-
Hakikisha Chakula HakikudhuruAmkeni!—2012 | Juni
-
-
Hakikisha Chakula Hakikudhuru
“Shule Nchini Ujerumani Yafungwa kwa Sababu ya Bakteria ya E. Coli.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, UJERUMANI.
“Miche Yashukiwa Kueneza Bakteria ya Salmonela Katika Majimbo Matano.”—USA TODAY.
“Nyama ya Ng’ombe 6 Waliolishwa Nyasi Yenye Sumu ya Nyuklia Yauzwa Katika Wilaya 9.”—THE MAINICHI DAILY NEWS, JAPANI.
HIVYO vilikuwa vichwa vikuu vya habari katika kipindi cha majuma mawili mwaka jana. Watafiti wanakadiria kwamba kila mwaka karibu asilimia 30 ya watu katika nchi zinazoendelea hupatwa na magonjwa yanayosababishwa na vyakula.
Wewe unaathiriwaje na habari hizo? Baba mmoja nchini Hong Kong anayeitwa Hoi anasema hivi: “Mambo hayo hunitia wasiwasi na kunikasirisha. Nina watoto wawili, nami huwa na wasiwasi chakula wanachokula kimetayarishwa wapi na jinsi gani.”
Katika nchi maskini, kila mwaka mamilioni ya watu, hasa watoto, hufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na vyakula na maji machafu. “Katika masoko ya huku, vyakula huachwa wazi na hivyo kuchafuliwa na nzi, mvua, upepo, na vumbi,” anasema Bola, anayeishi nchini Nigeria. “Ninaposoma au kusikia kuhusu magonjwa yanayosababishwa na vyakula mimi huogopa. Ninataka kuilinda familia yangu.”
Je, inawezekana kuilinda familia yako kutokana na chakula kinachoweza kutokeza madhara? Shirika la Kukagua Chakula la Kanada linasema hivi: “Chakula hatari kinapouzwa madukani, jambo hilo linatangazwa kotekote na vyombo vya habari. Na hilo linafaa. Lakini chakula kinaweza kusababisha magonjwa ikitegemea jinsi tunavyokitayarisha tunapokuwa nyumbani.”
Unaweza kufanya nini ili kuilinda familia yako kutokana na magonjwa yanayosababishwa na vyakula? Tutazungumzia njia nne za kuzuia chakula chako kisikudhuru.
[Sanduku katika ukurasa wa 3]
NI NANI WALIO HATARINI?
Watu wafuatao wanaweza kupatwa kwa urahisi na magonjwa yanayosababishwa na vyakula:
● Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano
● Wanawake waja-wazito
● Watu walio na umri wa zaidi ya miaka 70
● Watu walio na mfumo dhaifu wa kinga
Ikiwa wewe au yeyote anayekula pamoja nawe yuko katika kikundi hiki, unapaswa kuwa mwangalifu sana kuhusu chakula unachotayarisha, kupakua, na kula.
[Hisani]
Chanzo: Shirika la Usimamizi wa Chakula la New South Wales, Australia
-
-
1. Tumia Busara Unaponunua ChakulaAmkeni!—2012 | Juni
-
-
1. Tumia Busara Unaponunua Chakula
ISIPOKUWA uwe unakuza chakula chako mwenyewe, utakinunua sokoni au kwenye maduka makubwa. Utachaguaje na kununua chakula chenye lishe?
● Panga wakati wa kununua.
Baraza Linalotoa Habari Kuhusu Usalama wa Chakula nchini Australia linashauri hivi: “Kwanza nunua vyakula visivyoweza kuharibika haraka. Malizia kwa kununua vyakula vilivyowekwa kwenye friji au barafu.” Pia, nunua vyakula moto kabla tu ya kurudi nyumbani.
● Nunua vyakula vilivyotolewa moja kwa moja shambani.
Ikiwezekana, nunua vyakula vilivyotolewa moja kwa moja shambani.a Ruth, mama ya watoto wawili nchini Nigeria anasema: “Kwa kawaida, mimi huenda sokoni asubuhi na mapema wakati ambapo chakula kimeletwa tu kutoka shambani.” Elizabeth, anayeishi Mexico, pia hununua vyakula sokoni. Anasema: “Nikiwa sokoni ninaweza kununua matunda na mboga zilizotoka moja kwa moja shambani, na ninaweza kujichagulia mwenyewe. Kwa kawaida mimi hununua nyama iliyochinjwa siku hiyohiyo. Nisipoipika yote mimi huhifadhi inayosalia kwenye barafu.”
● Kagua chakula chako.
Jiulize: ‘Je, ngozi ya chakula ninachonunua imechubuka? Je, nyama ina harufu isiyo ya kawaida?’ Ikiwa chakula hicho tayari kimepakiwa, chunguza jinsi kilivyopakiwa. Upakiaji mbaya unaweza kuruhusu bakteria hatari kupenya kwenye chakula.
Chung Fai, anayeishi Hong Kong ambaye hununua chakula chake katika maduka makubwa anasema hivi, “Ni muhimu pia kuangalia tarehe iliyoonyeshwa ya muda wa kutumika kwa chakula kilichopakiwa.” Kwa nini? Wataalamu wanaonya kwamba hata ingawa huenda chakula ambacho kimepitisha muda wa kutumika kwake kikaonekana kuwa sawa, kikawa na ladha nzuri, au kisiwe na uvundo, bado kinaweza kukufanya uwe mgonjwa.
● Pakia chakula vizuri.
Ikiwa utatumia mfuko wa plastiki kubebea chakula, uoshe kwa ukawaida kwa maji moto yenye sabuni. Pakia nyama na samaki katika mifuko tofauti ili zisichafue vyakula vingine.
Enrico na Loredana, wenzi wa ndoa nchini Italia, hununua vyakula vyao karibu na nyumbani. Wanasema, “Kwa kufanya hivyo, hatusafirishi vyakula kutoka mbali na hivyo haviharibiki.” Ikiwa utatumia zaidi ya dakika 30 kufika nyumbani, weka chakula kilichogandishwa au chenye baridi katika mfuko unaohifadhi baridi ili kuhakikisha kwamba hakitapata joto.
Katika makala inayofuata, jifunze jinsi ya kuhakikisha kwamba chakula chako hakikudhuru unapokileta nyumbani.
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala yenye kichwa “Njia ya 1—Kula Vizuri,” katika toleo la Amkeni! la Machi 2011.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
WAZOEZE WATOTO WAKO: “Mimi huwafundisha watoto wangu kuangalia muda wa mwisho wa kutumika kwa chakula kilichopakiwa, kama vile vitafunio, kabla hawajavinunua.”—Ruth, Nigeria
-
-
2. Dumisha UsafiAmkeni!—2012 | Juni
-
-
2. Dumisha Usafi
KAMA vile tu daktari mpasuaji anavyolinda wagonjwa anaotibu kwa kunawa mikono, kusafisha vifaa anavyotumia, na kuhakikisha kwamba chumba cha upasuaji ni safi, unaweza kuilinda familia yako kwa kudumisha usafi wa mwili wako, wa jikoni, na wa chakula chako.
● Nawa mikono.
Shirika la Afya ya Umma la Kanada linasema kwamba “mikono hueneza asilimia 80 hivi ya magonjwa ambayo huambukizwa kwa ukawaida kama vile mafua na homa.” Kwa hiyo, nawa mikono yako vizuri kwa sabuni na maji kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na unapotayarisha chakula.
● Dumisha usafi jikoni.
Uchunguzi mmoja unaonyesha kwamba ingawa eneo la chooni ndilo safi zaidi ndani ya nyumba, “sponji ama vitambaa vya jikoni ndivyo vitu vyenye bakteria nyingi zinazopatikana katika kinyesi.”
Kwa hiyo, badilisha vitambaa vya jikoni mara kwa mara na utumie maji moto yenye sabuni au yenye dawa za kuua viini kusafisha meza na kaunta za jikoni. Ni kweli kwamba si rahisi kufanya hivyo. Bola anaishi katika nyumba isiyo na maji ya bomba anasema, “Hilo linafanya hali iwe ngumu, lakini sikuzote sisi huhakikisha kwamba kuna sabuni na maji ya kutosha kusafisha eneo la jikoni na nyumba yote.”
● Safisha mboga na matunda.
Huenda vyakula vilichafuliwa na maji machafu, wanyama, kinyesi, au vyakula vingine vibichi kabla ya kuuzwa. Kwa hiyo, hata kama utaondoa maganda ya matunda au mboga, yasafishe kabisa ili kuondoa bakteria hatari. Kufanya hivyo kunachukua muda. Mama mmoja nchini Brazili anayeitwa Daiane anasema hivi, “Ninapotayarisha saladi, huwa siharakishi ili nihakikishe nimeyasafisha majani yote vizuri.”
● Usiweke nyama mbichi pamoja.
Ili kuzuia kuenea kwa bakteria pakia vizuri nyama mbichi ya ng’ombe, kuku, na samaki, na uiweke mbali na vyakula vingine. Tumia ubao tofauti kukatia vyakula hivyo au uoshe ubao huo kwa sabuni na maji moto kabla na baada ya kukatia nyama mbichi au samaki.
Sasa kwa kuwa wewe, vifaa, na vyakula vyako ni safi, utatayarishaje chakula kwa njia ambayo haitakudhuru?
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
WAZOEZE WATOTO WAKO: “Sisi huwafundisha watoto wetu kunawa kabla ya kula na kuosha au kutupa chakula chochote kilichoanguka sakafuni.”—Hoi, Hong Kong
-
-
3. Tayarisha na Uhifadhi Chakula VizuriAmkeni!—2012 | Juni
-
-
3. Tayarisha na Uhifadhi Chakula Vizuri
M PISHI mmoja katika Israeli la kale ambaye hakuwa mwangalifu alikusanya maboga ya mwituni ambayo ‘hakuwa anayafahamu.’ Aliyatia ndani ya mchuzi. Walaji, waliohofia kwamba chakula hicho kilikuwa na sumu walilia na kusema: “Kuna kifo ndani ya chungu hiki.”—2 Wafalme 4:38-41.
Kama mfano uliotajwa unavyoonyesha, tunapaswa kuwa waangalifu kuhusu chakula ambacho hakikutayarishwa vizuri kwa kuwa kinaweza kutudhuru au hata kutuua. Kwa hiyo, ili kuzuia magonjwa yanayosababishwa na vyakula, jifunze kutayarisha na kuhifadhi chakula kwa uangalifu. Fikiria mapendekezo manne yafuatayo:
● Nyama iliyoganda isiyeyushwe nje ya friji.
Wizara ya Kilimo ya Marekani inasema kwamba “hata ingawa sehemu ya katikati ya nyama huwa bado imeganda inapoyeyuka nje ya friji, huenda sehemu ya nje ya nyama hiyo ikawa na joto la kati ya nyuzi 4 Selsiasi na nyuzi 60 Selsiasi, kiwango kinachosemwa kuwa hatari kwa sababu bakteria huongezeka haraka.” Badala yake, yeyusha chakula ndani ya friji, kwenye mikrowevu, au kitumbukize ndani ya maji baridi kikiwa kimepakiwa.
● Pika chakula hadi kiive kabisa.
Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kwamba “karibu viini vyote hatari hufa chakula kinapopikwa na kuiva kabisa.” Unapopika chakula hakikisha kwamba kinaiva kabisa, hasa ikiwa kina supu au mchuzi.a Kwa kuwa inaweza kuwa vigumu kujua halijoto ya vyakula fulani, wapishi wengi hutumia kifaa cha kupima joto la nyama. Au mtu anaweza kudunga nyama kwa kutumia uma au kuikata katikati ili kuhakikisha kwamba imeiva kabisa.
● Chakula kiliwe punde tu baada ya kupikwa.
Chakula kilichopikwa hakipaswi kuachwa nje kwa muda mrefu, kwa hiyo hakikisha kinaliwa punde tu baada ya kupikwa ili kisiharibike. Chakula baridi kinapaswa kuliwa kikiwa baridi na chakula moto kinapaswa kuliwa kikiwa moto. Ili chakula chako kisipoe, kiweke ndani ya joko lenye halijoto ya nyuzi 93 Selsiasi. Ikiwa huna joko, unaweza kuacha chakula juu ya jiko lisilo na moto mwingi.
● Chakula kinachosalia kishughulikiwe vizuri.
Anita, mama anayeishi huko Poland, hupakua chakula mara tu baada ya kukipika. Lakini ikiwa kuna chakula kilichobaki, “mimi hukipakia katika vifurushi vidogo-vidogo na kukigandisha ili iwe rahisi kukiyeyusha baadaye.” Ikiwa unahifadhi masalio ya chakula kwenye friji, lazima kiliwe kabla ya siku tatu au nne kwisha.
Unapoenda kwenye mkahawa unalazimika kula chakula kilichotayarishwa na mtu mwingine. Kwa hiyo, unawezaje kuilinda familia yako mnapokula kwenye mkahawa?
[Maelezo ya Chini]
a Nyama za aina fulani zinahitaji kupikwa kwa muda mrefu zaidi.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
WAZOEZE WATOTO WAKO: “Watoto wangu wanapopika chakula mimi huwakumbusha wasome na kufuata maagizo yaliyoonyeshwa.”—Yuk Ling, Hong Kong
-
-
4. Uwe Mwangalifu Unapokula Kwenye MkahawaAmkeni!—2012 | Juni
-
-
4. Uwe Mwangalifu Unapokula Kwenye Mkahawa
Jeff, mwanamume mwenye umri wa miaka 38 aliye na afya na nguvu, aliipeleka familia yake kwenye mkahawa mmoja karibu na Pittsburgh, Pennsylvania, Marekani. Mwezi mmoja baadaye, Jeff alikufa kwa sababu ini lake liliacha kufanya kazi. Ni nini kilichosababisha hilo? Ni vitunguu vya majani alivyokula ambavyo vilikuwa na virusi vya mchochota ini aina ya A.
KATIKA nchi moja huko Ulaya, karibu nusu ya pesa zote ambazo watu hutenga kwa ajili ya chakula hutumiwa katika mikahawa. Hata hivyo, katika nchi hiyohiyo, inasemekana kwamba karibu nusu ya magonjwa yanayosababishwa na vyakula yanahusianishwa na chakula cha mikahawa.
Ni kweli kwamba unapokula kwenye mkahawa mtu mwingine ndiye anayenunua chakula na kukipika na hata kusafisha eneo la jikoni. Hata hivyo, unaweza kuamua utakula wapi, utakula nini, na ikiwa utabeba chakula kinachosalia.
● Kagua mkahawa.
Daiane anayeishi Brazili anasema hivi, “Ninapoingia kwenye mkahawa kwa mara ya kwanza, mimi huangalia ikiwa meza, vitambaa vya meza, vyombo, na wahudumu ni safi na nadhifu. Ikiwa mkahawa huo si safi, sisi huondoka na kutafuta mwingine.” Katika nchi fulani, maofisa wa afya hukagua na kuipa mikahawa hiyo alama za usafi na kuandika matokeo ya ukaguzi wao kwa ajili ya umma.
● Jihadhari na masalio unayobeba nyumbani.
Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani linatoa shauri hili: “Ikiwa hutafika nyumbani saa mbili baada ya kula mkahawani, usibebe masalio yoyote.” Ikiwa umebeba masalio, nenda moja kwa moja nyumbani na uyahifadhi kwenye friji hasa ikiwa halijoto ya eneo lenu inapita nyuzi 32 Selsiasi.
Ukichukua hatua nne zilizotajwa katika mfululizo wa makala hizi, unaweza kufanya chakula chako kisiwe na madhara.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
WAZOEZE WATOTO WAKO: “Sisi huwafundisha watoto wetu kuepuka kula vyakula vinavyoweza kuwadhuru.”—Noemi, Filipino
-
-
Hivi Karibuni Wote Watakuwa na Chakula Chenye Lishe!Amkeni!—2012 | Juni
-
-
Hivi Karibuni Wote Watakuwa na Chakula Chenye Lishe!
UNAWEZA kuchukua hatua fulani ili ufurahie kula chakula kisichokudhuru. Hata hivyo, kuna mambo mengi ambayo huwezi kudhibiti. Kwa mfano, huwezi kukagua vyakula vyote kabla ya kuvinunua au kuvitayarisha. Huenda ukalazimika kununua vyakula ambavyo vimetengenezwa viwandani na kusafirishwa kutoka mbali. Na huenda vyakula fulani ambavyo unanunua tayari vimechafuliwa na kemikali hatari zilizo kwenye hewa, kwenye maji, au kwenye udongo.
Katika ripoti moja yenye kichwa “Kudhibiti Magonjwa Yanayosababishwa na Vyakula: Tatizo la Kimataifa,” maofisa wa Shirika la Afya Ulimwenguni wanasema kwamba matatizo fulani yanayohusiana na usalama wa chakula “hayawezi kutatuliwa na serikali moja peke yake; yanahitaji ushirikiano wa kimataifa.” Magonjwa yanayosababishwa na vyakula ni tatizo la ulimwenguni pote!
Inaeleweka kwamba wengi watajiuliza ni kwa nini tunasema kwa uhakika kwamba hivi karibuni watu wote watakuwa na chakula chenye lishe. Ni kwa sababu “Yehova, Bwana wa dunia yote,” anaahidi kwamba atatatua matatizo ya chakula yanayowakumba wanadamu. (Yoshua 3:13) Huenda watu fulani wakadai kwamba kuwepo kwa chakula kinachodhuru kunathibitisha kwamba Mungu hawezi kutumainika. Lakini hebu fikiria hili: Ikiwa mhudumu hotelini ataacha chakula kizuri kiharibike, je, ingefaa kumlaumu mpishi? La hasha.
Vivyo hivyo, ni wanadamu—na si Muumba—ambao wanapaswa kulaumiwa kwa kuharibu chakula kizuri kinachozalishwa na dunia. Kuwepo kwa chakula kinachodhuru ni tatizo lililotokezwa na wanadamu. Mungu anaahidi kwamba ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia.’—Ufunuo 11:18.
Ukweli ni kwamba tayari Mungu amethibitisha kwamba anajali kuhusu ubora wa chakula tunachokula. Yeye ndiye aliyeifanyiza dunia na kuumba miti ‘yenye kutamanika kwa macho ya mtu’ na pia inayofaa “kwa ajili ya chakula.” (Mwanzo 2:9) Hata baada ya wanadamu kuanza kuwa wagonjwa, Yehova Mungu aliwapa watu wake miongozo hususa ambayo ingelinda chakula chao na miili yao.—Ona sanduku “Mfumo wa Sheria Kuhusu Afya.”
Mungu anataka tufurahie chakula cha aina gani? Biblia inatuambia hivi: “Anafanya majani mabichi yachipuke kwa ajili ya wanyama, na mimea ili itumikie wanadamu, ili chakula kitokezwe duniani, na divai ambayo hufanya moyo wa mwanadamu anayeweza kufa ushangilie, kuufanya uso ung’ae kwa mafuta, na mkate unaotegemeza moyo wa mwanadamu anayeweza kufa.” (Zaburi 104:14, 15) Biblia pia inasema kwamba “kila mnyama anayetembea ambaye yuko hai anaweza kuwa chakula.”—Mwanzo 9:3.
Neno lake linaahidi hivi kuhusu wakati wetu ujao: “Naye hakika ataleta mvua kwa ajili ya mbegu yako unayoipanda katika udongo, na mkate kuwa mazao ya udongo, ambao utakuwa mnono na wenye mafuta. Mifugo yako italisha katika siku hiyo katika malisho mapana.” (Isaya 30:23) Naam, hivi karibuni badala ya kuwa na vichwa vya habari vyenye kuhuzunisha kutakuwa na tangazo hili: “Watu wote wana chakula chenye lishe!”
[Blabu katika ukurasa wa 9]
Muumba wetu anatuahidi wakati ujao ulio na chakula kingi kizuri
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
“MFUMO WA SHERIA KUHUSU AFYA”
Miaka 3,500 hivi iliyopita Waisraeli walipewa Sheria ya Musa. Sheria hiyo iliwalinda Waisraeli kutokana na magonjwa mengi yanayosababishwa na vyakula. Fikiria maagizo yafuatayo:
● Epukeni vyombo vyovyote ambavyo vimegusa mnyama aliyekufa: “Chombo chochote ambacho hutumiwa kwa njia fulani kitatiwa katika maji, nacho kitakuwa kisicho safi mpaka jioni halafu kitakuwa safi.”—Mambo ya Walawi 11:31-34.
● Msile mnyama aliyekufa mwenyewe: “Msile mwili wowote uliokufa tayari.” —Kumbukumbu la Torati 14:21.
● Chakula kilichobaki kinapaswa kuliwa baada ya muda mfupi: “Kesho yake kilichobaki kinaweza kuliwa. Lakini nyama inayobaki ya dhabihu katika siku ya tatu, itateketezwa kwa moto.”—Mambo ya Walawi 7:16-18.
Dakt. A. Rendle Short, anashangaa kwamba Sheria ya Musa—ikilinganishwa na sheria za mataifa mengine jirani—ilikuwa na “mfumo wa sheria kuhusu afya uliokuwa wenye hekima na rahisi kufuata.”
-