Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Tatizo Laenea
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Tatizo Laenea

      Robert mchanga alikuwa na umri wa miaka 11 tu, na bado alipatikana akiwa amelala kifudifudi chini ya daraja lililokuwa ukiwa. Kulikuwa na mashimo mawili ya risasi kisogoni mwake. Iliaminiwa, alikuwa ameuawa na washiriki wa genge lake la vijana.

      Alex mwenye umri wa miaka 15 alikuwa anaelekea kuwa mshiriki wa genge na labda alielekeana na kifo cha mapema. Lakini aliona rafiki yake akifa, na alifikiria: ‘Singependa kupatwa na jambo kama hilo.’

      MAGENGE ya mtaani yenye jeuri, ambayo wakati mmoja yalishirikishwa na magenge ya Los Angeles yenye kujulikana sana yaliyoitwa Bloods na Crips, yameenea ulimwenguni pote. Lakini popote yanapokuwa, kwa kustaajabisha magenge hufanana.

      Genge la Uingereza “Teddy Boys” lilishtua ulimwengu katika miaka ya 1950. Gazeti The Times la London lilisema kwamba lilitumia mashoka, visu, minyororo ya baiskeli, na silaha nyinginezo ili “kusababisha majeraha mabaya sana” kwa watu wasiokuwa na hatia. ‘Mapigano ya visu yalizuka, mikahawa iliharibiwa, na majengo ya kuuzia kahawa yalibomolewa.’ Watu walisumbuliwa, wakapokonywa, wakapigwa, na nyakati nyingine wakauawa.

      Gazeti la habari Die Welt la Hamburg, Ujerumani, liliripoti kwamba hivi karibuni vijana “wakiwa njiani kuelekea kwenye disko au wakiwa njiani kurudi nyumbani mwao” wameshambuliwa na magenge yenye kutumia “magongo ya besiboli, visu, na bunduki.” Gazeti la habari la Munich Süddeutsche Zeitung lilisema kwamba magenge yenye nywele fupi sana katika Berlin hushambulia mtu yeyote “ambaye huonekana kuwa dhaifu—wasiokuwa na makao, walemavu, wanawake waliostaafu.”

      Mleta-habari wa Amkeni! katika Hispania aliripoti kwamba tatizo la magenge ya matineja huko ni la karibuni lakini linakua. Gazeti la habari katika Madrid, ABC, lilikuwa na kichwa cha habari “Magenge Yenye Nywele Fupi Sana—Ogofyo Jipya la Mitaani.” Mshiriki mmoja wa genge lenye nywele fupi sana wa awali wa kutoka Hispania alisema kwamba wangegundua “kuku mgeni, makahaba, na wagoni-jinsia-moja.” Aliongezea: “Usiku usiokuwa na jeuri [haukufaa] kitu.”

      Katika Afrika Kusini Cape Times lilisema kwamba mwingi wa uhalifu huko ni “zaotuka la utamaduni wa genge wenye makosa.” Kitabu kilichochapishwa katika Cape Town husema kwamba magenge ya Afrika Kusini yalikuwa “vimelea” katika vitongoji vilivyo maskini zaidi na kwamba “yaliibia na kuwabaka washiriki wa jumuiya zao wenyewe na kujiingiza katika mapigano ya magenge juu ya maeneo, bidhaa zinazohitajiwa, na wanawake.”

      Gazeti la habari la Brazili O Estado de S. Paulo, lilisema kwamba huko magenge yalikuwa “yakiongezeka kwa kiwango chenye kuogopesha.” Lilitaarifu kwamba yangeshambulia magenge ya upinzani, vijana walio na hali bora, watu wa jamii nyingine, na wafanyakazi-wahamaji walio maskini. Pia lilisema kwamba siku moja magenge kadhaa yalifanyiza wavu, “yakawaibia watu waliokuwa katika ufuo . . . , yakapigana miongoni mwao wenyewe,” na kugeuza barabara moja ya Rio de Janeiro “kuwa ukanda wa vita.” Ripoti nyingine kutoka Brazili ilisema kwamba idadi ya magenge inaongezeka katika majiji makubwa kama vile São Paulo na Rio de Janeiro na katika miji midogo.

      Gazeti la Kanada Maclean’s lilisema kwamba katika mwaka wa 1995 kulingana na makadirio ya polisi, kulikuwa na angalau magenge ya mtaani manane yenye kutenda katika Winnipeg, Kanada. Na magazeti ya habari katika Marekani yamechapisha picha za washiriki wa magenge ambao wameingiza nguo za magenge na michoro ya ukutani hadi kwenye maeneo yaliyotengwa ya Wahindi wa Amerika ya Kusini-Magharibi.

      Katika New York City, ujeuri uliohusishwa na genge uliotokea mara nyingi na kwa muda mfupi uliibuka mwaka jana. Washiriki wa Bloods na Crips, magenge ambayo hapo awali yalikuwa mashuhuri katika Los Angeles, walisemekana kuwa walihusika. Kulingana na meya wa New York, kati ya Julai na Septemba, polisi waliwashika watu 702 katika visa vilivyohusiana moja kwa moja na magenge ya mtaani.

      Tatizo hili haliko tu katika majiji makubwa tena. Gazeti la habari Quad-City Times, linalochapishwa katika sehemu ya kati ya Marekani, lilisema juu ya “jeuri iliyoongezeka miongoni mwa matineja, matumizi yenye kuenea ya madawa ya kulevya na hisi inayokua ya kujiona kutofaa kitu.”

      Pigo la Kuhuzunisha Sana

      Genge moja lasemekana kuwa lilianza likiwa kikundi cha marafiki. Lakini sifa ya kiongozi wake ilipokua, ndivyo ilivyokuwa na jeuri. Kiongozi wa genge hilo aliishi katika nyumba ya nyanya yake, ambayo ilipigwa risasi mara kadhaa, hata wakati nyanya yake alipokuwa ndani. Gazeti moja la habari liliripoti kwamba kuliwako zaidi ya mashimo 50 ya risasi katika nyumba hiyo. Yaelekea risasi hizo zilirushwa kwa kulipiza kisasi kwa ajili ya matendo ambayo, genge la mjukuu huyo lilifanya. Kwa kuongezea, kaka ya kiongozi wa genge hilo alikuwa gerezani likiwa tokeo la utendaji uliohusiana na genge, na vilevile binamu yake, ambaye alikuwa amehama ili kuepa jeuri na aliyekuwa amerudi nyumbani kuzuru, alikuwa amepigwa risasi na mtu fulani aliyekuwa ndani ya gari la mizigo lililokuwa linapita.

      Katika Los Angeles, washiriki wa genge walipiga gari risasi na kumwua mtoto mchanga mwenye umri wa miaka mitatu asiyekuwa na hatia ambaye mama yake na rafiki wa kiume wa mama yake walikuwa wamepitia katika barabara fulani kwa makosa. Risasi ilivunja shule na kumpiga mwalimu aliyekuwa akijaribu kuwasaidia wanafunzi wajifunze namna ya kuboresha maisha zao. Wengine wengi wameuawa pia ambao hawakuhusika kabisa na magenge lakini ambao wamekuwa wahasiriwa wake. Mama mmoja wa Brooklyn, New York, alijulikana katika ujirani wake kwa sababu ya hali yake iliyohuzunisha sana na ya kipekee—kuwapoteza wana wake wachanga watatu kwa sababu ya jeuri ya genge.

      Ni nini kimesababisha tatizo hili la ulimwenguni pote la jeuri inayofanywa na vijana, na twaweza kuwalindaje watoto wetu wapendwa na jeuri? Kwanza magenge huanzaje, na kwa nini vijana wengi sana wanajiunga nayo? Maswali haya yanazungumziwa katika makala zinazofuata.

  • Mambo Tupaswayo Kujua Kuhusu Magenge
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Mambo Tupaswayo Kujua Kuhusu Magenge

      Wade, mshiriki wa hapo zamani wa genge la California, alisema: “Tulikuwa tu wajamaa walioishi katika ujirani mmoja. Tulianza shule ya msingi pamoja. Hatukufanya tu maamuzi yaliyofaa.”

      MARA nyingi magenge yalianza yakiwa vikundi vya kijirani. Watu waliokuwa katika umri wao wa utineja wa mapema au wachanga zaidi walikusanyika katika pembe moja ya mtaa. Walifanya mambo pamoja kisha wakaungana ili kujilinda na kikundi cha karibu kilichokuwa imara zaidi. Lakini upesi kikundi chao kikaanza kudidimia na kuwa chenye jeuri kama washiriki wake, na kikahusika katika utendaji wa jinai ulio hatari.

      Genge la upinzani kutoka mtaa mwingine huenda lilikiona kikundi hiki kipya kuwa adui wake. Kisha hasira ikaongoza kwenye jeuri. Walanguzi wa dawa za kulevya walitumia genge hilo kuuza dawa hizo haramu. Utendaji mwingine wa jinai ulifuata.

      Luis alikuwa na umri wa miaka 11 wakati marafiki wake wakubwa walipounda genge. Alipofikisha umri wa miaka 12 alianza kutumia dawa za kulevya. Alipofikisha umri wa miaka 13 alikamatwa kwa mara ya kwanza. Alishiriki katika wizi wa magari, uvunjaji wa nyumba, na unyang’anyi wa kutumia silaha. Na alifungwa jela mara kadhaa kwa sababu ya mapigano ya genge na ghasia.

      Nyakati fulani twaweza kushangazwa na washiriki wa magenge. Martha, mwenye sura ya kupendeza, mwanafunzi wa shule ya upili mwenye kufanya vizuri katika masomo, alipata maksi nzuri na alikuwa mwenye tabia nzuri shuleni. Hata hivyo, alikuwa kiongozi wa genge lililoshughulika na bangi, heroini, na kokeini. Haikuwa mpaka mmoja wa marafiki wake alipopigwa risasi mara kadhaa na kuuawa kwamba aliogopeshwa na kutaka kubadili maisha yake.

      Sababu kwa Nini Wao Hujiunga na Magenge

      Kwa kushangaza, washiriki fulani wa magenge husema walijiunga na magenge hayo ili kupata upendo. Walikuwa wakitafuta urafiki, undani ambao hawakuupata nyumbani. Gazeti la habari Die Zeit la Hamburg, Ujerumani, lilisema kwamba katika magenge ya mitaa vijana hujaribu kutafuta usalama ambao hawawezi kuupata mahali pengine. Eric, aliyekuwa mshiriki wa genge hapo zamani, alisema kwamba ikiwa hupati upendo nyumbani, “unaenda nje kwa watu wasio washiriki wa familia ukitafuta jambo fulani lililo bora zaidi.”

      Baba mmoja, aliyekuwa mshiriki wa genge wa hapo zamani, aliandika kuhusu mambo aliyopata katika maisha yake ya mapema: “Nilifungwa jela mara kadhaa kwa sababu ya mwenendo mbaya, mapigano ya genge, ghasia na hatimaye kwa kujaribu kuua kimakusudi kwa kumpiga risasi mtu fulani nikiwa naendesha gari.” Baadaye, alipopata mwana wake Ramiro, alikuwa na wakati mchache sana wa kutumia na mwana huyo. Ramiro alipokua, yeye pia alijiunga na genge, na alikamatwa na polisi baada ya pigano la genge. Wakati baba yake aliposisitiza atoke kwenye genge hilo, alipaaza sauti: “Sasa wao ni familia yangu.”

      Muuguzi mmoja katika hospitali ya Texas, ambaye alizungumza na wahasiriwa wachanga 114 waliokuwa wamepigwa risasi kwa kipindi kilichozidi kidogo mwaka mmoja, alisema: “Ni ajabu. Sifikiri nimewahi kusikia mmoja wao akiulizia mama yake au mshiriki yeyote wa familia.”

      Jambo la maana ni kwamba, si watoto watokao kwenye sehemu za mji zilizo maskini tu ambao hujiunga na magenge. Miaka kadhaa iliyopita gazeti la Kanada Maclean’s liliwanukuu polisi wakisema kwamba walikuwa wamewapata vijana kutoka sehemu zote mbili za jiji zilizo tajiri sana na za ujirani zilizo maskini sana wakiwa katika genge lilelile. Wachanga hawa kutoka malezi mbalimbali huungana pamoja kwa sababu inayofanana—wanatafuta hisi ya familia ya udugu ambayo hawaipati nyumbani.

      Katika maeneo fulani vijana hukua wakiona ushiriki wa genge kuwa njia ya kawaida ya maisha. Fernando mwenye umri wa miaka 16 alieleza: “Wanafikiri kujiunga na genge kutawasaidia watatue matatizo yao. Wao hufikiri: ‘Nitapata marafiki kadhaa. Wao ni wakubwa na hubeba bunduki. Watanilinda, na hakuna mtu atakayenidhuru.’” Lakini punde si punde washiriki wapya hugundua kwamba kuwa katika genge huwafanya wawe shabaha ya maadui wa genge.

      Mara nyingi magenge hupatikana katika ujirani ambao kuna pesa kidogo na bunduki nyingi sana. Ripoti za habari husema juu ya madarasa ya shule ya jiji kubwa ambayo wanafunzi 2 kati ya 3 huishi katika nyumba za mzazi asiye na mwenzi. Nyakati nyingine, mzazi wa mwanafunzi ni mraibu wa dawa za kulevya ambaye huenda asije nyumbani usiku, na nyakati nyingine mwanafunzi huyo mchanga akiwa mama asiye na mwenzi lazima ampeleke mtoto wake kwenye kituo cha kutunzia watoto kabla hajaenda shuleni asubuhi.

      Gavana wa California, Pete Wilson, alisema: “Tuna tatizo kubwa sana kwa sababu watoto wengi wanakua bila baba, bila kigezo cha kiume cha kuwapa upendo, mwongozo, nidhamu na maadili—bila hisi ya kwa nini wanapaswa kujistahi au kuwastahi wengine.” Alisema kwamba kutoweza huku kwa vijana hawa kushiriki hisia na wengine ni sababu inayofanya “waweze kulipua mtu fulani [kuwapiga risasi hadi wafe] bila kutikisika kwa majuto.”

      Ijapokuwa ukosefu wa udugu wa familia, mazoezi ya kibinafsi, na kielelezo thabiti cha adili ni mambo makuu yanayochangia ukuzi wa magenge, mambo mengine pia huhusika. Mambo haya hutia ndani vipindi vya televisheni na sinema ambazo huonyesha jeuri kuwa utatuzi rahisi wa matatizo, jamii ambayo huwaona maskini kuwa watu walioshindwa kufanikiwa maishani na kuwakumbusha sikuzote kwamba hawawezi kufanya mambo ambayo wengine hufanya, na idadi inayokua ya familia za mzazi asiye na mwenzi ambazo mama mchanga mwenye kufanyizwa kazi kupita kiasi lazima ajikaze kutegemeza mtoto mmoja au zaidi wasiosimamiwa. Muungano wa mengi ya mambo haya au wa yote, na labda mengine bado, umeongoza kwenye kukua kwa tatizo la magenge ya mitaani ulimwenguni pote.

      Ni Vigumu Kujiondoa

      Kweli, baada ya muda fulani washiriki fulani wa genge huondoka pole kwa pole kutoka kwenye genge lao, wakijishughulisha na utendaji mwingine. Wengine waweza kwenda kuishi na jamaa zao katika eneo jingine na hivyo kuponyoka maisha ya genge. Lakini mara nyingi, kujiondoa kutoka kwenye genge haliwi jambo rahisi.

      Kwa kawaida, washiriki wa genge lazima wapatwe na mapigo yenye jeuri kutoka kwa washiriki kadhaa kabla ya kuruhusiwa kuliacha genge wakiwa hai. Kwa kweli, watu waliotaka kuondoka kwenye magenge fulani kwa hakika walilazimika kuteseka kwa kupigwa risasi. Ikiwa waliokoka, waliruhusiwa kuondoka! Je, inastahiki kutendwa vikali namna hiyo ili kuondoka kwenye genge?

      Mshiriki mmoja wa genge wa hapo zamani alieleza kwa nini alitaka kutoka: “Marafiki wangu watano tayari wamekufa.” Kwa kweli, maisha ya kuwa mshiriki wa genge yaweza kukaribia kuwa yenye hatari isivyoaminika. Gazeti Time liliripoti kuhusu mshiriki mmoja wa genge la Chicago wa hapo zamani: “Katika kazi-maisha yake ya miaka saba, amepigwa risasi tumboni, akapigwa kichwani na chuma ya kuunganishia reli, akavunjwa mkono wake katika pigano na kufungwa jela mara mbili kwa wizi wa gari . . . Lakini sasa kwa kuwa hatimaye hahusiki na utendaji wa jinai hata marafiki wake wa zamani wananuia kumdhuru.”

      Maisha Yaliyo Bora Yawezekana

      Eleno, Mbrazili, wakati mmoja alikuwa mshiriki wa Headbangers, genge lililopigana kwa visu na nyakati nyingine bunduki. Akihisi kuwa amenyimwa haki za kimsingi za kijamii, alipata uradhi kwa kuvunja vitu na kuwashambulia watu. Mfanyakazi mwenzi alizungumza naye kuhusu Biblia. Baadaye Eleno alihudhuria kusanyiko la Mashahidi wa Yehova, ambapo alikutana na washiriki wa hapo zamani ambao walikuwa wametoka katika genge lake na vilevile mshiriki wa hapo zamani wa genge la upinzani. Walisalimiana kama ndugu—tofauti kabisa na vile ingaliweza kutokea hapo awali.

      Je, kwa kweli jambo hili hutukia? Kwa kweli hutukia! Hivi karibuni mwakilishi wa Amkeni! aliketi pamoja na washiriki wa hapo zamani wa magenge makubwa katika Los Angeles ambao sasa hutumika pamoja na makutaniko ya Mashahidi wa Yehova. Baada ya saa kadhaa za mazungumzo, mmoja wao alitua, akaegemea kiti chake, na kusema: “Ona jambo hili! Washiriki wa hapo zamani wa magenge ya Bloods na Crips wakiketi hapa wakipendana kama ndugu!” Walikubali kwamba badiliko lao kutoka kuwa washiriki wakatili wa genge hadi kuwa wanaume wenye fadhili na upendo lilikuwa tokeo la uhakika wa kwamba walikuwa wamejifunza kanuni za kimungu kupitia funzo lenye uangalifu la Biblia.

      Je, jambo hili lingeweza kutukia katika miaka ya 1990? Je, washiriki wa magenge kwa kweli waweza kufanya mabadiliko sasa? Wanaweza ikiwa wako tayari kutafuta kitia-moyo chenye nguvu kinachoandaliwa katika Neno la Mungu kisha kupatanisha maisha zao na kanuni za Biblia. Ikitukia kwamba wewe ni mshiriki wa genge, kwa nini usifikirie kufanya badiliko?

      Biblia hutuhimiza ‘tuweke mbali utu wa hapo zamani unaofuatana na njia yetu ya kwanza ya mwenendo’ na ‘tuvae utu mpya ulioumbwa kulingana na mapenzi ya Mungu katika uadilifu wa kweli na uaminifu-mshikamanifu.’ (Waefeso 4:22-24) Huo utu mpya husitawishwaje? “Kupitia ujuzi sahihi,” Biblia husema, utu wa mtu waweza ‘kufanywa kuwa mpya kulingana na mfano wa Mungu aliyeuumba.’—Wakolosai 3:9-11.

      Je, inastahili kujaribu kufanya badiliko kama hilo? Ndiyo, inastahili! Ikiwa wewe ni mshiriki wa genge, huenda utahitaji kufanya badiliko hilo. Kuna watu katika ujirani wako ambao wataterema kukusaidia. Lakini, mara nyingi wazazi huwa katika nafasi ya kudhihirisha uvutano unaofaa ulio mkubwa zaidi juu ya watoto wao. Kwa hiyo sasa tutafikiria yale wazazi wawezayo kufanya ili kuwalinda watoto wao na magenge.

  • Kuwalinda Watoto Wetu na Magenge
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Kuwalinda Watoto Wetu na Magenge

      “Watoto huhitaji watu wanaowajali.”—Not My Kid—Gang Prevention for Parents.

      BAADA ya uhusiano wetu pamoja na Mungu, watoto wetu ni miongoni mwa mali zetu zenye thamani ya juu zaidi. Twapaswa kuongea nao, kuwasikiliza, kuwakumbatia, na kuhakikisha kwamba wanajua kuwa wao ni wa maana sana kwetu. Lazima tuwafundishe mambo mazuri—kuwa wenye kufuatia haki na wenye nia ya kusaidia, jinsi ya kuwa na maisha mema, na jinsi ya kuwa wenye fadhili kuelekea wengine.

      Msimamizi wa kituo cha kizuizi cha watoto alitambulisha tatizo kubwa leo, akisema: “Maadili hayafunzwi katika familia.” Kwa hakika twahitaji kutoa uangalifu katika kufanya jambo hili. Lazima tuishi katika njia ambayo twawataka watoto wetu waishi na kuacha waone shangwe ambayo jambo hili huongezea maishani mwetu. Ikiwa hatuwafundishi thamani zinazofaa, twawezaje kuwatarajia wafuate kanuni kama hizo?

      Gazeti Today, linalochapishwa kwa ajili ya walimu wa shule wa Marekani, lilisema kwamba mara nyingi magenge huvutia vijana ambao “hujiona kuwa wasiofaulu maishani” na ambao “hutafuta usalama, uhusiano wa karibu, na kukubaliwa na jamii.” Ikiwa kwa kweli tunawapa watoto wetu mambo hayo nyumbani—usalama na hisi thabiti ya kufanikiwa katika familia na katika maisha yao wenyewe—wataelekea kuvutiwa kidogo sana na ahadi zisizo za kweli zinazotolewa na genge fulani.

      Kiongozi wa kikosi cha polisi cha kupambana na magenge cha California asema juu ya ishara ambazo yeye huona nyusoni mwa wazazi wakati polisi wanapobisha mlangoni pao kusema kwamba mtoto wao yuko taabani. Hawaamini kwamba yule waliyefikiri kuwa walimjua vema sana angeweza kufanya jambo lililo baya. Lakini mtoto wao alipata marafiki wapya na alikuwa amebadilika. Wazazi hawakutambua tu.

      Kutahadhari Ni Muhimu

      Watu wanaoishi katika maeneo ambapo magenge hutenda husema kwamba vijana na watu wazima wanapaswa kutumia uamuzi mzuri na si kutoa sai au tisho kwa genge. Jiepushe na vikundi vikubwa vya washiriki wa genge, na usiige namna wanavyoonekana au kutenda, kutia ndani mtindo na rangi ya mavazi wanayovalia. Kuwaiga kungeweza kukufanya uwe shabaha ya genge la upinzani.

      Pia, ikiwa mtu avalia au atenda kana kwamba anataka kuwa sehemu ya genge, washiriki wake wanaweza kumsonga awe mmoja wao. Umaana wa kujua mtazamo wa washiriki wa genge la mahali penu ulitolewa kielezi na baba mwenye watoto watatu katika Chicago. Alisema: ‘Ikiwa ninavalia kofia yangu ikiwa imetazama upande wa kulia, wao hufikiri ninawadharau.’ Na jambo hilo lingeweza kuongoza kwenye jeuri!

      Jihusishe na Watoto Wako

      Mama mmoja alisema: “Ni lazima tuwajue watoto wetu—kile wanachohisi na kile wanachofanya. Hatutaweza kuwasaidia watoto wetu ikiwa hatuonyeshi upendezi wa kibinafsi katika maisha zao.” Mwingine alisema kwamba tatizo la magenge halitaisha mpaka wazazi walimalize. Aliongezea: “Acheni tuwape upendo. Ikiwa wataharibika, tutakuwa tumepotea.”

      Je, twawajua marafiki wa watoto wetu, mahali watoto wetu huenda baada ya shule, na mahali wanapokuwa jioni baada ya giza? Bila shaka, si kila mama awezaye kuwa nyumbani wakati watoto wake wawasilipo nyumbani kutoka shule. Lakini akina mama wa wasio na wenzi ambao hung’ang’ana kwa ujasiri kulipia kodi na kuwalisha watoto wao huenda wakaweza kufanya mipango na mama wengine au mtu mwingine wanayemwitibari aandae usimamizi wakati wa mchana kwa watoto wao.

      Mwanamume mmoja anayeishi katika eneo kuu la magenge aliulizwa jinsi angewalinda watoto wake na magenge. Alisema angemchukua mwana wake kuzunguka ujirani ili kumwonyesha matokeo ya utendaji wa genge. Angeelekeza kwenye michoro iliyo ukutani na majengo yaliyobomoka ili kumwonyesha “kwamba eneo hilo si salama na kwamba washiriki wa genge wanarandaranda tu karibu na hapo, bila jambo la kufanya maishani.” Aliongezea: “Kisha ningemweleza kwamba kuishi kwa kupatana na kanuni za Biblia kungemzuia asipatwe na tokeo la namna hiyo.”

      Jambo la namna hiyo lililo sahili kama vile upendezi wa kweli kwa kazi ya shule ya watoto wetu laweza kuwa ulinzi. Ikiwa shule yao ina usiku uliotengwa kwa ajili ya wazazi au wakati mwingine ambao wazazi hualikwa wazuru madarasa na kuzungumza na walimu, hakikisha kuwa umeenda. Wajue walimu wa watoto wako, na acha wajue hangaiko lako kwa mtoto wako na upendezi wako katika kisomo chake. Ikiwa shule haina programu ya kutembelewa, jaribu kutafuta pindi za kuzungumza na walimu juu ya maendeleo ya mtoto wako katika shule na jinsi uwezavyo kusaidia.

      Ukaguzi katika jiji moja kubwa la Marekani ulipata kwamba miongoni mwa wanafunzi ambao familia zao ziliwasaidia au kuwatia moyo katika mgawo wao wa masomo ya nyumbani, asilimia 9 walijiunga na genge. Lakini katika familia ambazo uangalifu wa namna hiyo haukutolewa, idadi maradufu ya wanafunzi—asilimia 18—walijiunga na genge. Ikiwa familia yetu ni yenye upendo na iliyoshikamana kwa ukaribu na ikiwa twafanya mambo yajengayo, hili litapunguza uwezekano wa kwamba watoto wetu watavutiwa na ahadi zisizo za kweli za magenge.

      Kile Ambacho kwa Kweli Watoto Wetu Wanahitaji

      Watoto wetu wanahitaji mambo yaleyale tuhitajiyo—upendo, fadhili, na shauku. Watoto wengi hawajawahi kamwe kuguswa kwa njia yenye shauku, yenye upendo au kuambiwa kwamba kwa kweli yeye ni wa maana. Jambo hili lisitukie kwa watoto wetu kamwe! Na tuwakumbatie, tuwaambie kwamba twawapenda, na tujaribu kuona kwamba wanaishi maisha ya adili ambayo tumewafunza kuishi. Wao ni wenye thamani sana kwetu kuwatendea kwa njia yoyote nyingine.

      Gerald, mshiriki wa genge wa hapo zamani, alieleza: “Sikuwa na baba wa kumtegemea, kwa hiyo nilienda kwenye magenge ili kujazia pengo hilo katika maisha yangu.” Alianza kutumia dawa za kulevya alipofikisha umri wa miaka 12. Lakini alipofikisha umri wa miaka 17, mama yake alianza funzo la Biblia nyumbani la kawaida pamoja na Mashahidi wa Yehova. Alitumia kanuni bora za Biblia maishani mwake. Anasema: “Niliona badiliko kwa upande wake, na nikafikiri, ‘Lazima kuwe na jambo fulani lililo la kweli na linalofaa.’” Kielelezo kizuri cha mama yake kilimchochea abadili maisha yake.

      Watoto wetu wapaswa kuona kielelezo chetu kizuri—kwamba tunaishi kulingana na yale tunayowafunza. Wanapaswa kuwa na hisi nzuri kuelekea familia yao, si kwa kile ilicho nacho, bali kwa kile ifanyacho. Na watoto wanapaswa wasaidiwe kwa njia ambayo wataonea fahari tabia yao ya kiadili. Mwanasheria wa hapo zamani wa Mkoa wa Los Angeles, Ira Reiner, alieleza hivi: “Lazima tuwaonyeshe watoto hangaiko lenye upendo kabla hawajaishia kwenye magenge.”

      Kuwaandalia Wanachohitaji

      Si vitu vya kimwili ambavyo sisi huwaandalia watoto wetu vilivyo na umaana wa kwanza. Jambo lililo la maana ni kuwasaidia wakue wawe watu wazima wenye upendo na wenye kujali ambao wana viwango bora vya kiadili. Biblia husema kwamba Yakobo mwenye haki aliwaita wachanga wake ‘watoto Mungu alionipa kwa neema yake.’ (Mwanzo 33:5) Ikiwa tutawaona watoto wetu kwa njia hiyo—wakiwa zawadi ambazo Mungu ametupa sisi—tutakuwa tayari zaidi kuwatendea kwa upendo na kuwafundisha kuishi maisha ya kufuatia haki, manyoofu, na maisha yenye adili.

      Hivyo tutafanya yote tuwezayo kuishi maisha kwa namna ya kwamba twaweka kielelezo kinachofaa kwa ajili ya watoto wetu. Tutawapatia fahari inayofaa na ijengayo kuelekea familia yao, si kwenye mali za kimwili za familia, bali kutuelekea kwa ajili ya utu wetu. Hivyo, hawataelekea kutafuta msaada kutoka kwa wale walioko mitaani.

      Akitazama nyuma kwenye ujana wake, babu mmoja alisema: “Singefanya kamwe jambo la kuaibisha familia yangu.” Alikiri kwamba alihisi hivyo kwa sababu alitambua upendo ambao wazazi wake walikuwa nao kumwelekea. Kweli, kuonyesha upendo kwa watoto wao huenda kusiwe jambo rahisi kwa akina mama na baba fulani ambao hawakupokea kamwe upendo kutoka kwa wazazi wao. Hata hivyo, wazazi wanahitaji kufanya jitihada ya kuwapenda watoto wao.

      Kwa nini jambo hili ni la maana sana? Kwa sababu kama vile gazeti “What’s Up,” linalochapishwa na Shirika la Upelelezi la Genge la Utah, lilivyosema, “wakati vijana wahisipo kuwa wanapendwa na wako salama—si kuwa salama kiuchumi, bali salama kihisia-moyo—mahitaji ambayo huwasukuma kujiunga na magenge hutoweka.”

      Huenda wasomaji fulani wakafikiri kwamba familia zenye kuonyesha upendo kama hizo hazipatikani tena kamwe. Lakini zinapatikana. Unaweza kuzipata nyingi kati ya hizo miongoni mwa makutaniko ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote. Kweli, familia hizi si kamilifu, lakini zinapata faida kubwa: Zinajifunza kile ambacho Biblia husema kuhusu kulea watoto na hujitahidi kutumia kanuni za Biblia za kimungu katika maisha zao. Zaidi ya hayo, hufundisha watoto wao kanuni hizi.

      Mashahidi wa Yehova hukubaliana na taarifa iliyoandikwa katika The Journal of the American Medical Association: “Mtu hawezi kutumaini kuwa na . . . matineja ‘Wanaosema tu la’ bila kuwapatia jambo fulani la ‘Kusema ndiyo.’” Yaani, ikiwa twataka watoto wetu waseme ndiyo kwa mambo mazuri na yajengayo, lazima tuwaelekeze katika upande huo.

      Hakuna hata mmoja wetu ambaye angependa kamwe kusema, kama alivyosema baba mmoja: ‘Katika genge lake mwana wangu alipata ushirika na staha ambayo hakuwahi kuhisi hapo awali.’ Wala hatungependa kusikia watoto wetu wakisema, kama mwanamume mmoja mchanga alivyosema: “Nilijiunga na genge kwa sababu nilihitaji familia.”

      Sisi, wazazi, lazima tuwe familia hiyo. Na lazima tufanye yote tuwezayo ili kuona kwamba wachanga wetu wenye thamani wanabaki wakiwa sehemu yenye joto na upendo ya familia hiyo.

  • Kuwalinda Watoto Wetu na Magenge
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Orodha ya Kupimia kwa Wazazi Wanaohangaika

      ✔ Tumia wakati nyumbani pamoja na watoto wako, na fanyeni mambo pamoja mkiwa familia

      ✔ Jua marafiki wa watoto wako na familia zao, na fuatia kujua waendako watoto wako na huenda pamoja na nani

      ✔ Acha watoto wako wajue kwamba wanaweza kukufikia wakati wowote wakiwa na tatizo lolote

      ✔ Wafundishe watoto kuwaheshimu watu wengine, haki zao, na maoni yao

      ✔ Wategemeze watoto wako kwa kufahamiana na walimu wao, na wajulishe walimu kwamba unawathamini na unaunga mkono jitihada zao

      ✔ Usitatue matatizo kwa kupiga kelele au kwa kutumia jeuri

      Watoto wako wanahitaji shauku yako yenye joto

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki