-
Kutafuta Viongozi WazuriMnara wa Mlinzi—2004 | Novemba 1
-
-
Hivyo, kwa miaka mingi, kumekuwa na maasi, mapinduzi, uteuzi, uchaguzi, mauaji ya kisiasa, wengi wametawazwa, na pia mabadiliko ya serikali. Wafalme, mawaziri wakuu, wakuu, marais, makatibu wakuu, na madikteta wamechaguliwa na kuondolewa. Hata viongozi wenye nguvu wameondolewa mamlakani baada ya mabadiliko yasiyotarajiwa kutokea. (Ona sanduku “Kuondolewa Mamlakani kwa Ghafula,” kwenye ukurasa wa 5.) Hata hivyo, imekuwa vigumu kupata viongozi hodari na wenye kudumu.
‘Hatuna la Kufanya’ —Lazima Tuvumilie Tu
Kwa hiyo, haishangazi kwamba wengi wamepoteza kabisa tumaini la kupata viongozi wazuri. Katika nchi fulani, hisia za watu za kuwa wenye ubaridi na kukata tamaa huonekana hasa wakati wa uchaguzi. Geoff Hill, mwandishi-habari barani Afrika alisema hivi: “Kunakuwa na hali ya ubaridi au ya kususia [kupiga kura] watu wanapohisi kuwa hawana nguvu za kubadili hali yao mbaya maishani . . . Barani Afrika, watu wanapokosa kupiga kura, haimaanishi kwamba wameridhika. Mara nyingi, hicho ni kilio cha watu wanaohisi kwamba hakuna anayejali shida zao.” Vivyo hivyo, mwandishi mmoja wa gazeti huko Marekani aliandika hivi kuhusu uchaguzi uliokuwa ukikaribia: “Laiti tungekuwa na mgombezi bora kabisa wa kiti hiki.” Aliongeza kusema: “Hakuna mgombezi kama huyo. Hayuko kabisa. Lazima tuvumilie tu.”
-
-
Ni Kiongozi Gani Anayefaa Leo?Mnara wa Mlinzi—2004 | Novemba 1
-
-
Ni Kiongozi Gani Anayefaa Leo?
Mnamo mwaka wa 1940, kulikuwa na tatizo la uongozi katika Bunge la Uingereza. David Lloyd George, mwenye umri wa miaka sabini na saba, ambaye alisikiliza mjadala huo, alikuwa ameongoza Uingereza kushinda Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, na kwa sababu ya kuwa katika siasa kwa miaka mingi aliweza kuchanganua kwa makini kazi ya maofisa wa ngazi za juu. Katika hotuba aliyotoa kwa Bunge la Wawakilishi la Uingereza Mei 8, alisema: “Raia wako tayari kufanya yote wawezayo maadamu tu wana viongozi, mradi tu Serikali inaeleza malengo yake waziwazi na raia wana uhakika kwamba viongozi wao wanafanya yote wawezayo.”
MANENO ya Lloyd George yanaonyesha wazi kwamba watu wanatazamia viongozi wao wawe hodari na wajitahidi kikweli kuboresha mambo. Mwanamke anayeshiriki katika kampeni za uchaguzi alisema hivi: “Watu wanapopiga kura ili kuchagua rais, wao hupiga kura kuchagua mtu ambaye wataweka maisha yao, wakati wao ujao, na watoto wao mikononi mwake.” Ni kazi kubwa sana kudumisha tumaini hilo. Kwa nini?
Ulimwengu wetu una matatizo mengi sana ambayo huonekana kuwa magumu kutatua. Kwa mfano, ni kiongozi gani ambaye amethibitika kuwa mwenye hekima sana na nguvu hivi kwamba anaweza kukomesha uhalifu na vita? Kati ya viongozi wa leo, ni nani mwenye uwezo na huruma ya kumpa kila mwanadamu chakula, maji safi, na matibabu? Ni nani aliye na ujuzi na azimio la kulinda na kurudisha mazingira katika hali nzuri? Ni nani aliye hodari na mwenye nguvu vya kutosha kuhakikisha kwamba wanadamu wote wanaishi maisha marefu na yenye furaha?
Wanadamu Hawawezi Kufanya Kazi Hiyo
Ni kweli kwamba viongozi fulani wamefanikiwa kwa kadiri fulani. Hata hivyo, wanaweza kutumikia kwa miaka michache tu—kisha ni nani anayefuata? Mmojawapo wa viongozi hodari zaidi aliyepata kuishi, Mfalme Sulemani wa Israeli la kale, alitafakari juu ya swali hilo. Alifikia mkataa huu: “Nami, naam mimi, nikachukia kazi yangu yote iliyo ngumu ambayo niliifanya kwa bidii chini ya jua, ambayo ningemwachia mtu ambaye angekuja baada yangu. Na ni nani anayejua kama atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo, atachukua usimamizi wa kazi yangu yote iliyo ngumu niliyoifanya kwa bidii ambayo ndani yake nilitumia hekima chini ya jua. Hilo pia ni ubatili.”—Mhubiri 2:18, 19.
Sulemani hakujua iwapo mwandamizi wake angeendeleza kazi yake nzuri au angeiharibu. Sulemani aliona ule utaratibu wa viongozi wapya kuchukua mahali pa viongozi wa zamani kuwa “ubatili.”
Nyakati nyingine, jeuri hutumiwa ili kubadili viongozi. Viongozi wenye uwezo wameuawa wakiwa katika mamlaka. Pindi moja, Abraham Lincoln, rais wa Marekani aliyeheshimiwa sana aliwaambia wasikilizaji wake hivi: “Nimeteuliwa kuchukua wadhifa muhimu kwa muda mfupi tu, na sasa, mbele yenu, nimepewa mamlaka ambayo itakwisha hivi karibuni.” Kwa kweli, alitumika kwa muda mfupi. Licha ya mambo yote aliyofanya na tamaa yake ya kuwafanyia watu mengi zaidi, Rais Lincoln aliongoza nchi yake kwa miaka minne tu. Mwanzoni mwa muhula wake wa pili, aliuawa na mtu fulani aliyetaka badiliko la uongozi.
Hata viongozi bora zaidi wa kibinadamu hawawezi kuwa na uhakika kuhusu wakati wao ujao. Basi je, unapaswa kuwatumaini wakuhakikishie jinsi wakati wako ujao utakavyokuwa? Biblia inasema: “Msiweke tegemeo lenu katika watu wenye vyeo, wala katika mtu wa udongo, ambaye hana wokovu wowote. Roho yake hutoka, naye hurudi kwenye udongo wake; siku hiyo mawazo yake hupotea.”—Zaburi 146:3, 4.
-
-
Ni Kiongozi Gani Anayefaa Leo?Mnara wa Mlinzi—2004 | Novemba 1
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
KUONDOLEWA MAMLAKANI KWA GHAFULA
Kwa kawaida, mtawala hutarajia raia zake wamheshimu na kumuunga mkono ikiwa atawaletea amani ya kiasi fulani na hali nzuri ya maisha. Hata hivyo, watu wakikosa imani naye kwa sababu yoyote ile, huenda baada ya muda mfupi mtu mwingine akachukua nafasi yake. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya hali fulani zilizofanya watawala wenye nguvu waondolewe mamlakani kwa ghafula.
Hali za maisha zisizoridhisha. Kufikia karne ya 18, raia wengi Wafaransa walilazimika kulipa kodi za juu na kupata chakula kidogo. Hali hizo zilisababisha Mapinduzi ya Ufaransa, ambayo mwaka wa 1793, yalifanya Mfalme Louis wa Kumi na Sita anyongwe.
Vita. Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, vilikomesha baadhi ya maliki wenye nguvu zaidi katika historia. Kwa mfano, mnamo 1917, ukosefu wa chakula uliosababishwa na vita huko St. Petersburg, Urusi, ulibadilika na kuwa Mapinduzi ya Urusi. Mapinduzi hayo yalimwondoa mamlakani Mtawala Nicholas wa Pili na kutokeza utawala wa Kikomunisti. Mnamo Novemba 1918, Wajerumani walitaka amani, lakini washirika wao hawakutaka kuacha vita mpaka badiliko la utawala lifanywe. Kwa sababu hiyo, Maliki wa Ujerumani Wilhelm wa Pili, alilazimika kukimbilia uhamishoni huko Uholanzi.
Kutamani serikali za aina tofauti. Mwaka wa 1989, Pazia la Chuma liliondolewa. Serikali zilizoonekana kuwa ngumu kama mawe ziliporomoka, nao raia zake wakakataa Ukomunisti na kuanzisha tawala za aina mbalimbali.
-