Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuzuru Tena Sayari Nyekundu
    Amkeni!—1999 | Novemba 22
    • [Picha katika ukurasa wa 15]

      Mars Climate Orbiter

      [Picha katika ukurasa wa 15]

      Mars Polar Lander

  • Kuzuru Tena Sayari Nyekundu
    Amkeni!—1999 | Novemba 22
    • Kuzuru Tena Sayari Nyekundu

      “Wapelelezi” wawili kutoka Duniani wametumwa kwa jirani yetu wa karibu katika mfumo wa jua, Mihiri. Matokeo ya uchunguzi wao yaweza kusaidia kujibu baadhi ya maswali ya msingi kuhusu jiolojia ya kale ya sayari nyekundu na vilevile hali yake ya sasa.

      TANGU nyakati za kale, Mihiri imechochea mawazo ya kibinadamu. Wazazi wetu wa kale waliokufa walihisi kwamba kulikuwa na jambo fulani lisilo la kawaida kuhusu gimba hilo la kimbingu lenye kung’aa na la rangi nyekundu lililovuka anga ya usiku haraka zaidi kuliko nyota nyinginezo. Wababiloni, Wagiriki, na Waroma wa kale waliipa sayari hiyo majina ya miungu yao ya vita na kifo, bila kufahamu uhakika wa kwamba rangi yake nyekundu ilikuwa uthibitisho tu wa mandhari iliyofunikwa na vumbi la chuma oksidi.

      Katika nyakati za karibuni zaidi, waastronomia walipoelekeza darubini-upeo zenye nguvu zaidi kwenye mfumo wa jua, ilikuwa dhahiri kwamba jirani yetu mwekundu ana misimu, vizio vya barafu, na mambo mengine yanayotukumbusha yale yaliyo Duniani. Katika karne ya 20, uchunguzi wa kwanza wa Mihiri ulifanywa na vyombo vya kuchunguza mambo ya anga, au vyombo vya anga, kutia ndani vyombo vinavyozunguka na vinavyotua, vilivyopelekwa huko na Muungano wa Sovieti na Marekani. Kisha kukaja safari ya Mars Pathfinder, iliyovutia uangalifu wa mamilioni ya watazamaji wa televisheni katika Julai 1997.a

      Kwa sasa, chombo kingine kiitwacho Mars Global Surveyor kinakusanya habari kwenye sayari nyekundu. Ingawa safari hizo zimeandaa habari nyingi sana, kungali kunabaki maswali mengi ya msingi kuhusu Mihiri.

      Maji Hayo Yako Wapi?

      Jambo la kawaida kuhusu maswali hayo ni maji. Wanasayansi wanakisia kwamba hapo zamani za kale, Mihiri ilikuwa tofauti sana na kile wanachoona leo. Wanasema juu ya sayari iliyokuwa na tabia ya nchi yenye joto zaidi, hewa yenye unyevunyevu, na mito iliyokuwa ikitiririka. Hata hivyo, kwa njia fulani maji hayo yalitoweka, yakibakisha tufe lililofagiliwa na upepo, lililokauka, na lenye vumbi ambalo hufanya hata majangwa ya Dunia yaonekane kuwa yanasitawi sana. Maji hayo yalienda wapi? Ni wapi ambapo maji yanaweza kupatikana sasa katika Mihiri, na katika umbo gani? Maji huathirije halihewa na tabia ya nchi ya Mihiri?

      “Ni hadithi ya upelelezi,” asema Norman Haynes, aliyekuwa msimamizi wa ofisi ya Kuchunguza Mihiri kwenye kituo cha NASA Jet Propulsion Laboratory, huko Pasadena, California. “Jambo la ujasiri kwelikweli katika Mihiri ni kutafuta ni nini kilichoyapata maji hayo.” Wanasayansi wanatumaini hivi karibuni watakaribia kupata jibu. Karibu kila miaka miwili, wakati Dunia na Mihiri zinapokaribiana ifaavyo, watafiti wanapanga kupeleka roboti za kuchunguza fumbo la Mihiri.

      Jozi ya karibuni zaidi ya “wapelelezi” hao ni chombo kinachozunguka kwenye kizio cha kuangalia hali ya hewa na kingine ni roboti iliyo kwenye Mihiri itakayowasaidia wanasayansi waone sehemu ya chini ya Mihiri. Majina yake ni Mars Climate Orbiter na Mars Polar Lander.

      Kuangalia Kutoka juu

      Chombo kinachoitwa Mars Climate Orbiter kilirushwa angani Desemba 11, 1998, kutoka kwenye Kituo cha Anga cha Kennedy, huko Cape Canaveral, Florida, na kuanza safari yake ya miezi tisa hadi Mihiri. Kimebuniwa kudumisha mzunguko wa kilometa 400, ambapo kitaweza kuchunguza angahewa ya sayari hiyo, milima na vitu kama hivyo, na ncha zake. Uchunguzi huo utachukua muda wa mwaka mzima wa Mihiri—ambao ni siku 687 za Dunia.

      Safari ya chombo cha angani cha kuchunguza hali ya hewa inatia ndani kutazama sura na mwendo wa vumbi la angahewa na mvuke wa maji juu ya Mihiri. Pia chombo hicho kimebuniwa kuchunguza mabadiliko ya msimu ya sayari hiyo. Picha zenye habari kamili ya vitu vilivyoko kwenye sayari hiyo zaweza kuwaandalia wanasayansi madokezo ya maana kuhusu historia ya mapema ya halihewa ya sayari hiyo. Kwa kuongezea, huenda habari hizo zikawasaidia sana watafiti kuhusu uwezekano wa akiba ya maji iliyoko chini ya ardhi ya Mihiri.

      Chombo hicho kitatumika pia kama kituo cha kubadilishana na chombo andamani, Mars Polar Lander. Chombo cha pili kilirushwa angani Januari 3, 1999, na kimeratibiwa kuwasili Mihiri mapema mwezi wa Desemba mwaka huu. Hata hivyo, ni wapi ambapo chombo hiki kinapopaswa kutua ili kipate matokeo makubwa zaidi?

      Kitatua Wapi?

      Kumbuka, suala la maji ndilo kubwa zaidi katika uchunguzi wa Mihiri. Ni mahali gani panapofaa zaidi katika sayari hiyo pa kuchunguza maji hayo? Halihewa, tabia ya nchi, na duru ya maji Duniani huchunguzwa kwa kulinganisha matokeo ya maelfu ya uchunguzi mmoja-mmoja uliofanywa kwa kutumia vifaa vya aina mbalimbali katika sehemu tofauti-tofauti. Hata hivyo, kuchunguza sayari nyingine hutaka mbinu ya pekee zaidi. Kwa sababu kila fursa ya kuchunguza uso wa Mihiri ni adimu sana, wachunguzi wa sayansi lazima wawe waangalifu wanapoamua ni vifaa gani watakavyovipeleka na watakakovipeleka.

      Kwa uchunguzi wa tabia ya nchi ya Mihiri, maeneo ya nchani ndiyo bora—hata ingawa ni tofauti kabisa na maeneo tambarare yaliyojaa mawe mahali ambapo Mars Pathfinder ilitua miaka miwili iliyopita. Misimu inayopita kiasi hutukia katika maeneo ya nchani. Inadhaniwa kwamba vumbi la dhoruba ya misimu huleta tabaka nyembamba ya vumbi katika maeneo ya nchani. Majira ya baridi kali yanapofika, vumbi huganda chini ya kaboni dioksidi na barafu. Baada ya muda, tabaka nyingi hutokea. “Tabaka hizo hudumisha rekodi ya historia ya tabia ya nchi ya [Mihiri],” asema Ralph Lorenz, wa Chuo Kikuu cha Arizona. Wataalamu wanaamini kwamba kuvumbuliwa kwa eneo hilo jipya kutakuwa hatua ya maana katika utafiti wa Mihiri. Jinsi gani hivyo? Chombo kitakachotua kitafanya nini baada ya hapo?

      Kutazama Chini ya Ardhi ya Mihiri

      Mashine hiyo inayofanana na buibui yenye urefu wa meta moja, ina miguu mitatu na vilevile mkono wa roboti wa meta mbili wenye upawa mwishoni. Kitaanza uchunguzi kabla hakijatua kwenye ardhi ya Mihiri. Kabla tu ya kufika kwenye angahewa ya sayari nyekundu chombo hicho kitatoa jozi ya vifaa, kila kimoja kikiwa na ukubwa upatao wa mpira wa kikapu.

      Vifaa hivyo vitakuwa vikianguka chini na kugonga ardhi kwa mwendo wa angalau kilometa 700 kwa saa. Vifaa hivyo vimebuniwa kwa njia ya kwamba vitapasuka vinapoanguka na kutokeza jozi ya vyombo vidogo zaidi vitakavyopenyezwa ndani ya ardhi kwa kina cha meta moja. Mara baada ya kufukiwa, vyombo hivyo vitatokeza keekee ndogo sana na kuanza kufanyia majaribio kemikali zilizo katika udongo wa Mihiri. Mradi wa kwanza utakuwa kutafuta maji yoyote ambayo huenda yakawa yamegandamana chini ya ardhi.

      Muda mfupi baada ya vifaa hivyo kufika ardhini, chombo kitafuata, kitashuka kwa mwavuli. Chombo hicho kina kamera na sensa, na kimebuniwa kuchunguza mandhari na halihewa ya Mihiri. Kitapiga picha wakati kinapotua na baada ya kutua ardhini. Mikrofoni ambayo inabebwa na chombo hicho itarekodi sauti ya upepo wa Mihiri kwa mara ya kwanza. Chombo hicho kimepangiwa kufanya kazi kwa muda wa siku zipatazo 90 baada ya kutua.

      Kichocheo cha Uvumbuzi

      Bila shaka, itawachukua wanasayansi miaka kadhaa kuchunguza na kuchanganua habari zilizokusanywa na Mars Climate Orbiter na Mars Polar Lander. Chombo hiki cha anga cha hivi karibuni zaidi ni sehemu ya jitihada ya miaka 16 ya kujifunza mengi kuhusu Mihiri. Mbali na NASA, mashirika ya vyombo vya anga ya Ulaya, Japani na Urusi pia yanahusika katika safari hizo. Hatimaye, wanasayansi wanatumaini kwamba safari za wakati ujao zitarudisha sampuli za udongo wa Mihiri kwenye maabara yaliyoko Duniani ili kuchanganuliwa. Huenda hilo likawasaidia hatimaye kujibu lile swali kuhusu ni nini kilichoipata tabia ya nchi ya sayari nyekundu ambayo ni jirani yetu, Mihiri.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki