-
Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?Amkeni!—2006 | Septemba
-
-
Je, Mabadiliko ya Chembe za Urithi Yanaweza Kutokeza Jamii Mpya?
Habari nyingi kuhusu mimea na wanyama zinategemea maagizo yaliyo katika chembe za urithi, yaani, maagizo yaliyo katika kiini cha kila chembe.d Watafiti wamegundua kwamba mabadiliko ya chembe za urithi, au mabadiliko yasiyo na mpango ya maagizo katika chembe za urithi yanaweza kutokeza mabadiliko katika vizazi vya wanyama na mimea. Mnamo 1946, Hermann J. Muller, mshindi wa Tuzo la Nobeli na mwanzilishi wa uchunguzi wa mabadiliko ya chembe za urithi, alidai hivi: “Mabadiliko mengi madogo ambayo hayatokei mara nyingi si njia ya msingi ya mwanadamu kuboresha wanyama na mimea tu, bali ndiyo njia hasa ambayo mageuzi yakiongozwa na uteuzi wa kiasili yametukia.”
Kwa kweli, fundisho la mageuzi makubwa linategemea dai la kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayatokezi tu spishi mpya, yaani, aina za mimea na wanyama, bali pia jamii mpya kabisa. Je, kuna njia yoyote ya kuthibitisha dai hilo la kishupavu? Hebu fikiria kile ambacho kimefunuliwa katika miaka 100 hivi ya uchunguzi wa chembe za urithi.
Katika miaka ya 1930, wanasayansi walisisimkia wazo la kwamba ikiwa uteuzi wa kiasili, yaani, kusalimika kwa viumbe bora na kufa kwa visivyo bora, kungeweza kutokeza spishi mpya za mimea kutokana na mabadiliko yanayotukia bila mpango, basi mabadiliko hayo yakiongozwa na mwanadamu yanapaswa kuwa na matokeo makubwa zaidi. Wolf-Ekkehard Lönnig, mwanasayansi katika Taasisi ya Max Planck ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea nchini Ujerumani, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Msisimko huo hasa ulienea miongoni wa wanabiolojia, na hasa miongoni mwa wataalamu wa chembe za urithi na wazalishaji wa mimea na wanyama.” Kwa nini kulikuwa na msisimko huo? Lönnig, ambaye amechunguza mabadiliko ya chembe za urithi kwa miaka 28 hivi, anasema: “Watafiti hao walidhani wakati wa kubadili njia za msingi za kuzalisha mimea na wanyama ulikuwa umewadia. Walifikiri kwamba kwa kuchochea mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, wangeweza kutokeza mimea na wanyama wapya walio bora.”e
Wanasayansi nchini Marekani, Asia, na Ulaya walianzisha miradi ya utafiti iliyodhaminiwa kwa pesa nyingi, nao walitumia njia walizotarajia kwamba zingeharakisha hatua za mageuzi. Kumekuwa na matokeo gani baada ya utafiti mkubwa ambao umechukua miaka 40? “Licha ya gharama kubwa,” asema mtafiti Peter von Sengbusch, “majaribio ya kutokeza mabadiliko ya chembe za urithi kupitia njia fulani ya kisayansi, yaliambulia patupu.” Lönnig alisema: “Kufikia miaka ya 1980, matumaini na msisimko uliokuwapo miongoni mwa wanasayansi yaligonga mwamba ulimwenguni pote. Miradi ya uchunguzi wa kuzalisha mimea na wanyama kwa kubadili chembe za urithi ilitupiliwa mbali katika nchi za Magharibi. Karibu mimea na wanyama wote waliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi walikuwa na ‘dosari,’ nao walikufa au wakawa dhaifu kuliko wale ambao chembe zao zilibadilika kiasili.”f
Hata hivyo, habari ambayo imekusanywa kwa miaka 100 ya utafiti wa mabadiliko ya chembe za urithi na hasa miaka 70 ya utafiti wa kuzalisha mimea na wanyama kwa kubadili chembe hizo, imewawezesha wanasayansi kukata kauli mbalimbali kuhusu uwezo wa kutokeza jamii mpya kwa kubadili chembe hizo. Baada ya kuchunguza uthibitisho uliokuwa umetolewa Lönnig alisema: “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa. Kauli hiyo inapatana na majaribio na matokeo ya utafiti ambao umefanywa katika karne ya 20 na pia inapatana na sheria za uwezekano. Hivyo, sheria ya mabadiliko yanayojirudia-rudia huonyesha kwamba spishi ambazo zinatofautiana na spishi nyingine kwa kutegemea chembe za urithi huwa na mipaka hususa isiyoweza kuvunjwa au kuvukwa wakati mabadiliko ya chembe hizo yanapotokea kiaksidenti.”
Fikiria uzito wa kauli hiyo. Ikiwa wanasayansi stadi hawawezi kutokeza aina mpya za mimea na wanyama kwa kuchochea mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, je, mageuzi yasiyoongozwa na mtu mwenye akili yanaweza kuwa na matokeo bora? Ikiwa utafiti umethibitisha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadilisha spishi za awali na kutokeza mpya, mageuzi makubwa yangewezaje kutokea?
-
-
Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?Amkeni!—2006 | Septemba
-
-
f Katika majaribio mengi ya kubadili chembe za urithi, idadi ya viumbe wapya ilizidi kupungua huku aina zilezile za mimea na wanyama zikitokezwa. Hilo lilimfanya Lönnig aanzishe “sheria ya mabadiliko yanayojirudia-rudia.” Isitoshe, chini ya asilimia 1 ya mimea iliyotokezwa kwa kubadili chembe za urithi ilitumiwa katika uchunguzi zaidi, na chini ya asilimia 1 ya mimea hiyo ndiyo ilifaa kwa matumizi ya kibiashara. Matokeo ya utafiti uliohusisha wanyama yalikuwa mabaya sana kuliko yale ya mimea hivi kwamba majaribio hayo yakasimamishwa.
-
-
Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?Amkeni!—2006 | Septemba
-
-
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nzi-tunda ambaye chembe zake za urithi zilibadilika (juu), bado ni nzi-tunda, ingawa ana kasoro
[Hisani]
© Dr. Jeremy Burgess/Photo Researchers, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Majaribio ya kubadili chembe za urithi za mimea yalionyesha tena na tena kwamba idadi ya mimea mipya ilipungua sana, huku aina ileile ya mimea iliyobadilika ikitokezwa (Mmea ambao chembe zake za urithi zimebadilishwa una maua makubwa zaidi)
-