-
Mbinu Tano za Kutafuta KaziAmkeni!—2005 | Julai 8
-
-
Jitayarishie Mahojiano Vizuri
Utajitayarishaje kwa ajili ya mahojiano? Huenda ukataka kufanya utafiti kuhusu kampuni unayotaka kufanyia kazi. Kadiri unavyojua mengi kuhusu kampuni hiyo, ndivyo utakavyojieleza vizuri wakati wa mahojiano. Pia utafiti wako utakusaidia kujua ikiwa kweli kampuni hiyo ina kazi unayotaka au kama ungependa kuifanyia kazi.
Kisha, fikiria mavazi utakayovaa unapoenda kwenye mahojiano. Ikiwa kazi unayotafuta inahusisha kazi ngumu, valia mavazi safi, nadhifu, na yanayofaa kazi hiyo. Kuvalia na kujipamba kwa njia nadhifu kutamwonyesha mtu unayetazamia akuajiri kwamba unajiheshimu na hivyo yaelekea utajivunia kazi yako. Ikiwa unatazamia kufanya kazi ya ofisi, vaa mavazi ambayo huonwa kuwa yanafaa kazi hiyo mahali unapoishi. Nigel anasema: “Chagua mavazi yako muda mrefu kabla ya wakati unapopaswa kwenda kwenye mahojiano ya kazi ili usifanye mambo harakaharaka na kuwa na mkazo mwingi kabla ya mahojiano.”
Nigel pia anapendekeza ufike dakika 15 hivi kabla ya mahojiano. Bila shaka, si jambo la hekima kufika mapema sana. Lakini pia kufika ukiwa umechelewa kunaweza kuharibu mambo. Wataalamu wanasema kwamba sekunde tatu za kwanza za mahojiano ni muhimu sana. Katika sekunde hizo, yule anayekuhoji hukagua sura yako na tabia yako, mambo ambayo huamua maoni yake kukuhusu. Ukichelewa, atakuwa na maoni mabaya kukuhusu. Kumbuka kwamba hutapata nafasi nyingine ya kurekebisha maoni ambayo mtu hupata kukuhusu mara ya kwanza.
Pia, kumbuka kwamba yule anayekuhoji si adui yako. Huenda yeye pia alitoa ombi kwa ajili ya kazi yake, kwa hiyo anajua jinsi unavyohisi. Kwa kweli, huenda akawa na wasiwasi kwa kuwa labda hajazoezwa vya kutosha kuwahoji watu. Isitoshe, ikiwa yule anayekuhoji ndiye mwajiri, huenda akapata hasara kubwa akiajiri mtu asiyefaa.
Ili uanze vizuri, tabasamu na umsalimu yule anayekuhoji kwa mkono ikiwa hiyo ni desturi ya kwenu. Wakati wa mahojiano, fikiria hasa mambo ambayo mwajiri anatarajia kutoka kwako na yale unayoweza kutimiza. Nigel anasema hivi kuhusu mambo unayopaswa kuepuka: “Usisimame, kuketi au kutembea kizembe. Utulivu huonyesha kwamba mtu ana uhakika. Usizungumze sana au kwa urafiki sana, wala usitumie lugha chafu kamwe. Pia epuka kuwachambua waajiri na wafanyakazi wenzako wa awali kwa kuwa ukifanya hivyo yule anayekuhoji ataona kwamba utachambua kazi hiyo pia.”
Wataalamu wanapendekeza ufanye na kusema mambo yafuatayo wakati wa mahojiano: Mtazame yule anayekuhoji, tumia ishara za kawaida unapozungumza, na uzungumze kwa ufasaha. Jibu maswali kifupi na kwa unyoofu, na uulize maswali yanayofaa kuhusu kampuni hiyo na kazi unayotarajia kufanya. Omba kazi hiyo baada ya mahojiano ikiwa bado unaitaka. Kufanya hivyo kutaonyesha kwamba bado unataka kazi hiyo.
-
-
Mbinu Tano za Kutafuta KaziAmkeni!—2005 | Julai 8
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Maswali Unayoweza Kuulizwa Wakati wa Mahojiano ya Kazi
❑ Kwa nini umeomba kazi hii?
❑ Kwa nini unataka kufanya kazi katika kampuni hii hasa?
❑ Unajua nini kuhusu kazi/kampuni/ kiwanda hiki?
❑ Je, umewahi kufanya kazi hii?
❑ Unaweza kuendesha mashini zipi?
❑ Una uzoefu gani katika kazi hii?
❑ Una ustadi gani ambao utafaa kazi hii?
❑ Nieleze kuhusu maisha yako.
❑ Ni maneno gani matano yanayofafanua utu wako?
❑ Je, unaweza kufanya kazi chini ya mkazo?
❑ Kwa nini uliacha kazi uliyokuwa ukifanya?
❑ Kwa nini hujapata kazi kwa muda mrefu?
❑ Mwajiri wako wa zamani alikuwa na maoni gani kukuhusu?
❑ Ulikosa kwenda kazi mara ngapi mahali ulipoajiriwa awali?
❑ Una mipango gani kwa ajili ya wakati ujao?
❑ Unaweza kuanza kazi lini?
❑ Una stadi gani za kipekee?
-