-
Ustahimilivu—Kutoka Mwisho Mmoja Hadi Ule MwingineAmkeni!—1997 | Januari 22
-
-
Kutoka Ustahimilivu Hadi Ushupavu
Kinyume cha ustahimilivu ni ukosefu wa ustahimilivu, ambao huwa na viwango tofauti-tofauti vya mkazo. Ukosefu wa ustahimilivu waweza kuanza na kutokubali kwa akili iliyofungika mwenendo au njia ya mtu mwingine ya kufanya mambo. Kuwa na akili iliyofungika huzuia kufurahia maisha na kufanya akili ya mtu isipate mawazo mapya.
Kwa kielelezo, huenda mtu mgumu akachukizwa na idili nyingi za mtoto. Huenda kijana akachoshwa na njia za kutafakari za mtu mwenye umri mkubwa kupita wake. Mwulize mtu mwenye hadhari afanye kazi bega kwa bega na mtu ambaye hupenda sana kujasiria, na wote watachokozeka. Kwa nini mtu achukizwe, achoshwe, na achokozeke? Kwa sababu, katika kila kisa, mtu huona likiwa jambo gumu kustahimili mtazamo na mwenendo wa yule mwingine.
Mahali ambapo ukosefu wa ustahimilivu husitawi, kuwa na akili iliyofungika kwaweza kuongezeka kufikia ubaguzi, ambao ni kujiepusha na kikundi, jamii, au dini fulani. Ulio mbaya zaidi kuliko ubaguzi ni ushupavu, ambao waweza kujidhihirisha kwa chuki yenye jeuri. Tokeo ni taabu na umwagikaji wa damu. Fikiria kile ambacho ukosefu wa ustahimilivu ulitokeza wakati wa zile Krusedi! Hata leo, ukosefu wa ustahimilivu ni kisababishi kikuu cha mapambano katika Bosnia, Rwanda, na Mashariki ya Kati.
-
-
Usawaziko Ufaao Waweza Kufanya Maisha Yako YapendezeAmkeni!—1997 | Januari 22
-
-
“Wanadamu hawataki kuwa wastahimilivu,” akaandika Arthur M. Melzer, profesa mshiriki kwenye Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan. “Wanadamu wana mwelekeo wa asili wa kuonyesha . . . ubaguzi.” Kwa hiyo ukosefu wa ustahimilivu si tu kasoro ya utu ambayo hupata wachache tu; kuwa wenye akili iliyofungika hutupata sote kiasili kwa kuwa wanadamu wote si wakamilifu.—Linganisha Waroma 5:12.
Wenye Uwezekano wa Kuwa Wadadisi
Katika 1991, gazeti Time liliripoti juu ya hali inayoendelea kuongezeka ya akili iliyofungika Marekani. Makala hiyo ilifafanua “mtindo-maisha wa wadadisi,” watu ambao hujaribu kulazimisha kila mtu afuate viwango vyao wenyewe. Wasiokubaliana wamehasiriwa. Kwa mfano, mwanamke mmoja katika Boston alifutwa kazi kwa sababu ya kukataa kutumia virembeshi. Mwanamume mmoja katika Los Angeles alifutwa kazi kwa sababu ya kuwa mnene kupita kiasi. Kwa nini jitihada hiyo yote ya kufanya wengine wakubaliane?
Watu wenye akili iliyofungika hawakubali sababu, ni wenye ubinafsi, wenye shingo ngumu, na wenye kutaka watu wafuate maoni yao tu. Lakini je, watu wengi si ni wenye kukosa kukubali sababu, wenye ubinafsi, wenye shingo ngumu, au wenye kutaka maoni yao tu yafuatwe kwa kiwango fulani? Tabia hizi zikipata mizizi mizuri katika utu wetu, tutakuwa watu wenye akili iliyofungika.
Namna gani wewe? Je, wewe hudhihirisha hali ya kutokubali kwa habari ya ladha ya mtu mwingine ya chakula? Katika mazungumzo, je, kwa kawaida wewe hutaka kuwa mwenye neno la mwisho? Unapofanya kazi mkiwa kikundi, je, wewe hutarajia wengine wafuate njia yako ya kufikiri? Ikiwa ndivyo, lingekuwa jambo zuri kuongeza sukari kidogo katika chai yako!
Lakini, kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, ukosefu wa ustahimilivu waweza kuja katika namna ya ubaguzi wenye uhasama. Jambo moja liwezalo kufanya ukosefu wa ustahimilivu uongezeke ni hangaiko baya.
“Hisi Yenye Kina ya Kukosa Uhakika”
Wataalamu wa jamii na asili za wanadamu wamechunguza wakati uliopita wa mwanadamu ili wajue ni wakati gani na mahali gani ambapo ubaguzi wa jamii ulikuwa wazi. Walipata kwamba aina hii ya ukosefu wa ustahimilivu haiwi wazi wakati wote, wala haijidhihirishi katika kila nchi kwa kiwango kilekile. Gazeti la Ujerumani la sayansi ya asili GEO huripoti kwamba mikwaruzano ya kijamii hujitokeza katika wakati wa tatizo wakati ambapo “watu wana hisi yenye kina ya kukosa uhakika na kuhisi kwamba utambulisho wao umo hatarini.”
Je, hiyo “hisi yenye kina ya kukosa uhakika” imeenea sana leo? Bila shaka. Zaidi ya wakati mwingineo wote, wanadamu wanasumbuliwa na tatizo moja baada ya jingine. Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, kupanda kwa gharama ya maisha, idadi ya watu yenye kupita kiasi, kupungua kwa tabaka la ozoni, uhalifu majijini, uchafuzi wa maji ya kunywa, kuongezeka kwa joto tufeni pote—hofu yenye kusumbua ya lolote la mambo hayo huongeza hangaiko. Matatizo husababisha hangaiko, na hangaiko lisilofaa huongoza kwenye ukosefu wa ustahimilivu.
Ukosefu huo wa ustahimilivu hujidhihirisha, kwa mfano, mahali ambapo vikundi vya kikabila na tamaduni tofauti huchangamana, kama ilivyo katika nchi fulani za Ulaya. Kulingana na ripoti moja iliyotolewa na National Geographic katika 1993, nchi za Ulaya Magharibi wakati huo zilikuwa na wahamiaji zaidi ya milioni 22 kutoka nchi nyinginezo. Watu wengi wa ulaya “walihisi wamelemezwa na kuja kwa wingi wa wageni” wa lugha, tamaduni, au dini tofauti. Kumekuwa na ongezeko la maoni yaliyo dhidi ya wageni katika Austria, Hispania, Italia, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani.
Namna gani viongozi wa ulimwengu? Katika kipindi cha miaka ya 1930 na 1940, Hitler alifanya ukosefu wa ustahimilivu uwe sera ya serikali. Kwa kuhuzunisha, viongozi fulani wa kisiasa na wa kidini leo hutumia ukosefu wa ustahimilivu ili kupata malengo yao. Ndivyo imekuwa katika mahali kama vile Austria, Ireland, Marekani, Rwanda, Ufaransa, na Urusi.
-