-
Nishati Ni Muhimu kwa UhaiAmkeni!—2005 | Machi 8
-
-
Nishati Ni Muhimu kwa Uhai
MICAH alizaliwa mnamo Agosti 2003. Mama yake alipelekwa hospitalini kwa gari linalotumia petroli. Taa za hospitali ambamo alizaliwa ziliwashwa kwa umeme uliotoka kwenye kituo kinachotokeza umeme kwa makaa ya mawe. Mfumo unaotumia gesi ya asili ulitumiwa kupasha joto chumba ambamo alizaliwa. Iwapo mojawapo ya vyanzo hivyo vya nishati havingefanya kazi, uhai wa Micah ungekuwa hatarini.
Ulimwengu wa leo ambamo Micah alizaliwa unategemea vyanzo mbalimbali vya nishati. Kila siku sisi hutegemea vyanzo vya nishati kama vile mafuta, makaa ya mawe, na gesi ya asili kwa ajili ya usafiri tunapokwenda kazini, kupika, kuwasha taa, kupasha joto, na kufanya nyumba iwe baridi. Taasisi ya Mali za Asili za Ulimwengu inasema kwamba vyanzo hivyo vya nishati hutumiwa “kutosheleza asilimia 90 hivi ya mahitaji ya nishati katika biashara mbalimbali ulimwenguni.” Ripoti moja iliyochapishwa na Taasisi hiyo katika mwaka wa 2000 inasema: “Mafuta ndiyo hutosheleza mahitaji makubwa zaidi ya nishati ulimwenguni, yaani asilimia 40, kisha makaa ya mawe hutosheleza asilimia 26 na gesi ya asili hutosheleza asilimia 24 hivi.”a
Kulingana na jarida Bioscience, ‘kwa wastani, kila mwaka Mmarekani mmoja hutumia nishati inayolingana na lita 8000 za mafuta kwa matumizi yake yote yanayotia ndani usafiri na kupasha joto au baridi.’ Zaidi ya asilimia 75 ya nguvu za umeme ambazo hutumiwa huko Afrika Kusini, Australia, China, na Poland hutokezwa na mitambo inayoendeshwa kwa makaa ya mawe. Asilimia 60 ya umeme unaotumiwa nchini India na zaidi ya asilimia 50 ya umeme unaotumiwa huko Marekani na Ujerumani hutokezwa kwa makaa ya mawe.
Mwandishi wa habari anayeitwa Jeremiah Creedon anasema hivi katika makala yenye kichwa, “Jinsi Maisha Yatakavyokuwa Mafuta Yakiisha”: “Ni watu wachache tu wanaofahamu kwamba sasa mazao ya chakula yanayotokezwa ulimwenguni pote hutegemea mafuta. Leo, petroli na gesi ya asili ni muhimu sana katika hatua zote za kilimo, kuanzia hatua ya kutengeneza mbolea hadi ile ya usafirishaji wa mazao.” (Gazeti Utne Reader) Lakini vyanzo vya nishati vinavyoendeleza uhai wa wanadamu vinategemeka kadiri gani? Je, tunaweza kupata njia nyingine za kutokeza nishati bila kuchafua mazingira?
[Maelezo ya Chini]
a Ili upate habari zaidi kuhusu uchimbaji wa mafuta, ona gazeti la Amkeni! la Novemba 8, 2003, ukurasa wa 3-12.
-
-
Kwa Nini Tunahitaji Vyanzo Vipya vya Nishati?Amkeni!—2005 | Machi 8
-
-
Kwa Nini Tunahitaji Vyanzo Vipya vya Nishati?
“Leo ukosefu wa mafuta ni tatizo, lakini miaka 20 ijayo utakuwa janga kubwa.”—Jeremy Rifkin, wa Shirika la Masuala ya Uchumi, huko Washington, D.C., Agosti 2003.
KARIBU miaka 20 ijayo, wakati ambapo Micah anayetajwa katika makala iliyotangulia atakuwa na umri wa kutosha kuendesha gari, matumizi ya nishati ulimwenguni pote “yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 58,” yasema ripoti ya serikali ya Marekani inayoitwa International Energy Outlook 2003 (IEO2003). Gazeti New Scientist linasema kwamba hilo litakuwa “ongezeko kubwa zaidi la mahitaji ya nishati katika historia.” Je, vyanzo vya nishati ambavyo vimetumiwa kwa muda mrefu vitatosheleza uhitaji huo? Fikiria mambo yafuatayo.
MAKAA YA MAWE:
◼ Kati ya vyanzo vyote vya nishati vyenye kaboni, makaa ya mawe ndiyo hupatikana kwa wingi, kwani inakadiriwa kwamba yale yaliyopo yanaweza kutumiwa kwa miaka 1,000. Vituo vinavyotokeza nishati kwa makaa ya mawe hutokeza asilimia 40 hivi ya umeme unaotumiwa ulimwenguni. Australia ndiyo nchi inayouza kiasi kikubwa zaidi cha makaa ya mawe katika nchi za nje, kwani thuluthi moja hivi ya makaa ya mawe yanayotumiwa ulimwenguni hutoka huko.
Hata hivyo, ripoti moja ya hivi majuzi ya Taasisi ya Worldwatch inasema: “Kati ya vyanzo vya nishati vyenye kaboni, makaa ya mawe ndiyo hutokeza kiasi kikubwa cha kaboni, kwani hutokeza asilimia 29 ya kaboni kuliko mafuta na asilimia 80 kuliko gesi ya asili, yanapotumiwa kutokeza kiasi kilekile cha nishati. Kila mwaka makaa ya mawe hutokeza asilimia 43 ya kaboni ulimwenguni pote, yaani, tani bilioni 2.7 hivi.” Zaidi ya kuchafua mazingira, makaa ya mawe huathirije afya ya wanadamu yanapochomwa? Ripoti moja ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa ya Global Environment Outlook ilitoa mfano mmoja iliposema hivi: “Kila mwaka nchini China, moshi na chembechembe ambazo hutokezwa wakati makaa ya mawe yanapochomwa husababisha zaidi ya vifo 50 000 vya mapema na kusababisha watu 400 000 wapate ugonjwa wa mkamba katika majiji 11 ya nchi hiyo.”
MAFUTA:
◼ Ulimwenguni pote watu hutumia karibu lita bilioni 12 za mafuta kila siku. Kati ya lita trilioni 320 hivi za mafuta zilizokadiriwa kuwepo katika hifadhi za mafuta ulimwenguni, tayari lita trilioni 144 hivi zimetumiwa. Inatarajiwa kwamba mafuta yakiendelea kutokezwa kwa kiwango cha sasa, yatadumu kwa miaka mingine 40.
Hata hivyo, wataalamu Colin J. Campbell na Jean H. Laherrère walisema hivi katika mwaka wa 1998: “Katika kipindi cha miaka kumi ijayo, kiasi cha mafuta yanayopatikana kwa urahisi hakitaweza kutosheleza mahitaji.” Wataalamu hao wa mafuta walionya hivi: “Watu wengi hufikiri kimakosa kwamba tone la mwisho la mafuta litavutwa kutoka ardhini kwa urahisi sawa na vile mafuta yanavyovutwa kwa urahisi leo. Ukweli ni kwamba kiasi cha mafuta yanayovutwa kutoka katika kisima chochote au nchi yoyote ile hupanda hadi kiwango cha juu zaidi, kisha yanapokaribia kufikia nusu, kiwango hicho huanza kushuka polepole na hatimaye mafuta huacha kutoka. Kwa upande wa uchumi, jambo kuu si wakati ambapo mafuta yatakwisha kabisa bali ni wakati ambapo kiwango cha mafuta yanayovutwa kitaanza kupungua.”
Kiwango cha uzalishaji wa mafuta kitaanza kupungua lini? Mtaalamu wa mafuta Joseph Riva anasema kwamba “ongezeko la uzalishaji wa mafuta linalopangiwa . . . halifikii nusu ya kiasi cha mafuta ambacho Shirika la Kimataifa la Nishati linakadiria kitahitajiwa ulimwenguni pote kufikia mwaka wa 2010.” Gazeti New Scientist linaonya hivi: “Ikiwa viwango vya uzalishaji wa mafuta vitashuka huku mahitaji yakiendelea kuongezeka, huenda bei za mafuta zitapanda na kushuka mara nyingi na kusababisha matatizo ya uchumi, matatizo ya kusafirisha chakula na bidhaa nyinginezo, na hata vita baina ya mataifa yanayopigania kiasi kidogo cha mafuta yaliyosalia.”
Ingawa wataalamu fulani wanafikiri kwamba kupungua kwa mafuta ni tatizo, wengine wanafikiri kwamba ni afadhali tusikawie kuacha kutegemea mafuta. Jeremiah Creedon aliandika hivi katika gazeti Utne Reader: “Tatizo kubwa zaidi ya kutokuwa na mafuta ni kuendelea kuwa nayo. Ingawa kiasi cha kaboni-dioksidi inayotokezwa tunapotumia mafuta huendelea kuongeza joto la dunia, wakati masuala ya uchumi yanapozungumziwa masuala ya mazingira hayazungumziwi.” Tume moja ya Australia ilisema hivi kuonyesha jinsi nchi moja ilivyoathiriwa kwa kutegemea sana mafuta: “Magari milioni 26 yaliyoko Uingereza hutokeza thuluthi moja ya kaboni-dioksidi inayotokezwa nchini humo (ambayo husababisha ongezeko la joto la dunia) na thuluthi moja ya uchafuzi wa hewa nchini humo (ambao husababisha vifo vya watu wapatao 10,000 kila mwaka).”
GESI YA ASILI:
◼ Kulingana na ripoti ya IEO2003, katika kipindi cha miaka 20 hivi ijayo, “inatarajiwa kwamba gesi ya asili ndiyo itakayokuwa chanzo kikuu cha nishati ulimwenguni.” Kati ya vyanzo vya nishati vyenye kaboni, gesi ya asili ndiyo haichafui mazingira sana inapochomwa, na inasemekana dunia ina kiasi kikubwa sana cha gesi ya asili.
Hata hivyo, Shirika la Gesi ya Asili lililoko Washington, D.C., linasema kwamba “kiasi kilichopo cha gesi ya asili hakiwezi kujulikana hadi gesi hiyo inapovutwa” kutoka ardhini. Kisha linaongeza hivi: “Makadirio mbalimbali hutegemea dhana tofauti-tofauti . . . Hivyo ni vigumu sana kujua kiasi kilichopo cha gesi ya asili.”
Methani ndiyo hufanyiza sehemu kuu ya gesi ya asili, nayo ni “gesi inayosababisha sana ongezeko la joto la dunia. Kwa hakika, methani ina uwezo wa kunasa joto karibu mara 21 zaidi ya kaboni-dioksidi,” lasema shirika lililotajwa awali. Hata hivyo, shirika hilo linasema kwamba uchunguzi mkubwa uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Mazingira na Taasisi ya Uchunguzi wa Gesi “ulionyesha kuwa faida za kuongeza matumizi ya gesi ya asili ili kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vyanzo vingine vya nishati, ni kubwa kuliko madhara yanayotokezwa na methani.”
NISHATI YA ATOMU:
◼ Gazeti Australian Geographic linasema kwamba “mitambo 430 hivi ya nyuklia hutumiwa kutokeza asilimia 16 hivi ya umeme unaotumiwa ulimwenguni.” Mbali na mitambo ya nyuklia iliyopo, ripoti ya IEO2003 inasema: “Kufikia Februari 2003, mitambo 17 kati ya 35 inayojengwa ulimwenguni inapatikana katika nchi zinazoendelea za Asia.”
Licha ya uwezekano wa kutokea kwa misiba, kama ule uliotokea mwaka wa 1986 huko Chernobyl katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti, bado nishati ya nyuklia hutumiwa sana. Gazeti New Scientist linaripoti kwamba “mitambo ya nyuklia ya Marekani inashika kutu na kuharibika.” Pia linaripoti kwamba katika Machi 2002, mtambo wa Davis-Besse huko Ohio “ulikuwa karibu kuungua na kutokeza msiba mkubwa” kwa sababu ya kutu.
Kwa kuwa vyanzo vya nishati vinavyotumiwa sasa vinapungua na kuna hatari nyingi zinazosababishwa na kutokezwa kwa nishati, je, wanadamu wataiharibu dunia wakijaribu kutosheleza mahitaji yao makubwa ya nishati? Ni wazi kwamba tunahitaji vyanzo vinavyotegemeka ambavyo vinaweza kutumiwa kutokeza nishati bila kuchafua mazingira. Je, tunaweza kuvipata? Na je, vinaweza kutumiwa kutokeza nishati kwa gharama ya chini?
-
-
Njia Mpya za Kutokeza NishatiAmkeni!—2005 | Machi 8
-
-
Njia Mpya za Kutokeza Nishati
UPEPO:
◼ Kwa muda mrefu wanadamu wametumia upepo kuendesha merikebu, vinu, na kupiga maji. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, nchi nyingi ulimwenguni zimevutiwa na chanzo hicho cha nishati. Ulimwenguni pote, watu milioni 35 hupata umeme kutokana na vinu vya upepo vya hali ya juu ambavyo hutumiwa kutokeza nishati ya kutosha na inayodumu bila kuchafua mazingira. Nchini Denmark, upepo hutumiwa kutokeza asilimia 20 ya umeme unaotumiwa huko. Ujerumani, Hispania, na India zimeanza kutumia nishati inayotokana na upepo, na India ndiyo nchi ya tano ulimwenguni iliyo na uwezo mkubwa wa kutumia upepo kutokeza nishati. Kwa sasa, Marekani ina vinu vya upepo 13,000 vinavyotokeza umeme. Na wataalamu fulani wanasema kwamba maeneo yote yanayoweza kutokeza nishati ya upepo nchini Marekani yakitumiwa, nchi hiyo itaweza kutokeza zaidi ya asilimia 20 ya nguvu za umeme inazohitaji.
JUA:
◼ Betri fulani hutokeza umeme kwa kutumia mwangaza wa jua wakati miale ya jua inapochochea elektroni zilizo katika betri hizo. Ulimwenguni pote, karibu wati milioni 500 za umeme hutokezwa kwa njia hiyo, na uuzaji wa betri hizo huongezeka kwa asilimia 30 kwa mwaka. Hata hivyo, kwa sasa betri hizo hazitokezi nishati ya kutosha, na gharama ya kutokeza umeme kwa kutumia betri hizo ni kubwa ikilinganishwa na gharama ya kutumia vyanzo vingine kama vile makaa ya mawe, mafuta, na gesi ya asili. Isitoshe, kemikali zenye sumu kama vile salfaidi ya kadimiamu, aseniki, na gallium hutumiwa kutengeneza betri hizo. Kwa kuwa kemikali hizo huendelea kuwepo katika mazingira kwa karne nyingi, gazeti Bioscience linasema kwamba “huenda kuharibu betri zilizokwisha na kutumia tena vitu vilivyotumiwa kuzitengeneza kukawa tatizo kubwa.”
NISHATI YA MVUKE UNAOTOKA ARDHINI:
◼ Mtu akichimba shimo kuanzia tabaka la nje la dunia na kuelekea kwenye kiini cha dunia ambacho kinakadiriwa kuwa na joto la nyuzi 4,000 Selsiasi, joto litaongezeka kwa wastani wa karibu nyuzi 30 Selsiasi kwa kila kilometa moja anayochimba. Hata hivyo, watu wanaoishi karibu na chemchemi za maji ya moto au nyufa za volkeno wanaweza kutumia joto la dunia kwa urahisi ili kutokeza nishati. Maji ya moto au mvuke unaotoka kwenye tabaka la nje la dunia hutumiwa katika nchi 58 kupasha nyumba joto au kutokeza umeme. Karibu asilimia 50 ya nishati inayotumiwa nchini Iceland hutokezwa kwa mvuke unaotoka ardhini. Nchi nyingine, kama vile Australia, zinapanga kupata nishati kutoka kwenye miamba yenye joto iliyo kilometa chache tu chini ya uso wa dunia. Gazeti Australian Geographic linaripoti hivi: “Watafiti fulani wanasema kwamba maji yakisukumwa chini kwa pampu hadi kwenye maeneo hayo yenye joto, kisha yanapokuwa moto yatumiwe kuendesha injini za mvuke wakati yanaporudi juu kwa nguvu nyingi sana, tunaweza kutokeza nishati kwa miaka mingi au hata kwa karne nyingi.”
MAJI:
◼ Tayari zaidi ya asilimia 6 ya nishati inayotumiwa ulimwenguni hutoka katika vituo vya kutokeza umeme kwa kutumia maji. Kulingana na ripoti ya International Energy Outlook 2003, katika kipindi cha miaka 20 ijayo, “miradi mikubwa ya kutokeza nguvu za umeme kwa maji katika nchi zinazoendelea, hasa barani Asia, itasababisha ongezeko la matumizi ya vyanzo vya nishati visivyoweza kuisha.” Hata hivyo, gazeti Bioscience linaonya hivi: “Mara nyingi maji yaliyohifadhiwa hufunika mashamba yenye rutuba na yanayofaa sana kwa kilimo. Isitoshe, mabwawa huathiri mimea, wanyama, na viumbe wadogo katika mazingira.”
HIDROJENI:
◼ Hidrojeni ni gesi ambayo haina rangi wala harufu, lakini inaweza kushika moto. Ni elementi inayopatikana kwa wingi ulimwenguni. Hidrojeni inayopatikana duniani hufanyiza sehemu kubwa ya chembe za mimea na za wanyama, inapatikana katika makaa ya mawe, mafuta, na gesi ya asili, na ni kimojawapo cha vitu viwili vinavyofanyiza maji. Zaidi ya hayo, mazingira hayachafuliwi sana hidrojeni inapounguzwa na ina faida kubwa ikilinganishwa na makaa ya mawe, mafuta, na gesi ya asili.
Jarida Science News Online linasema kwamba maji “yanaweza kugawanywa kuwa hidrojeni na oksijeni kwa kutumia umeme.” Ijapokuwa mbinu hiyo inaweza kutumiwa kutokeza kiasi kikubwa cha hidrojeni, jarida hilo linasema kwamba “mbinu hiyo inayoonekana kuwa rahisi inagharimu pesa nyingi.” Ulimwenguni pote, tani milioni 45 hivi za hidrojeni hutokezwa viwandani ili kutengeneza mbolea na bidhaa za usafi. Lakini hidrojeni hiyo hutokezwa kwa kutumia makaa ya mawe, mafuta, na gesi ya asili, na hilo hutokeza gesi yenye sumu inayoitwa kaboni-monoksidi na gesi ya kaboni-dioksidi ambayo husababisha ongezeko la joto duniani.
Hata hivyo, watu wengi husema kwamba kati ya vyanzo vingine vya nishati vinavyopangiwa kutumiwa, hidrojeni ndiyo inayotarajiwa kuwa chanzo kikuu cha nishati na kwamba inaweza kutosheleza mahitaji ya wanadamu ya nishati ya wakati ujao. Maoni hayo yanategemea hatua kubwa iliyochukuliwa hivi majuzi kuboresha kifaa fulani cha kutokeza hidrojeni.
NISHATI INAYOTOKANA NA HIDROJENI:
◼ Kuna kifaa ambacho hutokeza umeme kwa kutumia hidrojeni. Badala ya kuunguza hidrojeni, kifaa hicho huiunganisha na oksijeni katika utendaji fulani wa kemikali unaodhibitiwa kwa usahihi. Hidrojeni safi inapotumiwa badala ya vyanzo vingine vya nishati vyenye hidrojeni nyingi, vitu vya ziada vinavyotokezwa ni joto na maji pekee.
Katika mwaka wa 1839, Sir William Grove, ambaye alikuwa hakimu na mwanafizikia Mwingereza, alibuni kifaa cha kwanza kinachotokeza umeme kwa kutumia hidrojeni. Lakini, kutengeneza vifaa hivyo kuligharimu pesa nyingi, na ilikuwa vigumu kupata vitu vilivyohitajiwa ili kutokeza nishati kwa njia hiyo. Hivyo, mbinu hiyo ya kutokeza nishati haikutumiwa hadi katikati ya karne ya 20, wakati ambapo vifaa hivyo vilipoboreshwa ili vitumiwe kutokeza nishati ya kuendesha vyombo vya angani vya Marekani. Vyombo vya angani vya kisasa vingali vinatumia vifaa hivyo ili kutokeza nishati vinapokuwa angani, lakini mbinu hiyo inaboreshwa ili itumiwe hasa duniani.
Leo vifaa vya aina hiyo vinaboreshwa ili vitumiwe badala ya injini za magari zinazotumia petroli, pia vinaboreshwa ili vitokeze umeme unaotumiwa katika majengo ya kibiashara na ya makazi, na katika vifaa vidogo vya elektroni kama vile simu za mkononi na kompyuta. Hata hivyo, wakati ambapo makala hii ilikuwa ikiandikwa, gharama ya kutokeza umeme kwenye vituo ambavyo hutumia vifaa hivyo ilizidi mara nne gharama ya kutokeza umeme kwa makaa ya mawe, mafuta, na gesi ya asili. Hata hivyo, mamia ya mamilioni ya dola hutumiwa kuboresha teknolojia hiyo mpya.
Ni wazi kwamba kuna faida za kuanza kutumia vyanzo vya kutokeza nishati bila kuchafua mazingira. Hata hivyo, gharama ya kutokeza nishati kwa njia hiyo ni kubwa sana hivi kwamba huenda isiwezekane kufanya hivyo. Ripoti ya IEO2003 inasema hivi: “Inasemekana kwamba wakati ujao watu wengi watataka . . . nishati inayotokana na vyanzo vya nishati vyenye kaboni (mafuta, gesi ya asili, na makaa ya mawe), kwani inatazamiwa kwamba nishati hiyo itapatikana kwa bei nafuu, na gharama ya kutokeza nishati kwa njia nyingine itakuwa juu zaidi.”
[Picha katika ukurasa wa 9]
Gari linalotumia vifaa vinavyotokeza nishati kwa hidrojeni, 2004
[Hisani]
Mercedes-Benz USA
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
DOE Photo
-
-
Kupata Chanzo cha Nishati YoteAmkeni!—2005 | Machi 8
-
-
Kupata Chanzo cha Nishati Yote
JUA ndicho chanzo kikuu cha nishati inayotumiwa duniani. Wanasayansi wengi wanasema kwamba makaa ya mawe na mafuta yametokana na miti na mimea iliyooza ambayo hapo zamani ilipata nishati kutoka kwa jua.a Maji yanayotumiwa katika mabwawa ya kutokeza umeme huvutwa kutoka baharini na joto la jua kisha yanapelekwa juu ya nchi kavu yakiwa mawingu. Miale ya jua husukuma pepo ambazo huendesha jenereta. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba nusu ya sehemu ya bilioni ya nishati inayotoka kwa jua ndiyo hufika duniani.
Ijapokuwa jua lina nishati nyingi sana, kuna mabilioni ya vyanzo vingine vikubwa vya nishati katika ulimwengu wote. Nishati yote hiyo hutoka wapi? Mwandikaji wa Biblia, Isaya, anasema hivi kuhusu nyota: “Inueni macho yenu juu, mwone. Ni nani ameviumba vitu hivi? Ni Yeye anayelileta jeshi lake kulingana na hesabu, ambaye zote anaziita kwa jina. Kutokana na wingi wa nguvu zenye msukumo, yeye pia akiwa hodari katika nguvu, hakuna hata moja kati ya hizo inayokosekana.”—Isaya 40:26.
Ijapokuwa sisi hustaajabia nishati nyingi sana ya nyota mbalimbali, sisi hustaajabu hata zaidi tunapomfikiria Muumba wa nyota hizo. Hata hivyo, Biblia hutuhimiza hivi: “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi.” (Yakobo 4:8) Naam, Muumba wa dunia na vyanzo vingi vya nishati vinavyopatikana duniani, yeye aliyetupa sisi uhai, anaweza kupatikana na wale wanaomtafuta.—Mwanzo 2:7; Zaburi 36:9.
Huenda watu fulani wakashindwa kuamini kwamba Mungu anaijali dunia na wanadamu wanapoona dunia na mali zake za asili zikichafuliwa na kutumiwa kwa ubaguzi. Hata hivyo, Biblia inatuhakikishia kwamba hivi karibuni kutakuwa na badiliko kubwa kuhusu uongozi wa dunia na ugawanyaji wa mali za asili zilizomo duniani. (Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10) Kwa kusimamisha serikali moja ya mbinguni itakayotawala ulimwengu wote chini ya uongozi wa Mwana wake, Kristo Yesu, Yehova Mungu atahakikisha kwamba wanadamu wote wanafaidika na mali za asili zilizomo duniani bila ubaguzi. (Mika 4:2-4) Isitoshe, ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia,’ yaani, wale wanaochafua mazingira ya dunia katika njia ya kiroho au ya kimwili.—Ufunuo 11:18.
Wakati huo, ahadi hii inayopatikana katika Isaya 40:29-31 itatimia kwa njia ya kiroho na ya kimwili: “Yeye anampa nguvu mtu aliyechoka; naye huzijaza nguvu kamili kwa mtu asiye na nguvu zenye msukumo. Wavulana watachoka na pia kuzimia, na vijana hakika watajikwaa, lakini wale wanaomtumaini Yehova watapata nguvu mpya. Wataruka juu kwa mabawa kama tai. Watakimbia wala hawatazimia; watatembea wala hawatachoka.” Ukijifunza Biblia, wewe pia unaweza kujua mengi zaidi kuhusu Chanzo cha nishati yote na kuhusu suluhisho la matatizo ya nishati yanayoikabili dunia.
[Maelezo ya Chini]
a Ona sanduku “Mafuta Yalitoka Wapi?” katika gazeti la Amkeni! la Novemba 8, 2003.
-