Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kutovumiliana kwa Kidini Leo
    Amkeni!—1999 | Januari 8
    • Kutovumiliana kwa Kidini Leo

      “Kila mtu ana haki ya uhuru wa kuwaza, wa dhamiri na wa kidini; haki hii yatia ndani uhuru wa kubadili dini au imani yake, na uhuru, wa kudhihirisha dini au imani katika kufundisha, kuabudu na kushika desturi, ama mtu akiwa peke yake ama akiwa katika jumuiya pamoja na wengine na akiwa hadharani au faraghani.” Kifungu Cha 18, Azimio Rasmi Kwa Wote La Haki Za Kibinadamu, 1948.

      JE, WEWE hufurahia uhuru wa kidini katika nchi yako? Nchi nyingi ulimwenguni hukubali kijuu-juu tu kanuni hii nzuri, ambayo mara nyingi imetiwa ndani ya maazimio ya kimataifa. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba katika nchi nyingi ambapo kutovumiliana na ubaguzi ni matatizo makubwa, mamilioni yasiyohesabika ya watu leo hawana uhuru wa kidini. Kwa upande mwingine, watu wengi wanaishi miongoni mwa jamii nyingi, makabila mengi, au dini nyingi ambapo uhuru hulindwa na sheria na uvumiliano huhifadhiwa na utamaduni wa taifa.

      Na bado, katika sehemu hizo, uhuru wa kidini wa watu fulani unatishwa. “Ubaguzi unaotegemea dini au usadikisho uko karibu katika mifumo yote ya kiuchumi, ya kijamii na ya kiitikadi katika sehemu zote ulimwenguni,” akasema Angelo d’Almeida Ribeiro, Katibu wa Pekee wa zamani aliyeteuliwa na Tume ya Haki za Kibinadamu ya UM. Katika kitabu chao Freedom of Religion and Belief—A World Report, kilichochapishwa mwaka wa 1997, wahariri Kevin Boyle na Juliet Sheen wasema hivi: “Kunyanyaswa kidini kwa dini ndogondogo [na] kupigwa marufuku kwa itikadi na ubaguzi wa kikaidi . . . ni mambo yanayotukia kila siku kwenye mwisho wa karne ya ishirini.”

      Hata hivyo, ubaguzi wa kidini hauathiri tu dini ndogondogo. Profesa Abdelfattah Amor, Katibu wa Pekee wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya UM Kuhusu Kutovumiliana kwa Kidini, anaona kwamba “hakuna dini isiyoweza kuvunjiwa haki.” Basi, yawezekana kwamba unakoishi, dini fulani zinakabili kwa ukawaida kutovumiliana na ubaguzi.

      Namna Mbalimbali za Ubaguzi

      Kuna ubaguzi wa kidini wa namna nyingi. Nchi fulani hupiga marufuku dini zote isipokuwa dini moja tu, ambayo hufanywa iwe dini ya Serikali. Katika nchi nyingine, sheria zinazozuia utendaji wa dini fulani hupitishwa. Nchi fulani zimetunga sheria ambazo zimefafanuliwa kwa njia isiyo na msingi maalumu. Fikiria uwezekano wa ukiukwaji wa sheria iliyopendekezwa nchini Israeli ya kukataza uingizaji, uchapishaji, ugawanyaji, au umiliki wa broshua au vitabu “ambavyo vinaweza kumshawishi mtu ageuze dini.” Haishangazi kwamba gazeti la habari la International Herald Tribune liliripoti hivi: “Katika Israeli, Mashahidi wa Yehova wamesumbuliwa na kushambuliwa.” Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova katika jiji la Lod lilivunjwa mara tatu na kuharibiwa mara mbili na mashabiki wa othodoksi wenye kushikilia kauli yao kupita kiasi. Polisi walikataa kuzuia jambo hilo.

      Kitabu Freedom of Religion and Belief chataja mifano mingine ya kutovumiliana: “Uzushi na wazushi si dhana ya kale. . . . Kukataliwa, kunyanyaswa na kubaguliwa kwa wale walio na imani tofauti kwabaki kuwa kisababishi kikuu cha kutovumiliana. Mifano ni kama vile kikundi kinachoitwa Ahmadi katika Pakistan na [Wabaha’i] katika Misri, Iran, na Malasia kama ilivyo na Mashahidi wa Yehova katika nchi kadhaa za Ulaya Mashariki, Ugiriki na Singapore.” Kwa wazi, uhuru wa kidini umo hatarini katika sehemu nyingi za ulimwengu.

      Kwa kuona mambo haya, Federico Mayor, mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, alitangaza kwamba kizazi kinachoibuka hivi karibuni “hakitokezi shauku kamili. . . . Uhuru mpya ambao watu wamefurahia umetokeza tena kumbukumbu za chuki.” Akithibitisha hofu hii, mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza, alisema: “Uthibitisho wote waelekeza kwenye mkataa wa kwamba hali ya kutovumiliana kwa kidini . . . haipungui badala yake inaongezeka katika ulimwengu wa kisasa.” Hali hiyo ya kuongezeka kwa kutovumiliana yatisha uhuru wa kidini, labda uhuru wako wa kidini. Lakini, kwa nini uhuru wa kidini ni wa maana?

  • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?
    Amkeni!—1999 | Januari 8
    • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?

      Mwanzo wa wazo la uhuru wa kidini uliambatana na uchungu wa uzazi katika Jumuiya ya Wakristo. Ulikuwa ni pambano dhidi ya kulazimisha kauli, ubaguzi, na kutovumiliana. Ulisababisha kupotezwa kwa maisha ya maelfu yasiyohesabika katika mapambano ya kidini yenye umwagikaji mwingi wa damu. Historia hii yenye kuhuzunisha hutufundisha nini?

      “MNYANYASO umekuwa jambo linaloendelea la historia ya Kikristo,” aandika Robin Lane Fox katika kitabu Pagans and Christians. Wakristo wa mapema waliitwa farakano na walilaumiwa kuwa walitisha utengamano. (Matendo 16:20, 21; 24:5, 14; 28:22) Tokeo lilikuwa kwamba, wengine walivumilia mateso na kuuawa na hayawani-mwitu katika nyanja za michezo za Roma. Kwa kuona mnyanyaso huo mkali, wengine, kama vile mwanatheolojia Tertullian (ona picha katika ukurasa wa 8), waliomba kuwepo uhuru wa kidini. Mwaka wa 212 W.K., aliandika hivi: “Ni haki ya kibinadamu ya msingi, pendeleo la asili, kwamba kila mtu apaswa kuabudu kulingana na masadikisho yake.”

      Mnamo 313 W.K., mnyanyaso dhidi ya Wakristo uliofanywa na mamlaka ya Roma ulifikia kikomo chini ya utawala wa Konstantino, kwa kutolewa kwa Amri ya Milan, ambayo ilitoa uhuru wa kidini kwa Wakristo na wapagani vilevile. Kuhalalishwa kwa “Ukristo” katika Milki ya Roma kulikomesha wimbi la mnyanyaso dhidi ya Wakristo. Hata hivyo, karibu mwaka wa 340 W.K., mwandishi aliyedai kuwa Mkristo alitoa mwito wapagani wanyanyaswe. Hatimaye, mwaka wa 392 W.K., kupitia kwa Amri ya Constantinople, Maliki Theodosius wa Kwanza alipiga marufuku upagani katika milki hiyo, na uhuru wa kidini ukakoma kabla haujasitawi. “Ukristo” wa Kiroma ukiwa dini ya Serikali, Kanisa na Serikali zilianzisha kampeni ya mnyanyaso ambayo iliendelea kwa karne kadhaa, ikifikia upeo wake katika Krusedi zenye umwagikaji wa damu za karne ya 11 hadi ya 13 na katika ukatili wa Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi, yaliyoanza katika karne ya 12. Wale waliothubutu kutilia shaka imani iliyothibitishwa, kuwapo pekee kwa fundisho hilo, waliitwa wazushi na kusakwa katika mazingira ya uonevu ya wakati huo. Ni nini kilichochochea hatua hizi?

      Hali ya kutovumiliana kwa kidini ilikubaliwa kwa msingi wa kwamba muungano wa kidini ulitokeza msingi ulio thabiti zaidi kwa Serikali na kwamba mahitilafiano ya kidini yalitisha utengamano. Nchini Uingereza, katika mwaka wa 1602, mmojawapo wa mawaziri wa Malkia Elizabeth alitoa hoja: “Serikali haiwezi kuwa salama kamwe inaporuhusu dini mbili.” Kwa kweli, ilikuwa rahisi zaidi kupiga marufuku wapinzani wa kidini kuliko kutafuta kama kwa kweli wanasababisha tisho kwa Serikali au kwa dini iliyothibitishwa. Kichapo The Catholic Encyclopedia chasema: “Wala mamlaka za kilimwengu wala za kidini hazikupambanua tofauti ndogo sana kati ya wazushi walio hatari na wasiodhuru.” Hata hivyo, badiliko lingetokea karibuni.

      Mwanzo Wenye Maumivu wa Uvumiliano

      Badiliko katika Ulaya lilichochewa na mageuzi yaliyosababishwa na Uprotestanti, harakati ya kifarakano ambayo haikukoma. Kwa mwendo wenye kushangaza, Marekebisho ya Uprotestanti yaligawanya Ulaya kwa misingi ya kidini, hilo likatokeza wazo la uhuru wa dhamiri. Kwa kielelezo, Mleta Mabadiliko mashuhuri Martin Luther, alitetea maoni yake katika mwaka wa 1521, akasema: “Dhamiri yangu imetiishwa kwa Neno la Mungu.” Migawanyiko pia ilichochea Vita vya Miaka Thelathini (1618-1648), mfululizo wa vita vyenye ukatili vya kidini ambavyo viliharibu kabisa Ulaya.

      Ingawa hivyo, katikati ya vita, wengi walikuja kutambua kwamba mapambano hayakuwa namna ya maendeleo. Hivyo, mfululizo wa amri kama vile Amri ya Nantes katika Ufaransa (1598), ilijaribu bila ya mafanikio kurejesha amani katika Ulaya iliyokumbwa na vita. Ni kupitia kwa amri hizi kwamba wazo la kisiku hizi la uvumiliano likatokea hatua kwa hatua. Hapo kwanza, “uvumiliano” ulidokeza mawazo yasiyofaa. “Ikiwa chini ya hali fulani tungevumilia mafarakano . . . , bila shaka lingekuwa jambo ovu—kwa kweli, uovu mbaya sana—lakini si mbaya kama vita,” akaandika mwanafunzi mashuhuri wa elimu ya binadamu Erasmus katika mwaka wa 1530. Kwa sababu ya maoni haya yasiyofaa, watu fulani kama vile Mfaransa Paul de Foix katika mwaka wa 1561, walipendelea kuongea juu ya “uhuru wa kidini” badala ya “uvumiliano.”

      Ingawa hivyo, baada ya muda, uvumiliano haukuonwa tena kuwa uovu hata kidogo, wala uovu wa kiwango cha chini, bali kuwa mlinzi wa uhuru. Haukuonwa tena kuwa kuruhusu udhaifu bali kuwa uhakikisho kamili. Itikadi mbalimbali na haki za kufikiri tofauti zilipoanza kukubaliwa kuwa msingi wa jamii ya kisasa, ushabiki ulianza kupungua.

      Kufikia mwisho wa karne ya 18, uvumiliano ukahusianishwa na uhuru na usawa. Hilo lilionyeshwa kupitia sheria na maazimio kadhaa, kama vile Azimio mashuhuri la Haki za Kibinadamu na Raia (1789), katika Ufaransa, au Mswada wa Haki (1791), katika Marekani. Kwa kuwa hati hizi ziliathiri kufikiri kwa uhuru kuanzia karne ya 19 na kuendelea, uvumiliano na hivyo uhuru haukuonwa tena kuwa laana bali baraka.

      Uhuru wa Kiasi

      Ujapokuwa ni wenye thamani sana, uhuru ni wa kiasi tu. Kwa kutumia udhuru wa uhuru zaidi kwa wote, Serikali hupitisha sheria zinazowekea mipaka uhuru fulani wa watu. Yafuatayo ni masuala fulani yanayohusiana na uhuru ambayo kwa sasa yanajadiliwa katika nchi nyingi za Ulaya: Sheria za kiserikali zapasa kuathiri maisha ya kibinafsi ya watu kwa kiwango gani? Ni zenye matokeo jinsi gani? Zinaathirije uhuru?

      Mjadala kuhusu uhuru wa umma na wa kibinafsi umekaziwa na vyombo vya habari. Madai ya kutia kasumba, kutoza fedha kwa nguvu, kutenda watoto vibaya, na uhalifu mwingi ulio mbaya sana yameelekezwa dhidi ya vikundi fulani vya kidini, mara nyingi bila ithibati yenye msingi. Vyombo vya habari vimesambaza sana habari zinazohusisha vikundi vidogo vidogo vya kidini. Majina yenye kushushia hadhi kama vile “dhehebu” au “farakano” sasa yanatumiwa kila siku. Zikiwa chini ya mkazo wa maoni ya umma, serikali hata zimetokeza orodha za zile zinazoitwa eti madhehebu hatari.

      Ufaransa ni nchi ambayo inajivunia utamaduni wake wa uvumiliano na utengano wa dini na Serikali. Nchi hii inajivunia kuwa bara la “Uhuru, Usawa, Udugu.” Lakini, kulingana na kitabu Freedom of Religion and Belief—A World Report, “kampeni ya elimu shuleni ya kuendelezwa kukataliwa kwa harakati mpya za kidini” imependekezwa katika nchi hiyo. Hata hivyo, watu wengi wanafikiri kwamba hatua hii inatishia uhuru wa kidini. Jinsi gani hivyo?

      Tisho kwa Uhuru wa Kidini

      Uhuru wa kweli wa kidini hupatikana tu wakati vikundi vyote vya kidini vinavyostahi na kutii sheria vinapotendewa na Serikali kwa njia sawa. Uhuru huu hukoma wakati Serikali inapoamua bila msingi wowote ni kikundi kipi kati ya vikundi vya kidini si dini, na hivyo kuinyima mapendeleo ambayo Serikali huzipa dini. Gazeti la Time katika mwaka wa 1997 lilisema hivi: “Wazo muhimu la uhuru wa kidini hupoteza maana serikali inapojitwalia bila haki, haki ya kuidhinisha dini kana kwamba inatoa leseni za kuendesha gari kwa madereva.” Hivi karibuni mahakama moja ya rufani nchini Ufaransa ilitangaza kwamba kufanya hivyo “huongoza kwa kufahamu au bila kufahamu, kwenye utawala wa kiimla.”

      Haki za msingi hutishwa pia kikundi kimoja kinapodhibiti vyombo vya habari. Kwa kusikitisha, mambo yanazidi kuwa hivyo katika nchi nyingi. Kwa kielelezo, katika jitihada za kufasiri kikundi kilicho sawa kidini, mashirika yanayopinga madhehebu yamejiweka yenyewe kuwa mwendesha-mashtaka, hakimu, na baraza la mahakama na kisha yamejaribu kutumia vyombo vya habari kulazimisha umma kukubali maoni yao yenye kupendelea. Hata hivyo, kama vile gazeti la habari la Kifaransa Le Monde lilivyosema, kwa kufanya hivyo, nyakati nyingine mashirika haya yanadhihirisha “ufarakano uleule ambao hudai kuuzuia na kutisha kuanzisha mazingira ya ‘uonevu.’” Hilo gazeti la habari liliuliza hivi: “Je, kushutumiwa kijamii kwa vikundi vidogo vidogo vya kidini . . . hakutishi uhuru wa kimsingi?” Martin Kriele, aliyenukuliwa katika Zeitschrift für Religionspsychologie (Gazeti la Saikolojia ya Dini), alisema: “Msako wa uonevu kwa madhehebu hutokeza hangaiko kubwa zaidi kuliko dini nyingi ziitwazo madhehebu na vikundi vyenye kuvutia hisia. Kwa wazi: Raia wasiokiuka sheria wapaswa kuachwa kwa amani. Dini na itikadi zapaswa kuwa huru na kubaki zikiwa huru, katika Ujerumani pia.” Acheni tufikirie kielelezo kimoja.

      “Raia Wenye Mifano Mizuri”—Washutumiwa Kuwa “Hatari”

      Ni kikundi kipi cha kidini kilichosemekana kuwa “hatari zaidi ya mafarakano yote” kulingana na maoni ya wenye mamlaka Wakatoliki walionukuliwa katika gazeti mashuhuri la habari la Hispania ABC? Huenda ukashangaa kujua kwamba ABC lilikuwa likiongea kuhusu Mashahidi wa Yehova. Je, mashtaka yaliyofanywa dhidi yao yana lengo lenye msingi usio na ubaguzi? Ona matangazo yafuatayo kutoka vyanzo vinginevyo:

      “Mashahidi hufundisha watu walipe kodi kwa uaminifu, wasishiriki kwenye vita wala matayarisho ya vita, wasiibe na, kwa ujumla, wafuate maisha ambayo yakifuatiwa na wengine yanaweza kuboresha hali ya jamii kuishi pamoja.”—Sergio Albesano, Talento, Novemba-Desemba 1996.

      “Kinyume cha visingizio ambavyo vimeenezwa kwenye pindi fulani, kwa upande wangu [Mashahidi wa Yehova] hawahatarishi hata kidogo mashirika ya Serikali. Wao ni raia wapendao amani, wenye kudhamiria, na wanaostahi mamlaka.”—Mbunge wa Ubelgiji.

      “Mashahidi wa Yehova wanatambuliwa kuwa watu wenye kufuatia haki zaidi katika Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani.”—Gazeti la habari la Ujerumani Sindelfinger Zeitung.

      “Unaweza kuwaona [Mashahidi wa Yehova] kuwa raia wenye mifano mizuri. Wanalipa kodi kwa bidii, wanawatunza wagonjwa, wanapigana na kutokujua kusoma na kuandika.”—Gazeti la habari la Marekani San Francisco Examiner.

      “Mashahidi wa Yehova hupata mafanikio makubwa zaidi kuliko washiriki wa dini nyingine katika kudumisha vifungo vya ndoa vilivyo imara.”—American Ethnologist.

      “Mashahidi wa Yehova ni miongoni mwa raia walio wanyoofu zaidi na wenye bidii wa nchi za Kiafrika.”—Dakt. Bryan Wilson, Chuo Kikuu cha Oxford.

      “Washiriki wa imani hiyo wamechangia sehemu kubwa kwa miongo mingi iliyopita kupanua uhuru wa dhamiri.”—Nat Hentoff, Free Speech for Me—But Not for Thee.

      “Wamechangia . . . kihususa kuhifadhiwa kwa baadhi ya vitu vilivyo na thamani zaidi katika demokrasia yetu.”—Profesa C. S. Braden, These Also Believe.

      Kama ionyeshwavyo na manukuu yaliyo juu, Mashahidi wa Yehova wanatambuliwa ulimwenguni pote kuwa raia walio kielelezo kizuri. Kwa kuongezea, wanajulikana kwa kutoa elimu ya Biblia bila malipo na kwa kuendeleza maadili ya familia. Madarasa yao ya kujifunzia kusoma na kuandika yamesaidia mamia ya maelfu kwa miongo mingi, huku kazi zao za kibinadamu zikiwasaidia maelfu, hasa katika Afrika.

      Umaana wa Kutopendelea

      Jamii imejaa watu wasio wanyoofu wanaowawinda wasiokuwa na hatia. Kwa sababu hiyo, kuna uhitaji hususa wa kuwa macho kuhusu madai juu ya dini. Lakini kunakuwa na lengo gani na inafaidi uhuru wa kidini jinsi gani wakati ambapo waandishi wa habari fulani, badala ya kuwafikia wataalamu wasiopendelea upande wowote, wanategemea habari kutoka kwa makanisa yanayoona idadi ya washiriki wake ikididimia au kupata habari kutoka kwa mashirika yanayopinga mafarakano ambayo kutopendelea kwao kunatiliwa shaka sana? Mathalani, gazeti la habari lililowaita Mashahidi wa Yehova “farakano lililo hatari kuliko yote” lilikiri kwamba fasiri yake ilitokana na “wataalamu wa Kanisa [Katoliki].” Kwa kuongezea, gazeti moja la Kifaransa lilisema kwamba makala nyingi zinazoshughulikia mafarakano yanayoshukiwa zilitokana na mashirika yanayopinga mafarakano. Je, jambo hili lasikika kuwa njia bora kabisa ya kupata habari isiyopendelea?

      Mahakama na mashirika ya kimataifa yanayoshughulika na haki za kibinadamu za msingi, kama vile UM, yanasema kwamba “tofauti iliyopo kati ya dini na farakano ni bandia sana kuweza kukubaliwa.” Basi kwa nini wengine wanaendelea kutumia neno lenye kushushia hadhi “farakano”? Huu ni ushuhuda zaidi kwamba uhuru wa kidini unatishwa. Ni jinsi gani basi, uhuru huu wa msingi unavyoweza kulindwa?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      Watetezi wa Uhuru wa Kidini

      Maombi yaliyo dhahiri ya kutaka uhuru wa kidini yalitokana na mauaji ya kikatili ya mapambano ya kidini katika Ulaya mnamo karne ya 16. Maombi haya yangali yanahusu mazungumzo ya uhuru wa kidini.

      Sébastien Chateillon (1515-1563): “Mzushi ni nani? Sina jingine isipokuwa kwamba tunawaona wazushi kuwa watu wote ambao hawakubaliani na maoni yetu. . . . Ikiwa katika jiji hili unaonwa kuwa mwamini wa kweli, katika jiji jingine utaonwa kuwa mzushi.” Mtafsiri wa Biblia Mfaransa aliye mashuhuri na mtetezi shupavu wa uvumiliano, Chateillon alitaja jambo moja kuu katika mjadala wa uhuru wa kidini: Ni nani anayefasiri mzushi ni mtu gani?

      Dirck Volckertszoon Coornhert (1522-1590): “Twasoma kwamba katika nyakati za kale . . . hata Kristo mwenyewe katika Yerusalemu na kisha wafia-imani wengi katika Ulaya . . . walivuruga [jamii] kwa maneno yao ya kweli. . . . Maana ya neno ‘vuruga’ yahitaji kufafanuliwa kwa usahihi na waziwazi.” Coornhert alitoa hoja kwamba tofauti ya kidini haipasi kulinganishwa na kuvuruga utengamano. Aliuliza: Je, watu ambao ni waadilifu sana katika kutii na kustahi sheria kwa kweli ni tisho kwa utengamano?

      Pierre de Belloy (1540-1611): Ni “kukosa ujuzi kuamini kwamba dini zikiwa nyingi huleta na kuendeleza msukosuko Nchini.” Mwanasheria Mfaransa Belloy, akiandika wakati wa Vita vya Dini (1562-1598), alitoa hoja kwamba upatano wa Nchi hautegemei usare wa kidini isipokuwa, bila shaka, serikali iwe inajinyenyekeza chini ya misongo ya kidini.

      Thomas Helwys (karibu 1550–karibu 1616): “Ikiwa watu wake [wa Mfalme] ni raia watiifu na waaminifu kwa sheria zote za binadamu, hawezi kuwadai mengi zaidi.” Helwys, mmojawapo wa waanzilishi wa Baptisti ya Uingereza, aliandika kwa kuunga mkono mtengano wa Kanisa na Serikali, akimhimiza mfalme atoe uhuru wa kidini kwa makanisa na mafarakano yote na aridhike na mamlaka ya kiraia na mali. Maandishi yake yalikazia swali la hivi karibuni: Serikali yapasa kudhibiti hali ya kiroho ya watu kadiri gani?

      Mwandishi Asiyejulikana (1564): “Ili kuanzisha uhuru wa dhamiri, haitoshi kumruhusu mtu aepuke kufuatia dini ambayo haipendelei ikiwa, kwa sababu hiyohiyo, hakuna uhuru wa kufuatia dini anayoipenda.”

  • Kulinda Uhuru—Jinsi Gani?
    Amkeni!—1999 | Januari 8
    • Kulinda Uhuru—Jinsi Gani?

      KATIKA mji mdogo wa Rengasdengklok, Indonesia, vikundi vya kikabila viliishi pamoja kwa amani kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, inaonekana uvumiliano ulifikia kikomo mnamo Januari 30, 1997. Jeuri ilizuka kabla tu ya saa tisa za usiku katika siku ya karamu ya kidini, wakati muumini alipoanza kupiga ngoma. Mtu mmoja wa dini tofauti alishawishika kumtupia matusi jirani yake kwa sababu ya kelele hiyo. Walianza kupaaziana sauti, na mawe yakaanza kutupwa. Kulipambazuka, na ghasia zikaendelea huku watu wengine wakijiunga na ugomvi huo. Mwishoni mwa siku, mahekalu mawili ya Wabudha na makanisa manne ya Jumuiya ya Wakristo yalikuwa yameharibiwa. Gazeti la habari la International Herald Tribune liliripoti kisa hiki chini ya kichwa “Moto wa Ghasia za Kikabila Wachochewa na Kutovumiliana.”

      Katika nchi nyingi, vikundi vidogo vya kikabila ambavyo haki zao zinalindwa na sheria, mara nyingi hujipata vikikosa kuvumiliwa. Kutoa uhakikisho wa uhuru kupitia sheria hakumalizi visababishi vya msingi vya kutovumiliana. Uhakika wa kwamba kutovumiliana hakuonekani waziwazi haumaanishi kwamba hali hiyo haiko. Ikiwa hali zabadilika wakati fulani ujao na labda kuongoza kwenye hali zenye ubaguzi, hali ya kutovumiliana iliyojificha yaweza kujitokeza kwa urahisi. Hata ikiwa watu hawanyanyaswi moja kwa moja, waweza kuonyeshwa uhasama au mawazo yao yaweza kukandamizwa. Hali hii yaweza kuzuiwa jinsi gani?

      Kufahamu Visababishi vya Kutovumiliana

      Kiasili sisi huelekea kukataa au kushuku kitu ambacho ni tofauti au kisicho cha kawaida, hasa maoni ambayo hutofautiana na yetu. Je, hii yamaanisha kwamba uvumiliano ni jambo lisilowezekana? Kichapo cha UM Elimination of All Forms of Intolerance and Discrimination Based on Religion or Belief chaorodhesha kukosa ujuzi na uelewevu kuwa “miongoni mwa visababishi vya maana sana vya kutovumiliana na kubaguana kuhusiana na mambo ya kidini na itikadi.” Hata hivyo, kukosa ujuzi, ambacho ni kisababishi cha kutovumiliana, chaweza kushindwa. Jinsi gani? Kupitia elimu yenye usawaziko. “Elimu yaweza kuwa njia kuu ya kupambana na ubaguzi na kutovumiliana,” yasema ripoti moja ya Tume ya UM ya Haki za Kibinadamu.

      Elimu hiyo yapasa iwe na lengo gani? Gazeti UNESCO Courier lapendekeza kwamba badala ya kuendeleza kukataliwa kwa harakati za kidini, “elimu kwa ajili ya uvumiliano yapaswa kuwa na lengo la kukinza mavutano yanayoongoza kwenye hofu na kuwatenga wengine, na yapaswa kusaidia vijana wasitawishe uwezo wa kujiamulia mambo, kufikiri kwa makini na kusababu kiadili.”

      Bila shaka, vyombo vya habari vyaweza kuchangia sehemu ya maana katika kuendeleza “kufikiri kwa makini na kusababu kiadili.” Mashirika mengi ya kimataifa yanatambua uwezo wa vyombo vya habari wa kuelekeza maoni ya watu na kuendeleza maafikiano. Ingawa hivyo, ikiwa vyombo vya habari vitaendeleza kuvumiliana badala ya kutovumiliana kama vile vingine hufanya, uandishi wa habari usiopendelea wahitajiwa. Pindi kwa pindi, waandishi wa habari wanapaswa kupuuza maoni yanayokubalika na wengi. Wanapaswa kutokeza mchanganuo na maoni yasiyopendelea. Lakini je, hilo latosha?

      Njia Bora ya Kupigana na Kutovumiliana

      Uvumiliano haumaanishi kwamba kila mtu apaswa kuwa na mawazo yaleyale. Watu wanaweza kukosa kuafikiana. Huenda wengine wakahisi kwa dhati kwamba itikadi za mtu yule mwingine ni zenye makosa sana. Huenda hata wakaongea hadharani juu ya kukosa kuafikiana kwao. Hata hivyo, maadamu hawaenezi uwongo ili kuchochea upendeleo, huku si kutovumiliana. Hali ya kutovumiliana yaonekana wakati kikundi fulani kinaponyanyaswa, sheria mahususi zinapoelekezwa kwake, kinapotengwa, kinapopigwa marufuku, au kinapozuiwa kufuata itikadi zake katika njia fulani. Katika kutovumiliana kunakopita kiasi, wengine huua na wengine hulazimika kufa kwa ajili ya itikadi zao.

      Hali ya kutovumiliana yaweza kushindwa namna gani? Yaweza kufunuliwa hadharani, kama vile mtume Paulo alivyofunua hali ya kutovumiliana ya viongozi wa kidini wa siku yake. (Matendo 24:10-13) Ingawa hivyo, inapowezekana, njia bora ya kupigana na kutovumiliana ni kufanya kazi pamoja—kuendeleza uvumiliano, yaani, kuelimisha watu wawaelewe wengine vizuri zaidi. Ile ripoti ya UM kuhusu kuondolewa kwa kutovumiliana iliyorejezewa mapema yasema: “Kwa kuwa chanzo cha namna zote za kutovumiliana na ubaguzi unaotegemea dini au itikadi kiko katika akili ya mwanadamu, kwa hiyo ni katika akili za mwanadamu ambapo hatua ya kwanza yapasa kuelekezwa.” Elimu ya namna hiyo yaweza hata kuongoza watu wachunguze itikadi zao wenyewe.

      Federico Mayor, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, aliandika hivi: “Uvumiliano ni wema wa mtu aliye na usadikisho.” Akiandika katika gazeti Réforme, kasisi wa Dominika Claude Geffré alisema: “Uvumiliano halisi hutegemea usadikisho imara.” Mtu anayeridhishwa na itikadi zake mwenyewe haelekei kutishwa na itikadi za wengine.

      Mashahidi wa Yehova wamepata kwamba njia bora ya kuendeleza uvumiliano ni kuongea na watu wengine wenye itikadi tofauti. Mashahidi huchukua kwa uzito unabii wa Yesu kwamba “habari njema hii ya ufalme itahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ajili ya kuwa ushahidi kwa mataifa yote,” na wanajulikana vizuri kwa huduma yao ya kueneza evanjeli peupe. (Mathayo 24:14) Katika kazi hii, wanapata fursa ya kuwasikiliza watu wa dini nyingi tofauti—vilevile waatheisti—wakieleza itikadi zao. Na Mashahidi wanakuwa tayari kueleza itikadi zao kwa wale wanaotaka kusikiliza. Hivyo wanaendeleza ukuzi katika ujuzi na kuelewana. Ujuzi na uelewevu huo hufanya iwe rahisi zaidi uvumiliano usitawi.

      Uvumiliano na Zaidi

      Licha ya makusudio mazuri ya wengi na jitihada za pamoja za wengine, kwa wazi hali ya kutovumiliana ya kidini ingali tatizo leo. Ili kuwe na badiliko halisi, kitu fulani zaidi chahitajiwa. Gazeti la habari la Kifaransa Le Monde des débats lilikazia tatizo hilo: “Mara nyingi zaidi jamii ya kisasa husumbuka kwa kukosa mambo ya kihisia-moyo na ya kiroho. Sheria yaweza kulinda wale wanaotisha uhuru wa kidini. Sheria yaweza na inapaswa kuhakikisha kuna usawa mbele ya sheria, bila ubaguzi usio na msingi.” Kitabu Democracy and Tolerance chakiri hivi: “Tuna mengi sana ya kufanyia kazi ili kufikia mradi wa kuafikiana na kustahi kiwango cha mwenendo kwa wote.”

      Biblia inaahidi kwamba karibuni wanadamu wote wataunganishwa katika ibada safi ya Mungu mmoja wa kweli. Muungano huo utatokeza udugu wa ulimwenguni pote, ambapo watu watastahiana. Wanadamu hawatakosa ujuzi tena, kwa kuwa Ufalme wa Mungu utawafundisha watu njia za Yehova, hivyo ukitosheleza mahitaji yao ya kiakili, ya kihisia-moyo na ya kiroho. (Isaya 11:9; 30:21; 54:13) Usawa na uhuru halisi utajaa duniani. (2 Wakorintho 3:17) Kwa kujipatia uelewevu sahihi juu ya makusudi ya Mungu kwa wanadamu, unaweza kushinda kukosa ujuzi na kutovumiliana.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

      Dini Yatishwa

      Katika miaka ya hivi majuzi wenye mamlaka wamejaribu kuwadhoofisha Mashahidi wa Yehova katika Ufaransa kwa kukataa kuwapa mapendeleo kama dini nyinginezo. Hivi majuzi, michango inayopokewa ili kutegemeza utendaji wa kidini wa Mashahidi ilitozwa kodi nyingi sana. Wenye mamlaka nchini Ufaransa waliweka isivyo haki kodi ya dola milioni 50 (kodi na adhabu), wakiwa na kusudi dhahiri la kudhoofisha kikundi hiki cha Wakristo 200,000 na watetezi wao katika Ufaransa. Hili ni tendo dhahiri la ubaguzi wa kidini ambalo linapingana na kanuni zote za uhuru, udugu, na usawa.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki