Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Watu Wanapendezwa Sana na Mwisho wa Dunia
    Amkeni!—2012 | Septemba
    • Watu Wanapendezwa Sana na Mwisho wa Dunia

      JE, UNA wasiwasi kuhusu wakati ujao? Ikiwa ndivyo, kuna watu wengi wanaohisi kama wewe. Tangu zamani za kale, watu wamekuwa wakikisia kuhusu wakati ujao wa ulimwengu huu, na wengi wamekata kauli kwamba hakuna matumaini. Kwa maelfu ya miaka, watu wametaka sana kujua jinsi mwisho wa dunia utakavyokuwa.

      Kwa mfano, fikiria hadithi za kubuniwa za hivi karibuni. Vitabu vya katuni, televisheni, mamia ya sinema, na maelfu ya vitabu vinasimulia jinsi ambavyo ulimwengu huu utaangamizwa. Hadithi hizo zinasimulia jinsi ambavyo wanadamu watavamiwa na kuangamizwa na vitu fulani vyenye nguvu sana kama vile, roboti zenye kuua, majitu ya kila aina, viumbe kutoka sayari nyingine, madubwana, mizimu, majoka, sokwe, ndege, panya wenye umbo lisilo la kawaida, na nyigu wakubwa sana. Kwa kweli, hakuna mtu anayeweza kuamini hadithi hizo!

      Lakini kuna hadithi na nadharia nyingine ambazo huwaogopesha watu fulani. Baadhi ya nadharia hizo zinasemekana kuwa za kisayansi. Nadharia moja inasema kwamba tabaka lote la juu la dunia litasonga ghafula na hilo litasababisha tsunami zenye nguvu, matetemeko ya nchi, na volkano. Nyingine inadai kwamba sayari zote zitajipanga katika mstari mmoja na hilo litasababisha kuongezeka kwa upepo kutoka kwenye jua ambao utaleta uharibifu mkubwa duniani. Na bado nadharia nyingine inasema kwamba ncha za dunia zenye nguvu za sumaku zitajigeuza ghafula kuelekea upande mwingine na kusababisha mnururisho kutoka kwenye jua utuue sisi sote. Usiwe na hofu. Mambo hayo hayatatendeka. Hata hivyo, matukio hayo ya kuwaziwa bado yanawavutia watu wengi.

      Namna gani vitabu vingi na Tovuti kuhusu mwisho wa dunia zinazotabiri kwamba ulimwengu utaisha Desemba 21 mwaka huu? Chanzo kimoja kinadai kwamba sayari ya kuwaziwa inayoitwa Nibiru (au Sayari X) iko mwendoni kuja kugongana na dunia na itafika hapa Desemba 2012. Nadharia hizo na nyingine ambazo haziungwi mkono na mambo hakika zinategemea kalenda ya kale ya Wamaya, ambayo watu fulani wanasema kwamba mwaka wake wa mwisho utakuwa Desemba 2012.

      Watu fulani ambao wameamini matabiri kama hayo ya maangamizi, wamejenga mahali pa kujificha nje ya nyumba zao au wamelipa pesa nyingi ili kujihifadhia vyumba katika mahandaki ya umma. Wengine wamehamia milimani mahali ambapo hakuna huduma za umma kama vile maji, vifaa vya kupasha nyumba joto, au umeme.

      Bila shaka, kuna watu ambao hawaamini hadithi na nadharia hizo. Wanapuuza wazo la kwamba mwisho wa dunia unakaribia. Kwa mfano, wanasayansi katika shirika la NASA wanasema hivi: “Dunia haitapatwa na madhara yoyote katika mwaka wa 2012. Kwa zaidi ya miaka bilioni 4 hakuna jambo lolote baya limeipata sayari yetu, na wanasayansi wenye kutumainika ulimwenguni pote hawana habari zozote kuhusu tisho linalohusianishwa na mwaka wa 2012.”

      Hata hivyo, ni kosa kukata kauli kwamba hakuna hatari yoyote inayowakabili wanadamu au kwamba ni watu wanaodanganyika kwa urahisi ndio huamini kwamba mwisho wa dunia ni jambo hakika. Kweli mwisho wa dunia utafika? Ikiwa ndivyo, utafika lini na jinsi gani?

  • Hofu Kubwa Kuhusu Mwisho wa Dunia
    Amkeni!—2012 | Septemba
    • Hofu Kubwa Kuhusu Mwisho wa Dunia

      MBALI na madai yaliyotajwa katika makala iliyotangulia kuhusu mwisho wa dunia, kuna mambo tunayopaswa kufikiria kwa uzito. Watu wengi wanahofu kwamba idadi ya watu itaongezeka sana duniani na kwa sababu hiyo kutakuwa na ukosefu wa maji na chakula. Wengine wana wasiwasi kuhusu matokeo ya kuporomoka kwa uchumi ulimwenguni pote. Namna gani kuhusu misiba ya asili, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, au vita vya nyuklia? Je, mambo hayo yanaweza kusababisha msiba mkubwa ulimwenguni pote?

      Acheni tuzungumzie kifupi hali fulani ambazo watu wanasema zitasababisha mwisho wa dunia. Si hali zote zinazotishia kuua kila mtu duniani, lakini zinaweza kuleta madhara makubwa kwa wanadamu. Hali hizo zinatia ndani mambo yafuatayo.

      Volkano Zinazosababisha Uharibifu Mkubwa

      Katika mwaka wa 1991, Mlima Pinatubo huko Filipino ulilipuka na kuwaua watu zaidi ya 700 na kuwaacha watu 100,000 hivi bila makao. Wingu kubwa la majivu liliinuka kilomita 30 angani na kisha kuanguka ardhini na kufunika mazao na kusababisha paa za majengo kuporomoka. Mlima Pinatubo na volkano nyingine kama hiyo husababisha mabadiliko ya hali ya hewa kwa miaka kadhaa baada ya kulipuka.

      Iwapo milipuko mikubwa itatokea, kama ile ambayo imetokea miaka mingi iliyopita, itakuwa mikubwa zaidi na mibaya zaidi kuliko milipuko yoyote ambayo imewahi kutokea katika historia na itasababisha uharibifu mkubwa zaidi. Mbali na kusababisha uharibifu mkubwa mara moja, mabadiliko ya hali ya hewa yataharibu mazao, yatasababisha ukosefu wa chakula, na hilo litafanya watu wengi wafe njaa.

      “Volkano za kawaida huua mimea na wanyama wanaoishi mbali sana na mahali ambapo mlipuko ulitokea; volkano zenye nguvu zaidi zinatishia kuangamiza jamii nzimanzima kwa kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni pote.”​—National Geographic.

      Mawe Kutoka Angani

      Asubuhi moja katika mwaka wa 1908, mwanamume fulani alikuwa ameketi nje ya duka moja katika kituo cha kibiashara huko Vanavara, Siberia wakati mlipuko fulani ulipomrusha kutoka katika kiti chake. Alihisi joto kali sana ni kana kwamba shati lake lilikuwa likiwaka moto. Mlipuko huo ulitokea umbali wa kilomita 60 hivi kutoka mahali alipokuwa. Mlipuko huo ulisababishwa na jiwe kutoka angani lililokuwa na kipenyo cha mita 35 na uzito wa kilogramu milioni 100 hivi. Baada ya kuingia kwenye angahewa la dunia, jiwe hilo lililipuka kwa sababu ya shinikizo kubwa na joto lililotokezwa jiwe hilo lilipokuwa likiteremka. Mlipuko huo ulitokeza nishati inayolingana na mabomu 1,000 kama yale yaliyoangushwa huko Hiroshima na uliharibu eneo lenye ukubwa wa kilomita 2,000 hivi za mraba katika msitu wa Siberia. Bila shaka, jiwe kubwa zaidi ya hilo linaweza kusababisha uharibifu mkubwa zaidi, kutokeza mioto mikubwa, na kusababisha kiwango cha joto ulimwenguni pote kupungua sana na hivyo kusababisha wanyama na mimea mingi kutoweka.

      “Katika historia yote ya dunia, nyota-mikia na mawe kutoka angani yameanguka duniani. Mambo hayo yalitukia mara nyingi zaidi zamani, na yatatukia tena. Lakini hatujui ni lini.”​—Chris Palma, mhadhiri mkuu wa astronomia na fizikia ya anga katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Pennsylvania.

      Mabadiliko ya Hali ya Hewa

      Wanasayansi wanaamini kwamba mambo kama vile kupanda kwa kiwango cha joto duniani, hali mbaya sana ya hewa, kuyeyuka kwa barafu iliyo kwenye vilele vya milima na miamba ya barafu, kutoweka kwa matumbawe na aina muhimu za wanyama na mimea, kunaonyesha kwamba hali ya hewa inabadilika ulimwenguni pote. Ingawa watu wana maoni yanayotofautiana, wengi wanaamini kwamba tatizo hilo linasababishwa na magari na viwanda vinavyotumia makaa ya mawe, mafuta, na gesi za asili​—nishati hizo za asili hutokeza kiasi kikubwa cha gesi ya kaboni dioksidi angani.

      Wataalamu fulani wanasema kwamba gesi hizo zinachangia kuongezeka kwa joto duniani kwa kuwa zinazuia joto lisitoke duniani na kurudi angani. Kwa sababu miti hufyonza kaboni dioksidi, huenda ukataji wa miti mingi ukachangia pia kubadilika kwa hali ya hewa.

      “Ikiwa kiwango cha sasa cha kuongezeka kwa joto duniani kitaendelea na utokezaji wa kaboni dioksidi hautapunguzwa, wanasayansi wengi wasema kwamba kiwango cha wastani cha joto duniani kitaendelea kuongezeka na kutokeza mabadiliko makubwa ya hali ya hewa na bahari zitafurika na kuhatarisha maisha ya watu wengi wanaoishi sehemu za pwani.”​—A Mind for Tomorrow: Facts, Values, and the Future.

      Kuenea kwa Magonjwa ya Kuambukiza

      Katika karne ya 14, Tauni iliua asilimia 33 ya watu wote barani Ulaya katika muda wa miaka miwili tu. Kati ya mwaka wa 1918 na 1920, Homa ya Hispania iliua watu milioni 50 hivi. Njia duni za usafiri zilizuia magonjwa hayo yasienee haraka. Hata hivyo, kwa kuwa leo kuna ukuzi mkubwa wa majiji na njia rahisi zaidi za usafiri wa kimataifa, magonjwa kama hayo yanaweza kuenea haraka sana katika mabara yote.

      Ugonjwa hatari kama huo unaweza kusababishwa na vitu vya asili. Lakini kuna hofu inayozidi kuongezeka ya silaha za kibiolojia, yaani, viini vya magonjwa vinavyotengenezwa na wanadamu kwenye maabara. Wataalamu katika nyanja hiyo wanasema kwamba watu wachache wenye ujuzi unaohitajika wanaweza kununua vifaa kwenye Intaneti na kutengeneza silaha hatari za kibiolojia.

      “Ugonjwa unaotokea kwa njia ya asili ni tisho kubwa kwa afya; hata hivyo, ikiwa adui mwenye ujuzi atapata viini hivyo​—au viini sugu visivyoweza kutibiwa kwa dawa, au vilivyotengenezwa katika maabara—anaweza kusababisha madhara makubwa sana.”​—Kituo cha Utafiti Kuhusu Ugaidi cha Bipartisan WMD.

      Kutoweka kwa Aina Muhimu za Viumbe Hai

      Katika muda wa miaka mitano iliyopita, wafugaji wa nyuki nchini Marekani wamepoteza karibu asilimia 30 ya nyuki wao kila mwaka kwa sababu ya kutoweka ghafula na kwa njia isiyoeleweka kwa vikundi vizima-vizima vya nyuki, jambo ambalo linatendeka ulimwenguni pote. Nyuki hufanya mengi zaidi ya kutengeneza asali. Wao huchavusha mazao muhimu kama vile zabibu, matofaa, soya, na pamba. Nyuki ni muhimu sana kwetu.

      Pia mwani ni muhimu kwetu. Mwani usipokuwepo, samaki hawatakuwepo. Bila minyoo ambayo husaidia kuingiza hewa kwenye udongo, tungevuna mazao machache. Kutoweka kwa aina hizo muhimu kungesababisha upungufu wa chakula na njaa, na hilo lingetokeza jeuri na vurugu. Uchafuzi, kuongezeka kwa idadi ya watu, kutumia mali za asili kupita kiasi, uharibifu wa mazingira, na mabadiliko ya hali ya hewa huchangia kutoweka kwa aina za wanyama labda zaidi ya mara 1,000 kuliko wanavyotoweka kwa njia ya asili.

      “Kila mwaka, kati ya aina 18,000 na 55,000 za viumbe hai hutoweka. Kisababishi: utendaji wa wanadamu.”​—Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo.

      Vita vya Nyuklia

      Mlipuko mmoja wa nyuklia unaweza kufutilia mbali mara moja jiji zima—ukweli wenye kuhuzunisha ambao ulionekana wazi mara mbili mnamo Agosti 1945. Mlipuko wa nyuklia una nguvu nyingi sana zenye kutisha, nao unaharibu na kuua kwa kutokeza wimbi la shinikizo la hewa, upepo, joto, moto, na mnururisho. Mnururisho hutia sumu kwenye chakula na maji. Vita vya nyuklia vingesababisha kiasi kikubwa cha vumbi kutupwa hewani na hivyo kufunika mwangaza wa jua na kusababisha kiwango cha joto ulimwenguni kushuka. Mazao na mimea mingine ingekufa. Bila chakula, wanadamu na wanyama wangekufa. Inasemekana kwamba nchi tisa hivi zina uwezo wa kurusha makombora ya nyuklia. Nchi nyingine chache ziko katika harakati ya kutengeneza silaha zao za nyuklia. Na mashirika ya kigaidi yanatamani sana kupata silaha hizo.

      “Silaha za nyuklia ndizo tisho kuu na hatari zaidi kwa jamii ya kibinadamu. . . . Bado kuna silaha 25,000 hivi za nyuklia ulimwenguni pote . . . Siku moja, magaidi watapata silaha hizo.”​—Muungano wa Wanasayansi Wanaojali.

  • Mwisho wa Dunia Huenda Usije kwa Njia Unayofikiri
    Amkeni!—2012 | Septemba
    • Mwisho wa Dunia Huenda Usije kwa Njia Unayofikiri

      MBALI na kuashiria mabaya, mambo yaliyotajwa katika makala zilizotangulia kuhusu mwisho wa dunia yanafanana katika njia tatu. Kwanza yanategemea makisio ya wanadamu, na historia inaonyesha kwamba wanadamu hawawezi kutabiri wakati ujao. Pili, ikiwa kuna wanadamu wowote watakaookoka, itakuwa kwa sadfa tu. Tatu, waokokaji wa mwisho wa dunia wataishi maisha magumu sana.

      Tofauti na hilo, yale ambayo Biblia inasema kuhusu wakati ujao yanapatana zaidi na akili. Biblia inasema kwamba kwa kweli kuna mabadiliko makubwa yanayokuja. Lakini wale wanaofanya mapenzi ya Mungu wataokoka hakika. Isitoshe, Biblia haisemi kwamba dunia italipuliwa iwe majivu au itageuka kuwa barafu. Badala yake, dunia nzima itageuzwa kuwa paradiso.

      Hata hivyo, watu wengi wanaona vigumu sana kuamini matabiri hayo ya Biblia. Watu walio na shaka huona kuwa yale ambayo Biblia inafundisha kuhusu dhiki kuu, Har–Magedoni, kipindi cha miaka elfu, na Paradiso ni mambo ya kuwaziwa tu. Kwa muda mrefu mafundisho hayo yamejadiliwa, kubishaniwa, na kufasiriwa na wanatheolojia. Maoni yao yanapingana. Mwandishi Bruce A. Robinson anasema hivi kuhusu wakati wa mwisho: “Kati ya mafundisho yote ya dini zinazodai kuwa za Kikristo, huenda hakuna maandishi mengine ya kitheolojia ambayo yameandikwa kwa njia isiyoeleweka wazi kuliko hayo.” Matokeo yamekuwa nini? Vurugu.

      Ingawa hivyo, Maandiko hayaelezi mambo katika njia isiyoeleweka. Biblia ni ujumbe kutoka kwa Mungu, naye hataki tutatanishwe kuhusu yatakayotukia wakati ujao. Chunguza baadhi ya maswali ambayo huulizwa mara nyingi, na yale ambayo Biblia yenyewe inasema. Ikiwa ungependa kujifunza mengi zaidi, unaweza kuomba kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      Je, dunia pamoja na wanadamu wote wataharibiwa?

      “Waadilifu wenyewe wataimiliki dunia, nao watakaa milele juu yake.”​—Zaburi 37:29.

      Je, kuna wanadamu wowote ambao watakufa?

      “Wanyoofu ndio watakaokaa duniani, na wasio na lawama ndio watakaobaki ndani yake. Nao waovu, watakatiliwa mbali kutoka duniani; nao wenye hila, watang’olewa kutoka ndani yake.”​—Methali 2:21, 22.

      Je, Mungu amewahi kuwaharibu watu wasiomwogopa nyakati za kale?

      Mungu “hakujizuia kuuadhibu ulimwengu wa kale, bali alimlinda Noa, mhubiri wa uadilifu, akiwa salama pamoja na wengine saba alipoleta gharika juu ya ulimwengu wa watu wasiomwogopa Mungu; na kwa kuyageuza majiji ya Sodoma na Gomora kuwa majivu aliyahukumia adhabu, akiweka kielelezo kwa watu wasiomwogopa Mungu juu ya mambo yatakayokuja.”—2 Petro 2:5, 6.

      Tunaweza kujua tarehe ambayo Mungu ataleta hukumu?

      “Kuhusu siku ile na saa ile hakuna mtu anayejua, wala malaika wa mbinguni wala Mwana, ila Baba tu. Kwa maana kama vile siku za Noa zilivyokuwa, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa. Kwa maana kama vile walivyokuwa katika siku hizo kabla ya gharika, wakila na kunywa, wanaume wakioa na wanawake wakiolewa, mpaka siku ambayo Noa aliingia ndani ya safina; nao hawakujali mpaka gharika ikaja na kuwafagilia mbali wote, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa.”​—Mathayo 24:36-39.

      Je, kuna dalili zozote zinazoonyesha kwamba mwisho utakuja hivi karibuni?

      “Katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda pesa, wenye kujidai, wenye majivuno, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio washikamanifu, wasio na upendo wa asili, wasiotaka makubaliano yoyote, wachongezi, wasiojizuia, wakali, wasiopenda wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kujivuna kwa kiburi, wanaopenda raha badala ya kumpenda Mungu wakiwa na namna ya ujitoaji-kimungu lakini wakizikana nguvu zake.”​—2 Timotheo 3:1-5.

      Wanadamu walio duniani watarajie nini wakati ujao?

      Mungu “atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.”—Ufunuo 21:4.

      Mungu “atafuta kila chozi kutoka katika macho yao”

      Ingawa Maandiko hayatuelezi kila kitu kuhusu wakati ujao, yanatuhakikishia kwamba kuna tumaini. Wakati ujao utakuwa mtukufu kuliko tunavyoweza kuwazia. Unaweza kuamini jambo hilo ukiwa na uhakika kwamba Yehova Mungu anaweza kutimiza kile ambacho ameahidi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki