Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo
    Amkeni!—2003 | Februari 22
    • Kwa nini utapiamlo unawashambulia hasa watoto? Watoto wanakua haraka na hivyo wanahitaji nishati na protini nyingi zaidi. Vivyo hivyo, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaweza kupata utapiamlo.

      Mara nyingi, mtoto mchanga huanza kuathiriwa akiwa tumboni. Ikiwa mama hapati chakula cha kutosha au hali chakula bora kabla na wakati wa mimba, basi atajifungua mtoto mwenye uzito kidogo. Mtoto huyo akiachishwa kunyonya mapema, asipolishwa vizuri, au usafi usipozingatiwa, anaweza kuugua utapiamlo.

      Mtoto hawezi kukua au kusitawi vizuri asipopata vitamini na madini muhimu. Yeye hulia bila sababu yoyote na kuwa mgonjwa-mgonjwa. Kadiri hali yake inavyozorota ndivyo anavyozidi kukonda, macho na utosi wa kichwa hubonyea, ngozi na tishu za mwili hukauka, na uwezo wa kudhibiti joto la mwili hupungua.

      Utapiamlo humwathiri mtoto kwa njia nyingine ambazo pia zinaweza kuathiri ukuzi wake. Kwa mfano, kutopata madini ya kutosha—hasa chuma, iodini, na zinki—na vitamini—hasa vitamini A—kunaweza kusababisha madhara hayo. Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema kwamba ukosefu wa vitamini A huathiri watoto wachanga milioni 100 hivi ulimwenguni na husababisha upofu. Vilevile unadhoofisha mfumo wa kinga, na hivyo kupunguza uwezo wa mtoto wa kukinza maambukizo.

      Madhara Mabaya Zaidi

      Utapiamlo hudhuru kabisa mwili, hasa mwili wa mtoto. Unaweza kudhuru viungo na mifumo yote mwilini kutia ndani moyo, mafigo, tumbo, matumbo, mapafu, na ubongo.

      Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba ukuzi wa polepole wa mtoto hudhoofisha maendeleo yake ya kiakili na uwezo wa kufikiri na kufanya vyema shuleni. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inasema hizo ndizo athari mbaya zaidi na za kudumu za utapiamlo.

      Mtoto anaweza kuendelea kuathiriwa na matokeo ya utapiamlo hata anapokuwa mtu mzima. Ndiyo sababu shirika la UNICEF lililalamika hivi: “Kudhoofisha uwezo wa akili wa binadamu kwa kadiri kubwa hivyo—kwa sababu ambazo zinaweza kuzuiwa—ni kosa kubwa sana la kimaadili na hasara kubwa.” Kwa hiyo matokeo ya kudumu ya utapiamlo ni mabaya sana. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba kutokula chakula cha kutosha wakati wa utotoni kunaweza kusababisha magonjwa hatari kama vile ugonjwa wa moyo, kisukari, na shinikizo la juu la damu mtu anapokuwa mtu mzima.

      Hata hivyo, watu wengi hawaugui utapiamlo hatari, kama shirika la UNICEF linavyokiri: “Zaidi ya robo tatu ya watu wanaokufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukosefu wa chakula, hufa kwa sababu ya utapiamlo mdogo au wa wastani.” (Italiki ni zetu.) Watoto wanaopatwa na utapiamlo mdogo au wa wastani wanaweza kupata matatizo ya kudumu ya afya. Kwa hiyo ni muhimu kugundua watoto wenye dalili za utapiamlo ili waweze kupata matibabu yanayofaa.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 7.

  • Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo
    Amkeni!—2003 | Februari 22
    • [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      JE, MTOTO WAKO ANA UTAPIAMLO?

      Wataalamu wa afya wanawezaje kujua kama mtoto ana utapiamlo? Huenda wakachunguza dalili fulani-fulani, wakauliza maswali kuhusu mazoea yake ya kula, na kuomba apimwe kwenye maabara. Hata hivyo, mara nyingi wao humpima mtoto moja kwa moja. Wao hupima mwili wa mtoto na kulinganisha vipimo hivyo na vipimo vya kawaida. Na hivyo wanajua mtoto anakosa chakula gani na athari za ugonjwa huo.

      Vitu muhimu sana wanavyopima ni uzito, kimo, na unene wa mkono. Wanaweza kujua athari za utapiamlo kwa kulinganisha uzito wa mwili na umri wake; mtoto aliyeathiriwa sana huwa amedhoofika na kukonda. Mtoto huonwa kuwa ameathiriwa sana na utapiamlo iwapo uzito wake umepungua kwa asilimia 40, na ameathiriwa kwa kadiri ikiwa uzito wake umepungua kwa asilimia 25 hadi 40, na ameathiriwa kidogo iwapo uzito wake umepungua kwa asilimia 10 hadi 25. Ikiwa mtoto ana uzito mdogo sana na umri wake ni mkubwa, hiyo ni ishara ya kwamba ni mgonjwa sana—na hakui kamwe.

      Ugonjwa wa marasmus, ugonjwa wa kwashiorkor, na mchanganyiko wa magonjwa hayo mawili husababishwa na aina ya utapiamlo ulio hatari sana wa kukosa vyakula vinavyojenga mwili. Ugonjwa wa marasmus huwapata watoto wanaonyonya wenye umri wa kati ya miezi 6 na miezi 18. Huanza polepole kwa upungufu mkubwa wa nishati, vitamini na madini na husababishwa na kutonyonya vya kutosha au kula vyakula vya badala visivyo na virutubisho vya kutosha. Mtoto mwenye ugonjwa huo hukonda sana, misuli yake hunyauka kiasi cha kubaki mifupa na ngozi, naye hakui. Uso wake huwa kama wa mtu aliyezeeka, anakasirika haraka na kulia sana.

      Neno la Kiafrika kwashiorkor linamaanisha “mtoto aliyeachishwa.” Linawahusu hasa watoto ambao wanaachishwa kunyonya ili ndugu au dada zao wachanga zaidi wanyonye. Ugonjwa huo huanza baada ya mtoto kuachishwa kunyonya. Unasababishwa na ukosefu mkubwa sana wa protini na upungufu wa kalori mwilini. Maji hurundamana mwilini na kumfanya mtoto avimbe tumbo, mikono na miguu. Nyakati nyingine uso wake huvimba na kuwa na umbo la mwezi mpevu. Vidonda hutokea kwenye ngozi na nywele hubadilika rangi na kukauka. Watoto wenye ugonjwa huu huvimba ini, hukosa uchangamfu na furaha. Ndivyo alivyokuwa Erik, aliyetajwa awali, ambaye alinyonyeshwa na mamaye kwa mwezi mmoja tu; kisha akaanza kunyweshwa maziwa ya ng’ombe yaliyotiwa maji. Alianza kunyweshwa mchuzi wa mboga na maji yenye sukari akiwa na umri wa miezi mitatu na kuachiwa jirani amtunze.

      Aina ya tatu ya utapiamlo huwa ni mchanganyiko wa ugonjwa wa marasmus na kwashiorkor. Magonjwa hayo yanaweza kuua yasipotibiwa haraka.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      MLINDE MTOTO WAKO ASIPATE UTAPIAMLO!

      ◼ Ni muhimu mama ale chakula bora. Akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji nishati na protini zaidi. Protini hasa humsaidia mama kuongeza maziwa. Kwa hiyo kunapokuwa na uhaba wa chakula, walisheni kwanza akina mama wenye umri wa kupata watoto na watoto wachanga.

      ◼ Mara nyingi, chakula bora zaidi kwa mtoto mchanga ni maziwa ya mama. Wanahitaji kunyonya hasa siku za kwanza-kwanza baada ya kuzaliwa kwa sababu maziwa ya mama yana kingamwili zinazomlinda mtoto asiambukizwe magonjwa. Katika miezi minne hivi ya kwanza, maziwa ya mama huwa na madini na vitamini zote ambazo mtoto anahitaji ili kukua ifaavyo.

      ◼ Ijapokuwa mtoto hutegemea sana maziwa ya mama, anaweza kulishwa vyakula vingine kati ya mwezi wa nne na wa sita. Mlishe hatua kwa hatua matunda na mboga zilizopondwa-pondwa. Kila mara mlishe mtoto chakula kipya. Siku mbili au tatu baadaye, akisha zoea chakula hicho, mlishe kingine tofauti. Bila shaka, unahitaji kuwa na subira na kumzoeza mara nyingi ili mtoto akubali chakula kipya. Unapotayarisha chakula hicho, kumbuka kwamba kila kitu chapaswa kuwa safi kabisa. Osha vyakula na vyombo vizuri!

      ◼ Kati ya mwezi wa tano na wa tisa, kwa kawaida watoto huhitaji nishati na protini zaidi kuliko zinazopatikana kwenye maziwa. Endelea kuwalisha vyakula vingine vipya bila kuacha. Anza kwa kuwalisha nafaka na vyakula vyenye mboga zinazoweza kuliwa na watoto, kisha uwalishe nyama na vyakula vilivyotengenezwa kutokana na maziwa. Ingawa mwanzoni vyakula vinavyoliwa na watoto huchujwa sana, baadaye vinaweza kukatwa-katwa vipande vidogo kuanzia mwezi wa sita na kuendelea. Hakuna haja wala haipendekezwi uongeze chumvi au sukari kwenye vyakula hivyo.

      ◼ Baada ya miezi minane, mtoto hategemei sana maziwa ya mama, bali hayo ni nyongeza tu. Yeye huanza kula vyakula vinavyoliwa na wengine katika familia. Vyakula vinapasa kuwa safi kabisa, na vinapasa kukatwa-katwa vipande vidogo ili mtoto avitafune kwa urahisi. Mlo unaofaa unatia ndani matunda na mboga, nafaka na kunde, nyama na vyakula vilivyotengenezwa kutokana na maziwa.b Watoto wanahitaji hasa vyakula vyenye vitamini A. Kwa mfano, maziwa ya mama, mboga za kijani, matunda na mboga zenye rangi ya machungwa kama vile maembe, mapapai, na karoti. Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu wanahitaji kula mara tano au sita kwa siku.

      ◼ Vyakula mbalimbali vilivyochanganywa kwa njia mbalimbali huwa na vitamini na madini yanayomlinda mtoto wako. Mama anapaswa kujitahidi kumlisha mtoto chakula bora, bila kumlazimisha ale wakati ameshiba wala kumnyima anapotaka kula zaidi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki