-
Sayari Ndogo, Nyotamkia, na Dunia—Je, Ziko Katika Mwendo wa Kugongana?Amkeni!—1999 | Januari 22
-
-
Kufunua Kreta, Milipuko, na Migongano
Si vigumu kuamini kwamba sayari yetu imegongwa na vitu vikubwa ambavyo vimeanguka kutoka angani wakati uliopita. Ithibati ya migongano hii yaweza kupatikana katika kreta zaidi ya 150 zilizogunduliwa ambazo zimetoboa uso wa dunia. Kreta nyingine huonekana waziwazi, nyingine zaweza kuonekana tu ukiwa kwenye ndege au kutoka kwa setilaiti, na bado nyingine zimefunikwa kwa muda mrefu au ziko kwenye sakafu ya bahari.
Kreta moja mashuhuri sana kati ya hizi, inayojulikana kuwa Chicxulub, ilitokeza kovu lenye kipenyo cha kilometa 180 kwenye uso wa dunia. Kreta hii iliyoko karibu na ncha ya Peninsula ya Yucatán, Mexico, ni kubwa sana na inaaminiwa kuwa eneo ambapo palitokea mgongano wa nyotamkia au sayari ndogo yenye upana wa kilometa kumi. Watu fulani wanadai kwamba mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyoanzishwa na mgongano huu yalisababisha kutoweka kwa dinosau na wanyama wengine wa bara na wa baharini.
Katika Arizona, Marekani, kipande cha chuma kilichotoka kwenye nyota kilitoboa Meteor Crater yenye kustaajabisha—shimo lenye upana upatao meta 1,200 na kina cha meta 200. Ni watu wangapi ambao wangekufa ikiwa kipande cha chuma kama hicho kingeangukia jiji? Wonyesho unaopendwa sana kwenye Jumba la Makumbusho la Marekani la Historia ya Asili, katika New York City, unaonyesha kwamba ikiwa kitu kama hicho kingeipiga Manhattan, mji huo uliojaa watu ungeharibiwa kabisa.
Mnamo Juni 30, 1908, sayari ndogo au kipande kikubwa cha nyotamkia kinachokadiriwa kuwa na upana unaopungua meta 100 kiliingia kwa mngurumo kwenye angahewa na kulipuka kilometa zipatazo kumi juu ya eneo lisilokuwa na watu wengi la Tunguska la Siberia, kama ilivyotajwa katika utangulizi. Mlipuko huo, uliokadiriwa kuwa wa megatoni 15, uliharibu eneo lenye kilometa mraba 2,000, ukiangusha miti, kuwasha mioto, na kuua kulungu. Ni watu wangapi ambao wangekufa iwapo mahali palipotokea mlipuko huo palikuwa eneo lenye watu wengi sana?
-
-
Sayari Ndogo, Nyotamkia, na Dunia—Je, Ziko Katika Mwendo wa Kugongana?Amkeni!—1999 | Januari 22
-
-
Mpangilio wa Misiba
Wakiwa na hofu, wanasayansi wamefikiria matokeo yenye kutisha ambayo yangesababishwa kwa sayari yetu na mgongano wa nyotamkia au wa sayari ndogo. Hivi ndivyo wanavyofikiri matokeo ya mara moja ya mgongano mkubwa yangekuwa. Kungekuwako mlipuko mkubwa wa mawe na vumbi. Vifusi vinavyoanguka vingetokeza manyunyu ya vipande vya nyota ambayo yangelifanya anga liwe moto kwelikweli na kuanzisha mioto kwenye misitu na mbuga za nyasi, ikiua wanyama wengi wa ardhini. Vumbi ambayo ingebaki ikielea juu ya angahewa kwa kipindi kirefu zaidi ingezuia nuru ya jua, ikisababisha halijoto iporomoke na kukomesha usanidinuru kwenye sehemu za chini zenye giza. Kukomeshwa kwa usanidinuru pia kungeongoza kwenye kukatizwa kwa mfuatano wa chakula wa baharini, kukisababisha vifo vya viumbe wengi wa majini. Kulingana na mpangilio huu, msiba wa kimazingira ungefikia kikomo kwa kunyesha mvua ya asidi ya tufeni pote na kuharibiwa kwa tabaka ya ozoni.
Iwapo sayari ndogo ya namna hiyo ingeanguka baharini, ingesababisha mawimbi ya maji yaliyojaa yenye uwezo mkubwa sana wa uharibifu. Mawimbi ya maji yangefikia mbali zaidi kutoka kwenye eneo la mgongano kuliko wimbi la kishindo la kwanza na yangetokeza uharibifu wenye kuenea katika maeneo ya pwani yaliyo umbali wa maelfu ya kilometa. Mwastronomia Jack Hills asema: “Mahali palipokuwa na majiji, pangekuwa tu na ardhi tambarare.”
Hata hivyo, mtu apaswa kuwa mwangalifu kuhusu madai hayo. Nyingi za nadharia hizo ni mambo ya kukisia tu. Bila shaka, hakuna mtu ameona au kuchunguza sayari ndogo ikigongana na dunia. Pia, vyombo vya habari vya leo vinavyotamani kusambaza habari zenye kushtua hutokeza upesi vichwa vya habari vyenye kushtua, vinavyotegemea habari isiyo kamili au hata isiyo sahihi. (Ona sanduku lililo juu.) Kwa kweli, inasemekana kwamba uwezekano wa kufa kutokana na kitu kinachoanguka kutoka angani ni mdogo sana kuliko uwezekano wa kufa katika aksidenti ya gari.
-