Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
    Amkeni!—2005 | Machi 8
    • Mamba wa Maji ya Chumvi

      Mamba wa maji ya chumvi ndio wanyama wakubwa zaidi wanaotambaa, kwani wanaweza kufikia urefu wa meta 7 au zaidi, na uzito wa kilo 1,000 hivi. Kwa kuwa wao huishi hasa katika maji ya chumvi, wao hupatikana katika vinamasi vya mikoko kwenye pwani, milango ya mito, na bahari, kuanzia India kuelekea mashariki huko Fiji. Wao hula nyama tu. Mamba hao hula panya, vyura, samaki, nyoka, kaa, kasa, na mbawala kwa kiasi kidogo. Mamba-dume wakubwa hula kati ya gramu 500 na 700 za chakula kwa siku. Hawahitaji nguvu nyingi kwa kuwa wao hutumia muda mrefu wakiota jua na kuelea majini na wana mfumo mzuri wa kusaga chakula. Mara kwa mara mamba hao huwashambulia wanadamu. Wao huogelea kwa kupepesa mkia wao huku wakiwa wamezamisha miili yao isipokuwa pua na macho. Wao hutumia miguu yao mifupi kutembea. Wanaweza kuruka ili kukamata windo, na nyakati nyingine hukimbiza windo lao. Sawa na mamba wengine, mamba hao wana uwezo mzuri wa kunusa, kuona, na kusikia. Wakati wa kujamiiana, mamba-dume hulinda eneo lake kwa ukali, naye mamba-jike huyalinda mayai yake kwa ukali pia.

      Mama Wanaojitoa Mhanga

      Mamba wa kike hutengeneza mahali pa kutagia karibu na maji, naye hupafanyiza kwa rundo la matope na majani yanayooza. Yeye hutaga karibu mayai 100 magumu, kisha huyafunika na kuyalinda kutokana na wavamizi. Halafu yeye huyamwagilia maji ili kufanya majani yaoze haraka, na hivyo kutokeza joto linalohitajiwa ili yaanguliwe.

      Kisha jambo fulani la ajabu hutukia. Jinsia ya mtoto hutegemea joto linalokuwapo wakati yai limefunikwa kwa majani. Hilo ni jambo la ajabu sana! Kunapokuwa na joto la nyuzi 28 Selsiasi hadi nyuzi 31 Selsiasi mamba-jike hutokezwa baada ya siku 100 hivi, na kunapokuwa na joto la nyuzi 32.5 Selsiasi mamba-dume hutokezwa katika kipindi cha siku 64 hivi. Mayai yanayopata joto la nyuzi 32.5 Selsiasi hadi nyuzi 33 Selsiasi yanaweza kutokeza mamba-dume au mamba-jike. Iwapo upande mmoja wa mahali pa kutagia uko kando ya maji na upande ule mwingine uko upande wa jua, mayai yaliyoko upande wenye joto yatatokeza mamba-dume, huku mayai yaliyoko upande usio na joto yakitokeza mamba-jike.

      Mamba-jike anaposikia sauti ndogo-ndogo zikitoka mahali hapo pa kutagia, yeye huondoa majani na matope, na nyakati nyingine yeye huyavunja mayai iwapo watoto hawajafanya hivyo kwa kutumia jino lao la kuvunjia yai. Yeye huwainua polepole kwa kutumia mataya yake makubwa na kuwabeba ndani ya kifuko kilicho chini ya ulimi wake hadi kando ya maji. Kwa kuwa watoto wa mamba hujitegemea mara tu wanapoanguliwa, wao huanza kutafuta wadudu, vyura, na samaki wadogo. Hata hivyo, mamba-jike fulani huwalinda watoto wao kwa kukaa karibu nao kwa miezi kadhaa, huku wakitenga sehemu fulani kwenye vinamasi ambako mamba-dume hushiriki kuwatunza na kuwalinda.

  • Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
    Amkeni!—2005 | Machi 8
    • [Picha katika ukurasa wa 11]

      Mamba wa maji ya chumvi

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Mamba-jike wa maji ya chumvi akimbeba mtoto wake kwa mataya yake

      [Hisani]

      © Adam Britton, http://crocodilian.com

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki