Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ubaguzi
    Amkeni!—2004 | Septemba 8
    • Ubaguzi

      “Hata jitihada za aina gani zikifanywa ili kumaliza ubaguzi, bado utarudi.”—Frederick Mkuu, Mfalme wa Prussia.

      RAJESH huishi katika kijiji cha Paliyad huko India. Sawa na watu wengine wanaobaguliwa na kuonwa kuwa wachafu, yeye hutembea dakika 15 ili kuteka maji kwa ajili ya familia yake. Anasema hivi: “Katika kijiji chetu, haturuhusiwi kuteka maji katika mifereji inayotumiwa na watu wa matabaka ya juu.” Alipokuwa shuleni, Rajesh na rafiki zake hata hawakuruhusiwa kuugusa mpira ambao watoto wengine waliuchezea. Anasema: “Badala yake, tulichezea mawe.”

      “Mimi huona kwamba watu wananichukia, lakini sijui sababu,” asema Christina, kijana kutoka Asia anayeishi Ulaya. Anaongeza hivi: “Inafadhaisha sana. Kwa kawaida, mimi hujitenga na wengine, lakini hilo pia halisaidii.”

      “Nilianza kuona ubaguzi nikiwa na umri wa miaka 16,” asema Stanley, wa Afrika Magharibi. “Watu nisiowajua hata kidogo waliniambia niondoke mjini. Nyumba za watu fulani wa kabila letu ziliteketezwa. Akaunti ya benki ya baba yangu ilifungwa. Hivyo, nilianza kulichukia kabila lililotubagua.”

      Rajesh, Christina, na Stanley ni baadhi tu ya watu waliobaguliwa. “Mamia ya mamilioni ya watu wanaendelea kuumia kutokana na ubaguzi wa rangi, upendeleo, chuki dhidi ya wageni, na kutengwa na jamii,” asema Koichiro Matsuura, mkurugenzi-mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO). “Matendo hayo ya kinyama yanayochochewa na ujinga na maoni ya chuki, yamesababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi nyingi na mateso mengi kwa wanadamu.”

      Ikiwa hujawahi kubaguliwa, huenda ikawa vigumu kwako kuelewa jinsi hali hiyo inavyofadhaisha sana. Kitabu Face to Face Against Prejudice kinasema kwamba “watu fulani huvumilia ubaguzi bila kulalamika. Wengine hulipiza kisasi wanapobaguliwa.” Ubaguzi huathirije maisha ya watu?

      Ikiwa wewe ni mtu wa jamii ndogo, huenda watu wakakuepuka, wakakutazama vibaya, au wakasema kwa madharau kuhusu utamaduni wenu. Usipokubali kazi za hali ya chini zinazoepukwa na wengi, huenda isiwe rahisi kupata kazi nyingine. Huenda ikawa vigumu kupata makao mazuri. Watoto wako wanaweza kutengwa na kukataliwa na wanafunzi wenzao shuleni.

      Isitoshe, ubaguzi unaweza kuwachochea watu kuwa wajeuri au hata kuua. Kwa kweli, historia ina mifano mingi yenye kuogopesha kuhusu jeuri ambayo imesababishwa na ubaguzi, kama vile mauaji ya kinyama ya watu wengi na mauaji ya jamii nzima-nzima.

      Ubaguzi Umekuwapo kwa Karne Nyingi

      Wakati mmoja, Wakristo hasa ndio waliobaguliwa. Kwa mfano, muda mfupi baada ya kifo cha Yesu, Wakristo walinyanyaswa kwa ukatili sana. (Matendo 8:3; 9:1, 2; 26:10, 11) Karne mbili baadaye, watu waliodai kuwa Wakristo walidhulumiwa kwa ukatili mara nyingi. Tertullian, mwandishi wa karne ya tatu, aliandika hivi: “Janga linapotokea, mara moja watu hupiga kelele hivi, ‘Wapelekeni Wakristo Wakaliwe na Simba.’”

      Hata hivyo, kuanzia karne ya 11, wakati wa vile Vita Vitakatifu, jamii ndogo ya Wayahudi ilianza kuchukiwa sana huko Ulaya. Tauni ya majipu ilipokumba Bara hilo na kusababisha vifo vya karibu robo ya watu katika muda wa miaka michache tu, ilikuwa rahisi kuwalaumu Wayahudi kwani tayari walichukiwa na wengi. Katika kitabu chake Invisible Enemies, Jeanette Farrell anaandika hivi: ‘Chuki hiyo iliwafanya watu ambao waliogopa tauni hiyo kudai kwamba ilisababishwa na Wayahudi.’

      Hatimaye, Myahudi mmoja kusini mwa Ufaransa alipokuwa akiteswa sana, “aliungama” kwamba Wayahudi ndio waliosababisha tauni hiyo kwa kutia sumu ndani ya visima. Bila shaka, alisema uwongo, lakini habari hizo zilienezwa kuwa habari za kweli. Muda si muda, jumuiya nzima-nzima za Wayahudi zilichinjwa huko Hispania, Ufaransa, na Ujerumani. Ni kana kwamba hakuna mtu awaye yote aliyezingatia kisababishi kikuu cha tauni hiyo, yaani, panya. Na ni watu wachache tu waliotambua kwamba Wayahudi pia walikufa kutokana na tauni hiyo!

      Ubaguzi ukiisha kuanza, unaweza kuendelea kichinichini kwa karne nyingi. Katikati ya karne ya 20, Adolf Hitler alichochea chuki dhidi ya Wayahudi kwa kuwalaumu kwamba walifanya Ujerumani ishindwe katika Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Ulimwengu, Rudolf Hoess, kamanda wa Nazi katika kambi ya mateso ya Auschwitz, alikubali hivi: “Mafunzo ya kijeshi na dhana zetu zilitufanya tuamini kwamba tulihitaji kuilinda Ujerumani dhidi ya Wayahudi.” Ili “kuilinda Ujerumani,” Hoess alisimamia mauaji ya watu 2,000,000 hivi, wengi wao wakiwa Wayahudi.

      Ijapokuwa miaka mingi imepita tangu wakati huo, inasikitisha kwamba ukatili haujakwisha. Kwa mfano, katika mwaka wa 1994, chuki ya kikabila ilizuka katika Afrika Mashariki kati ya Watutsi na Wahutu, na kusababisha vifo vya watu wapatao nusu milioni. “Hakukuwa na sehemu za kukimbilia,” laripoti gazeti Time. “Watu wengi waliuawa ndani ya makanisa ambamo walijificha. . . . Vita hivyo vilipiganwa ana kwa ana, vilichochewa na sababu za kibinafsi, na viliogopesha sana, kwani watu walikuwa na hamu kubwa ya kumwaga damu hivi kwamba wale waliofaulu kutoroka walichanganyikiwa kihisia na kushindwa kuongea kwa sababu ya woga.” Hata watoto hawakuepuka jeuri hiyo yenye kutisha. “Rwanda ni nchi ndogo,” alieleza raia mmoja. “Lakini sisi ndio wenye chuki zaidi ulimwenguni.”

      Mapigano yaliyotokana na kuvunjika kwa Yugoslavia, yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 200,000. Majirani waliokuwa wameishi kwa amani kwa miaka mingi waliuana. Maelfu ya wanawake walinajisiwa, na mamilioni ya watu wakafukuzwa makwao kwa sababu ya mauaji ya kikatili ya jamii nzima-nzima.

      Ijapokuwa mara nyingi ubaguzi hausababishi mauaji, kwa kawaida unawagawanya watu na kuchochea chuki. Licha ya kuongezeka kwa ushirikiano kati ya mataifa, inaonekana ubaguzi wa rangi na wa kijamii “unazidi katika sehemu nyingi ulimwenguni,” yasema ripoti moja ya karibuni ya shirika la UNESCO.

      Je, inawezekana kukomesha ubaguzi? Ili kujibu swali hilo, tunapaswa kufahamu jinsi ubaguzi unavyoingizwa katika akili na mioyo ya watu.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      Jinsi Ubaguzi Unavyoonyeshwa

      Katika kitabu chake The Nature of Prejudice, Gordon W. Allport anataja mambo matano yanayosababishwa na ubaguzi. Kwa kawaida, mtu mwenye ubaguzi hufanya jambo moja au zaidi kati ya haya.

      1. Kusema mambo yasiyofaa. Mtu huongea kwa madharau kuhusu jamii anayochukia.

      2. Kuwaepuka wengine. Yeye humwepuka mtu yeyote wa jamii anayochukia.

      3. Kuwa mwenye upendeleo. Yeye huwatenga watu wa jamii hiyo inayobaguliwa kwa kuwazuia wasipate kazi za aina fulani, wasiishi katika maeneo fulani, au wasipate huduma fulani za jamii.

      4. Kuwashambulia wengine. Yeye hushiriki katika matendo ya jeuri ili kuwatisha watu anaochukia.

      5. Kuua. Yeye hujihusisha katika visa vya mauaji na uchinjaji wa jamii nzima-nzima.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Kambi ya wakimbizi ya Benaco, huko Tanzania, mnamo Mei 11, 1994

      Mwanamke anapumzika kando ya vyombo vya kevya kutekea maji. Zaidi ya wakimbizi 300,000, hasa Wahutu kutoka Rwanda waliingia Tanzania

      [Hisani]

      Photo by Paula Bronstein/Liaison

  • Vyanzo vya Ubaguzi
    Amkeni!—2004 | Septemba 8
    • Vyanzo vya Ubaguzi

      UBAGUZI unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali. Hata hivyo, sababu mbili kuu ni (1) tamaa ya kumtafuta mtu wa kulaumu na (2) chuki inayosababishwa na dhuluma zilizofanywa zamani.

      Kama ilivyoonyeshwa katika makala inayotangulia, msiba unapotokea, mara nyingi watu humtafuta mtu wa kulaumu. Watu mashuhuri wanapolalamika mara nyingi kuhusu watu wa jamii ndogo, malalamiko hayo hukubaliwa na ubaguzi hutokea. Kwa mfano, matatizo ya kiuchumi yanapotokea katika nchi za Magharibi, watu ambao wamehamia huko hulaumiwa kwa kusababisha ukosefu wa kazi, hata ingawa kwa kawaida wao hufanya kazi ambazo wenyeji hawapendi.

      Lakini ubaguzi hausababishwi nyakati zote na tamaa ya kumtafuta mtu wa kulaumu. Ubaguzi unaweza kusababishwa pia na mambo yaliyotukia wakati uliopita. Ripoti ya UNESCO Against Racism inasema: “Si kutia chumvi kusema kwamba biashara ya watumwa iliweka msingi wa ubaguzi wa rangi na madharau dhidi ya utamaduni wa watu weusi.” Watu waliofanya biashara ya utumwa walitetea biashara yao yenye kuchukiza ya kuwanunua na kuwauza wanadamu kwa kudai kwamba Waafrika ni duni. Ubaguzi huo usio na msingi wowote, ambao baadaye uliwaathiri watu waliokuwa chini ya ukoloni, bado unaendelea.

      Ulimwenguni pote, matukio ya wakati uliopita ya uonevu na dhuluma huendeleza ubaguzi. Uhasama kati ya Wakatoliki na Waprotestanti nchini Ireland ulianza katika karne ya 16, watawala wa Uingereza walipowanyanyasa na kuwapeleka Wakatoliki uhamishoni. Ukatili uliofanywa na watu waliodai kuwa Wakristo wakati wa vile Vita Vitakatifu huwafanya Waislamu wa Mashariki ya Kati waendelee kuwa na chuki. Uhasama baina ya Waserbia na Wakroatia katika eneo la Balkan ulichochewa na mauaji ya raia wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Kama mifano hiyo inavyoonyesha, uadui ambao umekuwepo kati ya vikundi viwili unaweza kuzidisha ubaguzi.

      Kutofahamu Watu wa Jamii Nyingine

      Mtoto mchanga hana ubaguzi. Badala yake, watafiti wanasema kwamba mara nyingi ni rahisi kwa mtoto kucheza na mtoto wa jamii tofauti na yake. Hata hivyo, mtoto anapofikia umri wa miaka 10 au 11, huenda asipendezwe na watu wa kabila, rangi, au dini tofauti. Anapoendelea kukua, yeye husitawisha maoni tofauti-tofauti kuhusu watu wa jamii nyingine na anaweza kuendelea kuwa na maoni hayo katika maisha yake yote.

      Mtoto hupataje maoni hayo? Mtoto hupata maoni hayo mabaya hasa kupitia maneno na matendo ya wazazi wake, kisha kutoka kwa marafiki au walimu. Baadaye, anaweza kuathiriwa na majirani, magazeti, redio, au televisheni. Ingawa hajui mengi au hata hajui chochote kuhusu jamii asiyoipenda, anapokuwa mtu mzima yeye huwa amekata kauli kwamba watu wa jamii hiyo ni duni na hawaaminiki. Hata anaweza kuwachukia.

      Kwa sababu ya kusafiri na kufanya biashara sana, watu wa tamaduni na makabila mbalimbali katika nchi nyingi wanazidi kuchangamana. Hata hivyo, kwa kawaida mtu ambaye amesitawisha hisia kali za ubaguzi hushikilia maoni yake mabaya yasiyo na msingi. Pia anaweza kushikilia maoni yake mabaya kuhusu maelfu au hata mamilioni ya watu, akidai kwamba wote wana sifa mbaya. Akipatwa na jambo baya, hata ikiwa limesababishwa na mtu mmoja tu wa jamii hiyo, atazidi kuwa mwenye ubaguzi. Kwa upande mwingine, jambo lolote zuri linalofanywa na mtu wa jamii hiyo hupuuzwa na kuonwa kuwa jambo lisilotazamiwa.

      Kuacha Ubaguzi

      Ingawa watu wengi hushutumu ubaguzi kwa maneno, wao huendelea kuwa wenye ubaguzi. Kwa hakika, watu wengi wenye hisia kali za ubaguzi husisitiza kwamba hawana ubaguzi. Wengine husema kwamba si jambo zito, hasa ikiwa watu hawaonyeshi hisia zao za ubaguzi. Hata hivyo, ubaguzi ni jambo zito kwa sababu huwaumiza na kuwagawanya watu. Kutofahamu watu wa jamii nyingine hutokeza ubaguzi, nao ubaguzi hutokeza chuki. Mwandishi Charles Caleb Colton (1780?-1832) alieleza hivi: “Sisi huchukia watu fulani kwa sababu hatuwajui; na hatutawajua kwa sababu tunawachukia.” Lakini, ikiwa mtu anaweza kujifunza kuwa mwenye ubaguzi, anaweza pia kujifunza kuacha ubaguzi. Jinsi gani?

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      Je, Dini Zinawafanya Watu Wavumiliane au Wabaguane?

      Katika kitabu chake The Nature of Prejudice, Gordon W. Allport anasema kwamba “kwa kawaida, inaonekana washiriki wa Makanisa huwa wenye ubaguzi kuliko watu ambao hawashirikiani na Makanisa.” Hiyo haishangazi kwa kuwa mara nyingi dini imesababisha ubaguzi badala ya kuukomesha. Kwa mfano, makasisi walichochea chuki dhidi ya Wayahudi kwa karne nyingi. Kulingana na kitabu A History of Christianity, wakati fulani Hitler alisema hivi: “Kuhusu Wayahudi, mimi nitaendelea tu na maoni yaleyale ambayo kanisa Katoliki limekuwa nayo kwa miaka 1500.”

      Wakati wa visa vya ukatili katika eneo la Balkan, mafundisho ya dini ya Othodoksi na ya Katoliki hayakuwafanya watu wawavumilie na kuwaheshimu majirani wao wa dini tofauti.

      Vivyo hivyo, washiriki wa kanisa huko Rwanda waliwachinja waumini wenzao. Gazeti National Catholic Reporter lilisema kwamba mapigano yaliyotukia huko yalikuwa “mauaji halisi na ya kweli ya kabila moja ambayo kwa kusikitisha, hata Wakatoliki wanahusika.”

      Kanisa Katoliki limekubali kwamba limehusika katika visa vya ukatili. Katika mwaka wa 2000, Papa John Paul wa Pili aliomba msamaha kwa “matendo ya wakati uliopita ya kukiuka kanuni” wakati wa Misa ya hadhara huko Rome. Katika pindi hiyo, “chuki ya kidini na dhuluma dhidi ya Wayahudi, wanawake, wenyeji, wahamiaji, maskini, na watoto ambao bado hawajazaliwa” ilitajwa waziwazi.

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Juu: Kambi ya wakimbizi, Bosnia na Herzegovina, Oktoba 20, 1995

      Wakimbizi wawili Waserbia huko Bosnia wakitarajia mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe

      [Hisani]

      Photo by Scott Peterson/Liaison

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Kufundishwa kuwachukia wengine

      Mtoto anaweza kupata maoni mabaya kutoka kwa wazazi wake, televisheni, na vyanzo vingine

  • Mwisho wa Ubaguzi
    Amkeni!—2004 | Septemba 8
    • Mwisho wa Ubaguzi

      JE, TUNAWEZA kutambua ikiwa tuna mielekeo ya kuwa wenye ubaguzi? Kwa mfano, je, sisi hukata kauli kuhusu sifa za mtu kwa kutegemea rangi ya ngozi yake, taifa lake, jamii yake, au kabila lake ingawa hatumjui? Au, je, tunaweza kumthamini kila mtu kwa sababu ya sifa zake za pekee?

      Katika siku za Yesu, watu walioishi Yudea na Galilaya ‘hawakuwa na shughuli na Wasamaria.’ (Yohana 4:9) Msemo huu ulio katika Talmud unaonyesha wazi hisia za Wayahudi wengi: “Nisimwone Msamaria kamwe.”

      Yaelekea hata mitume wa Yesu waliwabagua Wasamaria kwa kiasi fulani. Pindi moja, hawakukaribishwa kwa fadhili katika kijiji kimoja cha Wasamaria. Yakobo na Yohana waliuliza ikiwa wanaweza kuomba moto ushuke juu ya watu hao wasioitikia. Yesu aliwakemea, hivyo akawaonyesha kwamba maoni yao hayakufaa.—Luka 9:52-56.

      Baadaye, Yesu alisimulia mfano wa mtu aliyeshambuliwa na wanyang’anyi alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu akielekea Yeriko. Wayahudi wawili waliofuata dini hawakutaka kumsaidia. Lakini, Msamaria mmoja alisimama na kumfunga majeraha yake. Kisha akapanga mtu huyo atunzwe ili majeraha yake yapone. Msamaria huyo alionyesha kwamba alikuwa jirani kwelikweli. (Luka 10:29-37) Yaelekea mfano wa Yesu uliwasaidia wasikilizaji wake kutambua kwamba ubaguzi wao uliwazuia kuona sifa nzuri za wengine. Miaka michache baadaye, Yohana alirudi Samaria na kuhubiri katika vijiji vyake vingi, huenda hata katika kijiji alichokuwa ameomba kiharibiwe.—Matendo 8:14-17, 25.

      Pia mtume Petro alihitaji kutenda bila upendeleo wakati malaika alipomwelekeza amhubirie Kornelio, ofisa wa jeshi la Roma, kumhusu Yesu. Petro hakuwa amezoea kushughulika na Wasio Wayahudi, na Wayahudi wengi hawakupenda askari-jeshi Waroma. (Matendo 10:28) Lakini Petro alipotambua kwamba Mungu alikuwa akielekeza mambo, alisema hivi: “Kwa hakika ninaona kwamba Mungu hana ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye anamwogopa na kutenda uadilifu anakubalika kwake.”—Matendo 10:34, 35.

      Sababu ya Kushinda Ubaguzi

      Ubaguzi haupatani na kanuni hii ya msingi ambayo Yesu alifundisha: “Kwa hiyo, mambo yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, lazima mwatendee wao pia vivyo hivyo.” (Mathayo 7:12) Ni nani ambaye angependa kudharauliwa kwa sababu tu ya mahali alipozaliwa, rangi ya ngozi yake, au malezi yake? Ubaguzi pia haupatani na kanuni za Mungu za kutoonyesha upendeleo. Biblia inafundisha kwamba Yehova “alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso wa dunia nzima.” (Matendo 17:26) Hivyo, watu wote ni ndugu.

      Isitoshe, Mungu hushughulika na kila mtu mmoja-mmoja. Yeye hamshutumu mtu kwa sababu ya matendo ya wazazi wake au ya mababu zake. (Ezekieli 18:20; Waroma 2:6) Hata taifa fulani linapotudhulumu, hiyo si sababu ya kuwachukia watu mmoja-mmoja wa taifa hilo, ambao hawahusiki kibinafsi na dhuluma hiyo. Yesu aliwafundisha wafuasi wake ‘kuwapenda adui zao na kusali kwa ajili ya wale wanaowatesa.’—Mathayo 5:44, 45.

      Mafundisho hayo yaliwasaidia Wakristo wa karne ya kwanza kushinda ubaguzi wao na kufanyiza udugu wa pekee wa kimataifa. Walijiona kuwa ndugu na dada na waliitana hivyo, ingawa walitoka katika tamaduni tofauti-tofauti. (Wakolosai 3:9-11; Yakobo 2:5; 4:11) Kanuni zilizowasaidia kufanya mabadiliko hayo, zinaweza kuwa na matokeo kama hayo leo.

      Kushinda Ubaguzi Leo

      Karibu sisi sote huwa na maoni fulani kuhusu watu tusiowajua, hata hivyo si lazima maoni hayo yatokeze ubaguzi. Kitabu The Nature of Prejudice kinasema: “Maoni yetu kuhusu mambo tusiyoyajua hutokeza ubaguzi tusipoyabadilisha baada ya kupata ujuzi zaidi.” Mara nyingi, ubaguzi unaweza kushindwa watu wanapojuana. Hata hivyo, kitabu hicho kinasema, “maoni yanaweza kubadilishwa ikiwa tu watu wanachangamana na kufanya mambo pamoja.”

      Hivyo ndivyo John, wa kabila la Ibo huko Nigeria, alivyoacha kuwabagua Wahausa. Yeye anasema hivi: “Nilipokuwa katika chuo kikuu, nilikutana na wanafunzi Wahausa nasi tukawa marafiki, nami nikagundua kwamba wana sifa nzuri. Tulifanya kazi fulani pamoja na mwanafunzi mmoja Mhausa, nasi tulielewana, hali mwanafunzi niliyeshirikiana naye awali, ambaye ni wa kabila la Ibo, alikuwa mvivu.”

      Njia ya Kushinda Ubaguzi

      Kulingana na ripoti ya UNESCO Against Racism, “huenda elimu ikawa njia muhimu ya kupambana na aina mpya za ubaguzi wa rangi, upendeleo, na kuwatenga watu wa jamii nyingine.” Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba elimu ya Biblia ndiyo msaada bora zaidi wa kushinda ubaguzi. (Isaya 48:17, 18) Watu wanapotumia mafundisho ya Biblia, wao huwaheshimu wengine badala ya kuwashuku, na upendo humaliza chuki.

      Mashahidi wa Yehova wametambua kwamba Biblia inawasaidia kushinda ubaguzi. Kwa hakika, Biblia huwachochea na kuwapa nafasi ya kushirikiana na watu wa tamaduni na jamii tofauti-tofauti. Christina, aliyenukuliwa katika makala ya utangulizi ya mfululizo huu, ni Shahidi wa Yehova. Anasema: “Mikutano yetu katika Jumba la Ufalme hunisaidia kujiamini. Nikiwa huko mimi hujihisi nikiwa salama kwa kuwa hakuna anayenibagua.”

      Jasmin, ambaye pia ni Shahidi, anakumbuka jinsi alivyobaguliwa kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka tisa. Anasema: “Alhamisi ndiyo siku bora kwangu kwa sababu jioni mimi huenda kwenye Jumba la Ufalme. Huko, watu huonyesha kwamba wananipenda. Wao hunifanya nijihisi kuwa mtu wa maana badala ya kunidharau.”

      Miradi ya kujitolea inayotegemezwa na Mashahidi wa Yehova huwawezesha pia watu wa malezi tofauti-tofauti kushirikiana. Simon alizaliwa Uingereza, ingawa familia yake ilitoka Karibea. Alibaguliwa sana alipokuwa akifanya kazi ya uashi katika kampuni za ujenzi. Lakini hilo halikutukia miaka yote aliyojitolea kutumikia katika miradi mbalimbali pamoja na ndugu zake wa imani moja naye. Simon anasema: “Nimefanya kazi pamoja na Mashahidi wenzangu wanaotoka katika nchi nyingi mbalimbali, lakini tumejifunza kuishi pamoja kwa amani. Baadhi ya marafiki zangu wa karibu walitoka katika nchi nyingine na malezi yao yalitofautiana na yangu.”

      Bila shaka, Mashahidi wa Yehova hawajakamilika. Hivyo, huenda wanapambana na mielekeo ya ubaguzi. Lakini, wao huchochewa sana kufanya hivyo kwa sababu wanajua kwamba Mungu hana ubaguzi.—Waefeso 5:1, 2.

      Kuna faida nyingi za kushinda ubaguzi. Tunaposhirikiana na watu wa malezi mbalimbali, maisha yetu huboreshwa. Zaidi ya hilo, kupitia Ufalme wake, hivi karibuni Mungu atafanyiza jamii ya kibinadamu yenye uadilifu. (2 Petro 3:13) Wakati huo ubaguzi utakomeshwa kabisa.

      [Sanduku katika ukurasa wa 11]

      Je, Nina Ubaguzi?

      Jiulize maswali yafuatayo ili uone ikiwa una ubaguzi:

      1. Je, mimi huona kwamba watu wa jamii, eneo, au taifa fulani wana sifa mbaya kama vile ujinga, uvivu, au uchoyo? (Mizaha mingi huendeleza maoni hayo ya ubaguzi.)

      2. Je, mimi huwalaumu wahamiaji au watu wa jamii nyingine ninapokuwa na matatizo ya kiuchumi au ya kijamii?

      3. Je, nimeruhusu uadui wa muda mrefu kati ya jamii yetu na watu wa taifa lingine unifanye niwachukie watu wa taifa hilo?

      4. Je, ninaweza kuona sifa za kibinafsi za kila mtu ninayekutana naye bila kujali rangi ya ngozi yake, utamaduni wake, au jamii yake?

      5. Je, mimi hutaka kuwajua watu wa tamaduni nyingine? Je, mimi hujitahidi kufanya hivyo?

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Katika mfano wake wa Msamaria mwema, Yesu alitufundisha jinsi ya kushinda ubaguzi

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Alipokuwa katika nyumba ya Kornelio, Petro alisema: “Kwa hakika ninaona kwamba Mungu hana ubaguzi”

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Mafundisho ya Biblia huwaunganisha watu wa malezi tofauti

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Mashahidi wa Yehova hutumia mambo ambayo wamejifunza

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Christina—“Mikutano yetu katika Jumba la Ufalme hunisaidia kujiamini”

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Jasmin—“Watu huonyesha kwamba wananipenda. Wao hunifanya nijihisi kuwa mtu wa maana badala ya kunidharau”

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Simon, mfanyakazi wa kujitolea wa ujenzi—“Tumejifunza kuishi pamoja kwa amani”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki