Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kupoteza Kiungo cha Mwili—Je, Waweza Kupatwa na Hali Hiyo?
    Amkeni!—1999 | Juni 8
    • Kupoteza Kiungo cha Mwili—Je, Waweza Kupatwa na Hali Hiyo?

      Benjamin alikuwa nje akifurahia jua lililoangaza jiji la Sarajevo wakati wa majira ya kuchipua, alipokanyaga bomu lililotegwa ardhini. Mguu wake wa kushoto ulilipuliwa. “Nilijaribu kusimama,” Benjamin akumbuka. “Nikashindwa.” Benjamin ni mmojawapo wa watu 20,000 wanaokufa au kulemazwa kila mwaka kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini.

      MABOMU ya kutegwa ardhini yapatayo milioni 15 yametapakaa katika nchi ya Angola—zaidi ya bomu moja kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto katika nchi hiyo. Sasa Angola ina watu 70,000 ambao wamepoteza kiungo fulani cha mwili. Nchi ya Kambodia, ambayo ina mabomu yaliyotegwa ardhini yapatayo milioni nane hadi kumi, ina uwiano mkubwa zaidi ulimwenguni wa watu waliopoteza viungo fulani vya mwili—inakadiriwa kuwa mtu 1 kati ya kila 236 hana kiungo fulani cha mwili. Imeripotiwa kwamba Bosnia na Herzegovina ina zaidi ya mabomu milioni tatu yaliyotegwa ardhini—mabomu 152 katika kila eneo la kilometa 59 za mraba.

      Lakini si katika nchi zenye vita tu ambako watu hupoteza viungo vya mwili. Kwa mfano, huko Marekani watu wapatao 400,000 wamepoteza viungo fulani vya mwili. Kinachowafanya watu wazima wengi kati ya idadi hiyo wapoteze viungo vya mwili ni maradhi sugu ambayo kwa ujumla yanaitwa “maradhi ya mishipa,” au PVD. Neno hili lawakilisha magonjwa mbalimbali. Kamusi ya Taber’s Cyclopedic Medical Dictionary hueleza PVD kuwa neno la ujumla linalotia ndani “maradhi ya ateri na vena za miisho ya mwili, hasa maradhi yanayoathiri mzunguko wa damu kwenye miisho ya mwili.” Kisababishi kikuu cha PVD ni ugonjwa wa kisukari. Kulingana na The World Health Report 1998, “idadi ya watu wazima wenye kisukari ulimwenguni pote itaongezeka zaidi ya maradufu kutoka milioni 143 mwaka wa 1997 hadi milioni 300 mwaka wa 2025.”

      Huko Marekani, majeraha—yanayosababishwa na aksidenti za magari, mashine, vifaa vya umeme, na bunduki—ndiyo kisababishi kikuu cha pili cha kupoteza viungo vya mwili, yakisababisha asilimia 20 hadi 30 ya visa vyote vya kukatwa viungo vya mwili. Visababishi vingine vya kupoteza viungo vya mwili hutia ndani uvimbe (takriban asilimia 6) na kasoro za kuzaliwa (takriban asilimia 4).

      Wazo la kupoteza kiungo muhimu cha mwili ni baya sana. Je, kuna njia yoyote ya kupunguza hatari hiyo? Na ikiwa tayari umepoteza kiungo cha mwili, unawezaje kufurahia maisha bora? Makala zifuatazo zinazungumzia swali hili na mengineyo.

  • Kupoteza Kiungo cha Mwili—Jinsi Uwezavyo Kupunguza Hatari Hiyo
    Amkeni!—1999 | Juni 8
    • Kupoteza Kiungo cha Mwili—Jinsi Uwezavyo Kupunguza Hatari Hiyo

      VISA vingi vya kupoteza viungo vya mwili vyaweza kuzuiwa! Na ndivyo ilivyo hata kwa watu wanaougua maradhi ya mishipa (PVD). Kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, mara nyingi PVD husababishwa na ugonjwa wa kisukari.a Kwa uzuri, ugonjwa wa kisukari unaweza kudhibitiwa.

      “Mlo ni muhimu sana katika kutibu ugonjwa wa kisukari iwe umeagizwa utumie insulini au la,” kichapo The Encyclopædia Britannica chasema. Dakt. Marcel Bayol, wa Kings County Hospital huko New York City, aliliambia gazeti la Amkeni! hivi: “Ikiwa watu wenye kuugua kisukari wanakuwa waangalifu kwa hali yao, na kuzingatia mlo wao, na kufuata mwelekezo wa kitiba, watapunguza hatari ya kupoteza kiungo cha mwili.” Wale walio na ugonjwa wa kisukari kisichohitaji insulini na ambao hufuata shauri hili huenda wakapata nafuu baada ya muda.b

      Mazoezi Ni Muhimu

      Mazoezi ni muhimu pia. Mazoezi husaidia mwili kudumisha vipimo vya glukosi, au sukari katika viwango vya kawaida. Ugonjwa wa PVD unapogunduliwa, kufanya mazoezi husaidia kudumisha nguvu, miendo, na mzunguko wa damu kwenye sehemu zenye madhara. Mazoezi pia husaidia kupunguza maumivu makali kwenye misuli ya shavu la mguu—maumivu ambayo huenda yakahisiwa na wale wanaougua PVD wanapotembea au kufanya mazoezi. Hata hivyo, wenye maradhi haya wanapaswa kuepuka kufanya mazoezi yanayokaza na kushtua miguu. Mazoezi yanayofaa zaidi yanatia ndani matembezi, kuendesha baiskeli, kupiga makasia, kuogelea, na mazoezi ya majini yanayofanya upumue kwa kasi. Mtu apaswa kupata ushauri wa daktari kabla ya kufuata utaratibu maalum wa mlo au mpango maalum wa kufanya mazoezi.

      Bila shaka, mtu yeyote anayetaka kuwa na afya njema ataepuka kuvuta sigareti. PVD ni mojawapo tu ya magonjwa mengi yanayosababishwa au kuzidishwa na uvutaji wa sigareti. “Uvutaji wa sigareti ni kisababishi kikuu cha kukatwa viungo, hasa ikiwa mvutaji anaugua kisukari na PVD,” asema Dakt. Bayol. Huchangia kwa kadiri gani? Kichapo kimoja cha kuwasaidia waliokatwa viungo vya mwili waishi maisha ya kawaida chasema kwamba “uwezekano wa wavutaji wa sigareti kukatwa kiungo cha mwili ni mara 10 zaidi ya wale wasiovuta sigareti.”

      Kutunza Viungo vya Mwili Vinavyougua

      Maradhi ya PVD yanaweza kupunguza mzunguko wa damu kwenye viungo vya mwili, hali inayoweza kutokeza ugonjwa unaoitwa neuropathy—kufa, au kufa ganzi kwa neva. Hivyo basi viungo vya mwili huwa katika hatari ya kujeruhiwa, hata wakati ambapo mtu anapumzika tu kitandani. Kwa mfano, kwa kuwa mgonjwa hawezi kuhisi maumivu yoyote, anaweza kuchomeka vibaya sana iwapo blanketi yake ya umeme au kitu chenye kupasha joto kitatoa joto jingi kupita kiasi! Hiyo ndiyo sababu watengenezaji wa vifaa hivyo huwatahadharisha wanaougua kisukari wawe waangalifu wanapotumia vifaa hivyo.

      Viungo vya mwili vinavyougua pia huweza kuambukizwa kwa urahisi. Mkwaruzo mdogo tu waweza kutokeza vidonda, au hata sehemu hiyo kuoza. Hivyo utunzaji wa miguu ni muhimu, na hii hutia ndani kuvaa viatu visivyofinya na vinavyotoshea vizuri na kudumisha miguu na nyayo zikiwa safi na kavu. Hospitali nyingi zina kliniki za kutibu miguu ambazo huwaelimisha wagonjwa juu ya utunzaji wa miguu.

      Wakati ambapo maradhi ya PVD yamefikia hali ambayo inahitaji upasuaji, kwa kawaida madaktari wapasuaji hujaribu kuepuka kukata kiungo cha mwili. Mojawapo ya tiba ya badala ni katheta ya puto. Daktari wa mishipa huingiza katheta iliyo na ncha yenye puto. Hewa huingizwa katika puto, na kisha puto hupanua mishipa iliyoziba. Tiba nyingine ni upasuaji wa kuondoa mishipa ya damu iliyoharibiwa na ugonjwa na mahali pake kuweka mishipa iliyotolewa sehemu nyingine ya mwili.

      Barbara, mwenye umri wa miaka 54, amevumilia ugonjwa wa kisukari kinachohitaji insulini tangu alipokuwa na umri wa miaka minne. Baada ya kujifungua mtoto wa kwanza, miguu yake ilishikwa na maradhi ya PVD. Baadhi ya madaktari walimshauri akatwe miguu hiyo. Hata hivyo, Barbara alimpata daktari mashuhuri wa mishipa aliyetumia mbinu ya katheta yenye puto kuboresha mzunguko wa damu kwenye miguu yake. Mbinu hiyo ilifanikiwa kwa muda fulani, lakini hatimaye Barbara alihitaji kufanyiwa upasuaji wa kubadili mshipa, ambao ulifaulu. Sasa Barbara hutunza miguu yake kwa uangalifu sana.

      Epuka Jeraha

      Jeraha ni kisababishi cha pili cha kupoteza viungo vya mwili. Kwa kuwa jeraha halichagui kiungo fulani hususa cha mwili, hilo laweza kuharibu sehemu yoyote ya mwili. Hata hivyo, kuwa na maoni ya kimungu juu ya maisha kwaweza kupunguza sana hatari ya mtu kujeruhiwa. Wakristo wanapaswa kuiona miili yao kuwa zawadi kutoka kwa Mungu, wawe wanafanya kazi, wanaendesha gari, au wanafurahia tafrija. Hivyo, watatii matakwa yote ya usalama na kuepuka kuhatarisha maisha yao kwa upumbavu.—Waroma 12:1; 2 Wakorintho 7:1.

      Ni hatua gani zinazochukuliwa ili kupunguza hatari ya kujeruhiwa katika nchi zenye mabomu yaliyotegwa ardhini? Serikali nyingi zimefadhili mipango ya kuwaelimisha watu kuhusu hatari za mabomu ya kutegwa ardhini. Kulingana na ripoti ya katibu-mkuu wa Umoja wa Mataifa, mipango hii huelimisha “watu walio hatarini . . . jinsi ya kupunguza hatari za kuyakanyaga wanapoishi na kufanya kazi katika maeneo yenye mabomu hayo.”

      Kwa kusikitisha, “watu huzoea kuishi kwenye sehemu za mabomu yaliyotegwa ardhini na kuanza kuyapuuza,” yasema ripoti moja ya Umoja wa Mataifa. “Nyakati nyingine mawazo ya kidini huwatia [watu] moyo wawe na maoni ya kwamba mambo kama haya ni mipango ya Mungu.” Hata hivyo, Neno la Mungu haliungi mkono maoni ya kwamba hiyo ni mipango ya Mungu. Kinyume na hilo, Biblia huwatia watu moyo wazingatie tahadhari na usalama.—Kumbukumbu la Torati 22:8; Mhubiri 10:9.

      Hivyo, kwa kutahadhari na kuchukua hatua zinazofaa kulinda afya yako, unaweza kupunguza sana hatari ya kupoteza kiungo cha mwili. Lakini namna gani wale ambao tayari wamepoteza viungo? Je, bado wanaweza kufurahia maisha bora?

      [Maelezo ya Chini]

      a Maradhi ya mishipa ya sehemu za chini kabisa za mwili yanaweza pia kusababishwa au kuzidishwa ikiwa mtu huvaa mavazi yanayobana sehemu za chini za mwili au viatu visivyomtosha au ikiwa ameketi (hasa akiwa amekingamanisha miguu) au kusimama kwa muda mrefu.

      b Watu wenye ugonjwa wa kisukari kinachohitaji insulini wanahitaji kupigwa sindano ya insulini kila siku. Mara nyingi wale wanaougua ugonjwa wa kisukari kisichohitaji insulini wanaweza kudhibiti hali yao kwa kuzingatia mlo na kufanya mazoezi. Katika Marekani, asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari wana aina ile isiyohitaji insulini.

  • Kuishi Maisha Bora Bila Kiungo cha Mwili
    Amkeni!—1999 | Juni 8
    • Kuishi Maisha Bora Bila Kiungo cha Mwili

      “MPANDA-MLIMA afika tena kwenye kilele.” Ndivyo gazeti moja lilivyotangaza, Tom Whittaker alipofika kwenye kilele cha Mlima Everest. Wengi wamepanda kilele hicho kirefu awali, lakini Tom Whittaker alikuwa mtu wa kwanza aliyekatwa kiungo cha mwili kufanya hivyo! Whittaker alipoteza mguu wake kwenye aksidenti ya gari. Lakini mguu bandia, ulimwezesha arejee mchezo anaoupenda. Vifaa kama hivyo vinawezesha maelfu ya watu wengine waliokatwa viungo vya mwili wafurahie maisha bora yenye kuridhisha. Kwa hakika, ni jambo la kawaida kuwaona watu waliokatwa viungo wakishiriki riadha, wakicheza mpira wa kikapu, au wakiendesha baiskeli.

      Miguu na mikono bandia ya kale ilikuwa vipande vya mbao au kulabu za chuma zenye kuumiza. Lakini maendeleo yalifanywa wakati maelfu ya watu walipopoteza viungo vya mwili vitani. Haishangazi kwamba daktari mpasuaji wa jeshi Mfaransa—wa karne ya 16 Ambroise Paré—ndiye anayedaiwa kuwa mwanzilishi wa viungo bandia vya kwanza vilivyo bora. Viungo bandia vya leo hutumia haidroliki, viungo vya goti vyenye muundo tata, miguu bandia iliyotengenezwa kwa kaboni, silikoni, plastiki, na vifaa vingine vya kisasa, vinavyowezesha watu wengi kutembea na kujongea kwa urahisi na bila matatizo kuliko ilivyowahi kudhaniwa. Maendeleo katika taaluma ya elektroni yanawezesha mikono isogezwe kwa njia ya kawaida zaidi. Umbo la viungo bandia limeboreshwa pia. Viungo bandia vya kisasa vina vidole, na hata vingine huonekana kama vina mishipa. Hata mwanamke mmoja mrembo, anayeonyesha mitindo ya nguo aliyepoteza mguu kwa sababu ya ugonjwa wa kansa, alitiwa mguu bandia ulioonekana kuwa wa asili sana hivi kwamba akaweza kuendelea na kazi yake ya kuonyesha mitindo ya nguo.

      Mtazamo wa Akilini Ni Muhimu

      Hata hivyo, mtaalamu wa afya ya akili Ellen Winchell atahadharisha hivi: “Unapopatwa na tatizo la kibinafsi kama vile kukatwa kiungo cha mwili, utu wako unajaribiwa sana katika kila hali—kimwili, kihisia-moyo, kiakili, na kiroho.” Fikiria William, ambaye mguu wake ulikatwa kwa sababu ya kuoza kulikosababishwa na jeraha. Yeye asema hivi: “Siri moja ya kushinda tatizo lolote maishani ni mtazamo wetu wa akilini. Mimi sijapata kamwe kuona kutojiweza kwangu kuwa kizuizi. Badala yake, nimedumisha mtazamo mzuri kuhusu matatizo yoyote ambayo nimekuwa nayo tangu nilipopata aksidenti.” Ellen Winchell, ambaye pia alikatwa kiungo cha mwili, amwunga mkono kwa kusema kuwa watu wenye maoni mazuri huelekea kukabiliana vema na tatizo la kukatwa kiungo cha mwili kuliko watu wenye maoni yasiyofaa. Ni kama vile Biblia isemavyo, “moyo uliochangamka ni dawa nzuri.”—Mithali 17:22.

      Amkeni! lilihoji baadhi ya Wakristo waliopoteza viungo vya mwili ambao wamekabiliana kwa mafanikio na hali yao. Wengi wao walidokeza kwamba watu waliokatwa viungo wanahitaji kuepuka kufikiria sana au kuficha kutojiweza kwao. “Nilisumbuka sana wakati wengine walipohisi kwamba ni mwiko kuzungumzia jambo hilo,” akasema Dell, aliyepoteza mguu chini tu ya goti lake la kushoto. “Naona kwamba jambo hilo humtahayarisha kila mtu.” Wataalamu fulani hupendekeza kwamba ikiwa huna mkono wa kulia na unajulishwa kwa mtu fulani, unapaswa kumsalimu kwa mkono wa kushoto. Na ikiwa mtu anaulizia habari za kiungo chako bandia, mweleze juu yake. Unapostarehe unawafanya watu wengine wahisi wamestarehe. Kwa kawaida, mazungumzo hubadilika upesi.

      Kuna “wakati wa kucheka.” (Mhubiri 3:4b) Mwanamke mmoja aliyepoteza mkono asema hivi: ‘Zaidi ya yote, uwe mcheshi! Ni lazima tukumbuke sikuzote kwamba mtazamo wa watu juu yetu hutegemea sana mtazamo tulionao juu ya hali yetu.’

      “Wakati wa Kulia”

      Hapo mwanzoni, baada ya kupoteza mguu, Dell alijiambia, “Kwisha. Maisha yamekwisha.” Florindo na Floriano walipoteza viungo vya mwili kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini huko Angola. Florindo asema kwamba alilia kwa siku tatu mchana na usiku. Floriano pia alisumbuliwa na hisia-moyo. “Nilikuwa na umri wa miaka 25 tu,” yeye aandika. “Siku moja ningeweza kufanya kitu chochote, na siku ifuatayo singeweza hata kusimama. Nilivunjika moyo na kushuka moyo sana.”

      Kuna “wakati wa kulia.” (Mhubiri 3:4a) Ni kawaida kuhuzunika kwa kipindi fulani unapokumbwa na msiba. (Linganisha Waamuzi 11:37; Mhubiri 7:1-3.) “Njia ya kukabiliana kwa mafanikio na huzuni hiyo ni kutoficha hisi hizo,” aandika Ellen Winchell. Kumweleza msikilizaji mwenye hisia-mwenzi jinsi unavyohisi mara nyingi husaidia sana. (Mithali 12:25) Lakini hisi za huzuni haziendelei milele. Kwa muda fulani baada ya kupatwa na msiba wa kukatwa kiungo cha mwili, huenda watu mmoja mmoja wakawa wenye kukasirika upesi, wenye kuchambua-chambua, wenye mahangaiko, au wenye kujitenga. Hata hivyo, kwa kawaida hisia hizi hupungua. Ikiwa sivyo, huenda akawa amepatwa na mshuko-moyo mbaya—ugonjwa unaohitaji kutibiwa na daktari. Washiriki wa familia na marafiki wanapaswa kuwa macho kuona dalili zozote zinazoonyesha kwamba mpendwa wao anahitaji msaada wa daktari.a

      W. Mitchell, ambaye amepooza miguu yote miwili, aandika hivi: “Sote twahitaji watu wanaojali. Mtu anaweza kuvumilia karibu kila hali mradi anahisi akiwa na marafiki wengi na washiriki wa familia, na kwa upande mwingine mtu anayejaribu kukazana maishani peke yake hushindwa na tatizo dogo. Na marafiki hawaji tu kimwujiza, jitihada inahitajiwa ili kuwapata na kudumisha urafiki nao, kama sivyo unaharibika.”— Linganisha Mithali 18:24.

      Kuishi Maisha Bora, Bila Kiungo cha Mwili

      Watu wengi waliopoteza viungo vya mwili wameweza kuishi maisha bora licha ya ulemavu huo. Kwa kielelezo, Russell alizaliwa akiwa na sehemu ya juu tu ya mguu wa kushoto. Sasa akiwa na umri wa miaka 78, yeye bado hufanya mazoezi kwa ukawaida naye anaishi maisha yenye kuridhisha, ingawa sasa anatembea kwa msaada wa mkongojo. Russell ambaye kwa asili ni mchangamfu, alikiri kwamba kwa muda mrefu aliitwa jina la utani Happy, (Mwenye Furaha).

      Douglas, aliyepoteza mguu wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, hutembea kwa msaada wa mguu bandia wa kisasa. Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, ametumikia kwa furaha akiwa painia wa kawaida, mweneza-evanjeli wa wakati wote, kwa miaka sita. Na je, wamkumbuka Dell, ambaye alifikiri kwamba maisha yake yalikuwa yamekwisha alipopoteza mguu? Yeye pia anaishi maisha ya kuridhisha akiwa painia, naye anajiruzuku.

      Ingawa hivyo, watu waliopoteza viungo vya mwili hukabilianaje na hali katika nchi maskini au zile zenye vita? Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lasema hivi: “Leo, ukweli ni kwamba ni idadi ndogo tu ya watu wasiojiweza wanaopata msaada.” Wengi wao hulazimika kutumia fimbo na mikongojo isiyofaa ili kutembea. Hata hivyo, nyakati nyingine msaada huwapo. Floriano na Florindo, waliopoteza viungo vya mwili kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini huko Angola, walipewa viungo bandia na Shirika la Msalaba Mwekundu na serikali ya Uswisi. Floriano hutumikia kwa furaha akiwa mtumishi wa huduma katika kutaniko la Mashahidi wa Yehova katika eneo lao, naye Florindo anatumikia akiwa mzee na mweneza-evanjeli wa wakati wote.

      Shirika moja linalowashughulikia walemavu hueleza vizuri hivi: “Watu walemavu ni wale tu waliovunjika moyo!” Kwa kupendeza, Biblia imetimiza fungu muhimu katika kuwatia moyo watu walemavu. “Kweli za Biblia nilizojifunza nilipokuwa nikipata nafuu zilinisaidia sana,” asema Dell. Vivyo hivyo, Russell asema hivi: “Tumaini langu linalotegemea Biblia limenisaidia kuvumilia magumu sikuzote.” Biblia ina tumaini gani kwa walemavu?

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona makala “Jinsi ya Kusaidia Walioshuka Moyo Wapate Shangwe Tena,” katika toleo la Mnara wa Mlinzi la Machi 15, 1990.

      [Sanduku katika ukurasa wa 8]

      Maumivu Bandia

      Hisi ya kuwa na kiungo hurejezea hisi halisi inayokufanya uhisi una kiungo chako ulichopoteza. Ni hisia ya kawaida ambayo watu waliokatwa viungo huwa nayo baada ya kukatwa, na ni halisi sana hivi kwamba kijitabu kwa ajili ya watu waliokatwa viungo vya mwili husema hivi: “Jihadhari na hisi ya kuwa una kiungo chako unapotoka kitandani au kitini bila kiungo chako bandia. Sikuzote tazama chini ili ukumbuke kwamba huna mguu.” Mgonjwa mmoja aliyepoteza miguu yote miwili aliinuka ili amsalimu daktari wake, lakini badala yake, akaanguka kwenye sakafu!

      Tatizo jingine ni maumivu bandia ya kiungo kilichopotezwa. Haya ni maumivu halisi ambayo mtu huhisi kana kwamba yanatoka kwa kiungo kilichokatwa. Ukali, aina, na muda wa maumivu bandia hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kwa uzuri, hisi ya kuwa na kiungo na maumivu bandia kwa kawaida hupungua baada ya muda.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki