Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Yusufu Anachukiwa na Ndugu Zake
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Ndugu za Yusufu wanamuuza kama mtumwa

      HADITHI YA 21

      Yusufu Anachukiwa na Ndugu Zake

      TAZAMA namna mvulana huyu hana furaha na tumaini. Ni Yusufu. Ndugu zake wamemwuza kwa wanaume hawa wanaokwenda Misri. Huko Yusufu atafanywa mtumwa. Sababu gani ndugu zake walifanya ubaya huo? Walikuwa na wivu.

      Yakobo baba yao alimpenda sana Yusufu. Alimpendelea kwa kumshonea vazi refu ambalo ni zuri sana. Ndugu zake wakubwa 10 walipoona namna Yakobo alivyompenda sana Yusufu, walianza kuwa na wivu na kumchukia Yusufu. Lakini kulikuwako sababu nyingine pia ya kumchukia.

      Yusufu aliota ndoto mbili. Katika ndoto zote mbili za Yusufu ndugu zake walimpigia magoti. Yusufu alipowasimulia ndugu zake ndoto hizo, chuki yao iliongezeka zaidi.

      Basi siku moja ndugu wakubwa wa Yusufu walipokuwa wakichunga kondoo za baba yao, Yakobo alimwomba Yusufu aende kuona kama walikuwa salama. Ndugu za Yusufu walipomwona akija, wengine kati yao walisema: ‘Tumwue!’ Lakini Reubeni ndugu mkubwa wao wote, alisema, ‘Tusifanye hivyo!’ Badala yake walimkamata Yusufu wakamtupa katika shimo kavu.

      Ndugu za Yusufu wanapokea pesa kutoka kwa Waishmaeli

      Karibu na wakati huo wanaume fulani Waishmaeli wakaja. Yuda akawaambia ndugu zake hivi: ‘Na tumwuze kwa Waishmaeli hawa.’ Ndivyo wanavyofanya. Wanamwuza Yusufu kwa vipande 20 vya fedha. Lo! walikuwa bila huruma kama nini!

      Ndugu zake watamwambia baba yao nini? Wanamwua mbuzi na kuchovya vazi zuri la Yusufu katika damu ya mbuzi huyo. Kisha wanampelekea Yakobo baba yao vazi hilo na kusema: ‘Tumeona hili. Ebu litazame, kama ni vazi la Yusufu.’

      Yakobo anaona hivyo. ‘Mnyama mkali amemwua Yusufu,’ analia. Hivyo ndivyo ndugu za Yusufu wanavyotaka baba yao afikiri. Yakobo anahuzunika sana sana. Anaomboleza siku nyingi. Lakini Yusufu hakufa. Tuone yanayompata kule alikopelekwa.

      Mwanzo 37:1-35.

  • Yusufu Anawekwa Katika Gereza
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Yusufu akiwa gerezani

      HADITHI YA 22

      Yusufu Anawekwa Katika Gereza

      YUSUFU ana miaka 17 tu anapopelekwa Misri. Anauzwa kwa Potifa. Potifa anafanya kazi ya mfalme wa Misri, anayeitwa Farao.

      Yusufu anafanya kazi ya bwana wake, Potifa, kwa bidii. Kwa nini Yusufu amewekwa humu ndani ya gereza? Ni kwa sababu ya mke wa Potifa.

      Yusufu anakuwa mwanamume mwenye sura nzuri sana, mke wa Potifa anataka alale naye. Lakini Yusufu anajua hilo ni kosa, hawezi kulifanya. Mke wa Potifa anakasirika sana. Basi mume anaporudi nyumbani, anamwambia uongo na kusema: ‘Yusufu huyo mbaya alitaka kulala nami!’ Potifa anamwamini mke wake, naye anamkasirikia sana Yusufu. Basi anamtupa gerezani.

      Upesi msimamizi wa gereza aona Yusufu ni mtu mzuri. Basi anamweka kuwa msimamizi wa wafungwa wengine wote. Baadaye Farao akamkasirikia mnyweshaji wake na mwokaji wake, na kuwatia gerezani. Usiku mmoja kila mmoja wao anaota ndoto ya pekee, lakini hawajui maana ya ndoto zao, kesho yake Yusufu anasema: ‘Niambieni ndoto zenu.’ Wanamwambia. Na kwa msaada wa Mungu, Yusufu anawaambia maana ya ndoto zao.

      Kwa mnyweshaji, Yusufu anasema: Kwa siku tatu utafunguliwa utoke gerezani , uwe mnyweshaji wa Farao tena.’ Lakini kwa mwokaji, Yusufu anasema: ‘Katika siku tatu Farao atakukata kichwa chako.’

      Katika muda wa siku tatu inakuwa kama Yusufu alivyosema. Farao anamkata kichwa mwokaji wake. Lakini mnyweshaji, anafunguliwa gerezani na kuanza kumtumikia mfalme tena. Lakini mnyweshaji huyo anamsahau Yusufu! Hamwambii Farao habari zake, naye Yusufu anaendelea kukaa gerezani.

      Mwanzo 39:1-23; 40:1-23.

  • Ndoto za Farao
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Farao akiota ndoto

      HADITHI YA 23

      Ndoto za Farao

      MIAKA miwili inapita, Yusufu angali gerezani. Mnyweshaji hamkumbuki. Ndipo usiku mmoja Farao anaota ndoto mbili za pekee sana, naye hajui maana yazo. Unamwona akilala pale? Kesho yake Farao anawaita wenye akili na kuwaambia mambo ambayo ameota. Lakini hawawezi kumwambia maana ya ndoto zake.

      Mwishowe yule mnyweshaji anakumbuka Yusufu. Anamwambia Farao hivi: ‘Nilipokuwa gerezani alikuwako mtu huko aliyeweza kuniambia maana ya ndoto.’ Farao anaagiza Yusufu atolewe gerezani mara moja.

      Farao anamsimulia Yusufu ndoto zake hivi: ‘Niliona ng’ombe saba wanono na wazuri. Kisha nikawaona ng’ombe saba waliokonda sana. Na wale waliokonda wakawala ng’ombe wanono.’

      Ng’ombe saba wanono, ng’ombe saba waliokonda

      ‘Katika ndoto yangu ya pili niliona masuke saba yenye kujaa nafaka zilizoiva, yakikua katika bua moja. Kisha nikaona masuke saba membamba, yaliyokauka sana ya nafaka. Na yale masuke membamba ya nafaka yalianza kumeza masuke mazuri saba ya nafaka.

      Yusufu anamwambia Farao hivi: ‘Maana ya ndoto zile mbili ni moja. Wale ng’ombe saba wanono na masuke saba ya nafaka yenye kujaa ni miaka saba, na wale ng’ombe saba waliokonda na masuke ya nafaka membamba saba ni miaka mingine saba. Kutakuwako miaka saba ya chakula kingi katika Misri. Kisha itakuwako miaka saba ya chakula kidogo sana.’

      Masuke saba membamba yaliyokauka sana ya nafaka, masuke saba yenye kujaa nafaka zilizoiva

      Basi Yusufu anamwambia Farao hivi: ‘Mchague mtu mwenye akili awe msimamizi wa kukusanya chakula wakati wa miaka mizuri saba. Hapo watu hawatakufa njaa wakati wa miaka mibaya saba inayofuata ya chakula kidogo.’

      Farao anapenda wazo hilo. Anamchagua Yusufu akusanye chakula, na kukiweka akiba. Yusufu anakuwa mkuu katika misri, wa pili kwa Farao.

      Miaka minane baadaye, wakati wa njaa kuu hiyo, Yusufu anaona watu fulani wakija. Unawajua? Ala, ni ndugu zake wakubwa 10! Yakobo baba yao amewatuma Misri kwa sababu chakula ni kidogo kule Kanaani. Yusufu anawajua ndugu zake, lakini wao hawamjui. Unajua sababu? Yusufu amekuwa mkuu, amevaa mavazi ya pekee.

      Yusufu anakumbuka kwamba alipokuwa mvulana aliota ndoto akiona ndugu zake wakija kumpigia magoti. Unakumbuka ulisoma habari hiyo? Hivyo Yusufu anafahamu kwamba ni Mungu aliyemtuma aende Misri, kwa sababu nzuri. Unadhani Yusufu anafanya nini? Na tuone.

      Mwanzo 41:1-57; 42:1-8; 50:20.

  • Yusufu Anajaribu Ndugu Zake
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Watumishi Wamisri wanakipata kikombe cha Yusufu katika mfuko mmoja wa ndugu zake

      HADITHI YA 24

      Yusufu Anajaribu Ndugu Zake

      YUSUFU anataka kujua kama ndugu zake 10 bado hawana huruma. Basi anasema hivi: ‘Ninyi ni wapelelezi. Mmekuja kuona udhaifu wa nchi yetu.’

      ‘Sivyo,’ wanasema. ‘Sisi ni watu wanyofu. Sote ni ndugu. Tuko 12. Lakini ndugu mmoja hayupo, na yule mdogo zaidi yuko nyumbani pamoja na baba yetu.’

      Yusufu anajifanya kuwa haamini. Anamweka ndugu anayeitwa Simeoni gerezani, na kuwaachilia wengine wakachukue chakula na kwenda kwao. Lakini anawaambia hivi: ‘Mtakaporudi, lazima mmlete ndugu yenu mdogo zaidi.’

      Wanaporudi kwao Kanaani, ndugu hao wanamwambia Yakobo baba yao yote yaliyowapata. Yakobo anahuzunika sana. ‘Yusufu hayupo,’ analia, ‘na sasa Simeoni hayupo. Sitawaruhusu mmchukue mwanangu mdogo zaidi Benyamini.’ Lakini chakula chao kinapoanza kuwa kidogo, Yakobo anawaruhusu wamchukue Benyamini kwenda Misri ili wakanunue chakula zaidi.

      Sasa Yusufu anawaona ndugu zake wakija. Anafurahi sana kumwona Benyamini mdogo wake. Lakini hakuna kati yao anayejua kwamba mkuu huyo ni Yusufu. Sasa Yusufu anawajaribu ndugu zake kumi.

      Anawaagiza watumishi wake wajaze mifuko yao yote chakula. Lakini bila kuwajulisha, anawaagiza pia watie kikombe chake cha pekee cha fedha katika mfuko wa Benyamini. Wote wakiisha kuondoka na kutmebea mwendo mfupi njiani, Yusufu anawatuma watumishi wake wawafuate. Wanapowakuta, watumishi hao wanasema hivi: ‘Kwa nini mmeiba kikombe cha fedha cha bwana yetu.’

      ‘Hatukuiba kikombe chake,’ ndugu wote wanajibu. ‘Ukiona kikombe hicho kwa yeyote kati yetu, mtu huyo na auawe.’

      Basi watumishi wanachunguza mifuko yote, wanakiona kikombe katika mfuko wa Benyamini, kama unavyoona hapa. Watumishi hao wanasema: ‘Ninyi wengine nendeni, lakini Benyamini atakwenda nasi.’ Sasa ndugu hao 10 watafanya nini?

      Wote wanarudi pamoja na Benyamini kwenye nyumba ya Yusufu. Yusufu anawaambia ndugu zake hivi: ‘Nyote nendeni kwenu, lakini Benyamini atakaa huku awe mtumwa wangu.’

      Yuda anapaza sauti, hivi: ‘Tukirudi kwetu bila kijana huyu, baba yangu atakufa kwa sababu ampenda sana. Tafadhali, unifanye mimi niwe mtumwa wako huku, lakini mruhusu kijana huyu aende nyumbani.’

      Yusufu anajua kwamba ndugu zake wamebadilika. Sasa wana huruma. Na tuchunguze tuone anayofanya Yusufu sasa.

      Mwanzo 42:9-38; 43:1-34; 44:1-34.

  • Jamaa Inahama Kwenda Misri
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Yakobo na Yusufu waungana tena kwa shangwe huko Misri

      HADITHI YA 25

      Jamaa Inahama Kwenda Misri

      YUSUFU hawezi kujizuia tena. Anawaambia watumishi wake wote waondoke chumbani. Anapokuwa peke yake pamoja na ndugu zake, Yusufu anaanza kulia. Twaweza kuwazia jinsi ndugu zake wanavyoshangaa, kwa sababu hawajui sababu analia. Mwishowe anawaambia hivi: ‘Mimi ni Yusufu. Je! baba yangu angali hai?

      Ndugu zake wanashangaa sana hata hawawezi kusema. Wanaogopa. Lakini Yusufu anawaambia hivi: ‘Tafadhali njoni karibu zaidi.’ Wanapokaribia zaidi, anawaambia hivi: ‘Mimi ni ndugu yenu Yusufu, ambaye mliuza Misri.’

      Yusufu anaendelea kusema kwa huruma hivi: ‘Msijilaumu kwa sababu mliniuza huku. Ni Mungu aliyenituma nije Misri niokoe maisha za watu. Farao amenifanya niwe mtawala wa nchi yote. Basi sasa fanyeni haraka mrudi kwa baba yangu mkamwambie hivyo. Mwambieni aje kukaa huku.’

      Kisha Yusufu anawakumbatia ndugu zake, na kuwabusu wote. Farao anaposikia kwamba ndugu za Yusufu wamekuja anamwambia Yusufu hivi: ‘Na wachukue magari waende kumchukua baba na jamaa zao warudi huku. Nitawapa nchi iliyo bora zaidi katika Misri yote.’

      Ndivyo walivyofanya. Hata unaweza kumwona Yusufu akimlaki baba yake anapofika Misri akiwa na jamaa yake yote.

      Ndugu za Yusufu na familia zao wanahamia Misri

      Jamaa ya Yakobo imekuwa kubwa sana. Walipohama kwenda Misri wote walikuwa 70, kutia Yakobo na watoto wake na wajukuu wake. Lakini walikuwako pia wake, na labda watumishi wengi. Wote hao wakahama kwenda Misri. Wakaitwa Waisraeli, kwa sababu Mungu alikuwa amebadili jina la Yakobo kuwa Israeli. Waisraeli wakawa watu wa pekee sana kwa Mungu kama tutakavyoona baadaye.

      Mwanzo 45:1-28; 46:1-27.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki