-
Yehova Anyenyekeza Jiji Lenye KujigambaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
“Raha Baada ya Huzuni Yako”
17, 18. Kushindwa kwa Babiloni kutaleta baraka gani kwa Israeli?
17 Anguko la Babiloni litakuwa kitulizo kwa Israeli. Anguko hilo litasababisha kuachiliwa kwao kutoka utekwani na kuwapa fursa ya kurudi katika Bara Lililoahidiwa. Basi, Isaya sasa asema: “BWANA atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo. Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya BWANA; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea.” (Isaya 14:1, 2) Hapo, neno “Yakobo” larejezea Israeli kwa jumla—makabila yote 12. Yehova atahurumia “Yakobo” kwa kuliruhusu taifa hilo lirudi nyumbani. Wataambatana na maelfu ya wageni, ambao wengi wao watakuwa watumishi wa hekaluni wa Waisraeli. Hata Waisraeli fulani watakuwa na mamlaka juu ya watekaji wao wa awali.c
18 Maumivu ya kuishi uhamishoni yatatokomea mbali. Badala yake, Yehova atawapa watu wake “raha baada ya huzuni ya[o], na baada ya taabu ya[o], na baada ya utumishi ule mgumu [wa]liotumikishwa.” (Isaya 14:3) Baada ya kuachiliwa kutoka katika utumwa wa kimwili, Israeli hatapatwa tena na huzuni na taabu ya kuishi miongoni mwa waabudu wa miungu isiyo ya kweli. (Ezra 3:1; Isaya 32:18) Kitabu cha Lands and Peoples of the Bible, kikielezea jambo hilo, chasema: “Miungu ya Babiloni ilifanana na Wababiloni, katika tabia yake mbaya sana. Hiyo ilikuwa yenye woga, ulevi na upumbavu.” Ni kitulizo kilichoje kuponyoka kutoka katika hali hiyo mbaya ya kidini!
19. Ni nini kinachohitajiwa ili Israeli ipate msamaha wa Yehova, nasi twaweza kujifunza nini kutokana na hilo?
19 Hata hivyo, rehema ya Yehova ina masharti. Lazima watu wake waonyeshe majuto kwa sababu ya uovu wao, uliomfanya Mungu awaadhibu vikali. (Yeremia 3:25) Ungamo la unyofu, litokalo moyoni, litafanya Yehova awasamehe. (Ona Nehemia 9:6-37; Danieli 9:5.) Kanuni hiyohiyo yatumika leo. Kwa maana “hakuna mtu asiyekosa,” sisi sote twahitaji rehema ya Yehova. (2 Mambo ya Nyakati 6:36) Yehova, Mungu mwenye rehema, hutuomba kwa upendo tuungame dhambi zetu kwake, tutubu, na tuache mwenendo wowote mbaya, ili tupate kuponywa. (Kumbukumbu la Torati 4:31; Isaya 1:18; Yakobo 5:16) Jambo hilo hutusaidia tupate upendeleo wake na pia hutufariji.—Zaburi 51:1; Mithali 28:13; 2 Wakorintho 2:7.
“Mithali” Dhidi ya Babiloni
20, 21. Jirani za Babiloni washangiliaje kuanguka kwake?
20 Zaidi ya miaka 100 kabla ya Babiloni kuinuka kuwa serikali kubwa ya ulimwengu, Isaya atabiri jinsi ulimwengu utakavyotenda Babiloni aangukapo. Kupitia unabii, awaamuru hivi Waisraeli ambao wameachiliwa kutoka utekwani Babiloni: “Utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri! BWANA amelivunja gongo la wabaya, fimbo ya enzi yao wenye kutawala. Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, kwa mapigo yasiyokoma; aliyewatawala mataifa kwa hasira, ameadhibiwa asizuie mtu.” (Isaya 14:4-6) Babiloni amejifanyia jina la kuwa mshindi mwenye kuonea, awafanyaye watu huru kuwa watumwa. Basi, yafaa kama nini kwamba kuanguka kwake kushangiliwe kwa “mithali” inayoelekezwa hasa kwa nasaba ya wafalme ya Babiloni—kuanzia kwa Nebukadreza na kuishia kwa Nabonido na Belshaza—iliyoongoza wakati wa siku za utukufu wa jiji hilo kubwa!
21 Kuanguka kwake kutaleta hali tofauti kama nini! “Dunia yote inastarehe na kutulia; hata huanzilisha kuimba. Naam, misunobari inakufurahia, na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, hapana mkata miti aliyetujia.” (Isaya 14:7, 8) Machoni pa watawala wa Babiloni, wafalme wa mataifa jirani walikuwa kama miti ya kukatwa na kutumiwa kwa malengo yao wenyewe. Lakini hayo yote yamekwisha. Mkata miti wa Babiloni amekata mti wake wa mwisho!
22. Kishairi, Sheoli yaathiriwaje na kuanguka kwa nasaba ya wafalme ya Babiloni?
22 Babiloni yaanguka kwa ajabu sana hivi kwamba kaburi lenyewe lajibu hivi: “Kuzimu [“Sheoli,” “NW”] chini kumetaharuki kwa ajili yako, ili kukulaki utakapokuja; huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, naam, walio wakuu wote wa dunia; huwainua wafalme wote wa mataifa, watoke katika viti vyao vya enzi. Hao wote watajibu na kukuambia, Je! wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, na sauti ya vinanda vyako; funza wametandazwa chini yako, na vidudu vinakufunika.” (Isaya 14:9-11) Huo ni mfano wa kishairi wenye nguvu kama nini! Ni kana kwamba kaburi la ujumla la wanadamu lapaswa kuwaamsha wafalme wote waliokufa kabla ya nasaba ya wafalme ya Babiloni ili wapate kumlaki mgeni huyo. Waidhihaki serikali inayotawala ya Babiloni, ambayo sasa haijiwezi, ikiwa imelala kwenye kitanda cha funza badala ya kitanda chenye bei ghali, ikiwa imefunikwa na vidudu badala ya vitani vyenye bei ghali.
“Kama Mzoga Uliokanyagwa Chini ya Miguu”
23, 24. Wafalme wa Babiloni waonyesha kiburi gani kikuu?
23 Isaya aendeleza mithali hiyo: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!” (Isaya 14:12) Kiburi chenye ubinafsi chawafanya wafalme wa Babiloni wajiinue juu ya jirani zao. Kama nyota ing’aayo sana katika anga la alfajiri, wao wadhihirisha uwezo na mamlaka yao kwa njia yenye kiburi. Jambo hasa linalosababisha kiburi ni ushindi wa Nebukadreza juu ya Yerusalemu, ambao Ashuru ilishindwa kutekeleza. Tamko la mithali laonyesha nasaba ya wafalme ya Babiloni yenye kiburi, ikisema: “Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye Aliye juu.” (Isaya 14:13, 14) Je, kuna utovu mkubwa kushinda huo?
24 Katika Biblia, wafalme wa nasaba ya Daudi hufananishwa na nyota. (Hesabu 24:17) Kuanzia kwa Daudi na kuendelea, “nyota” hizo zilitawala huko Mlima Sayuni. Baada ya Solomoni kujenga hekalu katika Yerusalemu, jina Sayuni likaja kumaanisha jiji lote. Chini ya agano la Sheria, ilikuwa lazima kwa wanaume wote Waisraeli kusafiri hadi Sayuni mara tatu kwa mwaka. Basi, jiji hilo likawa “mlima wa mkutano.” Kwa kuazimia kushinda wafalme wa Yuda na kuwaondoa katika mlima huo, Nebukadreza atangaza lengo lake la kujiinua juu ya “nyota” hizo. Yeye hamsifu Yehova kwa sababu ya ushindi wake juu yao. Badala yake, ni kana kwamba ajiweka kwa kiburi mahali pa Yehova.
25, 26. Nasaba ya wafalme ya Babiloni yakumbwaje na mwisho wenye kufedhehesha?
25 Basi kuna mambo yaliyo kinyume kama nini yanayoingojea nasaba ya wafalme ya Babiloni! Babiloni kamwe haitainuliwa juu kuliko nyota za Mungu. Badala yake, Yehova asema: “Utashushwa mpaka kuzimu [“Sheoli,” “NW”]; mpaka pande za mwisho za shimo. Wao wakuonao watakukazia macho, watakuangalia sana, wakisema, Je! huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, huyu ndiye aliyetikisa falme; aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?” (Isaya 14:15-17) Nasaba hiyo ya wafalme yenye kutamani makuu itashuka ndani ya Hadesi (Sheoli), kama binadamu mwingine yeyote.
26 Basi, serikali iliyoshinda falme, ikaharibu nchi inayozaa, na kupindua majiji mengi itakuwa wapi? Serikali ya ulimwengu iliyochukua mateka na ikakataa kuwaruhusu kurudi nyumbani kwao itakuwa wapi? Kwani, nasaba ya wafalme ya Babiloni hata haitazikwa inavyofaa! Yehova asema: “Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe; bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, kama chipukizi lililochukiza kabisa; kama vazi la wale waliouawa, wale waliochomwa kwa upanga, wale washukao mpaka misingi ya shimo; kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu. Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, kwa maana umeiharibu nchi yako, umewaua watu wako; kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.” (Isaya 14:18-20) Katika ulimwengu wa kale, ilikuwa aibu kwa mfalme kutozikwa kwa heshima. Basi, vipi kuhusu nasaba ya wafalme ya Babiloni? Ni kweli kwamba labda wafalme mmoja-mmoja wazikwa kwa heshima, lakini nasaba ya wafalme iliyotokana na Nebukadreza yatupwa ‘kama chipukizi linalochukiza kabisa.’ Ni kana kwamba nasaba hiyo ya wafalme imetupwa ndani ya kaburi lisilojulikana—kama mwanajeshi wa nchi kavu aliyeuawa vitani. Walitwezwa kama nini!
27. Vizazi vya baadaye vya Wababiloni vyatesekaje kwa sababu ya uovu wa baba zao?
27 Mwishoni mwa mithali hiyo, Wamedi na Waajemi wanaoshinda wapewa maagizo: “Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake. Kwa sababu ya uovu wa baba zao; wasije wakainuka na kuitamalaki nchi, na kuujaza miji uso wa ulimwengu.” (Isaya 14:21) Anguko la Babiloni litakuwa lenye kudumu. Nasaba ya wafalme ya Babiloni itang’olewa kabisa. Haitainuka tena. Vizazi vya baadaye vya Wababiloni vitateseka kwa sababu ya “uovu wa baba zao.”
28. Ni nini kilichosababisha dhambi ya wafalme wa Babiloni, nasi twajifunza nini kutokana na jambo hilo?
28 Hukumu iliyotolewa dhidi ya nasaba ya wafalme ya Babiloni inatupa fundisho muhimu. Tamaa ya makuu isiyo na kikomo ndiyo iliyosababisha dhambi ya wafalme wa Babiloni. (Danieli 5:23) Mioyo yao ilijaa tamaa ya kupata mamlaka. Walitaka kutawala wengine. (Isaya 47:5, 6) Nao walitamani utukufu wa wanadamu, ambao wafaa kupewa Mungu. (Ufunuo 4:11) Hilo ni onyo kwa yeyote aliye na mamlaka—hata katika kutaniko la Kikristo. Tamaa ya makuu na kiburi chenye ubinafsi ni tabia ambazo Yehova hatavumilia, katika watu mmoja-mmoja au katika mataifa.
29. Kiburi na tamaa ya makuu ya watawala wa Babiloni vilidhihirisha nini?
29 Kiburi cha watawala wa Babiloni kilidhihirisha roho ya “mungu wa huu mfumo wa mambo,” Shetani Ibilisi. (2 Wakorintho 4:4) Yeye pia ana hamu ya kupata mamlaka naye hutamani kujiinua juu ya Yehova Mungu. Kama ilivyokuwa kwa habari ya mfalme wa Babiloni na watu aliotiisha, tamaa ya Shetani isiyo takatifu imetokeza taabu na mateso kwa wanadamu wote.
30. Ni Babiloni gani mwingine anayetajwa katika Biblia, naye ameonyesha roho gani?
30 Zaidi ya hayo, twasoma juu ya Babiloni mwingine katika kitabu cha Ufunuo—“Babiloni Mkubwa.” (Ufunuo 18:2) Shirika hilo, milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli, pia limeonyesha roho yenye kiburi, yenye kuonea, na yenye ukatili. Basi, yeye pia lazima akabili ‘siku ya Yehova’ na aharibiwe wakati wa Mungu ufikapo. (Isaya 13:6) Tangu mwaka wa 1919 ujumbe huu umetangazwa kotekote duniani: “Babiloni Mkubwa ameanguka!” (Ufunuo 14:8) Aliposhindwa kuwazuia watu wa Mungu utekwani, alianguka. Karibuni ataangamizwa kabisa. Yehova aliamuru hivi kuhusu Babiloni la kale: “Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake; mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda; kwa sababu amefanya kiburi juu ya BWANA, juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.” (Yeremia 50:29; Yakobo 2:13) Babiloni Mkubwa atahukumiwa vivyo hivyo.
31. Ni nini kitakachompata Babiloni Mkubwa hivi karibuni?
31 Basi, taarifa ya mwisho ya Yehova kwenye unabii huu katika kitabu cha Isaya haihusu Babiloni ya kale peke yake, bali pia Babiloni Mkubwa: “Nitainuka, nishindane nao . . . na katika Babeli nitang’oa jina na mabaki, mwana na mjukuu . . . Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu.” (Isaya 14:22, 23) Magofu yaliyoachwa ukiwa ya Babiloni ya kale yaonyesha kile ambacho karibuni Yehova atautenda Babiloni Mkubwa. Ni faraja iliyoje kwa wapendao ibada ya kweli! Ni kitia-moyo kilichoje cha kujitahidi kutoruhusu kamwe tabia za Shetani za kiburi, dharau, au ukatili zisitawi ndani yetu!
-
-
Yehova Anyenyekeza Jiji Lenye KujigambaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
[Picha katika ukurasa wa 186]
Kama vile Babiloni la kale, Babiloni Mkubwa atakuwa rundo la magofu
-
-
Shauri la Yehova Dhidi ya MataifaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
1. Isaya arekodi tangazo gani la hukumu dhidi ya Ashuru?
YEHOVA aweza kutumia mataifa kuwatia nidhamu watu wake kwa sababu ya uovu wao. Ijapokuwa hivyo, hayapi msamaha mataifa hayo kwa ajili ya ukatili wao usiostahili, kiburi, na kuchukia kwao ibada ya kweli. Basi, muda mrefu mapema, yeye ampulizia Isaya kurekodi “ufunuo juu ya Babiloni.” (Isaya 13:1) Hata hivyo, Babiloni ni tisho la wakati ujao. Katika siku ya Isaya, Ashuru yawakandamiza watu wa agano wa Mungu. Ashuru yaharibu ufalme wa kaskazini wa Israeli na kuangamiza sehemu nyingi za Yuda. Lakini ushindi wa Ashuru ni wa muda tu. Isaya aandika: “BWANA wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa . . . kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao.” (Isaya 14:24, 25) Muda mfupi baada ya Isaya kutangaza unabii huo, tisho la Ashuru laondolewa nchini Yuda.
2, 3. (a) Katika nyakati za kale, Yehova anyosha mkono wake juu ya nani? (b) Usemi wa kwamba Yehova anyosha mkono wake juu ya “mataifa yote” wamaanisha nini?
2 Hata hivyo, namna gani kuhusu mataifa mengine ambayo ni adui za watu wa agano wa Mungu? Hayo pia sharti yahukumiwe. Isaya atangaza: “Hilo ndilo kusudi [“shauri,” “NW”] lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote. Maana BWANA wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?” (Isaya 14:26, 27) ‘Shauri’ la Yehova lamaanisha mengi zaidi kuliko pendekezo tu. Lamaanisha azimio lake thabiti, agizo lake. (Yeremia 49:20, 30) “Mkono” wa Mungu ni nguvu yake yenye kutenda. Kwenye mistari ya mwisho ya Isaya sura ya 14 na katika sura ya 15 hadi 19, shauri la Yehova liko dhidi ya Ufilisti, Moabu, Dameski, Ethiopia, na Misri.
3 Hata hivyo, Isaya asema kuwa mkono wa Yehova umenyoshwa juu ya “mataifa yote.” Basi, ingawa unabii huo mbalimbali wa Isaya watimizwa kwa mara ya kwanza katika nyakati za kale, kanuni ya unabii huo yahusu pia “wakati wa mwisho” Yehova anyoshapo mkono wake juu ya falme zote za dunia. (Danieli 2:44; 12:9; Waroma 15:4; Ufunuo 19:11, 19-21) Muda mrefu mapema, Mungu Mweza Yote, Yehova, afunua kusudi lake akiwa na uhakika. Hakuna awezaye kuuzuia mkono wake ulionyoshwa.—Zaburi 33:11; Isaya 46:10.
“Joka la Moto Arukaye” Dhidi ya Ufilisti
4. Ni yapi baadhi ya mambo makuu ya tangazo la Yehova dhidi ya Ufilisti?
4 Wafilisti wazingatiwa kwanza. “Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi. Usifurahi, Ee Ufilisti, pia wote, kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika; maana katika shina la nyoka atatoka fira, na uzao wake ni joka la moto arukaye.”—Isaya 14:28, 29.
5, 6. (a) Uzia alikuwaje kama nyoka kwa Wafilisti? (b) Hezekia athibitika kuwa nini dhidi ya Ufilisti?
5 Mfalme Uzia alikuwa na nguvu za kutosha kuzuia tisho la Ufilisti. (2 Mambo ya Nyakati 26:6-8) Machoni pao, Uzia alikuwa kama nyoka, na fimbo yake ilimpiga-piga jirani huyo mwenye uadui. Baada ya kifo cha Uzia—‘fimbo yake ilivunjika’—Yothamu mwaminifu akatawala, ingawa “watu waliendelea kufanya maovu.” Kisha Ahazi akawa mfalme. Hali ikabadilika, na Wafilisti wakafanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yuda kwa mafanikio. (2 Mambo ya Nyakati 27:2, BHN; 28:17, 18) Hata hivyo, sasa hali yabadilika tena. Mfalme Ahazi afa mwaka wa 746 K.W.K., na Hezekia mchanga achukua kiti cha ufalme. Iwapo Wafilisti wafikiri kuwa hali yao itaendelea kuwa shwari, basi wamekosea kabisa. Hezekia athibitika kuwa adui motomoto. Hezekia, aliye mzao wa Uzia (“uzao” kutoka katika “shina” lake), ni kama “joka la moto arukaye”—huku akipiga mbio kwenda kushambulia kwa haraka, na kutokeza madhara makali, kana kwamba anawadunga majeruhi wake sindano ya sumu.
6 Huo ni ufafanuzi ufaao kuhusu mfalme huyo mpya. Hezekia ndiye ‘aliyewapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake.’ (2 Wafalme 18:8) Kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria za Mfalme Senakeribu wa Ashuru, Wafilisti waja kutiishwa chini ya Hezekia. “Walio maskini”—ufalme wa Yuda uliofifia—wapata kufurahia usalama na wingi wa mali, huku Ufilisti ikidhikika kwa njaa.—Soma Isaya 14:30, 31.
7. Hezekia apaswa kutoa tangazo gani lenye imani kwa mabalozi waliomo Yerusalemu?
7 Yaonekana kwamba kuna mabalozi nchini Yuda—labda wanatafuta msaada dhidi ya Ashuru. Wapaswa kuambiwa nini? “Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani?” Je, Hezekia atafute usalama kwa kushirikiana na wageni? Hata! Yampasa awaambie wajumbe hao: “BWANA ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake wataona kimbilio.” (Isaya 14:32) Ni lazima mfalme huyo amtumaini Yehova kabisa-kabisa. Msingi wa Sayuni ni thabiti. Jiji hilo litadumu likiwa mahali salama kutokana na tisho la Ashuru.—Zaburi 46:1-7.
8. (a) Mataifa fulani leo yamekuwaje kama Ufilisti? (b) Yehova amefanya nini ili kuwasaidia watu wake leo, kama alivyofanya nyakati za kale?
8 Sawa na Ufilisti, mataifa fulani leo huwapinga vikali waabudu wa Mungu. Mashahidi Wakristo wa Yehova wametupwa magerezani na katika kambi za mateso. Wamepigwa marufuku. Baadhi yao wameuawa. Wapinzani wazidi ‘kuishambulia nafsi yake mwenye haki.’ (Zaburi 94:21) Machoni pa adui zao, kikundi hicho cha Wakristo huenda kikaonekana kuwa “maskini” na “wahitaji.” Hata hivyo, kwa msaada wa Yehova, wao hufurahia chakula kingi cha kiroho, huku adui zao wakidhikika kwa njaa. (Isaya 65:13, 14; Amosi 8:11) Yehova atakaponyosha mkono wake dhidi ya Wafilisti wa siku za kisasa, “maskini” hao watakuwa salama. Wapi? Kwa kushirikiana na ‘nyumba ya Mungu,’ ambamo Yesu ndiye jiwe la pembeni la msingi lililo thabiti. (Waefeso 2:19, 20) Nao watakuwa chini ya ulinzi wa “Yerusalemu la kimbingu,” Ufalme wa Yehova wa mbinguni, ambapo Yesu Kristo ndiye Mfalme wake.—Waebrania 12:22; Ufunuo 14:1.
-