Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Sayari Iliyo Hai
    Amkeni!—2009 | Februari
    • Sayari Iliyo Hai

      DUNIA ina viumbe wengi sana wa aina mbalimbali, huenda hata kuna mamilioni ya jamii za viumbe. Viumbe wengi wanaoishi kwenye udongo, hewa, na maji, ni wadogo sana hivi kwamba hawawezi kuonekana kwa macho. Kwa mfano, kwenye gramu moja ya mchanga kulipatikana jamii 10,000 hivi za bakteria bila kutaja idadi kamili ya vijidudu! Vijidudu fulani vimepatikana kilomita tatu hivi chini ya ardhi!

      Pia, anga limejaa viumbe hai, na hilo halimaanishi tu ndege, popo, na wadudu. Ikitegemea msimu, anga hujaa chavua na viumbe wengine wenye chembe moja, kutia ndani mbegu, na katika maeneo fulani maelfu ya vijidudu vya aina mbalimbali. “Hilo linafanya unamna-namna wa vijidudu hewani uwe sawa na ule wa vijidudu kwenye udongo,” linasema gazeti Scientific American.

      Wakati huohuo, si rahisi kuchunguza bahari yote kwa kuwa ili kuchunguza vilindi vya bahari, wanasayansi wanahitaji kutumia tekinolojia ghali sana. Hata matumbawe ambayo yanaweza kufikiwa kwa urahisi na ambayo yamechunguzwa kwa undani, huenda bado yana mamilioni ya jamii za viumbe ambao hawajagunduliwa.

      Hata hivyo, tunajua kwamba Dunia imejaa viumbe wengi sana hivi kwamba wamebadili kemikali katika sayari, hasa katika sehemu ya dunia iliyo na uhai. Kwa mfano, katika bahari, kalisi-kaboneti iliyo kwenye makoa na marijani inasaidia kusawazisha kemikali majini “kama tu dawa ya kutuliza kiungulia inavyosawazisha asidi tumboni,” inasema ripoti ya Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Bahari na Anga la Marekani. Mimea na miani yenye chembe moja inayopatikana katika maziwa na bahari, husaidia kudhibiti viwango vya kaboni dioksidi na oksijeni majini na hewani. Bakteria na kuvu hufanya kazi pamoja kumeng’enya madini katika udongo ili mimea iweze kuifyonza. Naam, dunia imeitwa kwa kufaa sayari iliyo hai.

      Hata hivyo, uhai haungekuwepo duniani kama hakungekuwa na vipimo fulani sahihi kabisa katika maeneo fulani. Baadhi ya vipimo hivyo havikujulikana kwa undani hadi karne ya 20. Vipimo hivyo sahihi vinatia ndani mambo yafuatayo:

      1. Mahali dunia ilipo katika kikundi cha nyota cha Kilimia na katika mfumo wa jua, kutia ndani mzunguko wa dunia, mwinamo wake, mwendo wa mzunguko, na mwezi

      2. Nguvu za sumaku ya dunia na anga ambazo hutenda kama ngao maradufu

      3. Maji mengi sana

      4. Mizunguko ya asili ambayo husafisha na kurekebisha dunia

      Unaposoma kuhusu mambo hayo katika makala zinazofuata, jiulize: ‘Je, mambo yaliyo duniani yalijitokeza yenyewe au yalitokezwa na mbuni mwenye akili? Ikiwa yalitokezwa na mbuni mwenye akili, Muumba alikuwa na kusudi gani alipoiumba dunia?’ Makala ya mwisho katika mfululizo huu itajibu swali hilo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 3]

      “HATUPASWI HATA KUFIKIRI KUNA MUUMBA”

      Ingawa uthibitisho uliopo unaonyesha kwamba ulimwengu umebuniwa kwa njia nzuri sana hivi kwamba haiwezekani kuwa ulijitokeza tu, wanasayansi wengi wanakataa kuamini kwamba kuna Muumba. Si kwamba sayansi inawalazimisha watu wanaoamini kwamba hakuna Mungu “wakubali ufafanuzi kwamba [ulimwengu] ulijitokeza,” anasema mwanamageuzi Richard C. Lewontin. Badala yake, anasema, wanachochewa na “uamuzi waliofanya mapema . . . kwamba [ulimwengu] ulijitokeza,” na wameazimia kubuni “dhana itakayowasaidia kuamini [ulimwengu] ulijitokeza.” Anaongezea hivi akizungumza kuhusu wanasayansi kwa ujumla: “Kwa kuwa wazo la kwamba ulimwengu ulijitokeza ndilo wazo pekee linalopatana na akili, hatupaswi hata kufikiri kuna Muumba.”

      Je, ni jambo la hekima kufikia mkataa huo sugu hasa ikiwa uthibitisho mwingi unaonyesha kwamba kuna Muumba? Unaonaje?—Waroma 1:20.

  • Dunia Ipo Mahali Bora Zaidi
    Amkeni!—2009 | Februari
    • Dunia Ipo Mahali Bora Zaidi

      KATIKA nchi nyingi anwani hutia ndani nchi, jiji, na barabara. Acheni basi tuseme “nchi” ya dunia ni kikundi cha nyota cha Kilimia, “jiji” lake ni mfumo wa jua, yaani, jua pamoja na sayari zake, kisha tuseme “barabara” ya dunia ni mzunguko wake katika mfumo wa jua. kwa sababu ya maendeleo katika elimu ya nyota na fizikia, wanasayansi wamefahamu zaidi kwa nini dunia ipo mahali bora zaidi katika ulimwengu.

      Kwanza, “jiji” letu, yaani, mfumo wetu wa jua, upo katika eneo la kikundi cha nyota cha Kilimia ambapo wanasayansi wengi wanasema ndipo tu panaweza kutegemeza uhai. Eneo hilo liko umbali wa miaka ya nuru 28,000 kutoka katikati ya kikundi hicho cha nyota na lina kiwango kinachofaa cha kemikali zinazohitajiwa kutegemeza uhai. Mbali zaidi na eneo hilo kemikali hizo ni chache zaidi; karibu zaidi na eneo hilo, ni hatari zaidi kwa sababu kuna miale hatari na vitu vingine. Gazeti Scientific American linasema, “tunaishi katika eneo bora zaidi.”

      “Barabara” Bora Kabisa

      Dunia iko katika “barabara” bora zaidi, yaani, njia ambayo dunia hutumia kulizunguka jua. Njia hiyo, ambayo iko umbali wa kilomita milioni 150 kutoka kwa jua, inapitia eneo ambalo wanasayansi wanasema ndilo eneo lililo karibu na jua linalofaa zaidi kwa uhai, mahali ambapo hakuna baridi wala joto kupita kiasi. Isitoshe, kwa kuwa dunia hulizunguka jua kwa kutumia njia inayokaribia kuwa na umbo la duara, umbali wake kutoka kwa jua hubaki vilevile mwaka mzima.

      Wakati huohuo, jua ndiyo “chanzo cha nishati kinachofaa kabisa.” Liko imara, lina ukubwa unaofaa, na linatoa kiasi kinachofaa cha nishati. Kwa kufaa, jua limeitwa “nyota ya pekee sana.”

      Jirani Bora Kabisa

      Ikiwa ungeambiwa uchague jirani anayefaa zaidi kwa ajili ya dunia, hungepata jirani bora kuliko mwezi. Kipenyo chake ni robo tu ya kile cha dunia. Hivyo, unapolinganishwa na miezi ya sayari nyingine zilizo katika mfumo wa jua, mwezi wa dunia ni mkubwa sana ukilinganishwa na dunia. Hata hivyo, kuna sababu nzuri kwa nini una ukubwa huo.

      Sababu moja ni kwamba mwezi huchangia sehemu kubwa katika kufanya maji yajae na kupwa baharini, jambo ambalo husaidia sana katika kuisafisha dunia. Pia, mwezi huchangia katika kufanya dunia izunguke katika mhimili wake bila kuyumbayumba. Kama mwezi uliobuniwa kwa njia inayofaa haungekuwepo, sayari yetu ingeyumbayumba kama pia inayozunguka, huenda hata nyakati nyingine ingepinduka na kulalia upande mmoja! Mabadiliko katika hali ya hewa, kiwango cha maji baharini, na mabadiliko mengine yangesababisha misiba.

      Mwinamo na Mzunguko Bora Kabisa wa Dunia

      Kwa kuwa dunia imeinama kwa digrii 23.5, hilo hufanya kuwe na majira mbalimbali katika mwaka, viwango mbalimbali vya joto, na kufanya kuwe na maeneo mbalimbali ya hali ya hewa. “Mwinamo wa sayari yetu katika mhimili wake unaonekana kuwa ‘bora kabisa’ ili kuendeleza uhai,” kinasema kitabu Rare Earth—Why Complex Life Is Uncommon in the Universe.

      Pia, urefu wa mchana na usiku ni sahihi sana kwa sababu ya mzunguko wa dunia. Ikiwa dunia ingezunguka kwa muda mrefu zaidi, upande wa dunia unaoelekea jua ungeunguzwa na ule upande mwingine ungeganda. Vivyo hivyo, ikiwa siku zingekuwa fupi zaidi, hata kwa saa chache tu, kuzunguka huko kasi kungesababisha pepo zenye nguvu sana na zisizokoma na vilevile madhara mengine.

      Naam, kila kitu kuhusu sayari yetu, iwe ni mahali dunia ilipo, au mwendo wa kuzunguka kwake, au mwezi wake, huthibitisha kwamba dunia ilibuniwa na Muumba mwenye hekima.a Mwanafizikia na mwanamageuzi Paul Davies anasema: “Hata wanasayansi ambao wanaamini kwamba hakuna Mungu watasifu sana ukubwa, utukufu, upatano, uzuri, na hekima iliyohusika katika kutokeza ulimwengu.”

      Je, hekima hiyo yote inayoonekana ulimwenguni ilijitokeza tu, au inaonyesha kuna mbuni mwenye akili? Fikiria swali hilo unaposoma makala fupi inayofuata, ambayo inazungumzia ngao mbili za ajabu zinazokinga uhai duniani kutokana na vitu hatari vinavyotoka angani.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ili ulimwengu wote uendelee kuwapo, kani nne za msingi zinahitajika: nguvu za uvutano, sumaku-umeme, na kani za nyuklia zenye nguvu na dhaifu. Zote zimepimwa kwa usahihi wa hali ya juu.—Ona sura ya 2 katika kitabu Je, Kuna Muumba Anayekujali? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      JE, UNASONGA HARAKA KULIKO RISASI?

      Utakapomaliza kusoma sanduku hili, utakuwa umesafiri maelfu ya kilomita bila kuhisi kana kwamba unarushwa-rushwa! Fikiria mambo yafuatayo.

      Dunia ina mzingo wa kilomita 40,000 na inazunguka mara moja kila saa 24. Hivyo, maeneo yaliyo kwenye ikweta au karibu yanasonga kwa kilomita 1,600 hivi kwa saa. (Bila shaka, ncha za dunia hazisongi, zinazunguka hapohapo.)

      Dunia yenyewe inazunguka jua kwa kilomita 30 hivi kwa sekunde, na mfumo wa jua kwa ujumla unazunguka kitovu cha Kilimia kwa mwendo wenye kustaajabisha wa kilomita 249 kwa sekunde. Kwa kulinganishwa, risasi husafiri kwa mwendo unaopungua kilomita mbili kwa sekunde.

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

      Milky Way: NASA/JPL/Caltech

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 5]

      Earth: Based on NASA/Visible Earth imagery

  • Ngao za Dunia Zenye Nguvu
    Amkeni!—2009 | Februari
    • Ngao za Dunia Zenye Nguvu

      ANGA za juu ni eneo hatari lililojaa mnururisho wenye sumu na vimondo. Hata hivyo, ni kana kwamba sayari yetu ya bluu inasonga katikati ya mawe hayo yanayoanguka bila kupata madhara mengi. Kwa nini? Kwa sababu dunia imekingwa na ngao za ajabu, yaani, nguvu za sumaku za dunia na anga-hewa.

      Nguvu za sumaku za dunia zinatoka ndani kabisa ya sayari hii na zinaenea kwenye anga za juu ambako zinafanyiza ngao isiyoonekana inayoitwa magnetosphere (picha upande wa kulia). Ngao hiyo inatukinga kutokana na mnururisho mwingi kutoka angani na hatari kutoka kwa jua. Hatari hizo zinatia ndani upepo wenye chembechembe zenye nishati; milipuko kutoka sehemu fulani ndogo ya jua ambayo inatokeza nishati inayolingana na mabilioni ya mabomu ya hidrojeni; na vilevile milipuko kutoka sehemu ya juu ya jua (CME) ambayo hurusha mabilioni ya tani ya mata katika anga za juu. Milipuko kutoka kwa jua hutokeza mimweko yenye rangi zenye kupendeza (picha upande wa kulia chini) zinazoonekana kwenye anga-hewa karibu na ncha za dunia zenye sumaku.

      Anga-hewa ya dunia inakinga dunia pia. Sehemu ya juu ya dunia inayoitwa stratosphere, ina aina fulani ya oksijeni ambayo inaitwa ozoni inayofyonza asilimia 99 ya mnururisho wa urujuanimno. Hivyo, ozoni inasaidia kukinga viumbe vingi, kutia ndani wanadamu na uduvi, kutokana na mnururisho hatari. Kwa kupendeza, kiwango cha ozoni kinalingana na mnururisho wa urujuanimno na hivyo kuifanya iwe ngao yenye nguvu na inayofaa kabisa.

      Pia, angahewa hutukinga kutokana na mamilioni ya vimondo vidogo na vikubwa. Vimondo vingi huteketea angani na kutokeza mwangaza unaoitwa nyota-mkia.

      Ngao za dunia hazizuii mnururisho ambao ni muhimu kwa uhai kama vile joto na mwangaza. Angahewa hata inasaidia kusambaza joto duniani, na usiku inakuwa kama blanketi inayozuia joto lisitoke haraka.

      Kwa kweli, angahewa na nguvu za sumaku za dunia ni maajabu ya ubuni ambayo bado hayajaeleweka kikamili. Tunaweza kusema pia kwamba maji mengi sana yaliyo duniani ni ubuni wa ajabu.

  • Maji Yanaendeleza Uhai
    Amkeni!—2009 | Februari
    • Maji Yanaendeleza Uhai

      MAJI ni fumbo. Maji yamefanyizwa kwa njia rahisi na pia iliyo tata. Kila molekuli ina atomu tatu peke yake, mbili za hidrojeni na moja ya oksijeni. Hata hivyo, bado wanasayansi hawaelewi kabisa jinsi molekuli za maji zinavyofanya kazi. Jambo ambalo sote tunajua ni kwamba maji ni muhimu kwa uhai na yanafanyiza asilimia 80 hivi ya uzito wa vitu vyote vilivyo hai. Fikiria mambo matano kuhusu kitu hicho cha ajabu.

      1. Maji yanaweza kuhifadhi kiasi kikubwa cha joto bila kiwango cha joto kuongezeka na hivyo yanasaidia kusawazisha hali ya hewa.

      2. Maji yanapoganda, huwa yanapanuka na hivyo kufanya barafu ielee na kufanyiza tabaka linalozuia joto lisitoke. Ikiwa maji yangekuwa kama vitu vingine vinavyoongezeka uzito kadiri vinavyoganda, basi maziwa, mito, na bahari zingeganda kutoka chini hadi juu na hivyo kuangamiza kila kitu kwa barafu!

      3. Mwangaza hupenya katika maji kwa urahisi na hivyo kuwezesha viumbe wanaotegemea mwangaza waendelee kuishi hata wakiwa chini sana majini.

      4. Molekuli za maji hutokeza nguvu fulani. Nguvu hiyo inawezesha wadudu kukimbia juu ya kidimbwi, inasaidia kufanyiza matone, na kuchangia kupitisha maji hadi kwenye mimea mirefu zaidi.

      5. Maji yanaweza kuyeyusha vitu vingi zaidi. Yanaweza kuyeyusha oksijeni, kaboni-dioksidi, chumvi, madini, na vitu vingine muhimu.

      Muhimu Katika Kusawazisha Joto Duniani

      Asilimia 70 hivi ya dunia imefunikwa na bahari na hivyo bahari hutimiza fungu muhimu katika kudhibiti hali ya hewa. Kwa kweli, bahari na angahewa zinafanya kazi pamoja, zikibadilishana joto, maji, gesi, na kuathiri kufanyizwa kwa upepo na mawimbi. Pia zinafanya kazi pamoja ya kuondoa joto kutoka maeneo ya Tropiki kuelekea ncha na hivyo kusawazisha joto duniani. Ili viumbe wengi waendelee kuwa hai, joto linahitaji kuwa katika kiwango kinachoruhusu maji yabaki yakiwa katika hali ya umajimaji. “Inaonekana kwamba hali za Dunia ni sawa kabisa,” kinasema kitabu Rare Earth—Why Complex Life Is Uncommon in the Universe.

      Bila shaka, dunia ilibuniwa na haikujitokeza. Lakini je, ilijitokeza kwa nasibu, au je, ilitokezwa na Muumba mwenye upendo? Biblia inasema kwamba ilitokezwa na Muumba. (Matendo 14:15-17) Katika makala inayofuata, tutaona jinsi mifumo ya ajabu inayofanya sayari yetu iwe safi na yenye afya na hivyo kuunga mkono maoni ya Biblia.

  • Mizunguko Inayotegemeza Uhai
    Amkeni!—2009 | Februari
    • Mizunguko Inayotegemeza Uhai

      IKIWA mifumo ya kuingiza hewa safi na kuleta maji katika jiji fulani ingekatizwa, nayo mifumo ya kuondoa maji-taka izibwe, hilo lingesababisha magonjwa na kifo. Hata hivyo, sayari yetu haihitaji hewa safi na maji kutoka kwa sayari nyingine wala haihitaji kupeleka takataka kwenye sayari nyingine! Basi ni nini kinachowezesha dunia iwe mahali safi na salama pa kuishi? Jibu ni: mizunguko ya asili, kama vile mizunguko ya maji, kaboni, oksijeni, na nitrojeni, ambayo imeelezewa na kurahisishwa hapa kwa njia rahisi.

      Mzunguko wa maji unatia ndani hatua tatu. 1. Nishati ya jua huvukiza maji na kuyainua kwenye angahewa. 2. Maji hayo safi hugandamana na kutokeza mawingu. 3. Nayo mawingu hutokeza mvua, mvua ya mawe, au theluji, ambayo hunyesha, na hivyo kukamilisha mzunguko huo. Lakini ni kiasi gani cha maji husafishwa na kutumiwa tena kila mwaka? Kulingana na makadirio, ni kiasi cha kutosha kufunika dunia yote kwa kina cha sentimita 100 hivi.

      2

      ← ◯

      ↓ 3 ↑

      ↓ 1 ↑

      ↓ ↑

      → →

      →

      Mzunguko wa kaboni na oksijeni unahusisha hatua mbili kuu—usanidimwanga na kupumua.a Usanidimwanga hutumia mwangaza wa jua, kaboni dioksidi, na maji ili kutokeza wanga na oksijeni. Wanyama na wanadamu wanapopumua, hewa hiyo huchanganyika na wanga na oksijeni na kutokeza nishati, kaboni dioksidi, na maji. Kwa hiyo, kile kinachotokezwa na mfumo mmoja hutumiwa na mfumo ule mwingine, na hilo hutendeka taratibu bila kutokeza takataka wala kelele yoyote.

      Oksijeni

      ←

      ← ←

      ↓ ↑

      ↓ ↑

      ↓ ↑

      → →

      →

      Kaboni dioksidi

      Mzunguko wa nitrojeni ni muhimu ili kutokeza amino asidi, protini, na molekuli za vitu vingine vilivyooza. A. Mzunguko huo huanza wakati radi na bakteria zinapobadili nitrojeni iliyo hewani kuwa mchanganyiko unaoweza kufyonzwa na mimea. B. Nayo mimea hutumia mchanganyiko huo kutokeza molekuli za vitu vilivyooza. Wanyama hula mimea na hivyo wao pia wanapata nitrojeni. C. Mimea na wanyama wanapokufa, jamii nyingine za bakteria humeng’enya mchanganyiko huo wenye nitrojeni na hivyo kurudisha nitrojeni kwenye udongo na hewani.

      ← ← ← ← ← ← ← ← ← ←

      ↓ ↑

      ↓ Angahewa lina ↑

      ↓ asilimia 78 ya nitrojeni ↑

      ↓ ↑

      ↓ ↓ Molekuli za ↑

      ↓ A ↓ vitu vilivyooza ↑

      ↓ Bakteria ↓ B ↑ ↓ C ↑

      → Mchanganyiko wa nitrojeni Bakteria →

      → → →

      Kusafisha na Kutumia Tena Takataka!

      Fikiria hili: Kila mwaka, tekinolojia ya wanadamu imetokeza tani nyingi sana za takataka zenye sumu zisizoweza kutumiwa tena. Ingawa hivyo, dunia inasafisha na kutumia tena takataka zake zote kupitia mbinu za hali ya juu. “Nasibu peke yake haingeweza kutokeza” upatano huo wa kimazingira, anasema mwandishi wa mambo ya kidini na kisayansi M. A. Corey.

      Ikimpa sifa yule anayestahili, Biblia inasema hivi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima.” (Zaburi 104:24) Wanadamu wameona hekima hiyo kwa njia ya pekee.

      [Maelezo ya Chini]

      a Huenda kemikali zilezile zikatumika katika mizunguko mbalimbali. Kwa mfano, kaboni dioksidi, wanga, na maji zina oksijeni. Kwa hiyo, oksijeni inatumika katika mzunguko wa kaboni na ule wa maji.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki