Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Yoshua
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Desemba 1
    • Neno la Yehova Liko Hai

      Mambo Makuu Katika Kitabu cha Yoshua

      WAKIWA wamepiga kambi kwenye Nchi Tambarare ya Moabu mwaka wa 1473 K.W.K., lazima Waisraeli wawe walisisimuka kusikia maneno haya: “Jitayarishieni chakula, kwa kuwa siku tatu kutoka sasa mtavuka huu mto Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Yehova Mungu wenu anawapa ninyi mpate kuimiliki.” (Yoshua 1:11) Ile miaka 40 ambayo wangekaa nyikani inakaribia kwisha.

      Zaidi ya miaka 20 hivi baadaye, kiongozi Yoshua asimama katikati ya nchi ya Kanaani na kuwatangazia hivi wanaume wazee wa Israeli: “Oneni, niliwagawia kwa kura mataifa haya yanayobaki yawe urithi kwa ajili ya makabila yenu, na mataifa yote ambayo nilikatilia mbali, kuanzia Yordani mpaka Bahari Kuu upande wa magharibi. Na Yehova Mungu wenu ndiye aliyeendelea kuwasukuma mbali kutoka mbele yenu, naye akawanyang’anya miliki yao kwa ajili yenu, nanyi mkaimiliki nchi yao, kama vile Yehova Mungu wenu alivyokuwa amewaahidi ninyi.”—Yoshua 23:4, 5.

      Kitabu cha Yoshua ambacho kiliandikwa na Yoshua mnamo mwaka wa 1450 K.W.K., kinasimulia mambo ya kihistoria yenye kusisimua yaliyotukia miaka hiyo 22. Tunapokaribia kuingia katika dunia mpya iliyoahidiwa, hali yetu inafanana na ile ya wana wa Israeli ambao walikuwa tayari kuimiliki Nchi ya Ahadi. Basi na tuchunguze kwa makini kitabu cha Yoshua.—Waebrania 4:12.

      HADI KWENYE “NCHI TAMBARARE ZA JANGWA LA YERIKO”

      (Yoshua 1:1–5:15)

      Kwa kweli, Yoshua anapokea mgawo muhimu Yehova anapomwambia hivi: “Musa mtumishi wangu amekufa; basi simama sasa, vuka huu mto Yordani, wewe na watu hawa wote, mwingie katika nchi ambayo ninawapa wao, wana wa Israeli.”! (Yoshua 1:2) Yoshua ana mgawo wa kuongoza taifa lenye watu milioni kadhaa kuingia Nchi ya Ahadi. Ili kujitayarisha, anawatuma wapelelezi wawili kwenda Yeriko—jiji litakalokuwa la kwanza kushindwa. Rahabu, yule kahaba ambaye amesikia juu ya kazi za Yehova zenye nguvu alizofanya kwa niaba ya watu wake, anaishi jijini humo. Anawalinda na kuwasaidia wapelelezi hao, nao wanamwahidi kwamba atahifadhiwa.

      Wapelelezi wanaporudi, Yoshua na Waisraeli wako tayari kuendelea na safari yao na kuvuka Yordani. Ingawa mto huo unafurika hadi kwenye kingo zake, hicho si kizuizi kwa kuwa Yehova anafanya mkondo wa maji ulio upande wa juu wa mto uinuke kama bwawa la maji na ule wa upande wa chini uelekee katika Bahari ya Chumvi. Baada ya kuvuka Yordani, Waisraeli wanapiga kambi huko Gilgali, karibu na Yeriko. Siku nne baadaye, jioni ya Nisani 14 siku ya Abibu, wanaadhimisha sikukuu ya Pasaka kwenye nchi tambarare za jangwa la Yeriko. (Yoshua 5:10) Siku inayofuata, wanaanza kula baadhi ya mazao ya nchi hiyo, nayo mana inakoma. Wakati huo, Yoshua anawatahiri wanaume wote waliozaliwa nyikani.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Yoshua
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Desemba 1
    • USHINDI WAENDELEA

      (Yoshua 6:1–12:24)

      Jiji la Yeriko ‘limefungwa imara, hakuna mtu anayetoka nje wala kuingia ndani.’ (Yoshua 6:1) Jiji hilo lingetekwaje? Yehova anamwonyesha Yoshua mbinu. Punde si punde, kuta zinaporomoka nalo jiji linaharibiwa. Rahabu tu pamoja na watu wa nyumbani mwake ndio wanaookoka.

      Ushindi unaofuata ni dhidi ya jiji la kifalme la Ai. Wapelelezi waliotumwa huko wanaripoti kwamba jiji hilo lina wakaaji wachache, kwa hiyo ni wanaume wachache tu wanaohitajiwa ili kulipiga. Hata hivyo, askari-jeshi wapatao 3,000 ambao walitumwa kushambulia jiji hilo wanawatoroka wanaume wa Ai. Kwa nini? Yehova hayuko pamoja na Waisraeli. Akani wa kabila la Yuda alifanya dhambi Yeriko lilipovamiwa. Baada ya kushughulikia jambo hilo, Yoshua anashambulia Ai tena. Mfalme wa Ai yuko tayari kupigana na Waisraeli kwa kuwa aliwahi kuwashinda pindi moja. Lakini kwa kuwa wanaume wa Ai wana uhakika kwamba watawashinda Waisraeli, Yoshua anatumia mbinu fulani na kuliteka jiji lao.

      Gibeoni ni ‘jiji kubwa—kubwa kuliko Ai, na wanaume wake wote ni wenye nguvu.’ (Yoshua 10:2) Hata hivyo, baada ya kusikia kuhusu ushindi wa Yoshua dhidi ya Yeriko na Ai, wanaume wa Gibeoni wanamdanganya Yoshua afanye agano la amani pamoja nao. Mataifa jirani yanaona uasi huo kuwa tisho kwao. Wafalme watano wa mataifa hayo wanaungana na kushambulia Gibeoni. Israeli lawaokoa Wagibeoni na kuwashinda kabisa washambuliaji hao. Ushindi mwingine ambao Israeli lilipata Yoshua alipokuwa kiongozi unatia ndani majiji yaliyo kusini na magharibi, na vilevile wafalme wa kaskazini walioungana. Wafalme wote walioshindwa ambao walikuwa upande wa magharibi ya Yordani ni 31.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Yoshua
    Mnara wa Mlinzi—2004 | Desemba 1
    • YOSHUA AFANYA KAZI YAKE KUBWA YA MWISHO

      (Yoshua 13:1–24:33)

      Sasa akikaribia umri wa miaka 90, Yoshua anaanza kugawanya nchi hiyo. Ni kazi kubwa kwelikweli! Makabila ya Rubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase tayari yamepokea urithi wao mashariki ya Yordani. Makabila yanayobaki yanapewa urithi upande wa magharibi kwa kupigwa kwa kura.

      Maskani inajengwa huko Shilo katika eneo la Efraimu. Kalebu anapokea jiji la Hebroni, naye Yoshua anapokea Timnath-sera. Walawi wanapewa majiji 48, kutia ndani majiji 6 ya makimbilio. Wakiwa njiani kurudi kwenye urithi wao mashariki ya Yordani, mashujaa wa vita wa Rubeni, Gadi, na nusu ya kabila la Manase wanajenga madhabahu “kubwa yenye kuonekana wazi.” (Yoshua 22:10) Makabila yaliyo magharibi ya Yordani yanaona jambo hilo kuwa tendo la uasi-imani na karibu vita vya kikabila vitokee, lakini umwagaji wa damu unazuiwa kwa sababu ya mawasiliano mazuri.

      Baada ya Yoshua kuishi Timnath-sera kwa muda fulani, anawaita wanaume wazee, vichwa, waamuzi, na maofisa wa Israeli na kuwahimiza wawe jasiri na kuendelea kuwa waaminifu kwa Yehova. Baadaye, Yoshua anakusanya makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akiwa huko, anazungumzia tena matendo ya Yehova tangu wakati wa Abrahamu na kuendelea, na kuwahimiza tena ‘wamwogope Yehova na kumtumikia kwa njia isiyo na kosa na katika kweli.’ Watu wanachochewa kujibu hivi: “Yehova, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia, na sauti yake ndiyo tutakayoisikiliza!” (Yoshua 24:14, 15, 24) Baada ya mambo hayo, Yoshua afa akiwa na umri wa miaka 110.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki