Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kamari Hupendwa Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2002 | Julai 22
    • Kamari Hupendwa Ulimwenguni Pote

      JOHN, aliyelelewa huko Scotland, alitamani sana kushinda zawadi katika mchezo wa bahati nasibu. Anasema hivi: ‘Nilinunua tiketi ya kushinda bahati nasibu kila juma. Tiketi hiyo haikuwa pesa nyingi, lakini ilinipa tumaini la kupata kila kitu ambacho nilikuwa nikitamani.’

      Kazushige, anayeishi Japani, alipenda sana mashindano ya mbio za farasi. Anasema hivi: “Nilifurahia sana kucheza kamari pamoja na rafiki zangu kwenye uwanja wa mbio za farasi, na nyakati nyingine nilishinda pesa nyingi.”

      Linda, anayeishi Australia, anasema hivi: ‘Nilipenda sana kucheza kamari aina ya bingo. Kila juma zoea hilo lilinigharimu dola 30 za Marekani, lakini nilisisimuka sana niliposhinda zawadi.’

      John, Kazushige, na Linda, waliiona kamari kuwa tafrija isiyodhuru sana. Mamilioni ya watu kotekote duniani wana maoni hayohayo. Mahojiano yaliyofanywa mwaka wa 1999 yalionyesha kwamba thuluthi mbili za Wamarekani waliona kucheza kamari kuwa zoea linalofaa. Wamarekani walitumia dola bilioni 50 hivi za Marekani katika michezo halali ya kamari mwaka wa 1998. Hizo ni pesa nyingi kuliko kiasi walichotumia kununua tiketi za sinema, kutazama michezo, na burudani mbalimbali, na kununua kaseti za muziki na michezo ya video.

      Kulingana na uchunguzi wa hivi majuzi, zaidi ya asilimia 80 ya Waaustralia walicheza kamari angalau mara moja katika kipindi cha mwaka mmoja, na asilimia 40 walicheza kamari kila juma katika kipindi hicho. Watu wazima katika nchi hiyo, hutumia dola 400 za Marekani kwa wastani kila mwaka katika michezo ya kamari. Kiasi hicho ni maradufu ya kiasi ambacho Watu wa Ulaya na Wamarekani hutumia. Kwa hiyo, Waaustralia ni miongoni mwa watu wanaopenda kucheza kamari zaidi ulimwenguni.

      Wajapani wengi wameshindwa kudhibiti zoea la kucheza pachinko, nao hutumia mabilioni ya pesa kila mwaka katika mchezo huo wa kamari. Wabrazili hutumia dola bilioni 4 za Marekani katika michezo ya kamari kila mwaka, na kiasi kikubwa cha pesa hizo hutumiwa kununua tiketi za kushinda bahati nasibu. Hata hivyo, si Wabrazili pekee wanaopenda michezo ya bahati nasibu. Hivi majuzi, gazeti la Public Gaming International lilikadiria kwamba kuna “michezo 306 ya bahati nasibu katika nchi 102.” Naam, ulimwenguni pote watu hupenda kucheza kamari. Jambo ambalo kwa maoni ya watu fulani ni lenye faida kubwa.

      Sharon Sharp, aliye mwakilishi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchezaji wa Kamari wa Umma, anasema kwamba kuanzia mwaka wa 1964 hadi 1999 huko Marekani, ‘serikali ilipata faida ya dola bilioni 125 hivi kutokana na michezo ya bahati nasibu, na sehemu kubwa ya faida hiyo imekuwa ikiingia tangu mwaka wa 1993.’ Kiasi kikubwa cha fedha hizo kilikusudiwa kutumiwa hasa kwa ajili ya elimu, mbuga za taifa, na majengo ya michezo. Pia, kampuni za kamari huajiri watu wengi. Kwa mfano, huko Australia kuna zaidi ya kampuni 7,000 za kamari ambazo zimewaajiri wafanyakazi wapatao 100,000.

      Kwa hiyo, wale wanaotetea uchezaji wa kamari husema kwamba mbali na kuwatumbuiza watu, kampuni halali za kamari huwaajiri watu, huiletea serikali faida, nazo huboresha uchumi unaoshuka.

      Kwa hiyo, watu wengi hujiuliza, ‘Kuna ubaya gani kucheza kamari?’ Huenda ukabadili maoni yako kuhusu kucheza kamari baada ya kupata jibu katika makala zinazofuata.

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      John

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      Kazushige

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      Linda

  • Kuna Ubaya Gani Kucheza Kamari?
    Amkeni!—2002 | Julai 22
    • Kuna Ubaya Gani Kucheza Kamari?

      “Waaustralia 290,000 hivi wana tatizo la kucheza kamari, na jambo hilo husababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 3 za Marekani kila mwaka. Hiyo ni hasara kubwa kwa watu wenye tatizo hilo na vilevile kwa wale watu wapatao milioni 1.5 wanaoathiriwa moja kwa moja kwa sababu ya kufilisika, talaka, kujiua, na wakati wa kazi unaopotea bure.”—J. Howard, waziri mkuu wa Australia, mwaka wa 1999.

      JOHN, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, ana tatizo la kucheza kamari.a Alihamia Australia na akamwoa Linda aliyekuwa pia mchezaji kamari. Tamaa ya John ya kucheza kamari ilizidi. Anasema hivi: “Niliacha kununua tiketi za kushinda bahati nasibu na kuanza kucheza kamari kwenye uwanja wa mbio za farasi na katika nyumba za kamari. Muda si muda, nilikuwa nikicheza kamari karibu kila siku. Nyakati nyingine nilipoteza mshahara wote na nilikosa fedha za kulipa mkopo wa nyumba na za kulisha familia. Hata niliposhinda fedha nyingi, niliendelea kucheza kamari. Nilisisimuka sana niliposhinda na hiyo ndiyo iliyonifanya nisiweze kuacha kucheza.”

      Watu wengi wana tatizo kama la John. Ni kana kwamba jamii nzimanzima zimeshikwa na kichaa cha kucheza kamari. Gazeti la USA Today lilisema kwamba kati ya mwaka wa 1976 na 1997, kiasi kilichotumiwa katika michezo halali ya kamari huko Marekani kiliongezeka kwa asilimia 3,200. Hilo lilikuwa ongezeko kubwa sana.

      Gazeti la The Globe and Mail la Kanada linasema kwamba “hapo awali kucheza kamari kulionwa kuwa jambo baya. Leo, zoea hilo huonwa na watu wengi kuwa tafrija isiyo na ubaya wowote.” Likitaja sababu moja inayowafanya watu wabadili maoni, gazeti hilo linasema: “Maoni ya watu yamebadilika moja kwa moja kwa sababu ya kampeni inayodhaminiwa na serikali ya Kanada ya kuwachochea watu wacheze kamari. Huenda kampeni hiyo iligharimu serikali ya Kanada pesa nyingi na kuchukua muda mrefu kuliko kampeni nyingine yoyote katika historia ya nchi hiyo.” Jitihada za kuendeleza kamari zimewaathiri watu kwa njia gani?

      Watu Wengi Wana Tatizo la Kucheza Kamari

      Kadirio lililofanywa na Idara ya Mazoea Sugu ya Chuo cha Tiba cha Harvard lilionyesha kwamba mwaka wa 1996 kulikuwa na “Wamarekani milioni 7.5 waliokuwa na tatizo la kucheza kamari na wachezaji sugu,” na vilevile “vijana Wamarekani milioni 7.9 walikuwa na matatizo hayohayo.” Kadirio hilo lilitiwa ndani ya ripoti iliyotayarishwa na Tume ya Kitaifa Inayochunguza Athari za Kamari (NGISC) na kusomwa mbele ya Bunge la Marekani. Ripoti hiyo ilionyesha kwamba huenda ikawa idadi ya watu walio na tatizo la kucheza kamari huko Marekani ni kubwa kuliko ilivyokadiriwa.

      Serikali ya Marekani hutumia mabilioni ya dola kila mwaka ili kuwasaidia watu ambao wamepoteza kazi zao, wale ambao wamekuwa wagonjwa, na wale wanaohitaji usaidizi wa kifedha kwa sababu ya kucheza kamari, na ili kuwasaidia wachezaji sugu kuacha zoea hilo. Hata hivyo, mbali na gharama hiyo kubwa ya kifedha, tatizo kubwa zaidi ni magumu na mateso ambayo watu wenye tatizo la kucheza kamari huwaletea watu wa familia, marafiki, na wafanyakazi wenzao. Magumu hayo husababishwa na wizi, udanganyifu, kujiua, ujeuri nyumbani, na kuwatenda watoto vibaya. Uchunguzi mmoja huko Australia ulionyesha kwamba kwa kila mtu mmoja aliye na tatizo la kucheza kamari, watu kumi huathiriwa moja kwa moja. Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti huko Marekani inasema kwamba “asilimia 50 ya wenzi wa ndoa na asilimia 10 ya watoto hupigwa na mchezaji sugu wa kamari.”

      Zoea Linaloambukizwa

      Inaonekana kwamba watoto walio na wazazi wenye tatizo la kucheza kamari wanaweza kuambukizwa zoea hilo. Ripoti ya tume ya NGISC inasema hivi: ‘Yaelekea kwamba watoto wa watu wenye tatizo la kucheza kamari mara nyingi huwa na tabia mbaya kama vile kuvuta sigara, ulevi, na kutumia dawa za kulevya. Na kuna uwezekano mkubwa kwamba wao pia watakuwa na tatizo la kucheza kamari au watakuwa wachezaji sugu.’ Ripoti hiyo inaongeza kwamba ‘yaelekea kuna uwezekano mkubwa kwa vijana wanaocheza kamari kushindwa kudhibiti zoea hilo au kuwa wachezaji sugu hatimaye kuliko vile ilivyo kwa watu wazima wanaocheza kamari.’

      Dakt. Howard J. Shaffer, msimamizi wa Idara ya Mazoea Sugu ya Chuo cha Tiba cha Harvard, anasema hivi: ‘Imethibitishwa kwamba idadi ya vijana wanaocheza michezo haramu ya kamari inaongezeka kwa kiwango kilekile au hata inazidi ile ya vijana wanaocheza michezo ya kamari iliyohalalishwa.’ Alisema hivi kuhusu uwezekano wa wachezaji sugu wa kamari kutumia Internet kwa njia mbaya: “Kama vile kokeini kali aina ya crack ilivyo hatari kuliko kokeini ya kawaida, ndivyo michezo ya kamari kwenye Internet itakavyokuwa na matokeo mabaya kuliko michezo ya kawaida ya kamari.”

      Kucheza kamari huonwa mara nyingi kuwa tafrija isiyodhuru. Lakini zoea la kucheza kamari linaweza kuwatawala vijana sawa na dawa za kulevya, nalo linaweza kuwaingiza katika uhalifu. Uchunguzi mmoja uliofanywa Uingereza ulionyesha kwamba “asilimia 46 [ya vijana waliocheza kamari] waliiba kutoka kwa familia yao” ili waweze kuendelea kucheza.

      Hata hivyo, shirika moja maarufu la michezo ya kamari linatetea uchezaji wa kamari kwa kusema hivi: “Wamarekani wengi wanaopenda kucheza kamari hawaathiriwi hata kidogo.” Huenda ukaona kwamba kucheza kamari hakuathiri hali yako ya kiuchumi wala afya yako. Lakini, vipi hali yako ya kiroho? Je, kuna sababu nzuri za kuepuka kucheza kamari? Makala inayofuata itajibu maswali hayo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona sanduku “Je, Nina Tatizo la Kucheza Kamari?” kwenye ukurasa wa 4 na 5.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4, 5]

      Je, Nina Tatizo la Kucheza Kamari?

      Kulingana na Shirika la Madaktari wa Akili la Marekani, dalili zinazotajwa kwenye ukurasa wa 5 zinaweza kukusaidia kutambua zoea sugu la kucheza kamari. Wataalamu wengi hukubali kwamba mtu mwenye dalili kadhaa ana tatizo la kucheza kamari na mtu aliye na mojawapo ya dalili hizo anaelekea kuwa na zoea hilo.

      Kufikiria kamari daima Unafikiri daima kuhusu kucheza kamari, unarudia akilini michezo iliyotangulia, unapanga kucheza tena, au unafikiria njia za kupata fedha ambazo unahitaji kucheza.

      Kutosisimuka Unahitaji kutumia kiasi kikubwa zaidi cha fedha unapocheza ili usisimuke.

      Athari za Kujaribu Kuacha Unaudhika au unakasirika haraka unapojaribu kupunguza muda wa kucheza au kuacha kucheza.

      Kuepa matatizo Unacheza kamari ili kuepa matatizo au kutuliza hisia za kushindwa, hatia, wasiwasi, au kushuka moyo.

      Kulipia hasara Baada ya kupoteza pesa katika kamari, unarudi siku nyingine ili kulipia hasara, yaani, kupata tena pesa ulizopoteza.

      Kusema uwongo Unawadanganya watu wa familia yako, madaktari, au watu wengine ili wasijue muda unaotumia kucheza kamari.

      Kushindwa kudhibiti zoea Umejaribu tena na tena kuacha lakini umeshindwa, umeshindwa kudhibiti zoea la kucheza kamari au kupunguza muda unaotumia kucheza kamari.

      Matendo ya uhalifu Umefanya matendo ya uhalifu, kama vile ulaghai, wizi, au udanganyifu ili upate fedha za kutumia katika michezo ya kamari.

      Kupoteza marafiki wa karibu Umehatarisha au kuharibu uhusiano mzuri pamoja na rafiki wa karibu, au umepoteza nafasi fulani ya kupata elimu au kazi, kwa sababu ya kucheza kamari.

      Kukopa Umeomba mkopo ili kulipia madeni yaliyosababishwa na kucheza kamari.

      [Hisani]

      Chanzo: National Opinion Research Center at the University of Chicago, Gemini Research, na The Lewin Group.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Ujumbe wa Matangazo ya Michezo ya Bahati Nasibu

      Watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Duke, nchini Marekani, walisema hivi katika ripoti moja ambayo walituma kwa Tume ya Kitaifa Inayochunguza Athari za Kamari: “Matangazo yanayowatia watu moyo kununua tiketi za michezo ya bahati nasibu . . . yanaweza kuonwa kuwa elimu ya maadili. Elimu hiyo inafundisha kwamba kucheza kamari si hatari na hata ni jambo jema.” Matangazo ya michezo ya bahati nasibu huwaathiri watu jinsi gani? Ripoti hiyo inasema hivi: ‘Hatutii chumvi tunaposema kwamba matangazo ya bahati nasibu huwadanganya watu yanapoahidi kwamba ufanisi maishani hutokana na kuchagua nambari bora. Huenda “elimu” hiyo inayopotosha, ambayo inaendelezwa na makampuni ya michezo ya bahati nasibu, hatimaye itapunguza mapato ya serikali kwa kufanya uchumi ushuke. Matangazo ya kuwachochea watu kucheza kamari yatafanya uchumi ushuke hasa ikiwa yatawafanya watu washindwe kufanya kazi, washindwe kuweka akiba ya fedha, na washindwe kutumia fedha kwa ajili ya elimu au kujifunza kazi. Kwa vyovyote vile, hatutaki kuwafundisha watoto wetu kwamba mafanikio maishani hutegemea kuchagua nambari bora katika mchezo fulani wa kamari.’

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      Inawezekana Kucheza Kamari Nyumbani

      Sasa, badala ya kujenga nyumba za michezo ya kamari, mashirika ya michezo ya kamari yanatumia pesa chache zaidi kuwawezesha watu kucheza kamari nyumbani kwao kwenye vituo vya Internet. Katikati ya miaka ya 1990 kulikuwa na vituo 25 hivi vya kucheza kamari kwenye Internet. Mnamo mwaka wa 2001 kulikuwa na vituo zaidi ya 1,200, na mapato yanayotokana na kucheza kamari kwenye Internet yamekuwa yakiongezeka maradufu kila mwaka. Vituo vya kucheza kamari kwenye Internet vilichuma faida ya dola milioni 300 za Marekani mwaka wa 1997. Mapato ya mwaka wa 1998 yalikuwa dola milioni 650. Ripoti moja ya shirika la habari la Reuters inasema kwamba katika mwaka wa 2000 vituo vya kucheza kamari kwenye Internet vilichuma dola bilioni 2.2, na mapato “yanatarajiwa kuongezeka hadi dola bilioni 6.4” kufikia mwaka wa 2003.

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Familia za watu walio na tatizo la kucheza kamari zinaweza kukosa pesa za kununua chakula

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Idadi ya vijana wanaocheza kamari inaongezeka kwa haraka

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto wa watu walio na tatizo la kucheza kamari watakuwa na tatizo hilohilo

  • Epuka Mtego wa Kucheza Kamari
    Amkeni!—2002 | Julai 22
    • Epuka Mtego wa Kucheza Kamari

      “Kucheza kamari hakukuathiri afya yangu, na sikuzote niliamua kimbele kiasi cha fedha ambacho nilitaka kutumia katika mchezo. Lakini kila nilipocheza kamari ya bahati nasibu, nilichagua nambari ambazo niliamini zilikuwa za bahati njema.”—Linda.

      WACHEZAJI wengi wa kamari huamini kwamba watabahatika wakichagua nambari fulani au wakitumia hirizi mbalimbali. Huenda wasione desturi hizo za ushirikina kuwa za maana, lakini, bado wanasisitiza kuzifuata.

      Wachezaji wengine wa kamari hata humwomba Mungu awasaidie kushinda mchezo waliochagua. Hata hivyo, katika Biblia, Mungu anawashutumu wale wanaosema kwamba wanamwabudu lakini ‘wanaandika meza kwa ajili ya [“mungu wa,” NW] Bahati.’ (Isaya 65:11) Ndiyo, Mungu huchukia mazoea yanayowatia watu moyo waamini ushirikina na bahati. Michezo ya kamari inawafanya watu wategemee bahati bila kutumia akili.

      Pia, kamari huwachochea watu moja kwa moja wapende fedha. Watu wengi leo hawajali mambo ya kiroho, kwa hiyo, fedha imekuwa mungu wao na kucheza kamari ndiyo njia ya kuiabudu. Siku hizi watu huenda kwenye nyumba za fahari za kuchezea kamari badala ya kwenda kanisani, na humo wao hufundishwa kwamba pupa ni sifa nzuri. Watafiti wamegundua ya kwamba watu wengi hucheza kamari ili washinde “kiasi kikubwa sana cha fedha,” wala si kwa sababu ya tafrija au raha. Hata hivyo, Biblia inaonya hivi: “Kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote, na kwa kujitahidi kufikilia kupenda huku wengine wameongozwa wapotee njia kutoka kwenye imani na wamejichoma wenyewe kotekote kwa maumivu mengi.”—1 Timotheo 6:10.

      Biblia inasema hivi waziwazi katika 1 Wakorintho 6:9, 10: “Msiongozwe vibaya. Wala . . . waabudu-sanamu . . . wala watu wenye pupa . . . hawatarithi ufalme wa Mungu.” Mbali na kuwa ugonjwa unaodhoofisha jamii, pupa ni ugonjwa wa kiroho wa kufisha, lakini huo ni ugonjwa unaoweza kutibiwa.

      Walipata Nguvu ya Kufanya Mabadiliko

      Kazushige, aliyetajwa katika makala ya kwanza, anasema hivi: “Nilijaribu mara nyingi kuacha kucheza kamari. Nilitambua kwamba kucheza kamari kwenye uwanja wa mbio za farasi kuliharibu familia yangu. Kila wakati nilipoteza fedha zote nilizoshinda. Hata nilipoteza fedha ambazo mke wangu alikuwa ameweka akibani alipokuwa akitarajia kujifungua mwana wetu wa pili, na hatimaye nilianza kutumia fedha za kampuni. Sikuweza kujiheshimu tena. Mke wangu alilia na kuniomba mara nyingi niache kucheza kamari, lakini sikuweza kuacha.”

      Kisha Kazushige akaanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Anasema hivi: “Nilipoendelea kusoma Biblia nilisadikishwa kwamba kuna Mungu na kwamba ningefaidika iwapo ningemsikiliza. Niliazimia kwamba ningeacha kucheza kamari kwa msaada wa Mungu. Jambo la kushangaza ni kwamba mbali na kuacha kucheza kamari, sasa nachukia sana zoea hilo. Mimi huhuzunika sana ninapokumbuka jinsi familia yangu ilivyoteseka kwa sababu ya zoea langu la kucheza kamari. Ninamshukuru sana Yehova Mungu kwa kunisaidia kuacha kucheza kamari na kwa kunisaidia kuishi maisha yenye kusudi.”—Waebrania 4:12.

      John, aliyetajwa katika makala ya kwanza, alianza pia kujifunza Biblia. Anasema hivi: “Funzo langu la Biblia lilinisaidia kuchunguza maisha yangu. Kwa mara ya kwanza, niliona waziwazi jinsi zoea langu la kucheza kamari lilivyonidhuru mimi na familia yangu. Nilielewa kwamba kamari huendeleza ubinafsi na pupa, sifa ambazo humchukiza Yehova. Nilipoendelea kujifunza, upendo wangu kwa Yehova ulinipa nguvu ya kuacha kucheza kamari. Nilianza kucheza kamari kwa sababu nilitaka kupata maisha bora. Sasa, kwa sababu nimeacha kucheza kamari na ninamtumikia Yehova kwa furaha, matazamio yangu yametimizwa.”

      Mke wa John, Linda, aliazimia pia kuacha kucheza kamari. Anasema hivi: “Haikuwa rahisi. Lakini mimi na mume wangu tulipoanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, nilianza kutanguliza mambo ya maana zaidi maishani. Nilianza kupenda mambo ambayo Mungu hupenda, na pia kuchukia mambo ambayo anachukia, kutia ndani aina zote za pupa. Mbali na kuwa na maisha yenye kusudi, nina pesa nyingi zaidi mkobani.”—Zaburi 97:10.

      Ukisitawisha uhusiano wa karibu pamoja na Yehova Mungu utapata nguvu na hekima unayohitaji ili kuepuka mtego wa kucheza kamari. Ukifanya hivyo utaboresha hali yako ya kiuchumi, ya moyoni, na ya kiroho. Kisha utafurahia kujionea ukweli wa maneno ya Mithali 10:22: “Baraka ya BWANA hutajirisha, wala hachanganyi huzuni nayo.”

      [Blabu katika ukurasa wa 11]

      Mbali na kuwa ugonjwa unaodhoofisha jamii, pupa ni ugonjwa wa kiroho wa kufisha

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

      Kucheza Kamari na Ushirikina

      Katika ripoti moja iliyotumwa kwa Tume ya Kitaifa Inayochunguza Athari za Kamari, watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Duke walionyesha jinsi matangazo ya michezo ya kamari yanavyowatia watu moyo kuamini ushirikina. Ripoti hiyo inasema hivi: “Matangazo mengi [ya mchezo wa bahati nasibu] huchochea moja kwa moja tamaa ya mali . . . Hata hivyo, hayo hayachochei tamaa ya kupata mali kwa kufanya kazi kwa bidii, bali huwatia watu moyo kutegemea majini na ushirikina, kwa kuamini matarajio, ndoto, na ushirikina. Na kila msimamizi wa mchezo wa bahati nasibu anajua kwamba wengi wa wateja wao wa kawaida hutegemea ushirikina, unajimu, waaguzi, na vitabu maarufu vya ndoto vinavyoonyesha uhusiano uliopo kati ya nambari fulani na majina, tarehe, na ndoto. Badala ya kukazia kwamba kila nambari ina uwezekano uleule wa kuchaguliwa na kwamba kuchagua nambari inayopendwa na wengi kunaweza kupunguza faida, mashirika ya mchezo wa bahati nasibu huwatia wachezaji moyo kuchagua (na kutumia kila wakati) nambari ambazo wanaamini zinaweza kushinda.”

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      “Upendo wangu kwa Yehova ulinipa nguvu ya kuacha kucheza kamari.”—John

      “Mbali na kuwa na maisha yenye kusudi, nina pesa nyingi zaidi mkobani.”—Linda

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      “Jambo la kushangaza ni kwamba mbali na kuacha kucheza kamari, sasa nachukia sana zoea hilo.”—Kazushige

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki