-
Je, Kweli Unahitaji Kufanya Mazoezi?Amkeni!—2005 | Mei 22
-
-
Hatari za Kukaa Tu Bila Kufanya Mazoezi ya Kutosha
Kwa sababu ya kupunguza mazoezi wanayofanya, watu wengi wanapatwa na matatizo ya kimwili, kiakili, na kihisia. Kwa mfano, hivi karibuni shirika moja la afya nchini Uingereza liliripoti hivi: “Watoto wasiofanya mazoezi wanaweza kukabili hatari ya kutojiheshimu, kuwa na wasiwasi mwingi na mifadhaiko mingi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto hao watavuta sigara na kutumia dawa za kulevya kuliko watoto wanaofanya mazoezi. Wafanyakazi wasiofanya mazoezi hukosa kwenda kazini mara nyingi kuliko wale wanaofanya mazoezi. Wanapozeeka, watu wasiofanya mazoezi hupoteza nguvu na uwezo wa kunyumbulika katika shughuli za kila siku. Matokeo ni kwamba wengi hushindwa kujitegemea na afya yao ya akili huzorota.”
Cora Craig, rais wa Taasisi ya Utafiti wa Mazoezi na Mtindo wa Maisha ya Kanada, anaeleza kwamba “Wakanada wengi hawafanyi kazi ngumu kama hapo awali . . . Kwa ujumla, ni wachache wanaofanya kazi hizo.” Gazeti la Kanada Globe and Mail linaripoti hivi: “Karibu asilimia 48 ya Wakanada ni wazito kupita kiasi, kutia ndani asilimia 15 ambao ni wanene kupita kiasi.” Gazeti hilo linaongezea kwamba huko Kanada, asilimia 59 ya watu wazima hawafanyi mazoezi. Dakt. Matti Uusitupa, wa Chuo Kikuu cha Kuopio, Finland, anaonya kwamba “ugonjwa wa kisukari ambao kwa kawaida huwapata watu wazima unaongezeka kwa haraka ulimwenguni pote kwa sababu watu wengi wamekuwa wanene kupita kiasi na hawafanyi mazoezi.”
Nchini Hong Kong, uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba huenda asilimia 20 hivi ya vifo vyote vilivyotokea miongoni mwa watu walio na umri wa miaka 35 au zaidi, vilisababishwa na kukosa kufanya mazoezi. Uchunguzi huo ulioongozwa na Profesa Tai-Hing Lam wa Chuo Kikuu cha Hong Kong na kuchapishwa na jarida Annals of Epidemiology katika mwaka wa 2004, ulimalizia kwa kusema kwamba kwa Wachina wanaoishi Hong Kong, “hatari za kutofanya mazoezi zinapita zile za kutumia tumbaku.” Watafiti wanatabiri kwamba raia wengine wa China “watapatwa na madhara hayohayo.”
Je, inafaa kuwa na wasiwasi kuhusu hali hiyo? Je, kweli kutofanya mazoezi kunaweza kudhuru afya yetu kuliko kuvuta tumbaku? Watu wengi hukubali kwamba watu wasiofanya mazoezi huelekea kupatwa na shinikizo kubwa la damu, hukabili hatari kubwa ya kupatwa na kiharusi na ugonjwa wa moyo, aina fulani za kansa, ugonjwa wa mifupa, na uwezekano mkubwa wa kuwa wanene kupita kiasi wanapolinganishwa na watu wanaofanya mazoezi.a
Gazeti The Wall Street Journal linaripoti hivi: “Katika kila bara ulimwenguni, kutia ndani maeneo yaliyo na utapia-mlo mwingi, idadi ya watu wazito au wanene kupita kiasi inaongezeka kwa kasi sana. Tatizo hilo linasababishwa hasa na kula vyakula vyenye kalori nyingi na kutofanya mazoezi, jambo ambalo limefanya watu wengi nchini Marekani wawe wanene kupita kiasi.” Dakt. Stephan Rössner, ambaye ni profesa wa masuala ya afya katika Taasisi ya Karolinska huko Stockholm, Sweden, anakubaliana na jambo hilo naye alisema: “Hakuna nchi ulimwenguni ambako tatizo la kunenepa kupita kiasi haliongezeki.”
-
-
Je, Kweli Unahitaji Kufanya Mazoezi?Amkeni!—2005 | Mei 22
-
-
a Kutofanya mazoezi kunaweza kuongeza sana hatari ya kupatwa na magonjwa fulani yanayotishia uhai. Kwa mfano, kulingana na Shirika la Moyo la Marekani, kutofanya mazoezi “huongeza maradufu hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo na huzidisha kwa asilimia 30 hatari ya kupatwa na shinikizo kubwa la damu. Pia huongeza maradufu uwezekano wa kufa kutokana na ugonjwa wa moyo na kiharusi.”
-
-
Je, Kweli Unahitaji Kufanya Mazoezi?Amkeni!—2005 | Mei 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Hasara za Kutofanya Mazoezi
Serikali na mashirika mengi ya afya yanafikiria kwa uzito hasara zinazoipata jamii kwa sababu ya watu kutofanya mazoezi.
● Australia - Nchi hiyo hutumia dola milioni 377 hivi kila mwaka kutibu matatizo ya afya yanayosababishwa na kutofanya mazoezi.
● Kanada - Kulingana na Shirikisho la Moyo Ulimwenguni, katika mwaka mmoja tu Kanada ilitumia dola zaidi ya bilioni mbili kutibu matatizo ya afya “yaliyosababishwa na kutofanya mazoezi.”
● Marekani - Katika mwaka wa 2000, Marekani ilitumia pesa nyingi sana, dola bilioni 76, kwa ajili ya gharama za matibabu yaliyosababishwa moja kwa moja na kutofanya mazoezi.
-