-
Visiwa VinavyojengwaAmkeni!—1998 | Mei 22
-
-
Kila volkano ilikua kutokana na kumwagika kwa maelfu ya mitiririko ya lava. Milipuko huanza chini ya maji, ambapo lava hupoa kwa haraka, ikifanyiza ganda na mitiririko yenye umbo la ulimi ambayo ikiwekwa pamoja huonekana kama mito. Wakati volkano inayokua inapojitokeza juu ya maji, mitiririko ya lava hubadili umbo. Wataalamu wa volkano hutumia maneno ya Hawaii “pahoehoe” kwa mitiririko ya umajimaji ulio na uso laini, wenye mawimbi, na uonekanao kama kamba na “aa” kwa lava ambayo si laini, yenye uso usiosawazika, na ifananayo na vifusi. Volkano hutokeza mlima mpana wenye miteremko ambao kwa umbo hufanana na ngao walizobeba wanavita Waroma. Kreta kubwa hutokea juu ya volkano wakati magma, au miamba iliyoyeyuka, inapofoka au kujiondoa kwenye mianya karibu na uso. Pia, hifadhi ya magma ndani ya volkano hutokeza kanieneo. Kanieneo hii husukuma sehemu ya volkano kuelekea baharini, ikifungua vikundi vikubwa vya miatuko. Mwishowe, kama katika kisa cha Mauna Kea, milipuko ya volkano zenye umbo la ngao huwa zenye kulipuka zaidi, zikitokeza marundo ya volkano yenye umbo la pia ya vipande vya lava ambavyo hufunika volkano.
-
-
Visiwa VinavyojengwaAmkeni!—1998 | Mei 22
-
-
Visiwa Vinavyosonga
Historia iliyorekodiwa kwa zaidi ya miaka 200 iliyopita yaonyesha kwamba ni volkano zilizo katika visiwa viwili tu vilivyo kusini-mashariki zaidi, Hawaii na Maui, ambazo zimekuwa zikitenda. Hali hii yenye kukoroweza iliwasukuma wanasayansi kuchunguza zaidi historia ya miamba ya safu ya kisiwa hicho. Ndani ya lava kuna kiasi kidogo sana cha potasiamu yenye nururishi pamoja na matokeo yake ya baada ya kuoza, agoni, ambazo wangeweza kupima katika maabara ili kukadiria umri wa miamba. Uchunguzi wa aina hiyo ulionyesha kusonga kuelekea kaskazini-magharibi kwa kuendelea kuzeeka kwa Jamii-Visiwa vya Hawaii kwa muda wa miaka milioni nyingi.
Kwa kuwa milipuko ya Hawaii imekuwa ikitokea sana katika sehemu ya kusini-mashariki ya safu ya kisiwa, je, hili lamaanisha kuwa chanzo cha magma chini yake kimekuwa kikisonga pia? Kwa kweli, wanajiolojia wamehakikisha kwamba chanzo cha magma, ambacho wao hukiita mahali moto, hakisongi. Badala ya hivyo, sakafu ya Bahari ya Pasifiki imekuwa ikisonga juu ya mahali hapo moto, ikiondoa volkano za kisiwa hicho kwenye mahali moto kama marundo ya miamba yaliyo juu ya mkanda wa kuchukulia unaosonga. Mwendo huuhuu husugua sakafu ya bahari ya Pasifiki kando ya matungamo ya mabara yanayopakana nayo na sehemu nyingine za sakafu ya bahari, ikisababisha mengi ya matetemeko ya dunia makubwa ambayo hutokea katika Ukingo wa Pasifiki. Ikiwa waishi Hawaii, nyumba yako imesonga sentimeta 7.5 kuelekea kaskazini-magharibi tangu mwaka jana!
Wanasayansi wanadokeza kwamba mahali moto pengine kama palipo chini ya Hawaii ndipo hutokeza volkano kote ulimwenguni, kwenye bara na baharini. Pengi pa mahali hapa moto huonyesha ithibati ya milipuko inayohama, ambalo lamaanisha kwamba huenda uso wa dunia umekuwa ukisonga mahali unapoishi pia.
Uumbikaji wa Visiwa Vipya . . .
Kwa kuwa mamia ya maelfu ya miaka imehitajika ili kujenga volkano kubwa kwenye Kisiwa Kikubwa, twaweza kutarajia kwamba kisiwa hicho kimekuwa kikisonga kutoka kwenye mahali moto katika wakati huo. Volkano mpya na visiwa vyapasa kutokea juu ya mahali hapo moto pia kwa kuwa panakabili sakafu ya bahari isiyovurugwa. Je, kuna uwezekano kwamba mwandamizi wa Kisiwa Kikubwa tayari amejidhihirisha?
Kwa kweli amejidhihirisha. Mlima wa chini ya maji unaotenda wa kivolkano, Loihi, unakua kusini mwa kisiwa cha Hawaii. Hata hivyo, usiutarajie ujitokeze kutoka baharini hivi karibuni. Ungali unahitaji kupaa meta 900 zaidi, ambazo zaweza kuchukua makumi ya maelfu ya miaka.
. . . Na Kuangamiza Visiwa vya Zamani
Ngao kubwa za kivolkano na mitiririko ya lava isiyo laini inayofanyiza Visiwa vya Hawaii huonekana kwa njia isiyo ya kweli kuwa salama kutokana na kuzamishwa tena ndani ya bahari. Lakini visiwa vidogo sana na milima ya baharini ya kaskazini-magharibi ya Hawaii haionyeshi hivyo. Kwa mfano, michanga na matumbawe ya visiwa visivyohusianishwa na Hawaii na visiwa vya Kure, vimejengwa juu ya milima mikubwa ya volkano ambayo vilele vyake sasa viko mamia ya meta chini ya usawa wa bahari. Kwa nini visiwa vya volkano hutoweka?
Visiwa hivi polepole humomonyolewa na maji ya mito, athari za mawimbi, na nguvu nyingine. Visiwa hivyo pia huzama kutokana na uzito wake vyenyewe vinaposukuma sakafu ya bahari. Majabali yenye miinamo yaliyo kando ya visiwa fulani huashiria utendaji mwingine ambao huozesha visiwa vya volkano—maporomoko ya ardhi. Vyombo vinavyotambua vitu vilivyozama baharini vinavyoonyesha vipande vya visiwa vilivyozama hufunua maporomoko makubwa ya ardhi ambayo huenea kwa makumi ya kilometa chini kwenye sakafu ya bahari.
-