-
Matukio ya Kuogopesha Matendo ya KutumainishaAmkeni!—2002 | Machi 22
-
-
Matukio ya Kuogopesha Matendo ya Kutumainisha
“MAJENGO YALITIKISIKA NA MIALE YA MOTO ILIWAKA KOTEKOTE. NILIPOKUWA NIKIKIMBIA NILISIKIA WATU KOTEKOTE WAKILIA, WAKISALI NA KUOMBA MSAADA. NILIFIKIRI MWISHO WA DUNIA ULIKUWA UMEFIKA.”—G. R., MWOKOKAJI WA TETEMEKO LA ARDHI.
Kila mwaka mamilioni ya matetemeko ya ardhi hutokea katika tabaka la nje la dunia linalosongasonga. Kwa wazi, hatuwezi kusikia mengi ya matetemeko hayo.a Hata hivyo, kwa wastani, karibu matetemeko ya ardhi 140 yenye nguvu sana hutokea kila mwaka. Kuna matetemeko “yenye nguvu,” matetemeko “makubwa,” na “makubwa zaidi.” Tangu zamani, matetemeko hayo yamesababisha vifo vya mamilioni ya watu na kuharibu mali nyingi sana.
Waokokaji wa matetemeko ya ardhi huathiriwa sana kihisia. Kwa mfano, matetemeko mawili ya ardhi yalipotokea nchini El Salvador mapema katika mwaka wa 2001, mratibu wa kamati ya ushauri wa tiba ya akili ya wizara ya afya ya nchi hiyo, alisema hivi: “Watu wanakumbwa na matatizo mengi sana ya akili yanayosababisha huzuni, mfadhaiko na hasira.” Basi haishangazi kwamba wafanyakazi wa huduma za afya nchini El Salvador waliripoti kwamba watu walioshuka moyo na wenye wasiwasi waliongezeka kwa asilimia 73. Kwa kweli, uchunguzi mbalimbali ulionyesha kwamba uhitaji mkubwa wa watu katika kambi za msaada ulikuwa maji, kisha matibabu ya magonjwa ya akili.
Lakini habari za matetemeko ya ardhi hazihusishi kifo, uharibifu, na mfadhaiko tu. Katika visa vingi, misiba hiyo imewachochea watu kusaidia sana na kujitoa mhanga. Kwa kweli, watu fulani wamefanya kazi kwa bidii kurekebisha majengo yaliyoharibiwa na kuwatia moyo watu waliofadhaika. Kama tutakavyoona, matendo hayo yamewapa watu tumaini hata wakati wa matukio ya kuogopesha sana.
[Maelezo ya Chini]
a Hiyo inatia ndani matetemeko madogo sana ya ardhi. Maelfu ya matetemeko hayo hutokea kila siku.
-
-
Tetemeko la ArdhiAmkeni!—2002 | Machi 22
-
-
Tetemeko la Ardhi
‘TUMEZOEA KUISHI KATIKA DUNIA ILIYO IMARA HIVI KWAMBA DUNIA INAPOANZA KUTIKISIKA TUNABABAIKA SANA.’—“THE VIOLENT EARTH.”
“Kichapo The World Book Encyclopedia chasema kwamba ‘matetemeko ya ardhi ni mojawapo ya matukio yenye kusababisha uharibifu mkubwa zaidi ulimwenguni.’ Maneno hayo ni ya kweli kabisa, kwani nishati ya tetemeko kubwa la ardhi yaweza kuwa mara 10,000 zaidi ya ile ya bomu la kwanza la nyukilia! Jambo hilo linaogopesha hata zaidi kwa kuwa matetemeko hayo yanaweza kutokea katika tabia yoyote ya nchi, msimu wowote, na saa zozote. Na ijapo wanasayansi wanaweza kujua kwa kadiri fulani mahala ambapo matetemeko yenye nguvu yatatokea, hawawezi kutabiri yatatokea lini.
Matetemeko ya ardhi hutokea kwa sababu ya kusonga kwa miamba mikubwa ambayo iko chini ya uso wa dunia. Miamba hiyo husonga daima. Mara nyingi, mawimbi ya tetemeko la ardhi ambayo hutokea huwa dhaifu sana hivi kwamba hayawezi kutambuliwa waziwazi kwenye uso wa dunia, lakini yanaweza kutambuliwa na kurekodiwa na kipima-tetemeko.a Nyakati nyingine, miamba mingi huvunjika na kusongasonga kiasi cha kutetemesha ardhi sana.
Lakini kwa nini miamba hiyo huendelea kusongasonga? ‘Jibu laweza kupatikana katika ile dhana kuhusu mabamba yaliyo kwenye tabaka la nje la dunia. Dhana hiyo imebadili kabisa maoni ya wanasayansi kuhusu dunia,’ chasema Kituo cha Taifa cha Habari za Matetemeko ya Ardhi (NEIC). ‘Sasa tunajua kwamba kuna mabamba saba makubwa yaliyo kwenye tabaka la nje la dunia ambayo yamegawanyika katika mabamba madogo-madogo. Mabamba yote hayo husonga daima na kwa wakati mmoja. Yanaweza kusonga umbali wa milimeta 10 hadi 130 kila mwaka.’ Kituo cha NEIC chasema kwamba matetemeko mengi ya ardhi hutokea kwenye maeneo membamba ambako mabamba hayo yametengana. Yaelekea asilimia 90 ya matetemeko makubwa ya ardhi hutokea katika maeneo hayo.
Ukubwa na Kiwango
Tetemeko la ardhi laweza kupimwa kulingana na ukubwa au kiwango chake. Katika miaka ya 1930, Charles Richter alibuni kipimo cha kuonyesha ukubwa wa matetemeko ya ardhi. Wakati vituo vya kupima matetemeko ya ardhi vilipoongezeka, vipimo vipya vilibuniwa kwa kutumia uvumbuzi wa Richter. Kwa mfano, kipimo cha nguvu za tetemeko la ardhi huonyesha kiasi cha nishati inayotokezwa kwenye chanzo cha tetemeko la ardhi.
Kwa wazi, nyakati nyingine vipimo hivyo havilingani na uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi. Kwa mfano, fikiria tetemeko la ardhi lililotokea kaskazini mwa Bolivia mnamo Juni 1994. Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 8.2 kwenye kipimo cha Richter na yaripotiwa kwamba watu watano tu walikufa. Lakini, mamia ya maelfu ya watu walikufa katika tetemeko la ardhi lililotokea mwaka wa 1976 huko Tangshan, China, ambalo lilikuwa na ukubwa wa 8.0!
Tofauti na kipimo cha ukubwa, kiwango cha tetemeko la ardhi huonyesha jinsi linavyoathiri watu, majengo, na mazingira. Kiwango cha tetemeko la ardhi huonyesha waziwazi hasa jinsi wanadamu wanavyoathiriwa sana nalo. Kwa hakika, matetemeko hayawajeruhi watu moja kwa moja. Badala yake, majeraha na vifo husababishwa na kuta zinazoanguka, mabomba ya gesi yanayolipuka, nyaya za nguvu za umeme zinazokatika, vitu vinavyoporomoka, na kadhalika.
Lengo moja la wataalamu wa matetemeko ni kutoa maonyo kuhusu matetemeko ya ardhi mapema. Programu ya kompyuta inayoitwa Mfumo wa Hali ya Juu wa Kuchunguza Matetemeko ya Ardhi inatayarishwa. Ripoti moja ya shirika la habari la CNN ilisema kwamba programu hiyo, pamoja na uwezo wa kupata habari haraka na pia programu nyingine tata za kompyuta, zitawasaidia wataalamu “kuweza kutambua mara moja mahala ambapo mtikisiko mkubwa wa tetemeko la ardhi umetokea.” Hivyo, jambo hilo litawasaidia wenye mamlaka kutuma msaada kwenye maeneo yaliyokumbwa na msiba.
Pasipo shaka, watu wanapotazamia tetemeko la ardhi wanaweza kupunguza majeraha, uharibifu wa mali na—zaidi ya yote—kuokoa uhai. Hata hivyo, matetemeko ya ardhi yanaendelea kutokea. Hivyo, swali hili lazuka: Watu wamesaidiwaje kukabiliana na hasara?
[Maelezo ya Chini]
a Kipima-tetemeko ni chombo kinachopima na kurekodi mtikisiko wa ardhi wakati tetemeko la ardhi linapotokea. Kipima-tetemeko cha kwanza kilibuniwa mwaka wa 1890. Siku hizi kuna vituo zaidi ya 4,000 ulimwenguni pote vinavyopima matetemeko ya ardhi.
[Chati katika ukurasa wa 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Idadi ya Matetemeko ya Ardhi
Kionyeshi Ukubwa Wastani wa Kila Mwaka
Kubwa Zaidi 8 na zaidi 1
Kubwa 7-7.9 18
Lenye Nguvu 6-6.9 120
La Kadiri 5-5.9 800
Nguvu Kidogo 4-4.9 6,200*
Dogo 3-3.9 49,000*
Dogo Sana Chini ya 3 Ukubwa wa 2-3:
karibu 1,000 kila siku
Ukubwa wa 1-2:
karibu 8,000 kila siku
* Imekadiriwa.
[Hisani]
Chanzo: National Earthquake Information Center By permission of USGS/National Earthquake Information Center, USA
[Picha katika ukurasa wa 5 zimeandaliwa na]
Mistari inayorekodiwa na kipima-tetemeko kwenye ukurasa wa 4 na 5: Figure courtesy of the Berkeley Seismological Laboratory
-
-
Kukabiliana na HasaraAmkeni!—2002 | Machi 22
-
-
Kukabiliana na Hasara
“TUMEKUWA TUKITEMBEA TANGU ASUBUHI. TUNATOROKA ILI KUJIOKOA. HAKUNA MAJI YA KUNYWA, HAKUNA CHAKULA. NYUMBA ZOTE ZIMEHARIBIWA.”—HARJIVAN, MWOKOKAJI WA TETEMEKO LA ARDHI HUKO INDIA, LENYE UKUBWA WA 7.9 KWENYE KIPIMO CHA RICHTER.
Tetemeko la ardhi huogopesha sana. Mwanamke mmoja aliyeokoka tetemeko la ardhi mwaka wa 1999 huko Taiwan anasema hivi: “Vitabu viliniangukia kutoka kwenye kabati la mbao lenye kimo cha meta 2.5 ambalo lilikuwa kando ya kitanda changu. Kofia mpya ya kujikinga wakati wa kuendesha pikipiki ilianguka kando tu ya kichwa changu kitandani.” Yeye aongezea hivi: “Kofia hiyo ingeniua badala ya kunikinga.”
Maisha Baada ya Tetemeko
Kuokoka tetemeko la ardhi ni jambo la kuogopesha, lakini huo ndio mwanzo tu. Saa chache baada ya tetemeko la ardhi kutokea, wafanyakazi wa kutoa msaada hujaribu kwa ujasiri kuwapata na kuwatibu watu waliojeruhiwa. Mara nyingi, wao hufanya hivyo hata kukiwa na hatari ya kutokea kwa tetemeko jingine la ardhi. “Tunahitaji kuwa waangalifu sana,” ndivyo alivyosema mwanamume mmoja aliyetaka kufukua nyumba zilizofunikwa kwa udongo mwingi sana baada ya tetemeko kutokea hivi majuzi huko El Salvador. “Ardhi ikitikisika tena kwa ghafula, udongo utaporomoka.”
Nyakati nyingine watu hujitoa mhanga ili kuwaokoa watu walioathiriwa. Kwa mfano, tetemeko kubwa la ardhi lilipotokea nchini India mapema katika mwaka wa 2001, Manu, mzee mmoja ambaye sasa anaishi nchini Marekani, alirudi kwenye nchi yake ya asili. Yeye aliwaza hivi: “Ni lazima niende ili nisaidie familia yangu na kila mtu anayeteseka.” Manu alipata hali mbaya sana katika maeneo aliyotembelea. Hata hivyo, alisema hivi: ‘Watu walikuwa na ujasiri mwingi sana.’ Mwandishi mmoja wa habari alisema hivi: “Watu wote niliowajua walichanga chochote walichokuwa nacho—ujira wa siku moja, juma moja, au wa mwezi mmoja, fedha fulani walizokuwa wameweka akibani au msaada wowote ambao wangeweza kutoa.”
Bila shaka, japo ni vigumu kuondoa vifusi na kuwatibu waliojeruhiwa, ni vigumu zaidi kuwasaidia watu ambao wameathiriwa kwa muda mfupi na tukio la kuogopesha kuishi kama hapo awali. Mfikirie Delores, mwanamke mmoja ambaye nyumba yake iliharibiwa na tetemeko la ardhi nchini El Salvador. Anasema hivi: “Tukio hili ni baya sana kuliko vita. Angalau wakati wa vita tulikuwa na nyumba.”
Kama ilivyosemwa katika makala yetu ya kwanza, japo watu walioathiriwa wanahitaji vitu vya kimwili, wanahitaji pia kufarijiwa. Kwa mfano, tetemeko la ardhi lilipoharibu jiji la Armenia lililoko magharibi mwa Kolombia mapema katika mwaka wa 1999, zaidi ya watu elfu moja walikufa, na wengine wengi walishtuka na kufadhaika. Roberto Estefan, daktari wa magonjwa ya akili ambaye nyumba yake iliharibiwa wakati wa msiba huo, alisema hivi: ‘Kokote uendako, watu wanaomba msaada. Ninapokwenda kula kwenye mkahawa, watu wengi wanaonisalimu wananieleza huzuni yao na jinsi wanavyoshindwa kulala.’
Kama Dakt. Estefan anavyofahamu, watu wengi hufadhaika sana baada ya kuokoka tetemeko la ardhi. Mwanamke mmoja aliyejitolea kusaidia kujenga kambi ya msaada alisema kwamba wafanyakazi fulani hawataki kwenda kazini kwani wanaamini kwamba watakufa hivi karibuni.
Kuwasaidia Watu Waliofadhaika
Majanga yanapotokea, Mashahidi wa Yehova huwasaidia waokokaji kimwili, kiroho na kihisia. Kwa mfano, mara tu baada ya tetemeko la ardhi lililotajwa awali kutokea huko Kolombia, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini humo ilianzisha halmashauri ya dharura kwenye eneo hilo. Maelfu ya Mashahidi kutoka sehemu zote za nchi hiyo walichanga chakula na fedha. Punde baadaye, tani 70 hivi za chakula zilitumwa kwenye eneo lililokumbwa na msiba.
Mara nyingi, watu wanahitaji sana msaada wa kiroho. Asubuhi moja baada ya tetemeko la ardhi kutokea huko Kolombia, Shahidi mmoja wa Yehova katika eneo hilo alimwona mwanamke aliyeonekana kuwa mwenye huzuni nyingi akitembea katika barabara moja ya jiji la Armenia lililokumbwa na msiba huo. Alimwendea mwanamke huyo na kumpa trakti yenye kichwa Kuna Tumaini Gani kwa Wapendwa Waliokufa?a
Mwanamke huyo alienda na trakti hiyo nyumbani na akaisoma kwa uangalifu. Baadaye, Shahidi mwingine wa Yehova alipomtembelea nyumbani kwake, mwanamke huyo alichochewa kusimulia mambo yaliyompata. Tetemeko hilo la ardhi lilikuwa limeharibu nyumba zake kadhaa katika jiji hilo ambazo zilikuwa zinamletea fedha nyingi. Sasa alikuwa ametumbukia katika umaskini. Lakini aliathiriwa hata zaidi. Tetemeko hilo lilibomoa nyumba yake ambamo yeye na mwanawe mwenye umri wa miaka 25 waliishi, na kumwua mwana huyo. Mwanamke huyo alimweleza Shahidi huyo kwamba hapo awali hakupendezwa kamwe na dini lakini sasa alikuwa na maswali mengi. Trakti hiyo ilikuwa imempa tumaini. Punde baadaye, alianza kujifunza Biblia.
Mashahidi wa Yehova wanasadiki kwamba kuna wakati ambapo wanadamu hawataathiriwa tena na misiba ya asili, kutia ndani matetemeko ya ardhi. Makala inayofuata itaonyesha ni kwa nini wanaamini hivyo.
[Maelezo ya Chini]
a Iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
JITAYARISHE!
◼ Hakikisha kwamba tanki za maji moto zimefungwa imara na kwamba vitu vizito viko sakafuni au kwenye rafu za chini.
◼ Wafundishe watu wa familia yako jinsi ya kuzima kabisa umeme, gesi, na kufunga maji.
◼ Weka kizima-moto na kisanduku cha huduma ya kwanza nyumbani mwako.
◼ Uwe na redio ndogo ya mawasiliano yenye betri mpya nyumbani.
◼ Panga mazoezi ya familia ili kuonyesha utaratibu wa kufuata wakati wa matukio ya dharura, na ukazie uhitaji wa (1) kutulia, (2) kuzima jiko na tanki za maji moto, (3) kusimama mlangoni au kukaa chini ya meza au dawati, na (4) kutokuwa karibu na madirisha, vioo, na mabomba ya kutolea moshi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
MATETEMEKO YA ARDHI HUKO ISRAEL
Profesa Amos Nur aliandika kwamba nchi ya Israel ndiyo “imekumbwa na matetemeko mengi ya ardhi kwa muda mrefu duniani.” Hiyo ni kwa sababu sehemu fulani ya Bonde Kuu la Ufa, yaani, ufa unaopita kati ya mabamba ya Mediterania na ya Arabuni, hupita katika nchi ya Israel kuanzia kaskazini hadi kusini.
Kwa kupendeza, wanaakiolojia fulani wanaamini kwamba wahandisi wa kale walitumia mbinu ya pekee ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na matetemeko ya ardhi. Wazo hilo lapatana na maelezo ya Biblia kuhusu ujenzi wa Solomoni: “Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya BWANA, na ukumbi wa nyumba.” (1 Wafalme 6:36; 7:12, italiki ni zetu.) Uthibitisho wa mbinu hiyo ya kuingiza mihimili ya mbao katika jengo la mawe umepatikana katika sehemu mbalimbali—kutia ndani lango moja huko Megiddo, ambalo inadhaniwa kuwa lilijengwa katika siku za Solomoni au kabla ya hapo. Msomi David M. Rohl anaamini kwamba huenda mihimili hiyo “iliingizwa ili kujaribu kuzuia jengo lisiharibiwe na tetemeko la ardhi.”
[Picha]
Magofu ya tetemeko la ardhi huko Bet Sheʼan, Israel
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
DAKIKA MBILI ZA KUOGOPESHA SIMULIZI LA MWOKOKAJI MMOJA
Familia yetu ilikuwa inajitayarisha kwa ajili ya arusi ya binamu yangu, huko Ahmadabad, India. Mnamo Januari 26, 2001, niliamshwa na mtikiso mkubwa badala ya kuamshwa na mlio wa saa yangu. Nilisikia kabati za metali zikisongasonga, na nikajua kwamba kulikuwa na hatari. Mjomba wangu alikuwa akisema hivi kwa sauti kubwa, “Tokeni nje ya nyumba!” Tulipokuwa nje tuliona nyumba ikitikisika. Ni kana kwamba kutikisika huko kuliendelea kwa muda mrefu. Lakini kwa kweli, tetemeko hilo lilitukia kwa muda wa dakika mbili tu.
Ilikuwa vigumu sana kukabiliana na hali hiyo ya ghafula. Tulihakikisha kwamba watu wa familia yetu walikuwa salama. Kwa kuwa nyaya za simu na za umeme zilikatika, hatukuweza kujua mara moja hali ya watu wa jamaa yetu katika miji mingine. Baada ya kuwa na wasiwasi kwa muda wa saa moja, tulipata habari kwamba walikuwa salama. Si watu wote walionusurika. Kwa mfano, huko Ahmadabad, zaidi ya majengo mia moja yalianguka, na zaidi ya watu 500 walikufa.
Watu wote walikuwa na wasiwasi kwa majuma kadhaa. Watu walikwenda kulala huku wakiogopa kwamba tetemeko jingine lingetokea, kwa kuwa ilikuwa imetabiriwa hivyo. Watu wengi walipoteza makao, na marekebisho yalifanywa polepole. Yote hayo yalisababishwa na tetemeko la ardhi ambalo tutalikumbuka daima hata ingawa lilitukia kwa muda wa dakika mbili tu. —Limesimuliwa na Samir Saraiya.
[Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Mwokokaji wa tetemeko la ardhi lililotokea huko India mnamo Januari 2001 anashika picha ya mama yake ambaye alikufa na sasa mwili wake unateketezwa
[Hisani]
© Randolph Langenbach/UNESCO (www.conservationtech.com)
-
-
Matetemeko ya Ardhi, Unabii wa Biblia, na WeweAmkeni!—2002 | Machi 22
-
-
Matetemeko ya Ardhi, Unabii wa Biblia, na Wewe
Kabla ya kifo chake, Yesu alitabiri matukio na hali ambazo zingeonyesha kwamba ulimwengu ulikuwa katika “umalizio wa mfumo wa mambo.” Yeye alisema kwamba magonjwa ya kuambukiza, upungufu wa chakula, na vita kila mahala ni mambo ambayo yangetukia katika kipindi hicho. Pia alisema kuhusu “matetemeko makubwa ya dunia” ambayo yangetokea “katika mahali pamoja baada ya pengine.” (Mathayo 24:3, 7; Luka 21:10, 11) Je, Yesu alikuwa anatabiri kuhusu siku zetu?
Watu wengi hupinga jambo hilo. Wanasema kwamba matetemeko ya ardhi hayajaongezeka sana katika miaka ya karibuni. Kituo cha Taifa cha Habari za Matetemeko ya Ardhi cha Marekani kinaripoti kwamba matetemeko ya ardhi ya ukubwa wa 7.0 au zaidi kwenye kipimo cha Richter “hayakuongezeka sana” katika karne yote ya 20.a
Hata hivyo, tambua kwamba si lazima utimizo wa unabii wa Yesu uhusishe ongezeko la idadi au la nguvu za matetemeko ya ardhi. Yesu alisema tu kungekuwapo na matetemeko makubwa ya ardhi mahali pamoja baada ya pengine. Kwa kuongezea, alisema kwamba matukio hayo yangeonyesha “mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.” (Mathayo 24:8) Taabu huonyeshwa kwa jinsi ambavyo watu huathiriwa wala si na idadi wala ukubwa wa matetemeko ya ardhi kwenye kipimo cha Richter.
Matetemeko ya ardhi huwataabisha watu sana siku hizi. Katika karne ya 20, mamilioni ya watu walikufa au kupoteza makao kwa sababu ya matetemeko ya ardhi. Wataalamu wanasema kwamba vifo vingi vingaliweza kuzuiwa. Shirika la Utangazaji la BBC laripoti hivi: “Katika nchi zinazoendelea, mara nyingi sheria za ujenzi hupuuzwa ili kujenga nyumba za bei rahisi haraka-haraka kwa minajili ya kuwawezesha watu wengi wanaohamia mijini kupata makao.” Ben Wisner, mtaalamu wa misiba inayotokea mijini alisema hivi alipozungumzia misiba miwili ya hivi majuzi: “Watu hao hawakufa kwa sababu ya matetemeko ya ardhi. Vifo vyao vilisababishwa na makosa ya wanadamu, kutojali, ufisadi, na pupa.”
Naam, tetemeko la ardhi linapotokea, nyakati nyingine watu hufa kwa sababu ya ubinafsi na uzembe. Sifa hizo zinaonyeshwa wazi katika unabii mwingine wa Biblia unaohusu “siku za mwisho” za mfumo huu. Biblia yasema kwamba katika kipindi hicho watu wangekuwa na “ubinafsi, wenye tamaa ya fedha,” na “wasio na upendo moyoni.” (2 Timotheo 3:1-5, Biblia Habari Njema) Unabii huo pamoja na maneno ya Yesu kuhusu umalizio wa mfumo wa mambo unaonyesha wazi kwamba tumekaribia wakati ambapo Mungu ataondoa visababishi vya maumivu na kuteseka—kutia ndani matetemeko ya ardhi.—Zaburi 37:11.
Je, unataka kujifunza mengi zaidi kuhusu tumaini hilo linalopatikana katika Biblia? Wasiliana na Mashahidi wa Yehova mahala unapoishi, au utume barua yako kwa kutumia anwani ifaayo iliyoorodheshwa kwenye ukurasa wa 5.
[Maelezo ya Chini]
a Watu fulani wanasema kwamba ripoti za kuongezeka kwa matetemeko ya ardhi zimetokana tu na maendeleo ya kitekinolojia yanayofanya iwe rahisi kutambua matetemeko mengi zaidi.
-