamba watu hao walifanya ionekane kana kwamba walikuwa na jambo la dharura la kumwambia Dario. Huenda walifikiri kwamba hangezusha maswali juu ya pendekezo lao ikiwa wangemwambia kwa usadikisho na kana kwamba ni jambo lililohitaji kuchukuliwa hatua mara moja. Kwa hiyo, wakataja jambo hilo moja kwa moja, wakisema: “Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.”a—Danieli 6:6, 7.

      8. (a) Kwa nini Dario angeona sheria iliyopendekezwa kuwa yenye kupendeza? (b) Mawaziri na maliwali walikusudia nini hasa?

      8 Rekodi za kihistoria zathibitisha kwamba lilikuwa jambo la kawaida kwa wafalme wa Mesopotamia kuonwa na kuabudiwa kama miungu. Kwa hiyo, bila shaka Dario alipendezwa na pendekezo hilo. Pia huenda jambo hilo lilionekana kuwa lenye faida. Kumbuka kwamba Dario alikuwa mgeni kwa watu waliokuwa wakiishi Babiloni. Sheria hiyo mpya ingemwimarisha akiwa mfalme, nayo ingechochea halaiki za watu waliokuwa wakiishi Babiloni wawe waaminifu na kuunga mkono serikali hiyo mpya. Ingawa hivyo, mawaziri na maliwali hawakupendezwa na hali nzuri ya mfalme walipokuwa wakipendekeza amri hiyo. Kusudi lao la kweli lilikuwa kumnasa Danieli, kwa kuwa walijua kwamba ilikuwa desturi yake kusali kwa Mungu mara tatu kwa siku kwenye madirisha yaliyo wazi katika chumba chake cha paa.

      9. Kwa nini sheria hiyo mpya haingewatatiza watu wengi wasio Wayahudi?

      9 Je, kizuizi hicho cha sala kingetatiza jumuiya zote za kidini za Babiloni? Sivyo, hasa kwa kuwa katazo hilo lingedumu mwezi mmoja tu. Isitoshe, ni watu wachache sana wasio Wayahudi ambao wangeona kuabudu mwanadamu kwa muda kuwa kuridhiana. Msomi mmoja wa Biblia ataarifu hivi: “Kumwabudu mfalme kulikuwa kawaida kwa mataifa hayo yenye kuabudu sanamu sana; na kwa hiyo Wababiloni walipoagizwa wamwabudu mshindi—Dario Mmedi—kama mungu, walikubali mara moja kufanya hivyo. Wayahudi peke yao ndio walioudhika na dai hilo.”

      10. Wamedi na Waajemi waliionaje sheria iliyotungwa na mfalme wao?

      10 Vyovyote vile, wageni wa Dario walimhimiza ‘apige marufuku, akatie sahihi maandiko hayo, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.’ (Danieli 6:8) Katika Mashariki ya kale, mapenzi ya mfalme yalionwa kuwa sheria kamili. Hilo lilitokeza dhana ya kwamba hangeweza kukosea. Hata sheria ambayo ingesababisha vifo vya watu wasio na hatia ilipaswa kuendelea kutumika!

      11. Danieli angeathiriwaje na amri iliyotolewa na Dario?

      11 Bila kumfikiria Danieli, Dario akatia sahihi amri hiyo. (Danieli 6:9) Kwa kufanya hivyo, alitia sahihi hati ya kuidhinisha kifo cha waziri wake aliyemthamini zaidi. Ndiyo, bila shaka Danieli angeathiriwa na amri hiyo.

      DARIO ALAZIMIKA KUTOA HUKUMU KALI

      12. (a) Danieli alifanya nini mara tu alipopata kujua juu ya sheria hiyo mpya? (b) Ni nani waliokuwa wakimtazama Danieli, na kwa nini?

      12 Upesi Danieli akapata kujua juu ya sheria hiyo iliyokataza kutoa sala. Mara moja, akaingia nyumbani mwake na kwenda kwenye chumba cha paa, ambapo madirisha yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu.b Huko, Danieli akaanza kusali kwa Mungu “kama ilivyokuwa kawaida yake.” (BHN) Huenda Danieli alifikiri alikuwa peke yake, lakini waliompangia njama walikuwa wakimtazama. Ghafula,“waliingia ndani,” yamkini kwa njia ileile walivyokusanyika kwa rabsharabsha walipomwendea Dario. Sasa walikuwa wakiona kwa macho yao wenyewe—Danieli alikuwa “akiomba dua na kumsihi Mungu wake.” (Danieli 6:10, 11, BHN) Mawaziri na maliwali walikuwa na uthibitisho wote waliouhitaji wa kumshtaki Danieli mbele ya mfalme.

      13. Adui za Danieli waliripoti nini kwa mfalme?

      13 Adui za Danieli walimwuliza Dario kwa hila: “Je! hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba?” Dario akajibu, akasema: “Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.” Sasa wapanga-njama hao wakasema mambo waziwazi. “Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.”—Danieli 6:12, 13.

      14. Yaonekana ni kwa nini mawaziri na maliwali walimrejezea Danieli kuwa “mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda”?

      14 Ni jambo lenye kutokeza kwamba mawaziri na maliwali walimrejezea Danieli kuwa “mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda.” Yaonekana kwamba walitaka kukazia kwamba Danieli ambaye Dario alikuwa amemkweza na kumpa umaarufu hivyo kwa hakika hakuwa mtu wa maana ila mtumwa Myahudi tu. Waliamini kwamba kwa sababu hiyo, alikuwa chini ya sheria—hata iwe mfalme alihisi namna gani juu yake!

      15. (a) Dario alitendaje alipopashwa habari na mawaziri na maliwali? (b) Mawaziri na maliwali walionyeshaje hata zaidi kwamba walimdharau Danieli?

      15 Huenda mawaziri na maliwali walimtarajia mfalme awathawabishe kwa kazi yao ya kupeleleza kwa werevu. Ikiwa ndivyo, basi waliambulia patupu. Dario alitaabishwa sana na habari alizopashwa. Badala ya kumkasirikia Danieli au kuagiza atupwe kwenye tundu la simba mara moja, Dario alijaribu siku nzima kumwokoa. Lakini hakufua dafu. Punde si punde wapanga-njama wakarudi, na bila haya wakadai Danieli auawe.—Danieli 6:14, 15.

      16. (a) Kwa nini Dario alimheshimu Mungu wa Danieli? (b) Dario alikuwa na matumaini gani kuhusu Danieli?

      16 Dario alihisi kwamba hana la kufanya kuhusu hilo. Sheria haingeweza kutanguliwa, wala “kosa” la Danieli halingeweza kusamehewa. Dario angeweza tu kumwambia Danieli “Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.” Yaonekana Dario alimheshimu Mungu wa Danieli. Yehova ndiye aliyekuwa amempa Danieli uwezo wa kutabiri kuanguka kwa Babiloni. Pia Mungu alikuwa amempa Danieli “roho bora,” iliyomtofautisha na wale mawaziri wengine. Huenda Dario alijua kwamba makumi ya miaka mapema, Mungu huyohuyo alikuwa amewaokoa vijana watatu Waebrania wasiteketee kwenye tanuru ya moto. Yamkini, mfalme alitumaini kwamba Yehova angemwokoa Danieli, kwa kuwa Dario hangeweza kubadili sheria aliyokuwa ametia sahihi. Basi, Danieli akatupwa katika tundu la simba.c Kisha, “likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.”—Danieli 6:16, 17.

      BADILIKO LENYE KUTOKEZA

      17, 18. (a) Ni nini kionyeshacho kwamba Dario alisononeshwa na hali ya Danieli? (b) Ni nini kilichotukia mfalme aliporudi kwenye tundu la simba asubuhi iliyofuata?

      17 Dario aliyesononeka akarudi kwenye makao yake. Hakuna wanamuziki walioletwa kumtumbuiza, kwa kuwa hakutaka. Badala yake, Dario alikesha kitandani usiku kucha, akifunga. “Usingizi wake ukampaa.” Alfajiri, Dario alienda haraka kwenye tundu la simba. Akapaaza sauti kwa huzuni: “Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?” (Danieli 6:18-20) Alishangaa na kutulizwa alipojibiwa!

      18 “Ee mfalme, uishi milele.” Kwa salamu hiyo yenye staha, Danieli alionyesha kwamba hakuwa na uhasama kumwelekea mfalme. Alitambua kwamba matatizo yake hayakutokana na Dario, bali yalitokana na mawaziri na maliwali wenye husuda. (Linganisha Mathayo 5:44; Matendo 7:60.) Danieli akaendelea kusema: “Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.”—Danieli 6:21, 22.

      19. Mawaziri na maliwali walikuwa wamemdanganyaje Dario na kumwongoza kwa hila?

      19 Lazima maneno hayo yawe yaliisumbua dhamiri ya Dario kama nini! Muda wote huo alijua kwamba Danieli hakuwa amefanya lolote la kustahili kutupwa kwenye tundu la simba. Dario alijua vizuri kwamba mawaziri na maliwali walikuwa wamepanga njama ya kumfanya Danieli auawe na kwamba walikuwa wamemwongoza mfalme kwa hila ili watimize nia zao zenye ubinafsi. Kwa kusisitiza kwamba “mawaziri wote wa ufalme” walikuwa wamependekeza amri hiyo ipitishwe, walidokeza kwamba Danieli pia alikuwa ameombwa maoni kuhusu hilo. (Italiki ni zetu.) Dario angewaonyesha watu hao wenye hila cha mtema kuni baadaye. Hata hivyo, kwanza alitoa amri Danieli atolewe kwenye tundu la simba. Kimuujiza, Danieli hakuwa amekwaruzwa hata kidogo!—Danieli 6:23.

      20. Ni nini kilichowapata adui za Danieli waliokuwa na uchungu na uovu?

      20 Sasa, kwa kuwa Danieli alikuwa salama salimini, Dario akawa na shughuli nyingine. “Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.”d—Danieli 6:24.

      21. Katika kushughulika na washiriki wa familia za wakosaji, ni tofauti gani iliyokuwapo kati ya Sheria ya Kimusa na sheria za tamaduni fulani za kale?

      21 Huenda kuua wapanga-njama pamoja na wake zao na watoto wao kukaonwa kuwa ukali wa kupita kiasi. Kinyume cha hilo, Sheria ambayo Mungu alitoa kupitia nabii Musa ilitaarifu hivi: “Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.” (Kumbukumbu la Torati 24:16) Hata hivyo, katika tamaduni fulani za kale, kwa kawaida washiriki wa familia waliuawa pamoja na mkosaji, ikiwa alifanya kosa kubwa. Huenda hilo lilifanywa ili washiriki wa familia wasiweze kulipiza kisasi baadaye. Hata hivyo, tendo hilo dhidi ya familia za mawaziri na maliwali halikusababishwa na Danieli. Yaelekea, Danieli alisononeshwa na maafa ambayo watu hao waovu walikuwa wamesababishia familia zao.

      22. Dario alitoa tangazo gani jipya?

      22 Mawaziri na maliwali wenye kupanga njama walikuwa wamekufa. Dario alitoa tangazo lililotaarifu hivi: “Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.”—Danieli 6:25-27.

  • Aokolewa Asiliwe na Simba!
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
    • [Picha katika ukurasa wa 121]

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki