-
Tazameni Mtekelezaji wa Mambo ya Ajabu!Mnara wa Mlinzi—2001 | Aprili 15
-
-
9 Kama tusomavyo katika kitabu cha Ayubu sura ya 38, ni jambo lenye kutokeza kwamba Yehova Mungu mwenyewe ana maoni kama hayo kuhusu kutafakari anapomwuliza Ayubu maswali muhimu. Ingawa Muumba wetu alimwuliza Ayubu maswali hayo, ni wazi kwamba yanatuhusu—yanahusu mtazamo wetu, kuwapo kwetu, na wakati wetu ujao. Kwa hiyo, hebu tuchunguze maswali ambayo Mungu aliuliza na kufikiria maana yake, naam, na tufanye yale ambayo andiko la Ayubu 37:14 latuhimiza tufanye.
10. Ayubu sura ya 38 yapasa kuwa na matokeo gani kwetu, nayo yazusha maswali gani?
10 Sura ya 38 yaanza hivi: “BWANA akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani huyu atiaye mashauri giza kwa maneno yasiyo na maarifa? Basi jifunge viuno kama mwanamume, maana nitakuuliza neno, nawe niambie.” (Ayubu 38:1-3) Utangulizi huo ulimsaidia Ayubu arekebishe maoni yake na kutambua kwamba anasimama mbele za Muumba wa ulimwengu wote, na anawajibika mbele zake. Yafaa sisi na wengine wanaoishi wakati huu tufanye hivyo pia. Kisha, Mungu azungumzia mambo yaleyale ambayo Elihu alikuwa amezungumzia. “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! sema, kama ukiwa na ufahamu. Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake? Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni?”—Ayubu 38:4-6.
11. Twapaswa kung’amua nini kutokana na andiko la Ayubu 38:4-6?
11 Ayubu alikuwa wapi, sisi tulikuwa wapi dunia ilipoumbwa? Je, yeyote kati yetu alichora ramani za ujenzi za dunia yetu, na kutumia ramani hiyo kupima vipimo mbalimbali kana kwamba kwa rula? Bila shaka la. Wanadamu hata hawakuwepo wakati huo. Akiifananisha dunia yetu na jengo, Mungu aliuliza hivi: “Ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni?” Tunajua kwamba dunia imewekwa umbali hususa kutoka kwa jua, umbali unaotuwezesha kuishi na kufurahia maisha. Nayo dunia ina ukubwa ufaao. Kama dunia yetu ingalikuwa kubwa zaidi ya vile ilivyo sasa, gesi ya hidrojeni haingeweza kutoka katika angahewa letu nayo dunia haingekalika. Ni wazi kwamba mtu fulani ‘aliliweka jiwe lake la pembeni’ mahali pafaapo. Je, Ayubu alistahili sifa kwa jambo hilo? Je, sisi twastahili sifa? Au Yehova Mungu ndiye anayestahili sifa?—Mithali 3:19; Yeremia 10:12.
Ni Mwanadamu Gani Awezaye Kutoa Majibu?
12. Swali linalopatikana kwenye Ayubu 38:6 lafanya tufikirie nini?
12 Mungu aliuliza hivi pia: “Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani?” Je, hilo si swali zuri? Huenda twajua nguvu za uvutano, jambo ambalo Ayubu hakujua. Wengi wetu twafahamu kwamba nguvu za uvutano za jua huwezesha dunia idumu mahali ilipo, kana kwamba misingi yake imekazwa. Hata hivyo, je, kuna yeyote kati yetu awezaye kuzielewa kikamili nguvu za uvutano?
13, 14. (a) Ni lazima tukiri nini kuhusu nguvu za uvutano? (b) Tuoneje hali inayokaziwa na andiko la Ayubu 38:6?
13 Kitabu kilichochapishwa hivi majuzi, The Universe Explained, chakiri kwamba ‘watu wengi wanazijua nguvu za uvutano, lakini hawazielewi vizuri kama wanavyoelewa nguvu nyinginezo za asili.’ Kitabu hicho chaendelea kusema: “Yaonekana kwamba nguvu za uvutano husafiri kasi angani, bila kufuata njia yoyote mahususi. Hata hivyo, katika miaka ya majuzi, wanafizikia wameanza kukisia kwamba huenda ikawa nguvu za uvutano husafiri kwa mawimbi ya chembe ndogo ziitwazo graviton . . . Lakini hakuna yeyote aliye na uhakika kwamba chembe hizo zipo.” Hebu wazia hilo lamaanisha nini.
14 Sayansi imepiga hatua kubwa kwa miaka 3,000 tangu Yehova alipomwuliza Ayubu maswali hayo. Hata hivyo, wala sisi wala wataalamu wa fizikia hawawezi kueleza kikamili jinsi nguvu za uvutano zidumishavyo dunia katika mzunguko wake, mahali hasa ipaswapo kuwa ili kutuwezesha kufurahia maisha. (Ayubu 26:7; Isaya 45:18) Kusema hivyo hakudokezi kwamba sote tunahitaji kuanza uchunguzi wenye kina juu ya mambo tusiyoelewa kuhusu nguvu za uvutano. Hata hivyo, kuzingatia hata sehemu hii moja tu ya kazi za Mungu za ajabu kwapasa kuathiri maoni yetu kumhusu. Je, unastaajabia hekima yake na ujuzi wake, na je, unaelewa ni kwa nini twahitaji kujifunza mengi zaidi juu ya mapenzi yake?
15-17. (a) Andiko la Ayubu 38:8-11 lakazia nini na linazusha maswali gani? (b) Twapaswa kukiri nini juu ya yale tunayojua kuhusu bahari na mahali zilipo duniani?
15 Muumba aliendelea kuuliza hivi: “Ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni. Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, nikaiagiza amri yangu; nikaiwekea makomeo na milango, nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa?”—Ayubu 38:8-11.
16 Kufungwa kwa bahari kwahusisha mabara, bahari, na mawimbi. Mwanadamu amechunguza na kuchanganua vitu hivyo kwa muda mrefu kadiri gani? Amefanya hivyo kwa maelfu ya miaka na kwa makini zaidi hasa katika karne iliyopita. Unaweza kuwazia kwamba kufikia sasa lazima mwanadamu awe anajua mambo mengi ambayo anapaswa kujua kuhusu vitu hivyo. Lakini, katika mwaka huu wa 2001, ungepata habari gani za karibuni zaidi kama ungechunguza juu ya vitu hivyo kwenye maktaba kubwa au kwenye Internet yenye uwezo mkubwa wa kufanya utafiti?
17 Kichapo kimoja maarufu cha marejezo, chakiri hivi: ‘Ni vigumu sana kwa wanasayansi kuchunguza kikamili au kutoa nadharia inayoweza kueleza ni kwa nini mabara, bahari na uumbaji mwingine, upo mahali ulipo.’ Baada ya kusema hayo, ensaiklopidia hiyo ilitoa mambo manne ambayo yawezekana yalisababisha hali hiyo, lakini ikasema kwamba mambo hayo ni “baadhi ya zile nadharia tete nyingi.” Huenda ukafahamu kwamba usemi nadharia tete “wamaanisha uthibitisho usiotosha ambao watoa ufafanuzi uwezao kubadilika.”
18. Andiko la Ayubu 38:8-11 lafanya tufikie mkataa gani?
18 Je, mambo hayo hayakazii kwamba maswali tusomayo kwenye Ayubu 38:8-11 yaliulizwa wakati ufaao? Bila shaka, hatuwezi kupokea sifa kwa kuwa sio sisi tulioviweka vitu hivyo mahali vilipo duniani. Hatukuuweka mwezi mahali ulipo ili nguvu zake za uvutano zisaidie kutokeza mawimbi ambayo kwa kawaida hayaharibu mwambao wala kutuathiri sisi binafsi. Tunajua kwamba Mtekelezaji wa mambo ya ajabu ndiye aliyefanya hayo yote.—Zaburi 33:7; 89:9; Mithali 8:29; Matendo 4:24; Ufunuo 14:7.
Mpe Yehova Sifa Anayostahili
19. Semi za kishairi kwenye Ayubu 38:12-14 zafanya tuzingatie mambo gani halisi?
19 Mzunguko wa dunia unaorejezewa kwenye andiko la Ayubu 38:12-14 haukutokezwa na wanadamu. Mzunguko huo wa dunia husababisha mapambazuko ambayo mara nyingi huvutia kwa uzuri. Jua lichomozapo, vitu vilivyomo katika dunia yetu huonekana vizuri zaidi na zaidi kama vile alama kwenye udongo laini. Tunapozingatia kwa kiasi kidogo mwendo wa dunia twastaajabu kuona kwamba haizunguki kwa kasi sana, jambo ambalo kama tujuavyo lingeleta madhara. Wala dunia haizunguki polepole sana hivi kwamba mchana na usiku zawa ndefu sana. Jambo hilo laweza kusababisha joto na baridi zinazopita kiasi na kufanya wanadamu wasiweze kuishi. Kusema kweli, yatupasa kufurahi kwamba Mungu ndiye aliyeanzisha mwendo wa mzunguko huo, wala si wanadamu fulani.—Zaburi 148:1-5.
20. Ungejibuje maswali yaliyoulizwa kwenye Ayubu 38:16, 18?
20 Sasa, hebu wazia Mungu akikuuliza maswali zaidi: “Je! umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi?” Hata mtaalamu wa mambo ya bahari hangeweza kutoa jibu kamili! “Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! sema, ikiwa unayajua hayo yote.” (Ayubu 38:16, 18) Je, umezuru na kutembelea sehemu zote za dunia au angalau sehemu nyingi za dunia? Kutembelea sehemu nzuri mbalimbali na kuona maajabu ya dunia yetu kungechukua muda mrefu kadiri gani? Nao ungekuwa wakati mzuri kama nini!
21. (a) Maswali yaliyoulizwa kwenye Ayubu 38:19 yanaweza kutokeza maoni gani ya kisayansi? (b) Mambo halisi kuhusu nuru yapasa kutuchochea tufanye nini?
21 Pia, tazama maswali mazito katika Ayubu 38:19: “Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi?” Huenda ikawa wajua kwamba kwa muda mrefu, wanasayansi walidhani kwamba nuru husafiri kama wimbi, kama viwimbi tuonavyo kwenye kidimbwi. Kisha katika mwaka wa 1905, Albert Einstein akaeleza kwamba nuru ni kama chembechembe za nishati. Je, ufafanuzi wa Einstein ulitoa jibu? Ensaiklopidia ya karibuni iliuliza hivi: “Je, nuru ni wimbi au ni chembechembe?” Nayo yajibu hivi: “Yaonekana kwamba, [nuru] haiwezi kuwa [wimbi na wakati uleule ikawa chembechembe] kwa sababu vitu hivyo viwili vyatofautiana sana. Jibu lifaalo kabisa ni kwamba nuru si wimbi wala si chembechembe.” Hata hivyo, ingawa mwanadamu hawezi kufafanua kikamili kazi hizo za Mungu jua bado laendelea kupasha joto (kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia nyingineyo). Twapata chakula na oksijeni kwa sababu mimea hupata nuru. Twaweza kusoma, kuona nyuso za wapendwa wetu, kutazama machweo, na kadhalika. Tufanyapo hivyo, je, hatupaswi kushukuru kwa sababu ya kazi za Mungu za ajabu?—Zaburi 104:1, 2; 145:5; Isaya 45:7; Yeremia 31:35.
-
-
Zingatia Kazi za Mungu za AjabuMnara wa Mlinzi—2001 | Aprili 15
-
-
2 Watu wengi leo hupuuza au hukataa uthibitisho huo ulio wazi wa matendo ya Muumba. (Waroma 1:20) Hata hivyo, ingefaa tuyatafakari na kufanya maamuzi yanayopatana na msimamo wetu na wajibu wetu mbele za Muumba. Ayubu sura ya 38 hadi 41 yaweza kutusaidia sana katika jambo hilo, kwa kuwa kwenye sura hizo Yehova alimjulisha Ayubu baadhi ya kazi Zake za ajabu. Fikiria masuala fulani yafaayo ambayo Mungu alizusha.
Kazi za Ajabu na Zenye Nguvu
3. Mungu aliuliza juu ya mambo gani kwenye Ayubu 38:22-23, 25-29?
3 Wakati mmoja, Mungu alimwuliza Ayubu hivi: “Je! umeziingia ghala za theluji, au umeziona ghala za mvua ya mawe, nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, kwa siku ya mapigano na vita?” Theluji na mvua ya mawe hutokea katika sehemu nyingi za dunia yetu. Mungu aliendelea kumwuliza: “Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, au njia kwa umeme wa radi; kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu; kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, na kuyameza majani yaliyo mororo? Je! mvua ina baba au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Barafu ilitoka katika tumbo la nani na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?”—Ayubu 38:22, 23, 25-29.
4-6. Ni katika maana gani mwanadamu amekosa ujuzi kamili kuhusu theluji?
4 Huenda watu fulani wanaoishi katika jamii zenye hekaheka nyingi, ambao ni lazima wasafiri, wakaiona theluji kuwa kizuizi. Hata hivyo, watu wengine huvutiwa sana na theluji wakati wa majira ya baridi kali kwa kuwa hiyo huwapa fursa ya kufanya mambo ya pekee. Unapofikiria swali ambalo Mungu aliuliza, je, wewe unaijua theluji vizuri, na je, umewahi kuiona? Tunajua jinsi rundo kubwa la theluji lilivyo, aidha kwa kuwa tumeliona kwa macho yetu wenyewe au tumeona picha zake. Lakini namna gani chembe za theluji? Je, wajua chembe za theluji zinafananaje, labda kwa kuchunguza jinsi zinavyotokea?
5 Watu fulani wamechunguza na kupiga picha chembe za theluji kwa makumi ya miaka. Chembe moja ya theluji inaweza kuwa na chembe ndogondogo mia moja za barafu zenye maumbo mbalimbali yenye kupendeza. Kitabu kiitwacho Atmosphere chasema: ‘Namna nyingi za chembe za theluji zajulikana sana, na ingawa wanasayansi wanasisitiza kwamba hakuna sheria ya asili ambayo huzuia chembe hizo zisifanane, hawajawahi kupata chembe mbili zinazofanana. Wilson A. Bentley alifanya uchunguzi mkubwa uliochukua muda wa miaka 40 kwa kutumia darubini kupiga picha chembe za theluji, lakini hakupata chembe mbili zinazofanana.’ Na hata kama angalipata chembe mbili zinazofanana, jambo ambalo ni nadra, je, hilo lingebadili kwa njia yoyote maajabu tunayoona katika namna nyingi za chembe za barafu?
6 Kumbuka swali la Mungu: “Je! umeziingia ghala za theluji?” Wengi hufikiria mawingu kuwa ghala za theluji. Je, waweza kuwazia ukiingia katika ghala hizo kuhesabu chembe za theluji za namna nyingi sana na kuchunguza jinsi zilivyotokea? Ensaiklopidia moja ya sayansi yasema hivi: ‘Asili ya kiini cha barafu, ambacho husababisha matone ya maji kwenye mawingu yagande wakati wa baridi kali, haijulikani bado.’—Zaburi 147:16, 17; Isaya 55:9, 10.
7. Mwanadamu ana ujuzi mwingi kadiri gani kuhusu mvua?
7 Namna gani mvua? Mungu alimwuliza Ayubu hivi: “Je! mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?” Ensaiklopidia hiyohiyo yasema hivi: ‘Ni vigumu kwa wanasayansi kueleza jinsi ambavyo mawingu na matone ya mvua hutokea kwa sababu kuna utendaji mwingi tata katika angahewa na kiwango cha mvuke na chembe zilizo hewani hubadilika-badilika.’ Kwa maneno sahili, wanasayansi wametoa dhana zenye maelezo mengi, lakini hawawezi kueleza kikamili jinsi ambavyo mvua hutokea. Hata hivyo, unajua kwamba mvua ambayo ni muhimu hunyesha na kuitia dunia maji. Husitawisha mimea na hutuwezesha kuishi na kufurahia maisha.
8. Kwa nini maneno ya Paulo kwenye Matendo 14:17 yafaa?
8 Je, hukubaliani na kauli aliyokata mtume Paulo? Aliwahimiza wengine waone kazi za Mungu za ajabu kuwa zatoa ushuhuda juu ya Yule aliyezifanya. Paulo alisema hivi kumhusu Yehova Mungu: “Hakujiacha mwenyewe bila ushahidi kwa kuwa alitenda mema, akiwapa nyinyi mvua kutoka mbinguni na majira yenye kuzaa matunda, akijaza mioyo yenu kikamili kwa chakula na uchangamfu.”—Matendo 14:17; Zaburi 147:8.
9. Kazi za Mungu za ajabu hudhihirishaje nguvu zake kuu?
9 Bila shaka Mtekelezaji wa mambo hayo ya ajabu na yenye kunufaisha ana hekima na nguvu nyingi sana. Fikiria jambo hili kuhusu nguvu zake: Yasemekana kwamba kuna mvua za umeme na ngurumo zipatazo 45,000 zinazotokea kila siku, zaidi ya milioni 16 kwa mwaka. Hilo lamaanisha kwamba kuna mvua za aina hiyo zipatazo 2,000 zinazonyesha sasa hivi. Mawingu tata ya mvua moja ya umeme na ngurumo hutokeza nguvu zinazotoshana na nguvu za mabomu kumi au zaidi ya nyuklia yaliyoangushwa katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. Baadhi ya nguvu hizo huonekana zikiwa umeme. Licha ya kuwa yenye kuogofya, mimweko ya umeme husaidia hasa kutokeza nitrojeni za namna mbalimbali zinazoufikia udongo na kufyonzwa na mimea zikiwa mbolea ya asili. Kwa hiyo umeme ni nguvu ionekanayo, yenye manufaa halisi.—Zaburi 104:14, 15.
Unafikia Mkataa Gani?
10. Ungejibuje maswali yanayoulizwa kwenye Ayubu 38:33-38?
10 Hebu wazia kuwa wewe ni Ayubu na unaulizwa maswali na Mungu Mweza Yote. Yaelekea utakubali kwamba watu wengi hawazingatii sana kazi za Mungu za ajabu. Yehova anatuuliza maswali tusomayo kwenye Ayubu 38:33-38. “Je! unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize? Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, ukakuambia, Sisi tupo hapa? Je! ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni? Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni? Wakati mavumbi yagandamanapo, na madongoa kushikamana pamoja?”
11, 12. Ni baadhi ya mambo gani yanayothibitisha kwamba Mungu ni Mtekelezaji wa kazi za ajabu?
11 Tumezungumzia mambo machache tu ambayo Elihu alimwuliza Ayubu, kisha tumeona baadhi ya maswali ambayo Yehova alimwuliza Ayubu ajibu “kama mwanamume.” (Ayubu 38:3) Twasema “baadhi” kwa sababu katika Ayubu sura ya 38 na 39, Mungu alikazia fikira uumbaji mwingine mbalimbali wenye kutokeza. Kwa mfano, alitaja makundi ya nyota yaliyo katika mbingu. Ni nani ajuaye amri au sheria zake zote? (Ayubu 38:31-33) Yehova alimtajia Ayubu wanyama fulani—simba na kunguru, mbuzi-mwitu na punda-milia, nyati na mbuni, kisha farasi na tai. Ni kana kwamba Mungu alimwuliza Ayubu iwapo alikuwa amewapa wanyama hao mbalimbali tabia zao na kuwawezesha kuishi na kusitawi. Huenda ukafurahia kusoma sura hizo, hasa ikiwa wewe unapendezwa na farasi au wanyama wengineo.—Zaburi 50:10, 11.
-
-
Zingatia Kazi za Mungu za AjabuMnara wa Mlinzi—2001 | Aprili 15
-
-
Mungu alimwuliza Ayubu hivi: “Je! umeziingia ghala za theluji, au umeziona ghala za mvua ya mawe, nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, kwa siku ya mapigano na vita?” Theluji, mvua ya mawe, dhoruba za mvua, upepo, na umeme, zote hizo ni silaha za Mungu. Nazo ni kani za asili zilizo nyingi kama nini!—Ayubu 38:22, 23.
16, 17. Nguvu kuu za Mungu hudhihirishwa na nini, naye ametumiaje nguvu hizo wakati uliopita?
16 Huenda wakumbuka msiba fulani uliosababishwa na mojawapo ya mambo hayo—iwe kimbunga, dhoruba ya mvua ya mawe, au furiko la ghafula. Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka wa 1999, dhoruba kubwa ilikumba kusini-magharibi mwa Ulaya. Iliwashangaza hata wataalamu wa hali ya anga. Pepo zenye nguvu zilifikia mwendo wa kilometa 200 kwa saa, ziking’oa maelfu ya paa, zikiangusha nguzo za chuma za kuegemeza nyaya za nguvu za umeme, na kuangusha magari. Hebu wazia hili: Dhoruba hiyo iling’oa au kuvunja miti ipatayo milioni 270. Miti 10,000 kati ya hiyo ilikuwa katika bustani ya Versailles, nje ya Paris. Mamilioni ya nyumba yaliachwa bila umeme. Karibu watu 100 walikufa. Uharibifu wote huo ulichukua muda mfupi sana. Ni nguvu zilizoje!
17 Mtu anaweza kuita dhoruba tukio lisilo la kawaida, lisilo na mwelekezo na lisilodhibitiwa. Hata hivyo, hali ingekuwaje iwapo Yule mwenye nguvu zote, angefanya kazi za ajabu kwa kutumia kani hizo kwa njia inayodhibitiwa, chini ya mwelekezo wake? Alifanya jambo kama hilo zama za Abrahamu, ambaye alijifunza kwamba Hakimu wa dunia yote alikuwa amezingatia uovu wa majiji mawili, Sodoma na Gomora. Majiji hayo yalikuwa na ufisadi mwingi sana hivi kwamba malalamiko mengi dhidi yake yalimfikia Mungu, ambaye aliwasaidia waadilifu wote kukimbia majiji hayo yaliyohukumiwa adhabu. Historia yasema hivi: ‘Ndipo BWANA akanyesha kiberiti na moto toka mbinguni,’ juu ya miji hiyo ya kale. Ilikuwa kazi ya ajabu kuwahifadhi waadilifu na kuwaharibu watu hao waliokuwa waovu kupita kiasi.—Mwanzo 19:24.
-