Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Sababu Inayofanya Wengi Wawe na Deni
    Amkeni!—1996 | Desemba 22
    • Sababu Inayofanya Wengi Wawe na Deni

      MICHAEL na Reena walisherehekea ukumbusho wa mwaka wa kwanza wa arusi yao kwa kurudi kwenye mahali walikoenda kwa ajili ya fungate. Lakini mwanzoni mwa mwaka wao wa pili wa ndoa, walikabili uhalisi usiopendeza. Haidhuru walijitahidi kufanya matumizi kwa uangalifu kadiri gani, hawakuweza kulipa bili zao zote.

      Fikiria wenzi wengine wa ndoa. Robert alikuwa na mkopo mdogo tu wa masomo yake alipomwoa Rhonda, naye Rhonda alikuwa na malipo ya gari tu. Robert asema: “Sote tulifanya kazi muda wote, na sote tulikuwa tukichuma dola 2,950 kila mwezi. Lakini hatukuwa tukisonga mahali.” Rhonda aeleza: “Hatukuwa tumefanya ununuzi wowote mkubwa au kufanya chochote kisicho cha kawaida. Nilishindwa kuelewa mahali zilipokuwa zikienda fedha zetu.”

      Robert na Rhonda hawakuwa wavivu. Wala Michael na Reena hawakuwa wavivu. Tatizo lao lilikuwa nini? Madeni ya kadi za mkopo. Mnamo mwaka wao wa kwanza wa ndoa, Michael na Reena waliwiwa dola 14,000 kwa kadi za mkopo. Baada ya miaka miwili ya ndoa, deni la Robert na Rhonda kwa kadi zao za mkopo lilijumlika kuwa dola 6,000.

      Anthony, mwanamume wa makamo mwenye familia, pia alikabili tatizo la kifedha katika maisha yake. Ingawa hivyo, matatizo yake hayakuhusiana na kadi za mkopo. Katika 1993 kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi ilipunguza utokezaji, Anthony akapoteza cheo chake cha usimamizi ambapo alikuwa akilipwa dola 48,000 kwa mwaka. Baada ya hilo, kuandalia familia yake ya watu wanne kukawa tatizo kwake. Vivyo hivyo, Janet, mzazi asiye na mwenzi aishiye New York City, hakuchuma fedha za kutosha kulipia matumizi yake kwa mapato yake ya kila mwaka ya dola 11,000 hivi.

      Ingawa ni kweli kwamba matatizo mengi ya fedha yaweza kuondoshwa kwa kuzishughulikia ifaavyo, uhakika ni kwamba tunaishi katika kipindi cha wakati ambapo wengi wanalemewa kwa sababu ya ‘kuenenda katika ubatili wa nia zao.’ (Waefeso 4:17) Grace W. Weinstein, katika kitabu chake The Lifetime Book of Money Management, aonelea hivi: “Nyingi za kanuni za mbinu za kifedha zimebadilika, zimebadilishwa kabisa na uchumi usiotabirika, mitazamo mipya kuelekea utumizi na uwekaji akiba, na mitindo-maisha yenye kubadilika.” Katika ulimwengu uliovurugika tunamoishi, watu wengi zaidi na zaidi wanapata ikiwa vigumu kushughulikia fedha za kibinafsi na za familia.

      Kwa furaha, Michael na Reena, Robert na Rhonda, Anthony, na Janet wamefaulu kushughulikia fedha zao kwa mafanikio. Kabla ya kufikiria kile kilichowasaidia, acheni tuchunguze aina ya fedha ipatikanayo kwa urahisi ambayo imeongezea ole wa kifedha kwa wengi—ndiyo, kadi za mkopo.

  • Kadi za Mkopo—Je, Zitakutumikia au Zitakutumikisha?
    Amkeni!—1996 | Desemba 22
    • Kadi za Mkopo—Je, Zitakutumikia au Zitakutumikisha?

      “KILA mwezi wakati nifunguapo taarifa zangu za kila mwezi za kadi ya mkopo ni kama msiba wa kuchekwa,” aonelea mwalimu wa Kiingereza katika Marekani. “Natazama kiasi ninachodaiwa kwa mshangao, kana kwamba utu wangu mwingine, ule mbaya, ulikuwa umekwenda katika ununuzi usiodhibitiwa katika maduka ya vichezeo, maduka ya vifaa vya nyumba, maduka makubwa ya bidhaa tofauti-tofauti na vituo vya petroli.”

      Dolores pia aona ikiwa rahisi kulimbikiza deni kwa kulipa kwa kadi ya mkopo. Yeye asema: “Kutumia kadi za mkopo hakutii mtu wasiwasi. Singeweza kutumia fedha halisi jinsi hiyo. Lakini kufanya ununuzi kwa kadi za mkopo ni tofauti. Huoni kamwe fedha ulizotumia hasa. Unachofanya tu ni kutoa kadi yako, nayo yarudishwa kwako.”

      Si ajabu kwamba deni la kadi za mkopo Marekani katika Juni 1995 lilifikia jumla ya dola bilioni 195.2—wastani wa zaidi ya dola 1,000 kwa kila mmiliki kadi! Hata hivyo, kampuni za kadi za mkopo huendelea kubembeleza wateja wapya kwa vichocheo kama vile viwango vya chini vya riba ya mwanzoni na kutokuwapo kwa malipo ya kila mwaka. Ni sihi ngapi za kadi za mkopo ambazo umepokea katika miezi ya majuzi? Nyumba ya wastani ya Marekani hupokea 24 hivi kila mwaka! Mmiliki kadi wa kawaida katika Marekani alitumia kadi kumi za mkopo katika 1994 ili kununua kwa mkopo asilimia 25 zaidi kuliko alivyofanya mwaka uliotangulia.

      Katika Japani, kadi za mkopo ni nyingi zaidi kuliko simu; kuna wastani wa kadi mbili kwa kila Mjapani mwenye umri wa zaidi ya miaka 20. Katika sehemu iliyobaki ya Asia, zaidi ya kadi za mkopo milioni 120 hutolewa, 1 hivi kwa kila wakazi 12. James Cassin, wa MasterCard International, asema: “Asia ndiyo kwa mbali eneo lenye kukua haraka zaidi kwa shughuli za kadi za mkopo.” Msimamizi wa Visa International, Edmund P. Jensen, atabiri: “Tutakuwa jamii yenye kutegemea kadi kwa muda mrefu.”

      Kadi za mkopo kwa wazi zitaendelea kuathiri maisha za watu kwa kiwango kikubwa. Zinapotumiwa vizuri, zaweza kufaidi. Hata hivyo, kuzitumia vibaya kwaweza kusababisha maumivu makali. Kuwa na ujuzi wa msingi kuhusu kadi za mkopo kwaweza kukusaidia kutumia kifaa hiki cha kifedha kwa manufaa yako.

      Aina za Kadi

      Kadi zilizo na sifa nzuri sana ni kadi za benki kama vile Visa na MasterCard. Kadi hizi hutolewa na mashirika ya kifedha na huwa na ada ya kila mwaka, kwa kawaida dola 15 hadi 25 kwa mwaka. Nyakati fulani, ada hii haitozwi, kutegemea rekodi nzuri ya kulipa ya mteja na utumizi wake wa kadi hiyo. Yawezekana kulipa malipo kamili kila mwezi, kwa kawaida bila kutozwa riba yoyote, au yawezekana kulipa kwa sehemu kila mwezi jambo ambalo huhusisha kutozwa riba ya juu. Kikomo cha utumizi huwekwa kutegemea rekodi nzuri ya kulipa ya mteja. Kikomo hicho mara nyingi hupandishwa kadiri uwezo wa kulipa unavyodhihirishwa.

      Kadi za benki pia zina maandalizi ya kupata fedha za kabla ya chumo kwa kutumia mashine za kuweka na kutoa fedha akibani au hundi zilizotolewa na benki. Hata hivyo, kupata fedha kwa njia hii hugharimu sana. Kwa kawaida mtu hutozwa kati ya dola 2 na 5 kwa kila dola 100 zilizokopwa. Na riba kwa fedha hizo za kabla ya chumo hujikusanya kuanzia siku ile fedha zatolewa.

      Mbali na benki, maduka mengi na mfumo wa maduka ya kitaifa yanayohusiana hutoa kadi za mkopo ambazo hukubaliwa kwenye maduka yao. Kwa kawaida hakuna ada ya kila mwaka kwa kadi hizo. Hata hivyo, ikiwa kiasi kinachodaiwa hakilipwi chote, riba yaweza kuwa juu zaidi kuliko kadi za benki.

      Makampuni ya mafuta pia hutoa kadi za mkopo ambazo hazina ada za kila mwaka. Kadi hizi kwa kawaida hukubaliwa kwenye vituo vya petroli vya makampuni hayo tu na nyakati fulani katika mahoteli fulani. Sawa na kadi zinazotolewa na maduka, hizo hurusu malipo kikamili bila riba au malipo baada ya muda fulani kukiwa na riba.

      Pia kuna kadi za kusafiri na za vitumbuizo, kama vile Diners Club na American Express. Aina hii ya kadi ina ada ya kila mwaka lakini haitozi riba, kwa kuwa malipo kamili yapaswa kufanywa mara tu bili ya kila mwezi ipokewapo. Hata hivyo, hakuna tofauti zilizo wazi kati ya kadi hizi na kadi za benki. Kwa kielelezo, American Express hutoa pia kadi ya Optima, ambayo inatoza riba na ni sawa na kadi ya benki.

      Aina tofauti ya kadi inayoingia katika soko la Marekani ni smart card, ikiitwa hivyo kwa sababu ya chipu ya kumbukumbu ya kompyuta iliyotiwa ndani yayo. Yaweza kutumiwa kama kadi ya kupata fedha za kabla ya chumo, kwa kuwa mtumizi aweza kuruhusu chipu hiyo iratibiwe kwa ajili ya kiasi cha fedha kilichowekwa. Gharama ya ununuzi yaweza kutolewa kutoka kwayo na mchuuzi anayehusika. Kufikia mwaka jana Wafaransa tayari walikuwa wakitumia smart cards milioni 23 na Wajapani milioni 11. Imetabiriwa kwamba idadi ya kadi hizo ulimwenguni pote itapanda kufikia zaidi ya bilioni moja kufikia mwaka 2000.

      Kabla ya kupata kadi ya mkopo, mtu angetenda kwa hekima kutoa uangalifu kwa masharti ya mkopo. “Masharti ya muhimu ya mkopo ya kufikiria,” kulingana na broshua iliyochapishwa na Federal Reserve System ya Serikali ya Marekani ni “kiwango cha asilimia cha kila mwaka (APR), ada ya kila mwaka, na kipindi cha kuhurumiwa.” Miongoni mwa mambo mengine ya kufikiria ni fedha za kabla ya chumo na ada zinazotozwa mtu akipita kikomo na vilevile malipo yanayotozwa kwa kuchelewa kulipa mkopo.

      Utozwaji wa Fedha—Ni wa Juu Kiasi Gani?

      Utozwaji wa fedha ambao watu hupaswa kulipa wanaposhindwa kulipa fedha zao za kila mwezi kikamili waweza kuwa wa juu sana kuliko wanavyofikiri watu wengi. Kwa kielelezo, fikiria ile APR, ambayo ni kiwango cha gharama halisi ya mkopo. Uhusiano wa kiwango cha riba ya kila mwaka na APR waweza kutolewa kielezi hivi. Tuseme unamkopesha rafiki dola 100 naye akulipa dola 108 mwishoni mwa mwaka. Katika kisa hicho, rafiki yako akulipa riba ya kila mwaka ya asilimia 8. Hata hivyo, tuseme yeye akulipa mkopo huo wa dola 100 nusu-nusu kwa miezi 12 kila mwezi akilipa dola 9. Jumla mwishoni mwa mwaka bado itakuwa dola 108, lakini wewe, mkopeshaji, umeweza kutumia fedha hizo kadiri malipo yalivyofanywa kila mwezi. Hiyo APR kwenye mkopo huo hupigwa hesabu kuwa asilimia 14.5!

      Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Federal Reserve System ya Marekani mwaka jana, APR ya kadi za mkopo za benki huanzia na asilimia 9.94 na kuendelea hadi asilimia 19.80, kawaida ikiwa kati ya asilimia 17 na 19. Ingawa mashirika fulani hutoa viwango vya chini vya kuanzia, kwa kawaida asilimia 5.9, hayo yaweza kuongeza mara tu kipindi cha kuanza kinapokwisha. Viwango pia hupandishwa ikiwa shirika la kutoa kadi lagundua kuongezeka kwa hatari. Watoaji fulani huadhibu wenye kuchelewa kulipa kwa kuongeza kiwango chao cha riba. Adhabu pia hutolewa kwa kupita kikomo cha utumizi.

      Katika nchi za Asia, viwango vya asilimia vya kila mwaka kwenye kadi vyaweza kuwa juu sana. Kwa kielelezo, kadi fulani za benki hutoza asilimia 24 katika Hong Kong, asilimia 30 katika India, asilimia 36 katika Indonesia, asilimia 45 katika Filipino, asilimia 24 katika Singapore, na asilimia 20 katika Taiwan.

      Kwa wazi, kadi za mkopo huandaa mkopo kwa urahisi lakini mkopo ulio ghali sana. Kuingia ndani ya duka na kupata madeni utakayolipa kwa kadi ya mkopo ni kama kuingia ndani ya benki na kukopa fedha kwa kiwango cha juu mno cha riba. Hata hivyo, karibu wamiliki kadi 3 kati ya 4 katika Marekani hufanya hivyo hasa! Hao huwa na deni kubwa sana ambalo hulipa kwa riba ya juu mno. Katika Marekani, deni la wastani la kila mwezi kwa Visa na MasterCard mwaka uliopita lilikuwa dola 1,825, na watu wengi huwa na madeni ya kiasi hicho katika kadi kadhaa za mkopo.

      Mtego Uwezao Kukutumikisha

      Ruth Susswein, mkurugenzi mkuu wa Bank Cardholders of America, asema kwamba watumizi wa kadi hawatambui matatizo ya kifedha yawezayo kuwapata. Yeye ataja kwamba kwa mtumizi wa kadi anayelipa malipo ya chini zaidi—dola 36 kwa mwezi—kwa deni la kadi ya mkopo la dola 1,825 ingemchukua miaka zaidi ya 22 kulipa deni hilo.a Kwa sababu ya malipo ya riba yaliyoongezeka, kwa wakati huo mteja huyo angelipa dola 10,000 hivi kwa deni la dola 1,825! Na itakuwa hivyo ikiwa hakutoza chochote kingine kwenye kadi yake! Kwa hiyo, ikiwa una mwelekeo wa kufanya ununuzi kupita kiasi, kadi za mkopo pochini mwako zaweza kuwa mtego.

      Watu huingiaje mtegoni? Robert, aliyetajwa katika makala ya kwanza, asema: “Tulinunua vitu ambavyo hatukuvihitaji. Tukajiunga na klabu cha mazoezi ya mwili ambacho hatukuenda. Tulinunua nyumba iwezayo kuhamishwa, na kutumia maelfu ya dola kuitengeneza bila kufikiri kama ilistahili hayo yote. Hatukufikiria kamwe matokeo ya madeni yetu.”

      Reena, aliyetajwa pia katika makala iliyotangulia, aeleza kilichompata yeye na mume wake, Michael: “Tulitumbukia katika deni tu. Baada ya ndoa tulinunua kila kitu tulichohitaji, tukitumia kadi za mkopo. Kwa ada za bima na ununuzi ambao hatukuweza kutumia kadi, tulitumia chaguo la fedha za kabla ya chumo kwenye kadi zetu za mkopo. Mnamo mwaka mmoja deni letu lilifikia dola 14,000. Kutambua kwamba mengi ya malipo yetu ya kadi za mkopo yalikuwa yakilipa riba kulitufungua macho.”

      Je, Umiliki Kadi?

      Baada ya kufikiria matatizo ya kifedha ambayo kadi za mkopo zimetumbukiza mamilioni ya watu, wengine huenda wakajibu la. Daphne, mwenye umri wa miaka 32, asema: “Wazazi wangu hawakuwa kamwe na kadi ya mkopo, na hawakuitaka.” Kwa wazi, mmiliki kadi 1 kati ya 4 wa Marekani hutumia kadi yake kwa hekima. Yeye hupata manufaa bila kupatwa na maumivu ya kulipa utozwaji wa riba ulio juu mno. Maria ni mtu wa aina hiyo. “Mimi hupenda urahisi wayo,” yeye asema. “Sihitaji kubeba fedha nyingi. Nikiona kitu ninachohitaji mahali ambapo vitu vimepunguzwa bei, naweza kukipata.”

      Maria aendelea: “Sikuzote mimi huhakikisha nina fedha za kutosha kulipia ununuzi huo. Sijapata kutumia chaguo la fedha za kabla ya chumo. Na sijapata kamwe kulipa utozwaji wowote wa kifedha.” Ni rahisi kutumia kadi ya mkopo wakati wa kuagiza chumba mapema katika hoteli, na ni ya lazima katika Marekani wakati wa kukodi gari.

      Hata hivyo, watu fulani huongozwa na msukumo kwa habari ya ununuzi. Huenda wakaweza kufanya ununuzi kuwa jambo la uangalifu mwingi zaidi kwa kutumia fedha taslimu. Michael na Reena hawakutaka kuwa katika deni kuwe njia ya maisha. Kwa hiyo waliamua kutotumia kadi zozote za mkopo kwa miaka mitano—isipokuwa wakati wa dharura.

      Iwe utaamua kutumia kadi za mkopo au la ni uamuzi wa kibinafsi. Lakini ukiamua, zitumie kwa uangalifu. Zitumie zikiwa kifaa cha kufanya mambo kuwa rahisi. Na uepuke kabisa kulimbikiza madeni. Kudhibiti utumizi wa kadi ya mkopo ni hatua muhimu ya kushughulikia fedha zako kwa mafanikio. Fikiria mengine zaidi uwezayo kufanya.

  • Jinsi ya Kujiepusha na Deni
    Amkeni!—1996 | Desemba 22
    • Jinsi ya Kujiepusha na Deni

      KATIKA nyakati hizi zenye kubadilika, kushughulikia mapato ya familia kwaweza kuwa jambo gumu. Waweza kukabilije ugumu huo kwa mafanikio?

      Jibu si lazima liwe kuchuma fedha zaidi. Wataalamu wa kifedha husema kwamba jibu lahusiana na kujua mahali zinakotoka fedha na mahali zinakoenda na vilevile kuwa tayari kufanya maamuzi yafaayo. Ili kufanya hili, wahitaji bajeti.

      Kushinda Ukinzani Dhidi ya Bajeti

      Hata hivyo, kufikiria bajeti “hutokeza mawazo tofauti-tofauti yasiyopendeza,” asema mshauri wa kifedha, Grace Weinstein. Kwa hiyo, watu wengi hawatayarishi yoyote. Wengine pia huhusianisha kuhitaji bajeti na mapato ya chini au ukosefu wa elimu. Lakini hata wataalamu wenye mapato ya juu wana matatizo ya kifedha. Mshauri mmoja wa kifedha asema: “Mmoja wa wateja wangu wa kwanza alikuwa akipata dola 187,000 kwa mwaka . . . Deni lao la kadi ya mkopo pekee lilikuwa chini tu ya dola 95,000.”

      Michael, aliyetajwa mbeleni, alisita kutafuta msaada wa kifedha kwa sababu nyingine. Yeye akiri: “Nilihofu kwamba wengine wangeniona kuwa asiyejua mambo na mpumbavu.” Lakini hofu kama hiyo haina msingi. Kushughulikia fedha huhitaji namna tofauti ya ustadi mbali na kuchuma fedha, na watu wengi hawajazoezwa kushughulikia fedha. Mfanyakazi wa kijamii ataja: “Sisi huhitimu kutoka shule ya sekondari tukiwa twajua mengi zaidi kuhusu pembetatu pacha kuliko jinsi ya kuweka fedha akiba.”

      Ingawa hivyo, kutayarisha bajeti ni rahisi kujifunza. Huhusisha kutengeneza orodha ya mapato na orodha ya matumizi—na kuzuia matumizi yasipite mapato. Kwa kweli, kutayarisha bajeti kwaweza kufurahisha, na kuishi kupatana nayo kwaweza kutosheleza.

      Kuanza

      Acheni tuanze kwa kutengeneza orodha ya mapato. Kwa wengi wetu, hii yapasa iwe rahisi kwa sababu kwa kawaida huhusisha vitu vichache tu—mshahara, mapato ya ziada kutoka akaunti ya akiba, na kadhalika.

      Lakini usifanye mipango kwa mapato yasiyo hakika, kama yale yatokanayo na malipo ya ovataimu, bakshishi, au zawadi. Washauri wa kifedha huonya kwamba kupanga kulingana na vyanzo vya mapato visivyo vya uhakika kwaweza kukuingiza katika deni. Mapato hayo yakijitokeza, huenda ukachagua kutumia fedha hizo kujifurahisha pamoja na familia, kusaidia walio na uhitaji, au kuchangia panapostahili.

      Hata hivyo, kutengeneza orodha ya matumizi kwaweza kutatanisha kidogo. Robert na Rhonda, waliotajwa katika makala zilizotangulia, hawakuweza kufahamu fedha zao zilizochumwa kwa jasho zilikokuwa zikienda. Robert aeleza jinsi walivyotatua tatizo hilo: “Kwa mwezi mmoja kila mmoja wetu alibeba kipande cha karatasi na kuandika kila ndururu tuliyotumia. Hata tuliandika fedha tulizotumia kwa kikombe cha kahawa. Na mwishoni mwa kila siku, tuliingiza kiasi hicho katika kitabu cha bajeti nilichokuwa nimenunua.”

      Kurekodi kwa uangalifu fedha zote unazotumia kutakusaidia ujue fedha zilitumiwa kwa vitu gani. Hata hivyo, ikiwa wajua mazoea yako ya utumizi, huenda ukaamua kuepuka kuweka orodha yenye mambo mengi ya fedha unazotumia kila siku na kuendelea kutengeneza makadirio ya fedha ya kila mwezi.

      Kuorodhesha Gharama za Kila Mwezi

      Huenda ukataka kutengeneza chati kama inayoonyeshwa hapo juu. Katika safu ya “Matumizi Hususa,” weka kiasi unachotumia wakati huu kwa kila kitu. Punguza idadi ya sehemu kuu, kwa kutumia vichwa kama vile “chakula,” “nyumba,” na “mavazi.” Hata hivyo, usisahau sehemu ndogo za maana. Kwa Robert na Rhonda, sehemu kubwa ya fedha zao ilikuwa ikitumiwa kula katika mikahawa, kwa hiyo kutenganisha “kula mikahawani” na “ununuzi wa vyakula” kulisaidia. Ikiwa wewe hufurahia kukaribisha wageni, hii pia yaweza kuwa sehemu ndogo chini ya “chakula.” Wazo ni kufanya chati hiyo ionyeshe utu na mapendezi yako.

      Unapotengeneza chati yako, usisahau gharama za baada ya kila miezi mitatu, nusu mwaka, kila mwaka, na gharama nyinginezo za pindi kwa pindi, kama vile malipo ya bima na kodi. Ingawa hivyo, kuviongeza katika chati ya kila mwezi, itakubidi ugawanye kiasi cha fedha kwa idadi ifaayo ya miezi.

      Kitu muhimu katika orodha ya gharama ni “akiba.” Ingawa huenda wengi wasione akiba kuwa gharama, utapangia kwa hekima baadhi ya mapato yako ya kila mwezi kwa ajili ya hali za dharura au makusudi ya kipekee. Grace Weinstein akazia umuhimu wa kutia ndani akiba katika orodha yako ya gharama: “Ikiwa huwezi kufaulu kuweka akiba angalau asilimia 5 ya mapato yako baada ya kodi (na hicho ni kiwango cha chini kabisa), itakulazimu kuchukua hatua kali. Achana na madeni, panga tena mtindo wako wa kuishi, na ufikirie mahitaji yako ya msingi.” Ndiyo, kumbuka kutia ndani akiba katika bajeti yako ya kila mwezi.

      Ili kupunguza athari ya matatizo wakati wa ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, wakati huu hupendekezwa kwa kawaida kwamba ujaribu kuweka akiba iwezayo kupatikana kwa urahisi ya angalau mapato ya miezi sita. “Ukiongezwa mshahara,” asema mshauri wa kifedha, “weka akiba nusu yao.” Je, wahisi kwamba huwezi kuweka akiba?

      Fikiria Laxmi Bai, ambaye sawa na wengi katika sehemu za mashambani za India ni maskini sana. Yeye alianza kuweka kando katika nyungu konzi moja ya mchele kutoka fungu la kila siku alilopikia familia yake. Baada ya kipindi fulani, alikuwa akiuza mchele huo na kuweka akiba fedha hizo katika benki. Hii ilikuwa hatua ya kupata mkopo wa benki ili kumsaidia mwana wake kuanzisha kibanda cha kurekebisha baiskeli. Akiba hizo ndogo-ndogo zimeleta mabadiliko yenye maana katika maisha za wengi, laripoti India Today. Hilo limefanya kujitegemea kiuchumi kuwe jambo halisi kwa watu fulani.

      Hata hivyo, kusawazisha bajeti ni zaidi ya kutengeneza orodha ya mapato na gharama. Huhusisha kudhibiti gharama zisipite mapato, jambo ambalo huenda likahitaji kupunguza matumizi yako.

      Je, Ni Muhimu?

      Ona kichwa “Ni Muhimu?” kwenye fomu katika ukurasa 9. Safu hii ni ya maana sana kuifikiria, hasa ikiwa unapata kwamba jumla katika safu ya “Kiasi Kilichopangiwa” ni kuu kuliko mapato yako. Hata hivyo, kuamua ikiwa kitu ni muhimu na ni kiasi gani cha fedha kinachohitajiwa kwa ajili yacho kwaweza kuwa tatizo. Ndivyo ilivyo hasa katika nyakati hizi zenye kubadilika wakati ambapo tunaletewa kwa wingi na kwa mfululizo bidhaa mpya ambazo zatangazwa kuwa ni mahitaji. Kupanga kila gharama kulingana na uhitaji hususa, uhitaji uwezekanao, au anasa ambayo ni nzuri kuwa nayo kutasaidia.

      Tazama kila gharama ambayo umeorodhesha, na baada ya kuchunguza kwa uangalifu, katika safu yako ya “Ni Muhimu?” weka “Ndiyo” ikiwa kitu hicho ni cha muhimu hasa; na “?” ikiwa ni uhitaji uwezekanao; na “Nzuri” ikiwa kitu hicho ni anasa nzuri ya kuwa nayo. Kumbuka, jumla iliyoorodheshwa katika safu ya “Kiasi Kilichopangiwa” haipaswi kuwa kuu kuliko mapato yako ya kila mwezi!

      Vitu vilivyotiwa alama “?” na “Nzuri” bila shaka vitakuwa vya kwanza kuondoshwa. Huenda gharama hizi zisihitaji kuondoshwa kabisa-kabisa. Wazo ni kuchunguza kila kitu na kuona ikiwa gharama yastahili raha inayoletwa na hicho kitu na kuondosha ifaavyo. Robert na Rhonda waliona katika orodha yao kwamba walikuwa wakitumia dola 500 kila mwezi kula mikahawani. Lilikuwa zoea ambalo walikuwa wameangukia kwa sababu hakuna mmoja wao aliyejua kupika. Lakini Rhonda alichukua hatua za kujifunza na asema: “Sasa kupika kunafurahisha, nasi hula nyumbani mara nyingi zaidi.” Robert aongeza: “Sasa sisi hula mikahawani katika pindi za pekee, au inapokuwa lazima.”

      Badiliko katika hali zako huenda likakufanya uchunguze tena hali yako kikamili kuhusu kilicho muhimu. Kama ilivyotajwa katika makala ya kwanza, mapato ya Anthony yalishuka sana. Kutoka dola 48,000 kwa mwaka hadi chini ya dola 20,000 na kubaki katika kiwango hicho kwa miaka miwili. Hili likikupata, huenda ukahitaji kuanzisha bajeti ya kusalimika, ukikata matumizi yote ya ziada.

      Hivyo hasa ndivyo alivyofanya Anthony. Kwa kukata sana fedha zitumiwazo kwa vyakula, mavazi, usafiri, na tafrija, yeye alifaulu kwa jitihada nyingi kulipia nyumba yake ili asiipoteze.a “Tukiwa familia ilitulazimu kupambanua mahitaji yetu ya lazima na mambo tunayotaka,” yeye asema, “nasi tumenufaika na ono hilo. Sasa twajua jinsi ya kuridhika na machache.”

      Punguza Deni

      Deni lisilodhibitiwa laweza kuharibu jitihada zako za kuishi kulingana na riziki yako. Ingawa deni la muda mrefu litumiwalo kulipia mali kama vile nyumba ambazo huongezeka katika thamani laweza kuwa na faida, madeni ya kadi za mkopo ya kulipia maisha ya kila siku yaweza kuleta msiba. Kwa hiyo, jihadhari na “usijiingize katika madeni ya kadi za mkopo,” lasema Newsweek.

      Wataalamu wa kifedha hutia moyo kulipa madeni ya kadi za mkopo hata ikiwa itakulazimu kutoa fedha katika akiba yako. Ni jambo lisiloeleweka kuwa na madeni yenye kiwango cha juu cha riba huku ukiwa na akiba yenye kiwango cha chini cha riba. Walipotambua hili, Michael na Reena walilipa madeni yao ya kadi za mkopo kwa kubadili kuwa fedha dhamana zao za akiba, kisha wakaazimia kutoingia tena katika hali hiyo.

      Robert na Rhonda, kwa kuwa hawakuwa na rasilimali hizo, waligeukia bajeti ya kusalimika. Robert asema: “Nilitengeneza grafu kwenye ubao mweupe kuonyesha jinsi deni lingekuwa likipungua mwezi baada ya mwezi kisha nikaangika ubao huo katika chumba chetu cha kulala mahali ambapo tungeweza kuuona kila asubuhi. Hilo liliandaa kichocheo cha kila siku.” Mwishoni mwa mwaka, walifurahi kama nini kuwa huru kutokana na deni lao la kadi za mkopo la dola 6,000!

      Katika nchi fulani hata amana si kitega-uchumi kizuri sana kama kilivyokuwa. Na kununua nyumba kwaweza kukugharimu fedha nyingi kwa sababu ya utozaji wa riba. Waweza kufanya nini ili kupunguza gharama ya amana? “Ama ulipe kiasi kikubwa cha malipo ya kwanza kuliko inavyohitaji benki au ununue nyumba isiyo ghali sana,” lapendekeza Newsweek. “Ikiwa tayari una nyumba, kinza tamaa ya kutaka kununua nyumba kubwa au bora zaidi.”

      Waweza kupunguza gharama ya mkopo wa gari kwa kulipa kiasi kikubwa cha malipo ya kwanza. Lakini utalazimika kuyawekea akiba muda mrefu kabla ya wakati huo kwa kuyafanyia safu kwenye bajeti ya familia. Namna gani kuchagua gari zuri lililotumiwa?b Gharama yalo ya mwanzoni huenda ikawa ya chini. Huenda hata ukaweza kununua moja bila hata ya kutafuta mkopo.

      Je, Utafaulu?

      Kufaulu kwako katika kufanya bajeti yako ifanikiwe hutegemea kwa sehemu kubwa jinsi ilivyo ya uhalisi. “Bajeti haitafanya kazi ikiwa kiasi kilichowekwa kando kwa ajili ya mambo ya nyumbani ni kidogo sana hivi kwamba hamwezi kumaliza mwezi mkikitegemea,” wasema mume na mke ambao wameishi kwa mafanikio wakitumia bajeti.

      Jambo jingine la maana sana katika kufanya bajeti ifaulu ni mawasiliano mazuri kati ya washiriki wa familia. Wale walioathirika kwa bajeti wapaswa kuwa na fursa ya kueleza maoni na hisia zao bila kudhihakiwa. Ikiwa washiriki wa familia wanaohusika wanafahamu mahitaji na kile anachotaka kila mmoja na kutambua jinsi hali ya kifedha ya familia ilivyo, yaelekea kutakuwa na ushirikiano na nafasi nzuri ya kufanikiwa kwa bajeti ya familia.

      Katika nyakati hizi zilizo ngumu, huku mandhari ya ulimwengu izidipo kubadilika, msongo kwa fedha za familia huongezeka. (2 Timotheo 3:1; 1 Wakorintho 7:31) Twahitaji kudhihirisha “hekima kamili” katika kukabili magumu ya uhai wa kisasa. (Mithali 2:7) Kuweka bajeti ndiyo hatua hasa itakayokusaidia kufanya hivyo.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki