Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mfalme Daudi na Muziki
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Desemba 1
    • Mfalme Daudi na Muziki

      MTU ambaye hutukumbusha kuhusu muziki wa nyakati za Biblia ni Daudi, mwanamume wa pekee aliyeishi miaka 3,000 iliyopita. Kwa kweli, mambo mengi ambayo tunajua kuhusu muziki wa nyakati hizo unatokana na rekodi ya Biblia ya maisha ya Daudi—kutoka wakati alipokuwa kijana mchungaji hadi alipokuwa mfalme mwenye uwezo wa kupanga mambo.

      Kuna mambo mengi ambayo tunaweza kujifunza kutokana na muziki wa nyakati za Biblia kupitia Daudi. Kwa mfano, ni ala gani za muziki walizotumia, na waliimba nyimbo gani? Muziki ulikuwa na sehemu gani katika maisha ya Daudi na kwa taifa la Israeli kwa ujumla?

  • Mfalme Daudi na Muziki
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Desemba 1
    • Mwanamuziki wa Kipekee

      Daudi alikuwa mwanamuziki wa kipekee kwa kuwa alikuwa mwimbaji na pia mtungaji wa mashairi. Inasemekana kwamba zaidi ya nusu ya Zaburi zilitungwa na Daudi. Alipokuwa mvulana, alikuwa mchungaji na akili yake yenye utambuzi na ufahamu wa hali ya juu ilihifadhi habari nyingi kuhusu maeneo ya malisho ya Bethlehemu. Alikuwa amefurahia kusikia sauti ya vibubujiko vya maji na sauti ya wana-kondoo wanapojibu anapowaita. Akivutiwa na umaridadi wa sauti hizo zilizomzunguka, alichukua kinubi chake na kuanza kumsifu Mungu kwa sauti. Lazima iwe ilipendeza kusikia muziki wa Daudi alipoimba Zaburi ya 23.

      Akiwa kijana, Daudi alicheza kinubi vizuri sana hata akapendekezwa kwenda kumchezea Mfalme Sauli. Sauli alipokuwa amefadhaika sana na kusumbuka kiakili, Daudi alicheza muziki mzuri kwa kinubi chake ulioutuliza moyo wa Sauli. Mawazo mabaya aliyokuwa nayo yaliondoka na akaacha kusumbuka kiakili.—1 Samweli 16:16.

      Muziki, ambao Daudi alipenda sana na uliomletea furaha, wakati mwingine ulimletea matatizo. Siku moja, Daudi na Sauli waliporudi kutoka vitani baada ya kuwashinda Wafilisti, mfalme muziki wa ushindi na wenye furaha. Wanawake walikuwa wakiimba hivi: “Sauli amepiga maelfu yake, na Daudi makumi ya maelfu yake.” Jambo hilo lilimkasirisha Sauli sana na kumfanya awe na wivu hivi kwamba “akawa akimtilia Daudi shaka tangu siku hiyo na kuendelea.”—1 Samweli 18:7-9.

      Muziki Ulimchochea Daudi

      Muziki wa Daudi ulioongozwa na roho takatifu, ulikuwa bora katika njia nyingi. Nyimbo zake zinatia ndani zaburi za mambo aliyokuwa ametafakari na maisha ya uchungaji. Zinatia ndani sifa na hadithi, shangwe ya mavuno ya zabibu na shamrashamra za kuwekwa wakfu kwa makao ya mfalme, kumbukumbu na nyimbo za tumaini, maombi na sihi. (Ona Zaburi 32, 23, 145, 8, 30, 38, 72, 51, 86 na maandishi ya utangulizi ya zaburi hizi.) Sauli na mwana wake Yonathani walipokufa, Daudi alitunga wimbo wa kuomboleza ulioitwa: “Upinde,” ulioanza kwa maneno haya: “Ee Israeli, uzuri umeuawa katika mahali pako pa juu.” Wimbo huo uliimbwa kwa sauti ya huzuni. Daudi alijua jinsi ya kueleza hisia mbalimbali, kwa maneno na pia kwa kinubi.—2 Samweli 1:17-19.

      Kwa sababu ya utu wake mchangamfu, Daudi alipenda nyimbo zenye furaha zinazochangamsha na miziki yenye midundo yenye kupendeza. Alipoleta sanduku la agano hadi Sayuni, Daudi alirukaruka na kucheza dansi kwa nguvu zake zote ili kusherehekea pindi hiyo. Simulizi hilo la Biblia linaonyesha kuwa huenda muziki huo ulikuwa wenye kusisimua sana. Je, unaweza kuwazia pindi hiyo? Mke wake Mikali alianza kumdhihaki. Daudi hakujali jambo hilo. Alimpenda Yehova, na muziki huo uliomfanya awe na shangwe nyingi sana, ulimchochea arukeruke mbele ya Mungu wake.—2 Samweli 6:14, 16, 21.

      Isitoshe, Daudi alijulikana kwa kutengeneza ala mpya za muziki. (2 Mambo ya Nyakati 7:6) Kwa ujumla, Daudi alikuwa msanii mwenye kipawa, kwa kuwa alikuwa mtengenezaji wa ala za muziki, mshairi, mtungaji, na mtumbuizaji. Hata hivyo, Daudi alifanya mambo makubwa hata zaidi.

      Muziki na Uimbaji Katika Hekalu

      Daudi hukumbukwa kwa kuwa yeye ndiye aliyepanga uimbaji na muziki katika nyumba ya Yehova. Alikuwa na waimbaji na wanamuziki 4,000 waliosimamiwa na Asafu, Hemani, na Yeduthuni (ambaye pia huenda aliitwa Ethani). Daudi aliwaweka chini ya wataalamu 288 ambao waliwafunza na kuwaongoza. Wanamuziki na waimbaji hao 4,000 walikuwepo wakati wa sherehe tatu kubwa zilizofanywa kila mwaka. Hebu wazia kwaya hiyo kubwa yenye kuvutia!—1 Mambo ya Nyakati 23:5; 25:1, 6, 7.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki