-
Ramani ya ElektronikiAmkeni!—2010 | Machi
-
-
Ramani ya Elektroniki
BILA shaka inaweza kuwa vigumu kwako kujua unakoelekea ukiwa katika mji usioufahamu. Kwa hiyo, baharia atajuaje anakoelekea kwa kuwa baharini hakuna alama zozote za kumwongoza? Kuwa tu na dira hakuwezi kumsaidia isipokuwa awe anajua mahali alipo na anapoelekea. Katika miaka ya 1730, mabaharia walianza kutambua mahali hususa walipo na kuamua ni njia gani watakayofuata kwenye ramani, baada ya kubuniwa kwa chombo kinachopima umbali wa jua au nyota kutoka kwenye upeo wa macho (sextant) na kifaa kinachosaidia kutambua mahali meli ilipo baharini. Lakini walitumia saa nyingi kupiga hesabu hiyo.
Leo madereva katika nchi nyingi hutumia vifaa visivyogharimu sana vilivyounganishwa na Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti (GPS). Unachohitaji kufanya ni kuingiza habari kuhusu mahali unapoelekea. Kifaa hicho kinaweza kukuonyesha mahali hususa unapotaka kwenda. Kisha kitakuelekeza huko. Mfumo huo unafanya kazi kwa njia gani?
Vifaa hivyo hutegemea setilaiti 30 hivi. Kila setilaiti hutuma habari ikionyesha mahali ilipo na kuonyesha saa kwa muda mfupi usiozidi sekunde moja. Mara tu kifaa chako kinapounganishwa na setilaiti kadhaa, kinapima kwa usahihi muda ambao habari hiyo inachukua kutoka kwenye setilaiti hadi kwenye kifaa chako. Kinapofanya hivyo, kinatambua mahali ulipo. Je, unaweza kuwazia jinsi hesabu hiyo ilivyo tata? Katika muda wa sekunde chache tu, kinapima umbali kati ya setilaiti tatu, zote zikiwa mbali sana na zikielekea upande tofauti kwa mwendo wa kasi sana.
Maprofesa Bradford Parkinson na Ivan Getting walibuni mfumo huo wa setilaiti mwanzoni mwa miaka ya 1960. Ingawa mwanzoni mfumo huo ulibuniwa ili utumiwe na jeshi, baadaye ulianza kutumiwa na kila mtu kufikia mwaka wa 1996. Kifaa cha kupokea habari kutoka kwenye setilaiti ni uthibitisho mkubwa wa maendeleo ya tekinolojia ya kompyuta, lakini je, hiyo ndiyo tekinolojia ya kwanza ya aina yake?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Globe: Based on NASA photo
-
-
Vitu vya Asili Vilitangulia vya WanadamuAmkeni!—2010 | Machi
-
-
Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
“Hata korongo juu mbinguni—anajua vema nyakati zake zilizowekwa.”—Yeremia 8:7.
MIAKA 2,500 hivi iliyopita, Yeremia aliandika kuhusu korongo anayehama-hama. Leo, bado watu wanastaajabia viumbe ambao huhamahama, kama vile samoni wanaoweza kuogelea maelfu ya kilomita baharini na kurudi kwenye mto ambako walizaliwa, na kasa aliye na ngozi laini mgongoni ambaye anaweza kusafiri mbali sana pia. Kasa mmoja ambaye alitaga mayai yake huko Indonesia alifuatwa aliposafiri kilomita 20,000 hadi ufuo wa Oregon nchini Marekani. Mara nyingi, kasa hao hurudi kwenye eneo hilohilo la Indonesia kutaga mayai yao.
Viumbe wengine wanaweza kujua mahali makao yao yalipo kwa usahihi, jambo ambalo ni lenye kustaajabisha sana kuliko tu kusafiri kutoka mahali pamoja hadi pengine kisilika. Kwa mfano, wachunguzi walibeba albatrosi 18 kwa ndege kutoka kwenye kisiwa kidogo katikati ya Bahari ya Pasifiki na kuwapeleka kwenye maeneo kadhaa maelfu ya kilomita kutoka huko halafu wakawaachilia. Wengine waliachiliwa karibu na ukingo wa magharibi wa bahari hiyo na wengine karibu na ukingo wa mashariki. Baada ya majuma machache, ndege wengi walikuwa wamerudi nyumbani.
Hua wamesafirishwa zaidi ya kilomita 150 hadi mahali ambako hawajui wakiwa wamedungwa sindano ya kuwafanya walale au wakiwa ndani ya mapipa yanayozunguka, lakini baada ya kuzunguka mara kadhaa, walitambua mahali walipo na wakageuka na kurudi nyumbani moja kwa moja. Kwa kuwa hua wanaweza kutambua jinsi ya kufika nyumbani hata wakiwa wamevishwa vioo vinavyowazuia kuona, watafiti wanaamini kwamba wao hukadiria mahali walipo na wanapoelekea kwa kutambua uvutano fulani unaowaongoza wanakoelekea.
Vipepeo wanaoitwa monarch kutoka maeneo mbalimbali ya Amerika Kaskazini husafiri kwa maelfu ya kilomita hadi sehemu ndogo ya Mexico. Hata ingawa hawajawahi kwenda Mexico tena, wao hutambua wanakoelekea, na mara nyingi wao hutua kwenye miti ambayo mababu zao walitua mwaka uliotangulia. Jambo hilo bado linawashangaza watafiti.
Tofauti na vifaa vya kutuongoza vinavyotegemea hasa habari kutoka kwa setilaiti, wanyama wengi hutumia njia mbalimbali za kutambua mahali walipo na wanapoelekea—iwe ni kutazama alama za dunia, jua, kutambua nguvu za sumaku za dunia, kunusa harufu fulani za pekee, na hata sauti. Profesa wa biolojia James L. Gould anaandika hivi: “Wanyama ambao maisha yao hutegemea kufuata ramani sahihi wamebuniwa kwa ustadi sana. . . . Wamebuniwa wakiwa na mbinu nyingine za kutumia ili kutambua walipo na wanapoelekea ikitegemea ni mbinu gani inayotoa habari zenye kutegemeka zaidi.” Bado watafiti wanashangazwa na utata wa ramani zinazowaongoza wanyama.
-