Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Uhai—Ulitokana na Muumba?
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Uhai—Ulitokana na Muumba?

      Uhai—Ulitokana na Muumba?

  • Ukurasa wa Kichwa/Ukurasa wa Wachapishaji
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Ukurasa wa Kichwa/Ukurasa wa Wachapishaji

      Uhai—Ulitokana na Muumba?

      Broshua hii haiuzwi. Ni sehemu ya kazi ya elimu ya Biblia ulimwenguni pote inayotegemezwa kwa michango ya hiari.

      Ikiwa ungependa kutoa mchango, tafadhali tembelea tovuti ya donate.jw.org.

      Isipokuwa iwe imeonyeshwa vingine, Maandiko yamenukuliwa kutoka katika Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya

      Chapa ya Julai 2023

      Swahili (lc-SW)

      © 2010

      WATCH TOWER BIBLE AND TRACT SOCIETY OF PENNSYLVANIA

  • Yaliyomo
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Yaliyomo

      UKURASA WA 4 Sayari Yenye Uhai Tele

      UKURASA WA 11 Ni Nani Aliyebuni Kwanza?

      UKURASA WA 18 Mageuzi—Dhana na Ukweli wa Mambo

      UKURASA WA 24 Sayansi na Kitabu cha Mwanzo

      UKURASA WA 29 Imani Yako Ni Jambo la Kuhangaikiwa?

      UKURASA WA 30 Bibliografia

  • Unaamini Nini?
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Binti akimtizama kipepeo

      Unaamini Nini?

      Watu fulani wanaodai kwamba wanaamini masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji husema kwamba dunia na vyote vilivyomo viliumbwa katika siku sita za saa 24, miaka elfu kumi hivi iliyopita. Wengine hudai kwamba hakuna Mungu, Biblia ni kitabu cha hekaya, na viumbe vyote vyenye uhai vilitokea kiholela.

      Watu wengi huunga mkono mojawapo ya dhana hizo, au wana imani iliyo tofauti kidogo. Huenda kuisoma kwako broshua hii kunaonyesha kwamba wewe pia unapendezwa na suala la chanzo cha uhai. Huenda unaamini kwamba kuna Mungu, na unaiheshimu Biblia. Wakati uleule, unaheshimu pia maoni ya wanasayansi waliobobea katika taaluma zao, ambao wanaamini kwamba uhai ulijitokeza wenyewe. Ikiwa wewe ni mzazi, huenda usijue jinsi ya kuwajibu watoto wako wanapokuuliza kuhusu mageuzi au uumbaji.

      Kusudi la Broshua Hii

      Habari zilizo katika broshua hii hazikusudiwi kudhihaki wenye maoni tofauti kuhusu uumbaji au wale wasioamini kuwapo kwa Mungu. Badala yake, tunatumaini kwamba broshua hii itakuchochea kufikiria kwa uzito ni kwa nini unaamini mambo unayoamini. Itachanganua masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji, masimulizi ambayo huenda hujawahi kuyafikiria kwa njia hiyo. Pia, itakazia kwa nini ni vizuri kuzingatia msingi wa mambo unayoamini kuhusu chanzo cha uhai.

      Je, utaamini madai ya wale wanaosema kwamba hakuna Muumba mwenye akili na kwamba Biblia haitegemeki? Au utachunguza yale hasa ambayo Biblia inasema? Ni mafundisho gani unayoweza kutegemea na kuamini: ya Biblia au ya wanamageuzi? (Waebrania 11:1) Tunakutia moyo uchunguze ukweli wa mambo.

  • Sayari Yenye Uhai Tele
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Sayari zikilizunguka jua

      Sayari Yenye Uhai Tele

      Hakungekuwa na uhai duniani ikiwa si kwa sababu ya “matukio” hususa, ambayo baadhi yake hayakujulikana au kueleweka vizuri mpaka katika karne ya 20. Matukio hayo yanatia ndani:

      • Mahali dunia ilipo katika kundi-nyota linaloitwa Kilimia na vilevile katika mfumo wa jua, hali kadhalika mzunguko wa dunia, mwinamo wake, mwendo wake inapozunguka, na mwezi wake usio wa kawaida

      • Ugasumaku na angahewa zinazoikinga dunia

      • Mizunguko ya asili ambayo husafisha na kurekebisha hewa na maji ya dunia

      Unapotafakari kila moja kati ya mambo hayo, jiulize, ‘Je, yote hayo yalijitokeza yenyewe tu au yalibuniwa kwa kusudi fulani?’

      “Anwani” Sahihi ya Dunia

      Mahali dunia ilipo katika mfumo wa jua

      Je, dunia ingeweza kuwa mahali bora panapotegemeza uhai kuliko mahali ilipo sasa?

      Je, dunia ingeweza kuwa mahali bora panapotegemeza uhai kuliko mahali ilipo sasa? Unapoandika anwani yako, unatia ndani habari gani? Huenda ukaandika jina la nchi, mji, au hata mtaa. Vivyo hivyo, tuseme kwamba kundi-nyota la Kilimia ndilo “nchi” ya dunia, nao mfumo wa jua—yaani, jua na sayari zinazolizunguka—ndio “mji” wa dunia, kisha mzunguko wa dunia katika mfumo wa jua tuuite “mtaa” wa dunia. Kwa sababu ya hatua ambazo zimepigwa katika ulimwengu wa kisayansi, wanasayansi wa leo wameweza kuelewa mengi sana kuhusu faida za dunia kuwa mahali pa pekee ilipo katika ulimwengu mzima.

      Kwanza kabisa, “mji” wetu, yaani, mfumo wa jua, uko mahali panapofaa kabisa katika kundi-nyota la Kilimia—si karibu sana na kitovu wala mbali sana. Mahali hapo, au “eneo linalokalika,” kama wanasayansi fulani wanavyopaita, pana kiwango sahihi cha kemikali zinazohitajika ili kutegemeza uhai. Tungekuwa nje zaidi, kemikali hizo zingekuwa chache mno; na kama tungekaribia ndani zaidi, tungekuwa katika mazingira hatari kwa sababu ya miale hatari na mambo mengine. “Tunakaa eneo bora zaidi,” lasema gazeti Scientific American.1

      “Mtaa” bora: “Mtaa” wa dunia katika “mji” wetu, yaani, mzunguko wetu katika mfumo wetu wa jua, ni mtaa “bora.” Ikiwa umbali wa kilomita milioni 150 kutoka kwenye jua, dunia inazunguka katika eneo bora kabisa, mahali ambapo viumbe vyenye uhai haviwezi kuganda kwa baridi wala kuteketea kwa moto. Isitoshe, kwa kuwa mzingo wa dunia ni karibu mviringo, kwa mwaka mzima tunabaki karibu umbali uleule kutoka kwenye jua.

      Jua nalo ni “kiwanda bora cha umeme.” Linategemeka, lina ukubwa unaofaa, nalo huandaa kiasi cha kutosha cha nguvu zinazohitajiwa. Ndiyo sababu jua huitwa “nyota ya pekee sana.”2

      “Jirani” mzuri kabisa: Ikiwa ungeombwa uchague “jirani” wa dunia, hungepata jirani mzuri kuliko mwezi. Kipenyo chake ni robo moja hivi ya kipenyo cha dunia. Kwa hiyo, kwa kulinganishwa na miezi mingine katika mfumo wetu wa jua, mwezi unaozunguka dunia ni mkubwa isivyo kawaida kwa kulinganishwa na miezi inayozunguka sayari zingine. Je, imetokea hivyo kwa nasibu tu? Haielekei.

      Kwanza kabisa, mwezi ndio husababisha kujaa na kupwa kwa maji ya bahari, jambo ambalo ni muhimu sana katika mazingira ya dunia. Pia, mwezi huisaidia dunia kuzunguka katika mhimili wake pasipo kuyumbayumba. Pasipo mwezi wetu wa pekee, dunia ingeyumbayumba kama pia, huenda hata kupinduka juu chini! Hali ya hewa, kujaa na kupwa kwa bahari, na mabadiliko mengine yangesababisha madhara makubwa.

      Mwinamo na mzunguko wa dunia

      Mwinamo na mzunguko barabara wa dunia: Majira ya kila mwaka, hali-joto, na hali-hewa tofauti-tofauti hutegemea mwinamo wa dunia wa nyuzi 23.4 hivi. Kitabu kimoja chasema: “Yamkini mwinamo wa sayari yetu ni ‘barabara kabisa.’”—Rare Earth—Why Complex Life Is Uncommon in the Universe.3

      Jambo jingine “barabara kabisa” ni urefu wa mchana na usiku, unaotegemea mzunguko wa dunia. Ikiwa dunia ingekuwa ikizunguka polepole kuliko inavyozunguka, siku zingekuwa ndefu zaidi nao upande wa dunia unaokabili jua ungeteketea huku upande wa pili ukiganda kwa baridi. Kwa upande mwingine, ikiwa dunia ingezunguka kasi kuliko inavyozunguka, siku zingekuwa fupi zaidi, zenye urefu wa saa chache tu, nao mzunguko huo wa kasi ungetokeza pepo zenye nguvu zinazovuma daima na kusababisha madhara makubwa.

      Ngao za Dunia

      Anga la nje ni mahali hatari penye miale na vimondo vingi. Hata hivyo, dunia yetu huonekana kana kwamba inasafiri katikati ya “uwanja wa kulenga-shabaha” bila kupatwa na madhara yoyote. Kwa nini? Kwa sababu dunia inalindwa na ngao ya ajabu—ugasumaku wenye nguvu na angahewa kabambe.

      Ugasumaku wa dunia ambao hauonekani

      Ugasumaku usioonekana unaoilinda dunia

      Ugasumaku wa dunia: Ndani katikati ya dunia kuna donge kubwa linalozunguka la chuma kilichoyeyuka. Hilo hutokeza ugasumaku mkubwa na wenye nguvu zinazofika anga la nje. Ngao hiyo hutulinda dhidi ya miale hatari kutoka katika anga la nje na pia dhidi ya nguvu hatari za jua. Nguvu hizo zinatia ndani chembechembe zenye nishati zinatoka kwenye jua kwa nguvu; miwako ya jua, ambayo kwa dakika chache hutokeza nguvu zinazoweza kulinganishwa na mabilioni ya mabomu ya hidrojeni; mabilioni ya tani ya mata zinazotupwa angani kunapotokea milipuko katika kile kinachoonekana kama taji la nuru kulizunguka jua, kinachoitwa korona. Mara kwa mara uthibitisho wa ulinzi huo wa ugasumaku huonekana katika anga la juu karibu na ncha-sumaku za dunia, wakati ambapo miwako na milipuko katika korona inatokeza maonyesho yenye kupendeza ya rangi mbalimbali yanayoitwa orora.

      Orora inayoitwa borealis

      Orora inayoitwa borealis

      Angahewa la dunia: Mbali na kutuandalia hewa ya kupumua, blanketi inayotuzunguka ya gesi mbalimbali hutupa ulinzi. Tabaka la nje la angahewa, linaloitwa tabakastrato, lina oksijeni ya aina fulani inayoitwa ozoni, ambayo hufyonza asilimia 99 ya miale hatari ya urujuani. Kwa hiyo, tabaka la ozoni hulinda aina nyingi za viumbe—kutia ndani wanadamu na mimea ambayo hutokeza oksijeni tunayopumua—dhidi ya miale hatari. Kiwango cha ozoni kwenye tabakastrato hubadilika-badilika kulingana na ukali wa miale ya urujuani. Kubadilika-badilika huko huifanya kuwa ngao murua.

      Kimondo

      hutulinda dhidi ya vimondo

      Angahewa hutulinda pia dhidi ya vifusi vinavyoanguka kila siku kutoka katika anga la nje—mamilioni ya vitu, vidogo kwa vikubwa. Vingi kati ya vitu hivyo, huteketea vinapoingia kwenye angahewa la dunia, vikitokeza nuru nyangavu inayoitwa vimondo. Wakati huohuo, ngao za dunia hazizuii miale ambayo ni muhimu kwa uhai, kama vile ile inayotokeza joto na nuru. Angahewa hutapanya vizuri joto duniani, na wakati wa usiku huhifadhi joto kama blanketi.

      Angahewa na ugasumaku wa dunia kwa kweli ni vitu vya ajabu ambavyo bado havieleweki kikamili. Twaweza kusema vivyo hivyo kuhusu mizunguko inayotegemeza uhai duniani.

      Je dunia yetu ilijikuta tu ikiwa na ngao mbili kabambe?

      Mizunguko Inayotegemeza Uhai

      Ikiwa nyumba ingekatiwa maji, madirisha yafungwe hivi kwamba hewa isiingie wala kutoka, na mifumo ya maji taka izibwe, muda si muda nyumba hiyo haingekalika. Lakini fikiria hili: Hivyo ndivyo dunia yetu ilivyo. Hatupati hewa na maji safi kutoka katika anga la nje, wala takataka zetu hazichukuliwi na kupelekwa katika anga la nje. Hivyo basi, dunia imewezaje kutegemeza uhai na kukalika kwa muda wote huo? Jibu ni: mizunguko yake, kama vile mizunguko ya maji, kaboni, oksijeni, na nitrojeni inayofafanuliwa na kuonyeshwa hapa kwa njia sahili.

      Mzunguko wa maji

      Mzunguko wa maji: Maji ni muhimu kwa uhai. Pasipo maji, kila mmoja wetu angekufa baada ya siku chache. Mzunguko wa maji huandaa maji safi duniani pote. Mzunguko huo una hatua tatu. (1) Nguvu za jua huyainua maji hadi angani yakiwa mvuke. (2) Maji hayo safi yaliyotoneshwa hufanyiza mawingu. (3) Nayo mawingu, hutokeza mvua, mvua ya mawe, au theluji ambazo hunyesha, kisha huinuka tena zikiwa mvuke, na hivyo kukamilisha mzunguko wa maji. Ni kiasi gani cha maji kinachorejelezwa kila mwaka? Kulingana na makadirio, ni maji ya kutosha kufunika kila sehemu ya uso wa dunia kwa kina cha karibu mita moja.4

      Mizunguko ya kaboni na oksijeni

      Mizunguko ya kaboni na oksijeni: Kama ujuavyo, ili kuendelea kuishi unahitaji kupumua, kutwaa oksijeni na kutoa kaboni dioksidi. Lakini kwa kuwa kuna mabilioni ya watu na wanyama wanaofanya vivyo hivyo, mbona angahewa letu haliishiwi na oksijeni na kulemewa na kiwango cha kaboni dioksidi? Jibu ni: mzunguko wa oksijeni. (1) Katika mchakato wa ajabu unaoitwa usanidimwanga, mimea hutwaa kaboni dioksidi tunayotoa na kuitumia pamoja na nguvu za nuru ya jua ili kutokeza kabohidrati na oksijeni. (2) Tunapopumua oksijeni, tunakamilisha mzunguko huo. Yote hayo hutendeka kwa njia safi, yenye ustadi, na kimyakimya.

      Mzunguko wa nitrojeni

      Mzunguko wa nitrojeni: Uhai duniani hutegemea pia kutokezwa kwa molekuli mahuluku kama vile protini. (A) Ili kutokeza molekuli hizo, nitrojeni inahitajika. Jambo la kupendeza ni kwamba, asilimia 78 ya angahewa letu ni gesi ya nitrojeni. Radi huibadili nitrojeni kuwa mchanganyiko ambao mimea inaweza kufyonza. (B) Kisha mimea hutumia michanganyiko hiyo na kufanyiza molekuli mahuluku. Hivyo, wanyama wanaokula mimea hiyo hunufaika kutokana na nitrojeni hiyo. (C) Hatimaye, mimea na wanyama wanapokufa, michanganyiko ya nitrojeni humeng’enywa na bakteria. Mchakato huo wa kuoza.

      Urejelezi Kamili!

      Kila mwaka, wanadamu, pamoja na hatua za kitekinolojia ambazo wamepiga, hutokeza takataka zenye sumu zisizoweza kurejelezwa. Hata hivyo, dunia hurejeleza takataka zake zote kikamili, ikitumia uhandisi-kemikali wa kiwango cha juu sana.

      Unafikiri mifumo ya urejelezi ya dunia ilitoka wapi? “Ikiwa kwa kweli mifumo ya ikolojia ya Dunia ilijitokeza yenyewe, haingeweza kufikia kiwango cha upatano kamili hivyo wa kimazingira,” asema M. A. Corey, mwandishi wa masuala ya kidini na sayansi. 5 Je, unakubaliana na maoni yake?

      Tausi

      Ungejibu Namna Gani?

      • Je, unafikiri kwamba maumbile ya dunia yalitokana na Muumba mwenye akili? Ikiwa ndivyo, ni jambo gani kati ya mambo yaliyozungumziwa katika sehemu hii linalokusadikisha?

      • Ungemjibuje mtu anayedai kwamba dunia si kitu cha pekee, ilitokana tu na mageuzi?

      Samaki ndani ya matumbawe

      Uhai Tele

      Hakuna anayejua kuna spishi ngapi za viumbe duniani. Inakadiriwa kwamba kuna spishi kati ya milioni 2 na milioni 100. .6 Uhai umesambaa kiasi gani?

      Gramu mia moja tu ya udongo inaweza kuwa na spishi 10,000 za bakteria,7 mbali na vijiumbe vingine vingi. Spishi fulani hupatikana kina cha karibu kilomita tatu udongoni!8

      Hewa: Mbali na ndege, popo, na wadudu wanaoruka, angani kuna chavua na spora chungu nzima, hali kadhalika mbegu, na katika maeneo fulani maelfu ya aina tofauti-tofauti za vijidudu. Kama vile kulivyo na aina nyingi mbalimbali za vijidudu angani, “ndivyo pia kulivyo na aina nyingi mbalimbali za vijidudu katika udongo,” lasema gazeti Scientific American.9

      Bahari zingali fumbo kuu kwa sababu, ili kujifunza kinachoendelea katika vina vya bahari, wanasayansi mara nyingi hulazimika kutumia tekinolojia inayogharimu pesa nyingi. Hata miamba ya matumbawe, inayofikika kwa urahisi na ambayo imechunguzwa sana, huenda bado ikawa na mamilioni ya spishi ambazo hazijajulikana.

      Je, aina zote hizo za vitu vyenye uhai zilijitokeza zenyewe? Wengi hukubaliana na malenga aliyeandika: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.”a​—Zaburi 104:24.

      Flamingo wakiwa angani

      a Katika Biblia, jina la Mungu ni Yehova. Zaburi 83:18

  • Ni nani aliyebuni kwanza?
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Shakwe-bahari na nyangumi

      Ni nani aliyebuni kwanza?

      Katika miaka ya karibuni, ­wanasayansi na wahandisi wamekubali kufundishwa kihalisi na mimea na wanyama. (Ayubu 12:7, 8) Wanachunguza na kuiga maumbile ya viumbe kadhaa​—ufundi unaoitwa biomimetics katika lugha ya kitaalamu​—wakijaribu kubuni vifaa vipya au kuboresha vifaa vilivyopo. Unapofikiria mifano ifuatayo, jiulize, ‘Ni nani kwa kweli anayestahili kusifiwa kwa ubuni huo?

      Kujifunza kutokanana vikono vya nyangumi

      Vikono vya nyangumi

      Wanaounda ndege za abiria wanaweza kujifunza nini kutokana na nyangumi mwenye nundu? Mengi. Nyangumi aliyekomaa huwa na uzito wa kilo 30,000 hivi​—uzito wa lori lililopakiwa mizigo​—naye ana mwili mkakamavu na vikono vikubwa vinavyofanana na mabawa. Inashangaza kwamba mnyama huyo mwenye urefu wa mita 12 husafiri kwa urahisi akiwa majini.

      Kilichowashangaza watafiti hasa ni jinsi kiumbe mwenye mwili mkakamavu hivyo anavyoweza kugeuka na kujipinda katika maeneo madogo sana. Waligundua kwamba siri ni umbo la vikono vyake. Upande wa mbele ya vikono vya nyangumi si laini kama bawa la ndege ya abiria, bali umechongoka-chongoka kama meno ya msumeno. Sehemu hizo zilizo kama meno zinaitwa tubercles

      Nyangumi huyo anaposafiri kwa kasi majini, sehemu hizo humsaidia kunyanyuka na kusonga kwa urahisi zaidi pasipo kuzuiliwa na maji. Jinsi gani? Jarida Natural History linasema sehemu hizo hufanya maji yapite kasi na kuzunguka kwa urahisi, hata anapoibuka kutoka majini akiwa wima.10

      Ni nani mwenye hataza ya vitu vya asili?

      Ugunduzi huo unaweza kutumiwaje? Mabawa ya ndege za abiria yanayoundwa kwa kuiga ubuni huo yatahitaji pindo chache au vifaa vingine vya kiufundi vya kubadili mkondo wa upepo. Mabawa kama hayo ni salama zaidi na rahisi kuyakarabati. Mtaalamu John Long, anaamini kwamba hivi karibuni “kuna uwezekano mkubwa kwamba ndege zote za abiria zitakuwa na vinundu kama vikono vya nyangumi.”11

      Kuiga mabawa ya shakwe-bahari

      Bila shaka, Bila shaka, mabawa ya ndege za abiria huundwa kwa kuiga mabawa ya ndege walio hai. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, wahandisi wamepiga hatua katika uigaji wao. Gazeti New Scientist linaripoti hivi: “Watafiti katika Chuo Kikuu cha Florida wameunda ndege ndogo isiyoendeshwa na rubani iliyo na uwezo kama wa shakwe-bahari wa kuumbia hewani, kushuka, na kupaa kwa kasi.”12

      Ndege ndogo ya abiria yenye mabawa kama ya shakwe-bahari

      Shakwe-bahari hufanya sarakasi zote hizo kwa kukunja na kukunjua mabawa yake kwenye viwiko na mabega. Gazeti hilo linasema kwamba kwa kuiga ubuni huo, “ndege hiyo ndogo yenye ukubwa wa sentimita 60 hutumia mtambo mdogo unaoendesha fito kadhaa za chuma ambazo nazo huendesha mabawa yenyewe.” Mabawa hayo yaliyoundwa kwa ustadi huiwezesha ndege hiyo ndogo kuumbia hewani na kushuka kasi katikati ya majengo marefu. Wanajeshi wana hamu ya kuunda ndege kama hiyo inayoweza kuendeshwa kwa njia za ajabu ili waitumie katika shughuli kama vile kutafuta silaha za kemikali na za kibiolojia katika majiji makubwa.

      Kuiga mabawa ya shakwe-bahari

      Shakwe-bahari hagandi kamwe, hata anaposimama kwenye barafu. Kiumbe huyo huhifadhi jinsi gani joto la mwili wake? Siri moja ni maumbile yake ya ajabu ambayo wanyama wengi wanaoishi maeneo yenye baridi kali huwa nayo. Maumbile hayo humwezesha kunururisha joto kinyume cha mkondo.

      Vinururishaji-joto vinavyotenda kinyume cha mkondo vilivyo kwenye miguu ya shakwe-bahari humwezesha kusimama juu ya barafu

      Heat transfers, remains in the body. Cold stays in the feet

      Unururishaji-joto kinyume cha mkondo ni nini? Ili kuelewa wazo hilo, wazia mabomba mawili ya maji yaliyofungwa pamoja. Bomba moja linapitisha maji ya moto, na lile lingine linapitisha maji baridi. Ikiwa maji ya moto na maji baridi yanatiririka kuelekea upande mmoja, karibu nusu ya joto la maji ya moto litahamia kwenye maji baridi. Lakini, ikiwa maji ya moto na maji baridi yanatiririka kuelekea pande tofauti, karibu joto lote la maji ya moto litahamia kwenye maji baridi.

      Shakwe-bahari anaposimama kwenye barafu, vinururishaji-joto kwenye miguu yake hupasha joto damu inaporudi kutoka kwenye miguu baridi ya ndege huyo. Vinururishaji-joto hivyo huhifadhi joto katika mwili wa ndege huyo na kuzuia lisipotee kupitia miguu yake. Arthur P. Fraas, mhandisi wa masuala ya ufundi na usafiri wa ndege, aliufafanua ubuni huo kuwa “mojawapo ya unururishaji-joto unaojifanyiza tena na wenye matokeo zaidi ulimwenguni.”13 Ubuni huo ni wa hali ya juu sana hivi kwamba wanadamu wameuiga.

      Ni nani anayestahili kusifiwa?

      Samaki anayeitwa boxfish pamoja na sampuli ya gari

      A concept car imitates the surprisingly low-drag and stable design of the boxfish

      Wakati huohuo, shirika la NASA liko katika harakati za kutengeneza roboti yenye miguu mingi inayotembea kama nge, na wahandisi huko Finland tayari wametengeneza trekta lenye miguu sita ambalo linaweza kupanda na kuruka vizuizi kama mdudu mkubwa afanyavyo. Watafiti wengine wamebuni kitambaa chenye pindo ndogo-ndogo zinazoiga jinsi ambavyo koni za msonobari hufunguka na kufungika. Vitambaa hivyo hubadilika kulingana na joto la mwili la mtu ­aliyevaa vazi lililoshonwa kwa kitambaa hicho. Kiwanda fulani cha magari kiko katika harakati za kutokeza gari jipya linaloiga umbo la samaki anayeitwa box fish ambaye huogelea kwa wepesi. Na watafiti fulani wanachunguza uwezo wa kufyonza mshtuko wa koa za aina fulani ya konokono anayeitwa abalone, wakiwa na lengo la kutengeneza ngao imara zaidi lakini nyepesi.

      Pomboo

      Sonar in dolphins is superior to the human imitation

      Dhana nyingi nzuri zimetokana na vitu vya asili hivi kwamba watafiti wametayarisha hifadhi ya data ambayo tayari ina maelfu ya mifumo mbalimbali ya kibiolojia. Wanasayansi wanaweza kufanya utafiti kwa kutumia data hizo ili kupata “utatuzi wa asili wanapokumbana na matatizo fulani ya kiufundi,” lasema jarida The Economist. Mifumo ya kiasili iliyo katika hazina hiyo inaitwa hataza za kibiolojia. Kwa kawaida, mwenye hataza ni mtu au kampuni iliyo ya kwanza kuandikisha kisheria wazo jipya au mashine mpya. Likizungumzia hifadhi ya data hizo za hataza za kibiolojia, jarida The Economist linasema: “Wanapourejelea ustadi wa kubuni vitu kwa kuiga vitu vya asili kuwa ‘hataza za kibiolojia’, watafiti hao wanakazia tu kwamba kwa kweli vitu vya asili ndivyo vyenye hataza.”14

      Koa la konokono

      Scientists are researching the shock-absorbing properties of abalone shells

      Ubuni huo wa ajabu katika vitu vya asili ulitokeaje? Watafiti wengi hudai kwamba ubuni wote huo ulio katika vitu vya asili ulijitokeza wenyewe kupitia mageuzi ambayo yametukia kwa mamilioni ya miaka. Hata hivyo, watafiti wengine wamefikia kauli tofauti. Mwanasayansi Michael J. Behe aliandika hivi katika gazeti The New York Times la Februari 7, 2005: “Ubuni mwingi uliopo [katika vitu vya asili] hutokeza hoja rahisi yenye kusadikisha: ikiwa [kitu fulani] kinafanana, kinatembea, na kulia kama bata, na hakuna ushuhuda wa kuthibitisha vinginevyo, basi lazima tukate kauli kwamba huyo ni bata.” Alimaanisha nini? “Ubuni wa kitu haupaswi kupuuzwa eti kwa sababu tu unaonekana kwa urahisi.”15

      Unyayo wa mjusi

      The gecko can cling to the smoothest of surfaces by using molecular forces

      Bila shaka, mhandisi anayebuni bawa la ndege ya abiria lililo salama zaidi na linalofanya kazi vizuri zaidi anastahili sifa. Vivyo hivyo, mbuni anayevumbua kitambaa laini zaidi, au gari bora zaidi, anastahili sifa kwa sababu ya ubuni wake. Mtu akiunda bidhaa kwa kuiga ubuni wa mtu mwingine na akose kumtaja mbuni mwenyewe, anaweza kushtakiwa.

      Sasa fikiria mambo yafuatayo: Watafiti ambao wamebobea katika taaluma zao,wamefanikiwa kwa kiasi kidogo sana kuiga mifumo ya kiasili ili kutatua matatizo ya kihandisi. Hata hivyo, baadhi yao wanadai eti hekima yote iliyo katika vitu vya asili wanavyojitahidi kuiga, haikutokana na chanzo chochote chenye akili, bali ni tokeo la mageuzi. Je, unafikiri dai hilo linapatana na akili? Ikiwa ubuni wenye akili nyingi unahitajika ili kuiga kitu cha asili, basi akili nyingi hata zaidi zinahitajika ili kutokeza kitu hicho cha asili kinachoigwa, sivyo? Kwa kweli, ni nani anayestahili sifa zaidi, mhandisi mkuu au mwanagenzi anayeiga ubuni wa mhandisi?

      Kauli inayopatana na akili

      Baada ya kuona ubuni wa ajabu katika vitu vya asili, watu wengi wanakubaliana na maneno ya mwandikaji wa Biblia Paulo, aliyesema: “Sifa [za Mungu] ambazo hazionekani, zinaonekana waziwazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinaeleweka kwa vitu vilivyofanywa, yaani, nguvu zake za milele na Uungu.”​—Romans 1:19, 20.

      Ungejibu namna gani?

      • Je, ni jambo linalopatana na akili kuamini kwamba uhandisi wa ajabu unaoonekana katika vitu vya asili ulijitokeza wenyewe tu?

      • Unaweza kumjibu jinsi gani mtu ana­yedai ya kuwa uhai unaonekana tu kana kwamba ulibuniwa, lakini sivyo ilivyo?

      Buibui anayetengeneza utando

      Je Zilibuniwa?

      Ikiwa nakala inahitaji mbuni, Namna gani kilichoigwa?

      Fuwele

      • Mabunda ya Kevlar

        Za Mwanadamu: Kevlar ni fumwele ngumu ambazo hutumiwa kutengeneza vitu kama fulana za kuzuia risasi. Ili kutengeneza fumwele hizo, halijoto za kiwango cha juu na kemikali hatari huhitajika.

      • Za Asili: Buibui wanaosokota utando hutengeneza aina saba za hariri. Hariri ngumu zaidi inayoitwa dragline, ni nyepesi kuliko pamba, lakini ngumu zaidi kuliko chumana hata Kevlar zinapolinganishwa kulinga na na uzito. Ukizidishwa ukubwa utoshane na uwanja wa mpira, utando wa hariri hiyo wenye unene wa sentimita moja ulio na fumwele zinazoachana kwa umbali wa sentimita 4, unaweza kusimamisha ndege kubwa ya abiria ikiwa mwendoni! Buibui hutengeneza hariri hiyo katika halijoto ya kawaida, wakitumia maji.

      Usafiri

      • Ndege kubwa ya abiria

        Wa Mwanadamu: Kampuni fulani za ndege zina mifumo ya kompyuta inayoweza kuongoza ndege kutoka nchi moja hadi nyingine na hata kuitua. Kompyuta iliyotumiwa katika ndege moja ya majaribio ilikuwa naukubwa wa kadi ya mkopo.

      • Wa Asili: Akiwa na ubongo unaotoshana na ncha ya kalamu, kipepeo anayeitwa monarch husafiri kilomita 3,000 hivi, kutoka Kanada hadi msitu mdogo nchini Mexico. Kipepeo huyo husafiri kwa kutegemea jua. Kwa kuwa ana uwezo wa kutambua kadiri jua linavyosonga angani, anaweza kubadili mkondo ili asipotee.

      Lenzi

      • Jicho lililotengenezwa na wanadamu lenye lenzi inayotoshana na kichwa cha pini

        Za Mwanadamu: Wahandisi wamebuni jicho tata lenye lenzi 8,500 linalotoshana na kichwa cha pini. Lenzi hizo zinaweza kutumiwa katika vifaa vinavyotambua mwendo kwa kasi yajuu na pia katika kamera fulani nyembamba sana zinazoweza kupiga picha pande nyingi kwa wakatimmoja.

      • Za Asili: Mdudu anayeitwa kereng’ende ana lenzi 30,000 hivi katika kila jicho! Picha ndogondogo zinazotokana na lenzi hizo huungana na kufanyiza picha moja ya eneo kubwa. Macho hayo yenye lenzi nyingi ya kereng’ende yana uwezo mkubwa wa kutambua kitu chochote kilicho mwendoni.

        Kereng’ende
  • Mageuzi—Dhana na Ukweli wa Mambo
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Orangutangu

      Mageuzi—Dhana na Ukweli wa Mambo

      “Mageuzi ni jambo hakika kama vile joto la jua lilivyo hakika,” adai Profesa Richard Dawkins, mwanasayansi maarufu wa mageuzi.16 Ni kweli kwamba majaribio na mambo yanayoonekana waziwazi yanathibitisha kwamba jua lina joto. Lakini je, majaribio na mambo yanayoonekana wazi yanatoa uthibitisho kama huo, usioweza kupingwa kuhusu fundisho la mageuzi?

      Kabla ya kujibu swali hilo, tunahitaji kutatua jambo fulani la msingi. Wanasayansi wengi wameona kwamba kadiri muda unavyopita, vizazi vya baadaye hubadilika kidogo. Kwa mfano, wanadamu wanaweza kuzalisha aina fulani za mbwa ili hatimaye mbwa watakaozaliwa wawe na miguu mifupi au wawe na manyoya marefu kuliko mbwa waliowazaa.a Wanasayansi fulani huyaita mabadiliko hayo madogo-madogo, “mageuzi madogo.”

      Hata hivyo, wanamageuzi wanafundisha kwamba mabadiliko madogo-madogo yalijumlika kwa mabilioni ya miaka na kutokeza mabadiliko makubwa hivi kwamba samaki wakawa amfibia na sokwe wakawa binadamu. Nayo hayo yanayorejelewa kuwa mabadiliko makubwa yanaitwa “mageuzi makubwa.”

      Charles Darwin na kitabu chake Origin of Species

      Charles Darwin na kitabu chake Origin of Species

      Kwa mfano, Charles Darwin, alifundisha kwamba mabadiliko madogo-madogo yanayoonekana ni uthibitisho wa kwamba mabadiliko makubwa zaidi, ambayo hakuna yeyote amepata kuyaona, yanawezekana pia.17 Alihisi kwamba katika vipindi virefu vya wakati, viumbe-hai sahili viligeuka polepole—kukiwa na “mabadiliko madogo-madogo sana”—na hatimaye kuwa mamilioni ya viumbe tofauti-tofauti ambavyo viko duniani leo.18

      Watu wengi hukubaliana na maoni hayo. Wanajiuliza, ‘Ikiwa mabadiliko madogo-madogo yanaweza kutokea katika spishi mbalimbali, mbona mageuzi yasitokeze mabadiliko makubwa-makubwa baada ya vipindi virefu vya wakati?’b Hata hivyo, kihalisi fundisho la mageuzi linategemea dhana tatu. Fikiria dhana zifuatazo.

      Dhana ya 1. Mabadiliko ya chembe za urithi hutokeza jamii mpya. Fundisho la mageuzi makubwa linategemea dai la kwamba mabadiliko ya chembe za urithi—au mabadiliko yasiyofuata mpangilio maalum katika chembe za urithi za mimea na wanyama—yanaweza kutokeza spishi mpya au hata makundi mapya kabisa ya wanyama na mimea.19

      Mmea wenye maua makubwa ambao chembe zake za urithi zimeabadilika

      Mabadiliko ya chembe za urithi yanaweza kuleta mabadiliko kwenye mimea​—kama huu mmea wenye maua makubwa—​lakini mabadiliko hayo yana mipaka

      Ukweli wa mambo. Sifa na tabia nyingi za mimea na wanyama hutegemea maagizo yaliyo katika chembe za urithi zilizo katika kiini cha kila chembe.c Watafiti wamegundua kwamba mabadiliko katika chembe za urithi yanaweza kutokeza mabadiliko katika vizazi vya baadaye vya wanyama na mimea. Hata hivyo, je, kweli mabadiliko katika chembe za urithi hutokeza spishi mpya kabisa? Utafiti ambao umefanywa kwa karne moja hivi kuhusu chembe za urithi umefunua nini?

      Kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1930, wanasayansi walianza kuunga mkono wazo jipya. Tayari walikuwa wakiamini kwamba ule mchakato wa uteuzi wa kiasili, yaani, kwamba viumbe bora zaidi katika mazingira yake ndio wanaoweza kuendelea kuishi na kuzaana, ungeweza kutokeza spishi mpya za mimea kutokana na mabadiliko yasiyofuata mpangilio maalum. Kwa hiyo, walikata kauli kwamba uteuzi mnemba, au unaofanywa na wanadamu, unaweza kutokeza spishi mpya kwa njia bora zaidi. “Msisimko huo ulienea miongoni wa wanabiolojia wengi, na hasa miongoni mwa wataalamu wa chembe za urithi na wazalishaji wa mimea na wanyama,” akasema Wolf-Ekkehard Lönnig, mwanasayansi katika taasisi moja nchini Ujerumani (Max Planck Institute for Plant Breeding Research).d Kwa nini kukawa na msisimko hivyo? Lönnig, ambaye kwa miaka 30 hivi amekuwa akichunguza mabadiliko ya chembe za urithi za mimea, anasema: “Watafiti hao walidhani wakati wa kubadili njia za msingi za kuzalisha mimea na wanyama umewadia. Walifikiri kwamba kwa kudukiza mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, wangeweza kutokeza mimea na wanyama wapya walio bora zaidi.”20 Hata wengine kati yao wananuia kutokeza spishi mpya kabisa.

      Nzi ambao chembe zao za urithi zimebadilika

      Nzi ambao chembe zao za urithi zimebadilika, ijapokuwa wana kasoro, bado ni nzi

      Wanasayansi nchini Marekani, Asia, na Ulaya walianzisha miradi ya utafiti iliyogharimu pesa nyingi, wakitumia mbinu walizodhani zingeharakisha mageuzi. Kumekuwa na matokeo gani baada ya utafiti huo ambao umechukua zaidi ya miaka 40? “Licha ya gharama kubwa,” asema mtafiti Peter von Sengbusch, “majaribio ya kutumia unururishaji [ili kubadili chembe za urithi] kutokeza aina mbalimbali zinazoweza kuzaana, yaliambulia patupu.”21 Pia, Lönnig alisema: “Kufikia miaka ya 1980, matumaini na msisimko uliokuwapo miongoni mwa wanasayansi yalikuwa yamegonga mwamba ulimwenguni pote. Utafiti kuhusu uzalishaji wa kudukiza ukiwa kitengo tofauti cha utafiti ulitupiliwa mbali katika nchi za Magharibi. Karibu mimea na wanyama wote waliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi . . . walikufa au walikuwa dhaifu kuliko wale wenye chembe za asili.”e

      Hata hivyo, data ambazo kufikia sasa zimekusanywa kwa miaka 100 hivi ya kutafiti mabadiliko ya chembe za urithi kwa ujumla, na hasa miaka 70 ya uzalishaji wa mimea na wanyama kwa kubadili chembe za urithi, zimewawezesha wanasayansi kukata kauli mbalimbali kuhusu uwezo wa kutokeza jamii mpya kwa kubadili chembe hizo. Baada ya kuchunguza matokeo ya utafiti huo, Lönnig alikata kauli hii: “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa. Kauli hiyo inapatana na majaribio na matokeo ya utafiti ambayo yamefanywa katika karne ya 20 na pia inapatana na sheria za welekeo.”

      Hivyo basi, je, mabadiliko ya chembe za urithi yanaweza kubadili spishi moja iwe kiumbe kingine kipya kabisa? Matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba haiwezekani. Kutokana na utafiti mbalimbali ambao amefanya, Lönnig amekata kauli kwamba “spishi zinazotambulika waziwazi zina mipaka ambayo haiwezi kufutiliwa mbali wala kukiukwa na mabadiliko yoyote katika chembe za urithi yanayotokea bila mpangilio wowote.”22

      Fikiria kinachomaanishwa na uthibitisho huo. Ikiwa wanasayansi stadi wameshindwa kutokeza spishi mpya kwa kudukiza mabadiliko na kuteua chembe bora za urithi, itawezekanaje basi mchakato usiotegemea akili yoyote ufaulu kufanya hivyo? Ikiwa utafiti unaonyesha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadilisha spishi za awali na kutokeza spishi mpya kabisa, basi, yale mageuzi makubwa yatawezekanaje?

      Dhana ya 2. Uteuzi wa kiasili ulitokeza spishi mpya. Darwin aliamini kwamba ule aliourejelea kuwa uteuzi wa kiasili ungetegemeza viumbe bora zaidi, ilhali viumbe dhaifu hatimaye vingekufa na kutoweka. Wanamageuzi wa kisasa wanafundisha kwamba kadiri spishi zilivyoenea na kutapakaa, ndivyo uteuzi wa kiasili ulivyoteua viumbe ambavyo chembe zao za urithi zilibadilika na kujipatanisha zaidi na mazingira yao mapya. Kwa hiyo, wanamageuzi wanadai kwamba spishi hizo zilizotapakaa hatimaye zilitokeza spishi mpya kabisa.

      Ukweli wa mambo. Kama tulivyoona, kuna uthibitisho wa kutosha unaoonyesha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kamwe kutokeza aina mpya kabisa za mimea na wanyama. Hata hivyo, wanamageuzi wana uthibitisho gani wa kuunga mkono dai lao kwamba uteuzi wa kiasili huchagua chembe bora za urithi zilizobadilika ili kutokeza spishi mpya? Broshua iliyochapishwa mnamo 1999 na Shirika la Kitaifa la Sayansi (NAS) nchini Marekani ilirejelea “spishi 13 za shore waliochunguzwa na Darwin katika Visiwa vya Galápagos, ambao leo wanaitwa shore wa Darwin.”23

      Katika miaka ya 1970, watafiti kadhaa wakiongozwa na Peter R. na B. Rosemary Grant wa Chuo Kikuu cha Princeton, walianza kuwachunguza shore hao nao wakagundua kwamba baada ya mwaka mzima wa ukame katika visiwa hivyo, kulikuwa na shore wengi zaidi wenye midomo mirefu kuliko wale wenye midomo mifupi. Kwa kuwa mojawapo ya njia za msingi za kuainisha spishi 13 za shore ni kuchunguza ukubwa na umbo la midomo yao, matokeo ya uchunguzi huo yalionwa kuwa muhimu sana. Broshua hiyo ya NAS yaendelea kusema: “Akina Grant wamekadiria kwamba ukame ukitokea mara moja kila baada ya miaka 10 katika visiwa hivyo, baada ya miaka 200 hivi tu, spishi mpya ya shore itatokea.”24

      Hata hivyo, broshua hiyo ya NAS inakosa kutaja kwamba katika miaka iliyofuata miaka ya ukame, kulikuwa na shore wengi zaidi wenye midomo mifupi. Watafiti hao waligundua kwamba jinsi hali ya hewa ilivyokuwa ikibadilika kisiwani, mwaka mmoja kulikuwa na shore wengi zaidi wenye midomo mirefu, lakini baadaye kukawa na shore wengi zaidi wenye midomo mifupi. Pia waligundua kwamba baadhi ya “spishi” hizo tofauti za shore zilizalishana kwa mtambuka na kutokeza vizazi vilivyostahimili vizuri zaidi kuliko vizazi vya awali. Walikata kauli kwamba ikiwa ndege hao wangeendelea kuzalishana kwa njia hiyo, “spishi” hizo mbili hatimaye zingeungana na kuwa spishi moja.25

      Shore wa Darwin

      Shore wa Darwin wanathibitisha jambo moja tu, kwamba wanaweza kuzoeleana na mazingira mageni

      Basi je, kwa kweli uteuzi wa kiasili hutokeza spishi mpya kabisa? Makumi ya miaka iliyopita, mtaalamu wa biolojia ya mageuzi George Christopher Williams alianza kutilia shaka ikiwa uteuzi wa kiasili unaweza kufanya hivyo.26 Mwaka wa 1999, mtaalamu wa nadharia ya mageuzi Jeffrey H. Schwartz aliandika kwamba uteuzi wa kiasili unaweza kusaidia spishi mbalimbali kubadilika kulingana na jinsi hali zinavyobadilika, lakini hautokezi chochote kipya.27

      Kwa kweli, shore wa Darwin hawajabadilika na kuwa “kitu chochote kipya.” Bado wao ni shore. Na uhakika wa kwamba shore hao wanazalishana kwa mtambuka unafanya mbinu za wanamageuzi fulani za kuainisha spishi zitiliwe shaka. Isitoshe, utafiti kuhusu ndege hao umefichua kwamba hata taasisi za kisayansi zenye kuheshimika zinaweza kuripoti matokeo ya utafiti mbalimbali zikiegemea upande mmoja.

      Dhana ya 3. Rekodi ya visukuku (mabaki ya viumbe na vitu vya kale) inathibitisha mabadiliko ya mageuzi makubwa. Broshua ya NAS iliyotajwa awali humfanya msomaji aamini kwamba visukuku ambavyo wanasayansi wamepata vinathibitisha kabisa kwamba mageuzi makubwa yalitokea. Inasema: “Visukuku vya hatua nyingi mbalimbali za mageuzi kati ya samaki na amfibia, kati ya amfibia na reptilia, kati ya reptilia na mamalia, na katika mamalia wa hali ya juu, vimegunduliwa hivi kwamba mara nyingi ni vigumu kuainisha kikamili wakati ambapo spishi moja inabadilika na kuwa spishi nyingine.”28

      Visukuu

      Ukweli wa mambo. Taarifa hiyo inayosemwa kwa usadikisho katika broshua hiyo ya NAS inashangaza sana. Kwa nini? Niles Eldredge, anayeshikilia sana fundisho la mageuzi, anasema kwamba rekodi ya visukuku haionyeshi kwamba kuna mabadiliko yanayotokea hatua kwa hatua, bali kwamba katika vipindi virefu vya wakati “ni mabadiliko madogo sana au hata hakuna mabadiliko yanayotokea katika spishi zilizo nyingi.”f29

      Kulingana na rekodi ya visukuku, vikundi vyote vikuu vya wanyama vilitokea ghafula navyo havijabadilika

      Kufikia leo, wanasayansi ulimwenguni pote wamechimbua na kurekodi visukuku vikubwa milioni 200 na mabilioni ya visukuku vidogo. Watafiti wengi wanakiri kwamba rekodi hiyo kubwa ya visukuku inaonyesha kwamba vikundi vyote vikuu vya wanyama vilitokea ghafula navyo havijabadilika sana, huku spishi nyingi zikitoweka ghafula jinsi tu zilivyotokea.

      Mageuzi—Fundisho Linalohitaji “Imani”

      Fuvu na umbo la tyrannosaurus rex

      Kwa nini wanamageuzi wengi mashuhuri hudai kwamba yale yanayoitwa mageuzi makubwa ni jambo hakika? Richard Lewontin, mtu mashuhuri anayeamini mageuzi aliandika waziwazi kwamba wanasayansi wengi hukubali kwa urahisi madai ya kisayansi ambayo hayajathibitishwa kwa sababu ya “agano ambalo tayari limefanywa, agano la uyakinifu.”g Wanasayansi wengi hukataa hata kufikiria uwezekano wa kuwa kuna Mbuni mwenye akili kwa sababu, kama Lewontin alivyoandika, “hatuwezi kumruhusu Mungu akanyage mlangoni petu.”30

      Kuhusiana na hilo, mwanasosiolojia Rodney Stark ananukuliwa katika jarida Scientific American akisema: “Wazo la kwamba ukitaka kuwa mwanasayansi lazima uepushe akili yako na minyororo ya dini limekuwa likipigiwa debe kwa zaidi ya miaka 200.” Pia anataja kwamba katika vyuo vikuu vya utafiti, “watu wenye maelekeo ya kidini hufyata midomo yao.”31

      Ikiwa unaamini fundisho la mageuzi makubwa kuwa la kweli, lazima uamini kwamba wanasayansi waagnosti au waatheisti hawawezi kamwe kuruhusu maoni yao yaathiri kauli zao wanapofanya utafiti. Lazima uamini kwamba vitu vyote vyenye uhai vilitokana na mabadiliko ya chembe za urithi na uteuzi wa kiasili, ijapokuwa utafiti ambao umefanywa kwa karne moja unaonyesha kwamba mabadiliko ya chembe hayajabadili hata spishi moja inayojulikana wazi iwe kitu kingine kipya kabisa. Lazima uamini kuwa viumbe vyote viligeuka polepole kutoka kwa kiumbe kimoja, ijapokuwa rekodi ya visukuku inaonyesha kwamba aina kuu za mimea na wanyama zilitokea ghafula na hazijabadilika na kuwa aina nyingine, hata baada ya muda mrefu sana kupita. Je, unafikiri imani kama hiyo inategemea ukweli wa mambo au dhana tu? Kwa kweli, ili kuamini mageuzi mtu anahitaji “imani.”

      a Mabadiliko katika mbwa wanaozalishwa mara nyingi hutokana na kasoro katika utendaji wa chembe za urithi. Kwa mfano, mbwa anayeitwa dachshund ana umbo dogo kwa sababu gegedu zake zimedumaa.

      b Ingawa neno “spishi” linatumiwa mara nyingi katika sehemu hii, kumbuka kwamba neno hilo halipatikani katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo. Kitabu hicho kinatumia neno “aina” ambalo lina maana pana zaidi. Mara nyingi kile ambacho wanasayansi hukiita spishi mpya ni tofauti ndogo-ndogo katika “aina” zinazozungumziwa katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo.

      c Utafiti unaonyesha kwamba uteseli, tando, na maumbile mengine ya chembe hutimiza fungu muhimu katika kutokeza umbo na utendaji wa kiumbe.

      d Lönnig anaamini kwamba uhai ulitokana na uumbaji. Maelezo yake katika broshua hii ni maoni yake mwenyewe wala hayawakilishi maoni ya taasisi ya Max Planck Institute for Plant Breeding Research.

      e Katika majaribio mengi ya kubadili chembe za urithi, idadi ya viumbe wapya ilizidi kupungua huku aina zilezile za mimea na wanyama zikitokezwa. Isitoshe, chini ya asilimia 1 ya mimea iliyotokezwa kwa kubadili chembe za urithi ndiyo iliyoteuliwa kwa ajili ya utafiti zaidi, na chini ya asilimia 1 ya mimea hiyo iliyoteuliwa ndiyo iliyofaa kwa matumizi ya kibiashara. Hata hivyo, hakuna hata spishi moja mpya kabisa iliyotokezwa. Matokeo ya utafiti uliohusisha wanyama yalikuwa duni hata kuliko yale ya mimea hivi kwamba majaribio hayo yalitupiliwa mbali.

      f Hata mifano michache kutoka katika rekodi ya visukuku ambayo watafiti wanarejelea kuwa uthibitisho wa mageuzi inaweza kuzua ubishi. Ona ukurasa wa 22 hadi 29 wa broshua, Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai, iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      g Katika muktadha huu, “uyakinifu” ni nadharia ya kwamba vitu vyote ulimwenguni, kutia ndani uhai wote, vilitokea bila nguvu zozote zisizo za kawaida kuingilia kati hata kidogo.

      Ungejibu namna gani?

      • Ungemjibu jinsi gani mtu anayedai kwamba mageuzi madogo-madogo ni uthibitisho wa kwamba mageuzi makubwa yametukia?

      • Uthibitisho wa rekodi ya visukuku kwamba spishi zilizo nyingi zilibadilika kidogo sana baada ya vipindi virefu vya wakati unaonyesha nini?

  • Sayansi na Kitabu cha Mwanzo
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Dunia na anga lenye nyota

      Sayansi na Kitabu cha Mwanzo

      Watu wengi hudai kwamba sayansi huthibitisha kwamba masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji si ya kweli. Lakini, tofauti iliyopo, si kati ya sayansi na Biblia, bali ni kati ya sayansi na vikundi vya Wakristo Wahafidhina. Baadhi ya vikundi hivyo hudai isivyo kweli kwamba kulingana na Biblia, vitu vyote viliumbwa kwa siku sita zenye urefu wa saa 24, miaka 10,000 hivi iliyopita.

      Hata hivyo, Biblia haiungi mkono dhana hiyo. Ikiwa ingekuwa hivyo basi mambo mengi ambayo yamevumbuliwa na wanasayansi katika kipindi cha miaka 100 ambayo imepita bila shaka yangethibitisha kwamba Biblia si ya kweli. Ukiichunguza kwa makini, utaona kwamba haipingani hata kidogo na mambo ya kisayansi ambayo yamethibitishwa. Kwa sababu hiyo, Mashahidi wa Yehova hawakubaliani na dhana za vikundi hivyo au wengine wenye imani kama hizo. Mambo yafuatayo yanaonyesha yale ambayo Biblia inafundisha hasa.

      Kitabu cha Mwanzo hakifundishi kwamba dunia na ulimwengu ziliumbwa katika siku sita zenye urefu wa saa 24, miaka 10,000 hivi iliyopita

      “Mwanzo” ni lini?

      Masimulizi ya kitabu cha Mwanzo yanaanza kwa taarifa hii sahili lakini yenye kujaa maana: “Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.” (Mwanzo 1:1) Wasomi kadhaa wa Biblia wanakiri kwamba taarifa hiyo inafafanua jambo tofauti na mambo yaliyofanywa katika zile siku za uumbaji zinazozungumziwa kuanzia mstari wa 3. Yaani, kulingana na maneno ya ufunguzi ya Biblia, tayari ulimwengu, kutia ndani Dunia yetu, ulikuwako kwa muda usiojulikana kabla ya siku za uumbaji.

      Wanajiolojia wanakadiria kwamba dunia imekuwako kwa muda wa miaka bilioni 4, nao waastronomia hukadiria kwamba huenda ulimwengu umekuwako kwa muda wa miaka bilioni 15. Je, mavumbuzi hayo​—na mengine yatakayovumbuliwa wakati ujao​—yanapingana na Mwanzo 1:1? Hapana. Biblia haitaji muda hususa ambao “mbingu na dunia” zimekuwako. Sayansi haipingani na mambo yanayosemwa katika Biblia.

      Urefu wa siku za uumbaji

      Siku za uumbaji zilikuwa na urefu gani? Je, zilikuwa siku halisi, zenye urefu wa saa 24? Watu fulani hudai kwamba kwa kuwa Musa, aliyeandika kitabu cha Mwanzo, alirejelea siku iliyofuata siku sita za uumbaji kuwa kigezo cha Sabato ya kila juma, kila moja ya siku za uumbaji lazima ilikuwa siku yenye urefu wa saa 24. (Kutoka 20:11) Je, maneno ya kitabu cha Mwanzo yanaunga mkono maoni hayo?

      Hapana. Mbali na kipindi cha saa 24, neno la Kiebrania linalotafsiriwa “siku” laweza pia kurejelea vipindi vyenye urefu tofauti-tofauti. Kwa mfano, akitoa muhtasari wa kazi za Mungu za uumbaji, Musa anazirejelea siku zote sita za uumbaji kana kwamba ni siku moja. (Mwanzo 2:4) Bila shaka, hakuna msingi wowote wa Kimaandiko unaoonyesha kwamba kila siku ya uumbaji ilikuwa na urefu wa saa 24.

      Hivyo basi, siku za uumbaji zilikuwa na urefu gani? Biblia haijibu; hata hivyo, maneno ya Mwanzo sura ya 1 na ya 2 yanadokeza kwamba siku zinazozungumziwa ni vipindi virefu vya wakati.

      Vipindi sita vya uumbaji

      Musa aliandika masimulizi yake katika Kiebrania, naye aliyaandika kwa njia inayopatana na maoni ya mtu aliye duniani. Mambo hayo mawili pamoja na ukweli wa kwamba ulimwengu ulikuwako kabla ya mwanzo wa vile vipindi au siku za uumbaji, yanasaidia kutatua ubishi mwingi kuhusu masimulizi ya uumbaji. Jinsi gani?

      Siku sita za uumbaji

      Matukio yaliyoanza “siku” moja yaliendelea katika “siku” ya pili au zaidi zilizofuata

      Kuchunguza kwa makini masimulizi ya kitabu cha Mwanzo kunafunua kwamba matukio yaliyoanza “siku” moja yaliendelea katika “siku” ya pili au zaidi zilizofuata. Kwa mfano, kabla ya “siku” ya kwanza ya uumbaji, mwanga wa jua, ambalo tayari lilikuwako, haukuwa ukifika duniani, labda kwa sababu ya mawingu mazito. (Ayubu 38:9) Katika “siku” ya kwanza, mawingu hayo yalianza kutanzuka na kuuruhusu mwanga upenye angani.a

      Katika “siku” ya pili, yaonekana kwamba anga lilizidi kutanzuka na kutokeza mgawanyiko kati ya mawingu mazito yaliyo juu na bahari. Katika “siku” ya nne, anga lilikuwa limetanzuka vya kutosha hivi kwamba jua na mwezi vingeweza kuonekana “katika anga la mbingu.” (Mwanzo 1:14-16) Yaani, kwa mtu aliye duniani, jua na mwezi vilianza kuonekana. Yote hayo yalitukia hatua kwa hatua.

      Pia, kulingana na masimulizi ya Mwanzo, kadiri anga lilivyozidi kutanzuka, viumbe vinavyoruka​—kutia ndani wadudu na viumbe vingine vyenye mabawa​—vilianza kuonekana katika “siku” ya tano.

      Kutokana na masimulizi ya Biblia, inawezekana kwamba matukio fulani muhimu ya kila siku, au kipindi cha uumbaji, hayakutendeka mara moja bali hatua kwa hatua, huenda hata baadhi ya matukio hayo yaliendelea hadi “siku” ya uumbaji iliyofuata.b

      Kulingana na aina yake

      Kwa kuwa mimea na wanyama walitokezwa hatua kwa hatua, je, hilo linamaanisha kwamba Mungu alitumia mageuzi kutokeza aina mbalimbali za vitu vilivyo hai? Hapana. Masimulizi yanataja waziwazi kwamba Mungu aliumba “aina” zote za msingi za mimea na wanyama. (Mwanzo 1:11, 12, 20-25) Je, “aina” hizo za awali za mimea na wanyama ziliumbwa zikiwa na uwezo wa kiasili wa kuzoeleana na mazingira mapya? Ni nini kinachomaanishwa na neno “aina”? Biblia haifafanui. Hata hivyo, inasema kwamba viumbe vyenye uhai ‘vilijaa kulingana na aina zake.’ (Mwanzo 1:21) Taarifa hiyo inadokeza kwamba kuna mipaka ya kiasili inayodhibiti tofauti za viumbe katika kila “aina.” Rekodi ya visukuku na utafiti wa karibuni zinaonyesha wazi kwamba kumekuwa na mabadiliko madogo sana katika aina za msingi za mimea na wanyama hata baada ya vipindi virefu sana vya wakati.

      Tembo, pengwini, na flamingo, wakiwa na watoto wao

      Watafiti wa siku zetu wanathibitisha kwamba viumbe vyote vyenye uhai huzaana “kulingana na aina yake”

      Tofauti na madai ya wahafidhina wa kidini, kitabu cha Mwanzo hakifundishi kwamba ulimwengu, kutia ndani dunia na viumbe vyenye uhai, uliumbwa katika kipindi kifupi cha wakati, miaka 10,000 hivi iliyopita. Badala yake, masimulizi ya Mwanzo kuhusu kuumbwa kwa ulimwengu na viumbe vyenye uhai duniani yanapatana na mavumbuzi ya karibuni ya kisayansi.

      Twiga na mtoto wake

      Kwa sababu ya imani zao za kifalsafa, wanasayansi wengi hupinga fundisho la Biblia kwamba Mungu aliumba vitu vyote. Hata hivyo, katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo kilichoandikwa zamani za kale, Musa aliandika kuwa ulimwengu ulikuwa na mwanzo na uhai ulitokezwa hatua kwa hatua, katika vipindi virefu vya wakati. Musa angewezaje kupata habari hizo zilizo sahihi kisayansi yapata miaka 3,500 hivi iliyopita? Kuna jibu moja tu linalopatana na akili. Mwenye hekima na nguvu za kuumba mbingu na dunia ndiye aliyempa Musa habari hizo zilizo sahihi kisayansi. Hilo linaunga mkono dai la Biblia kwamba ‘imeongozwa na roho ya Mungu.’c​—2 Timotheo 3:16.

      Huenda ukasema, kile ninachoamini si hoja, iwe ninaamini masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji au hapana, yote ni mamoja. Hata hivyo, fikiria sababu kadhaa zinazoonyesha uzito wa suala hilo.

      a Katika masimulizi kuhusu “siku” ya kwanza, neno la Kiebrania linalotafsiriwa mwanga ni ’ohr, linaloweza kurejelea mwanga wowote ule, lakini kuhusu “siku” ya nne, neno lililotumiwa ni ma·’ohrʹ, linalorejelea chanzo cha mwanga..

      b Kwa mfano, katika siku ya sita ya uumbaji, Mungu aliagiza kwamba wanadamu ‘wawe wengi waijaze dunia.’ (Mwanzo 1:28, 31) Hata hivyo, hilo lilianza kutimia katika “siku” inayofuata.​—Mwanzo 2:2.

      c Unaweza kupata habari zaidi kwa kutazama video fupi yenye kichwa Tunawezaje Kuwa na Hakika Kwamba Yale Yaliyoandikwa Katika Biblia ni ya Kweli? inapatikana kwenye jw.org/sw.

      Samaki ndani ya matumbawe

      Ungejibu namna gani?

      • Watu fulani huamini mambo gani yasiyo ya kweli kuhusu masimulizi ya Biblia ya uumbaji?

      • Kwa nini hatuwezi kupuuza uhakika wa kwamba Biblia na sayansi zinapatana katika mambo mengi?

  • Imani Yako ni Jambo la Kuhangaikiwa?
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
    • Imani Yako ni Jambo la Kuhangaikiwa?

      Unafikiri maisha yana kusudi? Mwana-mageuzi William B. Provine anasema: “Mambo ambayo tumejifunza kuhusu mageuzi yamekuwa na matokeo makubwa kwetu, yanaathiri maoni yetu kuhusu kusudi la maisha.” Alikata kauli gani? “Sioni kusudi lolote la mwanadamu wala ulimwengu.”32

      Binti

      Fikiria uzito wa maneno hayo. Ikiwa maisha hayana kusudi lolote, basi kuwa kwako hai hakuna kusudi lolote isipokuwa labda tu kufanya mema kidogo na ikiwezekana kuachia vizazi vijavyo sifa na tabia zako. Kisha ukifa, umetoweka milele. Ubongo wako, pamoja na uwezo wake wa kufikiri na kutafakari kusudi la maisha, ungekuwa tu tokeo la matukio yasiyo na mpangilio wowote.

      Isitoshe, watu wengi wanaoamini mageuzi hudai kwamba hakuna Mungu au kwamba hataingilia mambo ya wanadamu. Vyovyote vile, wakati wetu ujao ungetegemea viongozi wa kisiasa, kielimu, na kidini. Tukizingatia jinsi ambavyo wamekuwa wakijiendesha, basi hakungekuwa na mwisho wa machafuko, mapigano, na ufisadi ambao umeikumba jamii ya wanadamu. Ikiwa kwa kweli fundisho la mageuzi ni la kweli, basi kungekuwa na sababu za kuishi kulingana na kauli-mbiu hii hatari: “Tule na tunywe, kwa maana kesho tutakufa.”—1 Wakorintho 15:32.

      Tofauti na hilo, Biblia inafundisha kwamba kwa Mungu “iko chemchemi ya uzima.” (Zaburi 36:9) Maneno hayo yanastahili kufikiriwa kwa uzito.

      Ikiwa yale ambayo Biblia inasema ni kweli, basi maisha yana kusudi. Muumba wetu ana kusudi lenye upendo kwa ajili ya wale wanaochagua kuishi kulingana na mapenzi yake. (Mhubiri 12:13) Kusudi hilo linatia ndani ahadi ya kuishi katika ulimwengu mpya usio na machafuko, mapigano, ufisadi, wala kifo.—Zaburi 37:10, 11; Isaya 25:6-8.

      Wakiwa na sababu nzuri, mamilioni ya watu ulimwenguni pote wanaamini kwamba kujifunza kumhusu Mungu na kumtii huwapa kusudi halisi maishani! (Yohana 17:3) Imani hiyo si ndoto. Kuna uthibitisho mwingi wa kwamba uhai uliumbwa.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki