Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Gabon—Hifadhi ya Wanyama-Pori
    Amkeni!—2008 | Januari
    • Ni nini kinachofanya hifadhi hizo ziwe muhimu sana? Bado asilimia 85 hivi ya Gabon ni msitu, na asilimia 20 hivi ya jamii za mimea katika misitu hiyo hazipatikani sehemu nyingine yoyote ulimwenguni. Isitoshe, misitu ya ikweta ni makao ya sokwe wa aina mbalimbali, tembo, na wanyama wengine wanaokabili hatari ya kutoweka. Mbuga zilizoanzishwa hivi karibuni zitafanya Gabon isaidie sana kutunza unamna-namna wa viumbe wa Afrika.

  • Gabon—Hifadhi ya Wanyama-Pori
    Amkeni!—2008 | Januari
    • Ndani ya misitu ya ikweta, tumbili hurukaruka kwenye matawi ya juu, nao vipepeo wenye rangi maridadi hurukaruka hapa na pale. Popo wala-matunda hukaa kwenye miti wanayopenda wakati wa mchana, na usiku wanafanya kazi yao muhimu ya kudondosha mbegu msituni. Kwenye kingo za msitu, chozi hula chavua kutoka kwenye miti na vichaka vinavyotoa maua. Haishangazi kwamba mbuga hiyo ya Loango imefafanuliwa kuwa “mahali unapoweza kufurahia mazingira ya ikweta ya Afrika.”

      Lopé—Mahali Ambapo Sokwe Bado Wanapatikana kwa Wingi

      Mbuga ya Taifa ya Lopé inatia ndani sehemu kubwa za msitu wa mvua ambao haujaharibiwa na wanadamu. Mbuga hiyo ina eneo kubwa la savana na msitu ulio kando ya maji upande wa kaskazini. Watu wanaopenda vitu vya asili ambao wanataka kuona sokwe au nyani wakubwa wa Afrika katika mazingira yao ya asili wanaweza kufurahia eneo hilo. Kuna sokwe kati ya 3,000 na 5,000 katika eneo lililohifadhiwa la kilomita 5,000 za mraba.

      Augustin, aliyekuwa ofisa wa mbuga hiyo, anakumbuka jinsi alivyokutana na sokwe mnamo 2002. “Nilipokuwa nikitembea msituni, nilikutana na familia ya sokwe wanne,” anasema. “Sokwe mkubwa wa kiume mwenye miaka 35 hivi, aliye na manyoya meupe mgongoni, alisimama mbele yangu. Uzito wake ulikuwa karibu mara tatu ya uzito wangu. Nilifuata mapendekezo ambayo hutolewa unapokutana na sokwe, yaani, kuketi chini mara moja, kuinamisha kichwa, na kuangalia chini kuonyesha kuwa nimejitiisha. Sokwe huyo alikuja, akaketi kando yangu na kuweka mkono juu ya bega langu. Kisha akachukua mkono wangu, akaukunjua, na kuchunguza kiganja changu. Alipohakikisha kwamba nisingehatarisha familia yake, aliondoka. Siku hiyo ambayo sitawahi kuisahau, niligundua uzuri wa kukutana na wanyama katika mazingira yao ya asili. Ingawa watu huwaua sokwe kwa ajili ya nyama au kwa sababu ya maoni ya uwongo kwamba wao ni hatari, wao ni wanyama watulivu wanaohitaji kulindwa.”

      Huko Lopé, nyani wakubwa hukusanyika katika vikundi vikubwa ambavyo nyakati nyingine huwa na nyani zaidi ya elfu moja. Hapo ndipo kuna wanyama wengi zaidi wa jamii ya nyani ulimwenguni, nao hupiga kelele nyingi sana. Mgeni kutoka Kamerun anaeleza kuhusu wakati alikutana na kikundi kimoja kikubwa.

      “Mtu aliyekuwa akituongoza alitambua kuwa nyani hao wanakuja kwa sababu ya vifaa fulani ambavyo baadhi yao wamevishwa. Tulisonga mbele ya nyani hao, tukajificha, na kuwangoja. Kwa dakika 20 tulisikiliza muziki wa msitu uliotolewa na ndege na wadudu. Utulivu huo ulikatishwa ghafula nyani hao walipokaribia. Kelele za matawi yakivunjika na sauti zao za juu zilinifanya nifikiri dhoruba kali inakaribia. Lakini nilipoona [nyani waliokuwa wakioongoza], walionekana kama kikosi cha kwanza cha askari-jeshi wanaoongoza uvamizi. Nyani wakubwa wa kiume waliongoza, wakitembea haraka, nao nyani wa kike na vijana waliruka kutoka tawi moja hadi lingine. Ghafula, nyani mmoja wa kiume akasimama na kuangalia huku na huku kama anashuku jambo fulani. Nyani mdogo, aliyekuwa juu ya mti, alikuwa ametuona na kutoa onyo. Kikundi chote kikaongeza mwendo, na kelele zikaongezeka walipotoa sauti za kukasirishwa. Baada ya dakika chache, wote waliondoka. Aliyekuwa akituongoza alikadiria kuwa kikundi hicho kilichotupita kilikuwa na nyani 400 hivi.”

      Sokwe wana kelele nyingi kama nyani hao na hawaonekani kwa urahisi kwa kuwa wao husonga haraka sana wakitafuta chakula. Kwa upande mwingine, wageni huona tumbili wenye pua zenye rangi ya kijivu ambao mara kwa mara huonekana kwa wingi kwenye maeneo ya savana yaliyo kando ya msitu. Tumbili mwenye mkia wa rangi nyangavu aliyegunduliwa miaka 20 hivi iliyopita, ndiye anayeonekana mara chache sana huko Lopé.

      Ndege wakubwa wenye rangi maridadi—kama vile shorobo na hondohondo—hutoa sauti kubwa. Jamii 400 hivi za ndege zimeonekana katika mbuga hiyo, na hivyo kufanya eneo hilo liwavutie watu wanaopenda kutazama ndege.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki