-
Uumbaji Unathibitisha Hekima ya MunguMnara wa Mlinzi—2008 | Mei 1
-
-
Uumbaji Unathibitisha Hekima ya Mungu
“Ni Yeye anayetufundisha sisi kuliko wanyama wa dunia, naye anatufanya tuwe na hekima kuliko hata viumbe vinavyoruka vya mbinguni.”—AYUBU 35:11.
NDEGE ni viumbe wenye uwezo mbalimbali wenye kustaajabisha. Watu wanaotengeneza ndege (eropleni) wanavutiwa sana kuona jinsi ndege wanavyoruka angani bila tatizo lolote. Aina fulani ya ndege wanaweza kuruka maelfu ya kilomita juu ya bahari na kufika mahali wanapokwenda bila kukosea na pasipo mwongozo wowote.
Jambo lingine lenye kustaajabisha kuhusu ndege—ambalo linafunua mengi zaidi juu ya hekima ya Muumba wao—ni uwezo wao wa kuwasiliana kwa milio na nyimbo. Fikiria mifano fulani.
Jinsi Ndege Wanavyowasiliana
Ndege wa aina fulani wanaanza kuwasiliana hata kabla ya kutoka ndani ya yai. Kwa mfano, kware wa kike anataga mayai manane, yai moja kila siku. Ikiwa mayai yote yangekomaa kwa kadiri ileile, yangetokeza vifaranga kwa kipindi cha siku nane. Hivyo, kware wa kike angekuwa na kazi ngumu ya kutunza vifaranga wa juma moja, huku akiendelea kulalia yai ambalo halijakomaa. Hata hivyo, vifaranga vyote vinane vya kware vitatoka ndani ya yai katika muda wa saa sita. Hilo linawezekana jinsi gani? Sababu moja kuu ambayo watafiti wametoa ni kwamba kifaranga cha kware ambacho bado kingali ndani ya yai kinawasiliana na vifaranga vingine vilivyo ndani ya mayai na kwa njia moja au nyingine vinafanya mipango ili vitoke wakati mmoja.
Ndege wanapokomaa, kwa kawaida ni ndege wa kiume anayeimba. Anafanya hivyo hasa wakati wa kujamiiana ili kuweka mipaka ya eneo lake au kuvutia ndege wa kike. Ni kana kwamba kila moja ya maelfu ya jamii za ndege ina lugha yake na hilo linawasaidia ndege wa kike kutambua ndege wa kiume wa jamii yao.
Kuna sababu nzuri inayofanya ndege waimbe hasa asubuhi na mapema na jua linapotua. Nyakati hizo hakuna upepo wala kelele nyingi. Wachunguzi wamegundua kwamba asubuhi na jioni nyimbo za ndege zinasikika vizuri zaidi mara 20 kuliko zinavyosikika mchana.
Ingawa mara nyingi ndege wa kiume ndio wanaoimba, ndege wa kike na wa kiume wanatoa milio mbalimbali au sauti za chini ambazo zina maana tofauti. Kwa mfano, ndege wa aina ya Chaffinch wana milio tisa. Wanatoa mlio fulani ili kuonya kuhusu hatari iliyo angani—kama vile ndege anayetafuta mawindo—lakini wanatoa mlio tofauti ili kuonya kuhusu hatari iliyo ardhini.
Zawadi Kubwa Zaidi
Kwa kweli, hekima ya kisilika ya ndege inastaajabisha. Lakini wanadamu wana uwezo mbalimbali wa kuwasiliana ambao unastaajabisha hata zaidi. Andiko la Ayubu 35:11 linasema kwamba Mungu amewafanya wanadamu kuwa wenye “hekima kuliko hata viumbe vinavyoruka vya mbinguni.” Wanadamu wana uwezo wa pekee wa kueleza mambo magumu kupitia ishara au sauti zinazotokezwa na misuli ya koo.
Tofauti na viumbe wengine, inaelekea watoto wachanga wa kibinadamu wanazaliwa wakiwa na uwezo wa kujifunza lugha ngumu. Gazeti moja kwenye Intaneti (American Scientist) linasema hivi: “Watoto wanajifunza lugha ambayo hata wazazi wao hawazungumzi nao moja kwa moja; watoto ambao ni viziwi hata wanaanzisha lugha yao ya ishara ikiwa hawafundishwi lugha ya ishara nyumbani.”
-
-
Uumbaji Unathibitisha Hekima ya MunguMnara wa Mlinzi—2008 | Mei 1
-
-
Unahisi Jinsi Gani?
Unahisi jinsi gani unaposikia nyimbo tamu za ndege au mtoto anapojifunza kutamka maneno yake ya kwanza? Je, unaona hekima ya Mungu katika vitu ambavyo amefanya?
Baada ya kutafakari kuhusu jinsi alivyoumbwa, mtunga-zaburi Daudi alichochewa kumwambia Mungu: “Nitakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa njia ya ajabu yenye kuogopesha. Kazi zako ni za ajabu, kama vile nafsi yangu inavyojua vema.” (Zaburi 139:14) Unapochunguza kwa uthamini uthibitisho wa hekima ya Mungu katika uumbaji, bila shaka imani yako katika uwezo wake wa kukupa mwongozo mzuri itakua.
-