-
TelevisheniAmkeni!—2010 | Machi
-
-
Televisheni
MUDA fulani baada ya wanadamu kujifunza kupeperusha sauti kwa kutumia redio, wavumbuzi walijiuliza ikiwa pia wangeweza kupeperusha picha za moja kwa moja. Ili uelewe kwa nini jambo hilo ni gumu, fikiria jinsi televisheni inavyofanya kazi leo.
Kwanza, kamera ya video hupiga picha na kuituma kwenye kifaa fulani kilicho na uwezo wa “kusoma” picha hiyo, kama tu unavyofanya unaposoma kitu kilichochapishwa. Hata hivyo, badala ya kusoma herufi, inasoma madoa (au pikseli) katika picha. Kisha inabadili chochote inachoona kuwa mawimbi ya video yanayoweza kutumwa mahali pengine. Mawimbi hayo yanapopokewa kwenye kipokezi, yanabadilishwa kuwa picha.
Inasemekana kwamba John Logie Baird kutoka Scotland, ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuonyesha jinsi televisheni inavyofanya kazi. Baird ambaye alikuwa injinia wa vifaa vya umeme aliacha kazi yake kwa sababu ya ugonjwa na kuanza kufuatilia jambo lililokuwa limempendeza tangu alipokuwa kijana, yaani, kubuni mashini ambayo ingeweza kuonyesha picha moja kwa moja.
Kamera ya televisheni ya Baird ilitumia diski iliyokuwa na matundu 30 yaliyopangwa kwa mzunguko. Diski hiyo ilipozunguka, matundu hayo yalipita yakichunguza kila sehemu ya picha na kuruhusu mwangaza upite juu ya betri inayopata umeme kutokana na mwanga. Betri hiyo ilitoa mawimbi ya video yaliyotumwa kwenye kipokezi. Kwenye kipokezi hicho, mawimbi hayo yaliongezwa ukubwa na kutokeza mwangaza nyuma ya diski nyingine inayozunguka kutokeza picha hiyo. Changamoto kubwa ilikuwa kufanya diski hizo zizunguke kwa upatano. Baird alipokuwa akishughulikia mradi huo, alijiruzuku kwa kupiga viatu rangi.
Oktoba 2, 1925 (2/10/1925) Baird alipeperusha picha za kwanza za televisheni kutoka mwisho mmoja wa dari lake hadi ule mwingine. Mtu wa kwanza kuonekana katika televisheni alikuwa kijana aliyekuwa na wasiwasi mwingi sana ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye ofisi iliyokuwa kwenye orofa ya chini ya nyumba ya Baird. Alishurutishwa kufanya hivyo baada ya kuahidiwa kuwa angelipwa shilingi mbili na senti sita za Scotland. Mnamo 1928, Baird alipeperusha picha za kwanza za televisheni hadi ng’ambo ile nyingine ya Bahari ya Atlantiki. John Baird alipowasili huko New York, alishangaa sana alipokaribishwa kwa mbwembwe za bendi ya wapiga zumari. Sasa alikuwa mtu maarufu. Lakini je, yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kupeperusha picha moja kwa moja?
-
-
Vitu vya Asili Vilitangulia vya WanadamuAmkeni!—2010 | Machi
-
-
Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
“Sikio lenye kusikia na jicho lenye kuona—Yehova ndiye aliyevifanya vyote viwili.”—Methali 20:12.
MACHO yako ni kama kamera ndogo za televisheni. Yanabadili picha kuwa mawimbi na kuyatuma kupitia neva ya jicho hadi nyuma ya ubongo wako ambako mawimbi hayo hubadilika tena kuwa picha halisi.
Jicho ni lenye kustaajabisha na limeundwa kwa akili nyingi sana hata ingawa ni dogo sana. Lina kipenyo cha milimita 24 na uzito wa gramu 7.5. Kwa mfano, jicho lina mifumo tofauti ya kuliwezesha kuona mahali palipo na mwangaza mdogo na mwangaza mwingi hivi kwamba dakika 30 baada ya kuingia katika chumba kilicho na giza, macho yako yanaanza kuathiriwa na nuru mara 10,000 zaidi ya kawaida.
Unapokuwa mahali penye mwangaza wa kawaida, ni nini kinachokusaidia kuona vizuri? Jicho lako lina chembe zenye uwezo wa hali ya juu wa kutambua mwangaza mara 100 kuliko uwezo wa kamera nyingi za video. Pia, nyingi ya chembe hizo zimehifadhiwa katika sehemu ndogo katikati ya retina inayoitwa fovea, ambayo ndiyo sehemu inayoona vizuri zaidi. Kwa kuwa unatazama mahali mbalimbali mara kadhaa kwa sekunde, unaweza kuona kila kitu vizuri. Kwa kushangaza, fovea ya jicho lako ina ukubwa unaokaribia kulingana na kituo kilicho mwishoni mwa sentensi hii.
Mawimbi kutoka kwenye chembe zenye uwezo wa hali ya juu wa kutambua mwangaza hupita kutoka kwenye chembe moja ya neva hadi kwenye neva ya jicho. Lakini chembe hizo hazipitishi tu mawimbi hayo. Zinachanganua habari hiyo, kuboresha habari muhimu na kuchuja habari isiyohitajika.
Sehemu ya ubongo ambayo hupokea habari kutoka kwa jicho ili tuweze kuona, hufanya kazi kama kipokezi cha video cha hali ya juu. Inaboresha picha kwa kuzifanya sehemu zote zionekane vizuri na kulinganisha mawimbi kutoka kwa chembe ambazo hutambua zile rangi za msingi, hivyo unaweza kutofautisha mamilioni ya rangi. Ubongo wako pia hulinganisha tofauti ndogo sana ambazo macho yako mawili yanaona ili uweze kutambua umbali kati ya vitu.
Fikiria jinsi macho yako yanavyotazama nyuso katika umati wa watu walio mbali na kutuma habari kwenye ubongo wako ambao hubadili habari hiyo kuwa picha. Pia, fikiria jinsi habari hususa kuhusu nyuso hizo inavyolinganishwa na habari zilizo katika kumbukumbu yako hivi kwamba unaweza kumtambua rafiki yako mara moja. Je, hilo si jambo lenye kustaajabisha?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Njia ambayo jicho huchanganua habari inaonyesha kwamba akili nyingi ilitumika kulibuni
-