-
Je, Msingi wa Mageuzi Wakosekana?Amkeni!—1997 | Mei 8
-
-
Mfumo-Tegemeano—Je, Ni Kizuizi cha Mageuzi?
Darwin alipositawisha nadharia yake, wanasayansi hawakujua jinsi chembe-hai ilivyo tata sana. Biokemia ya kisasa, ambayo ni kuchunguza uhai katika kiwango cha molekuli, imefunua baadhi ya utata huo. Pia imezusha maswali mazito na shaka juu ya nadharia ya Darwin.
Sehemu za chembe zimefanyizwa kwa molekuli. Chembe ndizo vitu vyenye kujenga viumbe hai vyote. Profesa Behe ni mfuasi wa Katoliki ya Kiroma naye anaamini katika mageuzi katika kueleza maendeleo ya baadaye ya wanyama. Hata hivyo, yeye anazusha shaka nzito kama kweli mageuzi yaweza kueleza jinsi chembe ilivyopata kuwapo. Yeye asema juu ya mashine za molekuli ambazo “hutoa mizigo kutoka mahali fulani hadi fulani katika chembe hiyo kupitia ‘barabara kuu’ zilizofanyizwa kwa molekuli nyinginezo . . . Chembe husafiri kwa kutumia mashine, hujinakili kwa kutumia mashine, humeng’enya chakula kwa kutumia mashine. Kwa ufupi, mashine za hali ya juu sana za molekuli huongoza kila utendaji wa chembe. Kwa hiyo kila kijambo kidogo cha uhai kimefanyizwa kwa njia bora zaidi, na mashine ya uhai ni tata sana.”
Sasa, utendaji huu wote unatukia katika nafasi inayotoshanaje? Chembe ya kawaida ina upana wa milimeta 0.03 pekee! Katika nafasi hiyo ndogo sana, kuna utendaji tata ambao ni muhimu kwa uhai. (Ona picha, ukurasa wa 8-9.) Si ajabu kwamba imesemwa: “Jambo kuu ni kwamba chembe—ambayo ni msingi wenyewe wa uhai—ni tata sana.”
Behe abisha kwamba chembe inaweza kutenda ikiwa tu ina sehemu zayo zote. Kwa hiyo, haiwezi kutenda inapobadilika polepole na hatua kwa hatua kupitia mageuzi. Yeye atumia mfano wa mtego wa panya. Chombo hiki sahili chaweza tu kufanya kazi ikiwa sehemu zacho zote zimewekwa. Kila sehemu ikiwa peke yayo—kikanyagio, spring’i, kishikilio, kipigio, kishikio—si mtego wa panya nao hauwezi kufanya kazi. Sehemu zote zinahitajika wakati uleule na lazima zote ziwekwe mahali pazo ndipo zifanyize mtego wa panya ufanyao kazi. Hali kadhalika, chembe yaweza tu kufanya kazi wakati sehemu zayo zote zipo. Yeye atumia mfano huo kueleza kile anachokiita “mfumo-tegemeano.”b
Jambo hilo hutokeza tatizo kubwa kwa hatua za mageuzi, ambazo huhusisha kutokea kitaratibu kwa sehemu fulani-fulani zenye mafaa. Darwin alijua kwamba nadharia yake ya mageuzi ya kitaratibu kupitia uteuzi asilia ilikabili tatizo kubwa aliposema: “Ikiwa inaweza kuthibitishwa kwamba kuna kiungo chochote tata, ambacho hakiwezekani kufanyizwa kwa marekebisho madogo-madogo ya mfululizo, nadharia yangu ingeambulia patupu.”—Origin of Species.
Chembe ya mfumo-tegemeano ni kizuizi kikuu kwa kuitikadi nadharia ya Darwin. Kwanza, mageuzi hayawezi kueleza jinsi vitu visivyo na uhai vilivyopata kuwa hai. Kisha, kuna tatizo la chembe ya kwanza iliyo tata, ambayo ni lazima ingetokea kwa ghafula ikiwa na kila sehemu. Yaani, chembe (au, mtego wa panya) ni lazima ijitokeze yenyewe, ikiwa na kila sehemu na kufanya kazi!
Mfumo-Tegemeano wa Kuganda kwa Damu
Kielelezo kingine cha mfumo-tegemeano ni utendaji ambao sisi huchukua kivivi-hivi—kuganda kwa damu. Kwa kawaida, maji yoyote yale yatavuja mahali ambapo pana tundu nayo yataendelea kuvuja mpaka kiwekeo hicho kiwe kitupu. Lakini, sisi tunapotoboa au kukata ngozi yetu, mvujo huo huzibwa haraka kwa mgando wa damu. Na kama madaktari wajuavyo, “kuganda kwa damu ni mfumo tata sana na wenye mambo mengi ambao una sehemu nyingi za protini zinazotegemeana.” Hizo huchochea kile kiitwacho mfululizo wa kuganda. Hatua hiyo tata ya kupona “hutegemea sana wakati na mwendo ambao utendanaji tofauti-tofauti hutukia.” La, sivyo, mtu aweza kuganda damu yote na kuwa ngumu, au kwa upande mwingine, anaweza kuvuja damu hadi afe. Wakati na mwendo ni muhimu sana.
Uchunguzi wa kibiokemia umeonyesha kwamba kuganda kwa damu hutia ndani mambo mengi sana, ambayo hata moja haliwezi kukosa ili damu igande. Behe auliza: “Mara damu ianzapo kuganda, ni nini kinachoifanya isiendelee kuganda hadi damu yote . . . iwe ngumu?” Yeye aeleza kwamba “mfanyizo, vizuizi, uimarisho, na kuondolewa kwa mgando wa damu” ni sehemu zinazotegemeana za mfumo wa kibiolojia. Sehemu yoyote ikishindwa, basi mfumo wote utashindwa kufanya kazi.
Russell Doolittle, ambaye ni mwanamageuzi na profesa wa biokemia katika Chuo Kikuu cha California, auliza: “Mfumo huu tata na wenye usawaziko ulifanyizwaje kupitia mageuzi? . . . Yaani, ikiwa kila protini ilitegemea kutendeshwa na nyingine, basi mfumo huo wa mgando wa damu ungeanzaje kuwapo? Ama sehemu yoyote ile ingetumikaje bila sehemu nyinginezo zote?” Akitumia hoja za kimageuzi, Doolittle ajaribu kueleza chanzo cha mfumo huo. Hata hivyo, Profesa Behe ataja kwamba “bahati kubwa sana inahitajika kuweka jeni zifaazo katika sehemu zifaazo.” Aonyesha kwamba maelezo ya Doolittle na lugha yake rahisi yaficha magumu mengi sana.
Kwa hiyo, mojawapo mambo makuu yenye kupinga mageuzi ni kizuizi kikubwa sana cha mfumo-tendeano. Behe asema: “Nakazia kwamba uteuzi wa asili, ambalo ndilo jambo kuu la nadharia ya Darwin, unafaulu tu ikiwa kuna kitu cha kuteua—kitu ambacho kina manufaa sasa hivi, wala si kwa wakati ujao.”
-